Sam Gidori
Senior Member
- Sep 7, 2020
- 165
- 414
Kampuni ya Teknolojia ya Huawei inatarajiwa kurusha satelaiti mbili angani mwezi Julai, 2021 ikilenga kuingia katika teknolojia ya intaneti ya 6G.
Kampuni hiyo ya China imekuwa mstari wa mbele duniani kuboresha kasi ya upatikanaji wa mtandao wa intanet, hii ikiwa ni mara ya pili kurusha satelaiti angani kwa lengo la kujaribisha teknolojia hiyo.
Teknolojia ya 6G inatarajiwa kuwa na kasi mara 100 ya ile ya 5G. Kwa wastani, mtandao wa 5G una kasi ya juu zaidi ya Gigabits 20 kwa sekunde (Gbps) na kasi ya wastani ya 100+ Megabits kwa sekunde (Mbps).
Kampuni hiyo inatarajiwa kuzindua rasmi mtandao huo pamoja na kuweka miundombinu ya mtandao wa 6G ifikapo mwaka 2030. Huawei inatarajiwa pia kutoa maelezo kuieleza dunia teknolojia ya 6G ni nini hasa.
Hii inakuja wakati China ikijitutumua katika matumizi ya mtandao wa 5G, ikitajwa kuwa na watumiaji milioni 202 mwishoni mwa mwaka jana, idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka kufikia watumiaji milioni 822 ifikapo mwaka 2025.
Kwa sasa, Korea Kusini ndio nchi inayoongoza kwa matumizi ya mtandao wa 5G, ikiwa na asilimia 67 ya watumiaji wa mtandao huo, Marekani ikiwa na asilimia 55 na Japan ina asilimia 50. Asilimia 3 tu ya simu za mkononi duniani ndio zimeunganishwa na teknolojia ya 5G, nchi za bara la Asia zikiwa kileleni.
Wakati dunia ipo mbioni kwenda teknolojia ya 6G, Afrika bado inapambana na teknolojia ya 3G! Ripoti ya Mtandao wa Uchambuzi wa Teknolojia wa GSMA unasema kuwa takriban asilimia 51 ya simu za mkononi barani Afrika zimeunganishwa na teknolojia ya 3G.
Ingawa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara zimeanza kujiongeza kufikia teknolojia ya 5G, teknolojia ya 3G bado itaendelea kutawala katika nchi hizo kwa kipindi kirefu mbeleni. Mapema mwezi Aprili, Kenya ilikuwa nchi ya pili barani Afrika kujiunga na teknolojia hiyo baada ya Afrika Kusini, ikitajwa GSMA kuwa “hatua kubwa kwa Afrika kuelekea dunia ya 5G.”
Chanzo: Insidetelecom