Halima Mdee, Mbatia hakuna amani
- Posted on October 4, 2010 at 10:30am
Na Mwandishi Wetu
Joto la kisiasa limezidi kupanda, Jimbo la Kawe wagombea wawili wenye nguvu lakini wote wakiwa na tiketi za vyama vya upinzani, Halima Mdee (CHADEMA) na James Mbatia (NCCR-Mageuzi), hawapatani na katika mapambano yao ya kisiasa hakuna amani.
Habari zisizo na shaka zinasema kuwa kila upande umekuwa ukimshutumu mwenzake kwamba unamhujumu kisiasa, hivyo kukuza mtifuano kati yao huku wakimsahau mpinzani wao mkubwa, Angela Kizigha (CCM).
Wiki iliyopita, gazeti hili lilizungumza na msaidizi wa Mbatia, Hamis Athuman ambaye alisema kuwa wanasheria wa NCCR chini Mhadhiri, Sengondo Mvungi wanafuatilia kauli za Halima kabla ya kuamua cha kufanya baadaye.
Alhamisi iliyopita, gazeti hili lilipewa taarifa na chanzo chake cha kuaminika kuhusu Halima kumpigia simu Mbatia na kumshutumu kwamba amekuwa akiendesha kampeni chafu dhidi yake, ikiwemo kumtangazia kuwa amejitoa kinyanganyiro cha kuwania Ubunge Kawe.
Amempigia simu na hawakuongea vizuri, unaweza kuona jinsi hali ilivyo. Ni siasa lakini hakuna aliye tayari kuona mwenzake anakuwa na mtaji mkubwa wa kisiasa kuliko yeye, kwahiyo hakuna maelewano hasa pale inapoonekana kuna mtu amezungumza kitu cha kumuathiri mwingine, alisema mtoa habari wetu.
Halima, alipoulizwa na gazeti hili kuhusu kumpigia simu Mbatia, alikiri na kusisitiza kwamba alifanya hivyo kumuonya kwa sababu amekuwa akizungumza maneno ya kumchonganisha na wapigakura wake.
Kwenye mkutano wao Tegeta Jumatano iliyopita, walitangaza nimejitoa kugombea Ubunge Kawe kwa sababu nimeshinda Viti Maalum CHADEMA kitu ambacho si cha kweli. Ilikuwa ni kunichonganisha na wapigakura wangu, kwahiyo Mbatia na chama chake hawakunitendea haki ndiyo maana nilimpigia simu.
Nilimwambia aache, mimi shida yangu si Ubunge, lengo langu ni kuwatetea wananchi. Kusema nimeshinda Viti Maalum wakati si kweli ni kuniharibia. Nagombea jimbo na lengo langu la Kawe ili niwatetee wananchi, alisema Halima.
Mbatia alipotafutwa, simu yake ilipokelewa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Jimbo la Kawe, Hemed Msabaha ambaye alisema kuwa kama Halima alipiga simu, basi alifanya hivyo kirafiki kwa sababu sheria hazitamki alivyofanya.
Iweje Halima ampigie simu mtuhumiwa wake? Angekwenda kushtaki, kitu kingine siku hiyo inasemwa ni gazeti liliandika Halima ameshinda Viti Maalum lakini Mbatia hakuzungumza hayo maneno na vizuri ni kwamba sisi huwa tunajadili hoja badala ya watu, alisema Hemed.
Source: GPL