SoC03 Hospitali Hazipaswi kuwa na Upungufu wa Damu Salama

Stories of Change - 2023 Competition

Tukuza hospitality

JF-Expert Member
Jul 30, 2022
242
615
Utangulizi

Kwa muda mrefu nimekuwa nasikia kampeni ya kuchangia damu kwa hiari kwa ajili ya kuwekeza katika Benki ya Damu Salama, kwa ajili ya kuwaongezea wagonjwa (wenye uhitaji huo) mahospitalini. Katika pita pita yangu, nimebahatika kuchangia damu kwa hiari mara mbili.

Hivi karibuni nimewahi kuwa na ndugu zangu wagonjwa wawili ambao kwa vipindi tofauti walihitaji huduma ya kuongezewa damu. Ndugu tulitakiwa kwenda kuchangia damu, na pale ambapo hatukuweza kuchangia kwa sababu mbalimbali (ikiwemo kutokanana na sababu za kiafya), mgonjwa/wagonjwa walipaswa kulipia huduma hiyo.

Nadhani hospiatali zipo sahihi kutoza malipo kwa huduma ya kuongezewa damu kutoka kwenye Benki ya Damu, pengine kutokana na gharama za kukusanya damu (usafiri, gharama za kampeni kuhamasisha watu kujitokeza kuchangia damu, nk). Lakini pia, kwa mtizamo wangu, kiasi kinachokusanywa kila mwaka ni kidogo ukilinganisha na mahitaji.

Kumbe kuna haja ya serikali pamoja na wadau wengine kuwajibika zaidi, na hivyo kupanua wigo wa kukusanya damu nchini, kwa kuongeza rasilimali na ubunifu, ili kupata damu ya kutosha, kiasi cha kutowalazimisha ndugu wa wagonjwa wanaohitji damu kuchangia damu au kulipia gharama ya huduma hiyo.

Taarifa ya Ukusanyaji wa Damu
Kila mwaka, Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Damu Salama huzunguka maeneo mbalimbali nchini kuhamasisha makundi mbalimbali ya watu kujitolea kuchangia damu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya (Machi, 2023), Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Damu Salama, kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI iliendesha kampeni ya ukusanyaji wa damu kuanzia tarehe 20-24 Machi, 2023, lengo lilikuwa ni kukusanya chupa za damu 22,000 kwa Mikoa yote 26. Jumla ya chupa za damu zilizokusanywa ni 18,334 sawa na asilimia 83.34 ya lengo kwa kipindi hicho.

Kwa mujibu wa mtandao wa TanzaniaWeb (Aprili 4, 2022), Wizara ya Afya Tanzania, imesema, zinahitajika jumla ya chupa za damu 500,000 ili kukidhi mahitaji ya mwaka ya damu salama nchini.

Kielelezo Na. 1: Zoezi la Uchangiaji wa Damu Tanzania
Damu Salama.png

Chanzo: www.nbts.go.tz

Kiasi cha Damu Kinachokusanywa ni Kidogo

Kwanza, kwa mtizamo wangu, lengo lililowekwa na Wizara ni dogo, kwa sababu kwa wagonjwa wanaohudumiwa hospitali zaidi ya 200 katika wilaya zote za Tanzania, ni sawa na wastani chupa 2500 tu kwa mwaka kwa kila hospitali. Naamini, mahitaji ya damu kwa kila hospitali kwa kila mwezi ni zaidi ya chupa 200, ukizingatia ukweli kuwa karibu kila siku kuna kina mama wajawazito na wanaojifungua, na baadhi huhitaji huduma ya kuongezewa damu; kuna ajali za kila mara, ambapo baadhi ya waathirika huhitaji kuongezewa damu; kuna wagonjwa wa saratani ya damu wanahitaji kuongezewa damu, pamoja na wagonjwa wengine, ambao baadhi yao huhitaji kuongezewa damu.

Sina takwimu rasmi ya mahitaji ya damu mahospitalini, lakini, ninapozingatia idadi ya watu Tanzania kwa sasa, ambapo tunakaribia milioni 62, naona benki ya damu inapaswa kuwa na chupa nyingi zaidi kwa mwaka.

Pamoja na Mpango wa Taifa wa Damu Salama kuweka lengo la kukusanya chupa 500,000 kwa mwaka (ambalo kwa mtizamo wangu ni dogo!), kwa mujibu wa Dkt. Magdalena Lyimo wa Wizara ya Afya (Aprili, 2022), kiasi cha chupa 331,000 kilikusanywa nchi nzima, ambapo ni sawa na asiimia 60.

Pamoja serikali kujiwekea lengo dogo la ukusanyaji wa damu, bado halikuweza kufikiwa kwa asilimia 100! Hii ina maana gani? Jitihada za kukusanya damu ziko chini; nasema hivyo kwa sababu, kwa sasa imepita zaidi ya miaka miwili toka nilipochangia damu kwa mara ya mwisho, kwa sababu sijafikiwa tena.

Haya yanathibitishwa na mtandao wa TanzaniaWeb (Aprili 4, 2022), uliponukuu Serikali kupitia Wizara ya Afya, ikisema “Kuna upungufu wa damu salama kwa asilimia 40 na kwamba chupa 150,000 za damu zinahitajika ili kuondokana na uhaba wa damu salama nchini.

TanzaniaWeb iliendelea kusema, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel alisema serikali ipo kwenye zoezi la kuzunguka nchi nzima kukusanya damu ili kuhakikisha suala la damu salama si tatizo tena nchini. Naibu Waziri Mollel alisema “Tunawaomba Watanzania damu, maana haiuzwi dukani, damu haitengenezwi, ni wananchi wenyewe kujitokeza; wakumbuke tunapoteza wakina mama wengi wajawazito kutokana na upungufu wa damu, tunapoteza watu wengi wa ajali za magari, tunapoteza wagonjwa wengi wa saratani ya damu kutokana na upungufu wa damu”.

Ninaamini watu sii wagumu kuchangia damu, bali wanahitaji hamasa na kufikiwa walipo; iwe ni mashuleni, vyuoni, makazini, masokoni, mashambani, mitaani, vijijini, na kadhalika.

Kiasi cha Damu Inayokusanywa Kinaweza Kuongezeka
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2022, kati ya karibu watu milioni 62, takribani watu milioni 30 ni wa umri kati ya miaka 18 na 60. Hili ni kundi ambalo linafuzu kuchangia damu!

Sasa, kwa mwaka mzima, tuchukulie asilimia 10 tu ya watu hawa inafikiwa na kuchangia damu; kiasi kisichopungua chupa 1,500,000 kitapatikana. Kwa maoni yangu, damu ipo ya kutosha, ila haikusanywi. Naamini, endapo damu itapatikana ya kutosha kila mwaka, basi mgonjwa yoyote anayehitaji kuongezewa damu, atapatiwa huduma hiyo bure, bila kuwalazimisha ndugu zake kuchangia damu au kulipia.

Mapendekezo
Serikali kupitia Mpango wa Taifa wa Damu Salama ijiwekee malengo makubwa ya kukusanya damu kwa kuwa na mpango mkakati wa kufikia asilimia 10 ya watu wote (karibu milioni 3) wenye uwezo wa kuchangia damu nchini.

Serikali, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ipanue wigo wa kukusanya damu, kwa kuhakikisha pamoja na vituo vilivyopo, vituo vingine vinafunguliwa kila kata nchini vitakavyofanya kazi hii kila siku, ili kuhakikisha damu inapatikana ya kutosha kukidhi mahitaji ya kila mwaka nchini.

Sambamba na hamasa ya kuchangia damu kupitia majukwaa mbalimbali (kama matamasha, matangazo nk.), serikali iangalie namna ya kutoa motisha kwa watu wanaojitolea kuchangia damu ili kuongeza kasi katika zoezi la ukusanyaji wa damu.

Hitimisho
Tanzania ina watu wa kutosha wa kujitolea kuchangia damu ya kutosha kukidhi mahitaji ya damu salama kila mwaka nchini; kinachotakiwa ni serikali kuongeza ubunifu na kuweka mpango mkakati wa kuwafikia.

Marejeo
TanzaniaWeb (Aprili 4, 2022), Tanzania Yakabiliwa na Upungufu wa Damu Salama.

Wizara ya Afya (Disemba 4, 2022), Hospitali za Rufaa za Mikoa Nchini Zaanza Kuzalisha Mazao ya Damu

Instagram, wizara_afyatz, Waziri Ummy Aagiza Hospitali za Rufaa za Mikoa Kuanza Kutengeneza Mazao ya Damu.
 

Attachments

  • Uchangiaji Damu nbts.go.tz.png
    Uchangiaji Damu nbts.go.tz.png
    412.1 KB · Views: 4
Kuna tatizo kubwa sana katika nchi zinazoendelea. Hata kukusanya damu kwa Watanzania, tunahitaji hela msaada wa wahisani kutoka nje ya nchi!
 
Njia bora ya kupata damu kwa njia endelevu, ni kusimamia lishe kwenye taasisi za umma (mashule, vyuo, makambi ya jeshi). Hii ni rasilimali kubwa sana ya kuchangia damu.
 
Back
Top Bottom