SoC01 Hata katika Majanga, Mashujaa huinuka na kusonga mbele

Stories of Change - 2021 Competition
Dec 17, 2012
15
15
Katika historia ya dunia tumekuwa tukipoteza wapendwa wetu siku hadi siku kwasababu nyingi. Takwimu za mwaka 2017, zinaonesha kulikuwa na vifo zaidi ya millioni 50 vya mwaka huo dunia nzima, 72.67% ya vifo vya dunia vimesababishwa na magonjwa yasivyoambukiza, na huku 19.49% ya vifo vikiletwa na magonjwa ya kuambukiza; na 7.84% ya vifo duniani vikisababishwa na mambo mengine kama ulevi, ajali n.k
1630681089736.png



Pichani: Takwimu za vifo kulingana na Shirika la Afya Duniani WHO.

Kuanzia Disemba 2019 dunia imeingia katika kipindi kipya ambacho kimefanya Ulimwengu kuwa na mtikisiko wa uchumi, majonzi, anguko la shughuli mbalimbali za binadamu kama biashara, usafiri na utalii. Mzizi ukiaminika kutokea Wuhan nchini China ambapo visa vilianza vya ugonjwa wa COVID-19 (Corona Virus Disease- 2019).

Wakati tunaunga mkono juhudi za Serikali na jumuiya ya kimataifa kupambana na huu ugonjwa unaoisumbua dunia kwa sasa wa COVID-19, niruhusu nikupe msomaji wangu baadhi ya magonjwa na majanga mengine yaliyowahi kuitesa dunia; kwasababu ninaamini kuwa historia ni mwalimu mzuri sana wa kutupa mwanga linapotokea suala ambalo limejirudia kwa kipindi fulani.

1. VVU/UKIMWI (HIV/AIDS); (1976- )
  • Kuanzia mlipuko wa ugonjwa huu kule Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwaka 1976 hadi kusambaa kwake Ulimwenguni kote ukisababishwa na kirusi kiitwacho HIV (Human Immunodeficiency Virus), ugonjwa huu hatari umeweza kuondoa maisha ya watu takribani millioni 36 duniani. Ugonjwa huu unaoambukizwa zaidi kwa ngono isiyo salama, hauna kinga wala tiba hadi leo hii ikiwa ni zaidi ya miaka 40 tangu kulipuka kwake.
  • Waathirika wa ugonjwa huu wanatumia dawa za kupunguza makali ya virusi zinazoitwa ARV lakini hadi sasa hakuna tamko rasmi kutoka Shirika la Afya Duniani kuhusu kupatikana kwa aidha kinga au dawa ya kirusi hichi hatari.
  • Tunashauriwa zaidi kuepuka ngono zembe, kuacha kushirikiana vitu vyenye nchi kali, kutowekewa damu isiyo salama na mama mjamzito aliyeathirika kuhudhuria kliniki ili kupata ushauri wa kumkinga mtoto atakayezaliwa mbali na ugonjwa huu.

2. SPANISH FLU; (1918 – 1920)
  • Haya yalikuwa mafua makali yaliyoitesa dunia kwa miaka miwili mfululizo na kuondosha zaidi ya watu millioni 20 hadi 50 Ulimwenguni kote na kuripoti zaidi ya wagonjwa millioni 500. Hatari sana hii!! Mafua haya kwa wiki 25 tu yaliua zaidi ya watu millioni 25, imezoeleka magonjwa mengi huwa yanaua watoto, wazee na wale wenye kinga hafifu, lakini ugonjwa huu uliwamaliza zaidi wale vijana wenye nguvu na rijali sana. Ugonjwa huu unasababishwa na kirusi cha mafua kiitwacho H1N1 Virus ambacho kimeleta aina mbalimbali za mafua ikiwemo yale mafua ya mwaka 2009
  • Cha kujifunza kwenye ugonjwa huu, ni kuwa baa hili lilikuwa na awamu tatu, baada ya awamu ya kwanza kuisha watu walijisahau sana, wakasahau tahadhari zote, wakajiachia na kurudi maisha ya kawaida, awamu ya pili ikaondoa watu wengi zaidi. Awamu ya tatu iliwafungua watu ufahamu wakachukua tahadhari na unafuu ukaanza kuonekana
Tuwe na ufahamu kuwa Serikali inaweza kupumzika na kulegeza masharti ya kujikinga lakini ugonjwa haupumziki kamwe!

3. BLACK DEATH au KIFO CHEUSI (1346-1353)


Jina lenyewe la kifo cheusi linatisha, hii ilikuwa tauni ambayo ilisambazwa kwa njia ya panya, almaarufu kama Bubonic Plague, tauni hii iliua watu takribani millioni 75 hadi millioni 200 kwa kipindi cha miaka 7. Ugonjwa huu uliathiri Afrika, Asia na Ulaya, iliaminika kuwa ilianza Asia na panya hawa waliobeba vimelea vya ugonjwa walikuwemo katika baadhi ya meli za biashara zinazosafiri katika mabara haya.

1630682102618.png

Pichani: Miili ya watu iliogundulika kufa kutokana na kifo cheusi cha tauni.

Na kwasababu meli hizi zilikuwa zikitua kwenye bandari ambazo zilikuwa maeneo ya mjini na sehemu zenye mzunguko mkubwa wa watu basi ilikuwa rahisi kwa ugonjwa huu kusambaa.

1630682143789.png

Pichani: Barakoa zilizotumiwa na madaktari kipindi wanahudumia wagonjwa wa tauni.

1630682178490.png

Panya walitumika kusambaza ugonjwa huu.

Wataalamu wa historia wanasema ilikuwa ikionekana unaumwa ugonjwa huu, basi unachimbiwa kaburi mapema, tena sio lako tu, bali lako na familia yako na watu waliokuwa karibu na wewe. Madaktari kipindi hichi walikuwa na barakoa zao maalumu za kujikinga kama zinavyoonekana pichani hapa chini, ambazo zilikuwa zinafunika uso, pua na mdomo. Aisee!

Asikwambie mtu, huu haukuwa tu ugonjwa bali ni kama fagio la malaika Israel linakufyeka na kupona ni kudra za Mwenyezi Mungu pekee.

4. TAUNI YA JUSTINIANI (541-542)
  • Hii ilikuwa karne ya 6, nyuma sana, lakini bado historia yake imeandikwa kwasababu ya watu zaidi ya millioni 25 kuondoka kwa tauni hii ikiwa chanzo chake ni kama ya kifo cheusi ikisababishwa na Bubonic Plague. Nadhani unaona jinsi historia ilivyojirudia; kumbe kifo cheusi cha karne ya 15 kilianzia na tauni hii ya Justiniani ya karne ya 6.
  • Ugonjwa huu uliweza kuua zaidi ya watu 5,000 kwa siku na ukasambaa maeneo ya bahari ya Mediterania, vivuko vyake pamoja na miji ya jirani kama Constantinople ukiathirika zaidi, huku zaidi ya 40% ya wakazi wake wakifa kwa ugonjwa huu hatari

5. KIPINDUPINDU (1852-1860)
  • Huu ni ugonjwa wa mlipuko ambao hutokea na kuua watu kadhaa kisha kupotea, uchafu wa mazingira hasa kwenye vyanzo vya maji ni chanzo kikuu cha kusambaa kwa ugonjwa huu. Ila sasa kuna kipindupindu cha kipekee, waswahili wanasema kipindupindu cha kiwango cha lami kilichotokea karne ya 19 na kusambaa Asia, America ya Kaskazini, Ulaya na Afrika na kiliua watu zaidi ya Millioni 1.
  • Mara nyingi ugonjwa wa kipindupindu huwa haudumu zaidi ya miezi 6, lakini kilichotokea hiyo miaka kilitembeza kichapo kwa miaka 8 bila kuchoka
  • Hata katika jamii zetu siku hizi, uchafu uliokithiri unaweza kuleta mlipuko kwenye eneo husika.
Mazingira machafu ni sababu tosha ya magonjwa ya mlupuko, na hata kuua watu wengi kama kipindupindu

6. Ebola Virus Disease (EVD)
  • Ilisambaa zaidi Afrika Magharibi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
  • Imeua watu takribani 11,323 kuanzia Disemba 2013- Juni 2016

7. Malaria
  • Imeathiri maeneo ya Tropiki kama Afrika,
  • Zaidi ya watu millioni 1 wanakufa na malaria kila mwaka, wengi wao wakitokea kwenye nchi zilizoko kusini mwa jangwa la Sahara na huku karibu 57% ya vifo vikiwa ni vya watoto wa umri chini ya miaka mitano.
Mbali na magonjwa, vita na matatizo ya uchumi yamekuwa majanga makubwa katika Historia ya Dunia.

Naamini kuna ambao tunakumbuka vita vya kwanza na vya pili vya dunia. Vimetokea vita vingi duniani, lakini vita vya kwanza na vya pili vimekuwa ni vita vikubwa ambavyo dunia imeathrika navyo hata kuwa sababu ya anguko la kiuchumi. Twende pamoja sasa!


1. VITA VYA KWANZA VYA DUNIA (Julai 28, 1914- Novemba 11,1918)


Vita hizi zilikuwa baina ya nchi za kibepari zilizoko Ulaya, lakini zikahusisha hadi makoloni yao yaliyoko Afrika na Asia. Zaidi ya watu millioni 9 walifariki katika vita hizi zilizodumu kwa zaidi ya miaka minne mfululizo. Sababu kuu ya vita hizi ni ugomvi wa kugombani rasilimali, na vita hizi ziliibuka ghafla baada ya Ujerumani kuvamia na kumnyang’anya Mfaransa millki zake za Alsace na Loraine. Watu wengi walikufa dunia nzima na baada ya vita uhariibifu ule ukasababisha

2. ANGUKO KUU LA KIUCHUMI LA MWAKA 1929-1933

Anguko hili la kiuchumi lilianzia kule New York Marekani baada ya kushuka kwa soko la hisa mwezi wa kumi tarehe 24 1929 hadi siku hiyo ikaitwa Alhamisi Nyeusi. Hapa ndio anguko la kiuchumi lilipoanza na hata kusambaa dunia nzima.

Pamoja na hayo walikuwepo watu miaka hiyo waliojipatia utajiri katikati ya janga hilo la uchumi. Wapo kina Bank Rober Dilinger aliyekuwa muigizaji na baada ya anguko la uchumi akaitumia faida yake kuanzisha kampuni yake iliyokuja kumzalishia faida ya zaidi ya Dola za kimarekani 20,000 kila wiki. Yaani alikuwa anaingiza Dola 80,000 zaidi ya millioni 160 za kitanzania kila mwezi.

3. VITA VYA PILI VYA DUNIA (Septemba 1, 1939- Septemba 2,1945)

Vita hizi hadi Mmarekani alishiriki, Mjerumani alionekana kuwa na nguvu sana katika vita za kwanza za dunia. Hivyo, zilipoisha wakamwekea vikwazo vingi kupitia ule mkataba wa Versaille uliosainiwa Ufaransa. Alinyang’anywa na makoloni yake mengi Afrika ikiwemo Tanganyika na Namibia. Manyanyaso yale yalimpelekea kuibua vita ya pili ya dunia chini ya kiongozi wake dikteta Adolf Hitler.

Zaidi ya watu millioni 24 walipoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa wakiwemo hata babu zetu miaka hiyo.
Nilichojifunza baada ya vita hii, Mmarekani alianza kuinuka kama Taifa lenye nguvu sana na kupelekea kuwa nchi ya kwanza ya uchumi mkubwa duniani mpaka leo. Unajua kwanini? Mmarekani alitumia ile fursa ya vita kuuza dawa na silaha kwa nchi zinazopigana. Yeye alijijenga wakati wengine wakijibomoa

Fursa katika maisha ziko hivyo hivyo, hata kama ni majanga, bado yanaweza kuwa fursa ya kubadiisha maisha yako!

1630683212860.png

Vita ni majanga.

Kipi cha kujifunza kutokana na majanga haya ya kibinadamu yanapoikumba duniani??
  • Napenda sana msemo mmoja unaosema “History reminds; some heroes arised during a crisis” ikimaanisha, historia hukumbusha kuwa baadhi ya mashujaa walizaliwa kipindi cha majanga.
  • Wanadamu tunapaswa kuwa wabunifu, kila tatizo ni fursa. Kama jinsi lockdown hii ilivyomnufaisha mwenye mtandao wa Zoom, Bwana Eric Yuan ambae amejivunia kuongeza utajiri wake kwa zaidi ya dola za kimarekani billioni 7.88 kwa miezi miwili tu – hata kwako inawezekana.
1630683353818.png

Eric Yuan mmiliki wa Zoom

Kipindi cha lockdown ya karne ya 17 iliyosababishwa na tauni huko Ulaya, akiwa nyumbani wakati anamsaidia mama yake shughuli za kilimo huko Uingereza, mwanafunzi wa chuo mmoja aliona tunda likianguka kutoka mtini, ndipo ubunifu wake wa kugundua baadhi ya sheria za kisayansi ukazaliwa (Law of Gravity); kijana huyu Isaac Newton umahiri wake wa sayansi ulizaliwa kipindi cha karantini.

Wachambuzi wakasema “Millions saw an apple falling down from a tree, but only Isaac Newton asked why?”
Shauku ya kujifunza ulimfanya Isaac Newton ajiulize kwanini tunda hili limeanguka ilhali ni wengi wamekuwa wakishuhudia tunda kuanguka kutoka kwenye mti.


1630683513733.png

Isaac Newton chini ya mti.


Kipindi hiki bado ni fursa, naweza kusema ukiwa na ubunifu, mawazo yakinifu na moyo wa kujifunza hii itakuwa ni wakati wa neema ambao utabadilisha sehemu kubwa ya maisha yako.

Wewe ni shujaa, onesha mchango wako katika kuiokoa dunia.

Na: Humphrey Mrema.
 
"Hata katika Majanga-Mashujaa huamka na kusonga mbele".Nchi(pamoja na watu Binafsi) pia zinatakiwa zijiandae kukabilian na majanga Kama hya kwa Sababu magonjwa mengi (zoonotic diseases) yanasababishwa na mabadiliko ya Tabia ya nchi( climate change)

_Success comes when opportunity and preparation meets!
 
Back
Top Bottom