Muhimbili yakabiliwa na uhaba wa damu

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,119
Wakati ikiwa na uhitaji wa chupa 150 za damu kwa siku, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imekua ikikusanya chupa 35 mpaka 60 pekee hali inayochangia uwepo wa uhaba wa damu hospitalini hapo.

Makundi yaliyotajwa kuwa hatarini zaidi ni yale yenye idadi ndogo ya watu yaani asilimia 1 ya Watanzania ambayo ni makundi hasi yaani ‘negative’ yakihusisha A- B- AB- na O-.

Muhimbili ambayo imekuwa ikitoa matibabu ya kibingwa na hivyo kuhitaji kiasi kikubwa cha damu kwa siku, imesema kuna changamoto ya kukosa wachangiaji wa hiari ambao ndiyo wanaohitajika zaidi katika huduma hiyo.

Hayo yamebainishwa leo Jumatano, Oktoba 25 na Mtaalamu wa maabara na Msimamizi wa Kitengo cha Damu Muhimbili, Mussa Suko wakati wa ziara maalum ya vyombo vya habari iliyoandaliwa na Wizara ya Afya kuhusu umuhimu wa huduma za uchunguzi na vipimo kupitia maabara za afya ya binadamu ili kuwezesha matibabu sahihi kwa wagonjwa.

"Mahitaji ni chupa 150 kwa siku na hapo tunazungumzia mjumuisho wote wa mazao yote ya damu kwa maana ya damu yenyewe, chembe sahani, seli nyekundu na zile protini zinazosaidia damu kuganda," amesema.

Kufuatia hali hiyo, Suko ametoa wito kwa watu wote kujitokeza kuchangia damu kwa ajili ya wahitaji, "'Wahitaji ni mimi, wewe na mtu mwingine yeyote kwa maana mtu anaweza kuumwa ghafla, hatujui saa yoyote unaweza kupata ajali au ukapata tatizo lolote ukahitaji msaada wa damu sekunde chache zijazo hatujui hatma yetu."

Akizungumzia changamoto hiyo amesema kwa siku wachangiaji wanaowapata kwa siku ni asilimia 33 pekee kwa hiyo ni kamą chupa 60 kushuka chini ndizo hupatikana.

"Kwa hiyo utaona idadi inayohitajika ni kubwa ukilinganisha na idadi ya chupa zinazohitajika kwa siku."

Amesema kuchangia damu hakuna madhara yoyote baada ya kuchangia alisisitiza umri uwe kuanzia miaka 18 na kuendelea mpaka miaka 62 kwa kinamama na 65 kwa kina baba na uzito wa kilo 50 na kuendelea na wingi wa damu usiwe chini ya 12.5 g/d.

Mazao ya damu

Suko amesema damu inayovunwa inaweza kuchakatwa na kupata mazao mengi ya damu kupitia mashine mbalimbali ambazo zinasaidia kupatikana kwa chembe sahani zinazosaidia wagonjwa wanaotokwa na damu nyingi hasa mama wajawazito.

"Pia tunavuna seli nyekundu ambazo zinakuwa nyingi, chembe sahani ni chache na majimaji yenye protini yanakuwa machache lakini kupitia mashine hii unavuna mazao mengi ya damu."

Amesema wapo wagonjwa wanakaa wodini kusubiri chembe sahani kwa muda mrefu, hivyo mashine hiyo ya kuchuja mazao ya damu imesaidia.

"Wanaosuburu muda mrefu ni wagonjwa wa saratani ambao awali walitumia watu sita mpaka nane kuvuna chembe sahani sita au 12 lakini kwa sasa zinapatikana kutoka kwa mgonjwa mmoja kupitia hii mashine ambayo inatumika kuvuna uloto au chembe sahani na pia inapandikiza uloto na kuvuna chembe nyeupe," amesema.

Mteknolojia maabara kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Elizabeth Malapwa amesema damu inakaa siku 35 baada ya kuvunwa kabla ya kuharibika lakini bado upatikanaji wa damu bado ni mdogo sana kwa chupa 30 mpaka 60 kwa siku.

Amesema mazao ya damu yanakaa mpaka mwaka mmoja na chembe sahani zinakaa siku tano lakini hazifiki siku 5 huwa zimeisha kutokana na uhaba uliopo.

"Uhitaji wa damu asilimia 47 ni grupu 0±. Hawa ndiyo wahitaji wakubwa lakini grupu O- ni asilimia 1 Hawa huwa tunapata changamoto kubwa tukiwapata, tunawasiliana na wenzetu hospitali zingine na vitengo vinavyokusanya damu.

"Ili kupambana na hii changamoto tunayo mawasiliano ya wenye grupu la damu O± na hawa huwa tunawasiliana nao ili waje kutoa damu kwa dharura iwapo tutakosa aina hiyo ya damu," amesema Elizabeth.

Makundi yenye uhaba

Makundi adimu ya damu ni yale yenye vinasaba (-) ambayo yana uwezo wa kuyachangia makundi yote, mfano kundi la damu la O-(O negative).

Kuna makundi makuu manne ya damu ambayo ni A, B, AB, O na kila kundi lina aina yake ya vinasaba ambavyo (+) na (-).

Kizito amesema licha ya kukusanya damu nyingi, bado wanakabiliwa na uhaba kwa kundi la wenye vinasaba hasi yaani ‘negative’.

Asilimia moja 1 ya Watanzania wana kundi maalum liitwalo ‘negative’ huku asilimia 99 yao wakisalia kuwa kundi ‘positive’.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom