Hadithi ya kusisimua: Vita ya wachawi

Hadithi ya kusisimua: Vita ya wachawi

HADITHI YA KUSISIMUWA VITA YA WACHAWI-19

ILIPOISHIA:
Watu waliumia kutokana na tabia za Bupe kila mvulana alipenda awe mkewe, wengi waliamini mchezo ule umefanywa palepale kijijini kwa wivu wa kuolewa yeye na kuwaacha wasichana wengine. Kilasilo kila mtu alisema lake lakini mzee Ambokile alijua kila kitu.
SASA ENDELEA...


Kutokana na mwili kutoka kwenye maji hawakutaka kuuweka sana, walipanga mazishi yake siku ya pili asubuhi. Siku ya pili yalifanyika mazishi yaliyohudhuriwa na umati wa watu ambao waliguswa na msiba ule ambao nguvu za giza zilitawala na kutishia ndoa za wasichana wa Kilasilo ambao walikuwa mbioni kuolewa kwa kuamini nao watakufa kama Bupe.
Baada ya mazishi, jioni mganga alikuwa na mazungumzo na familia ya mzee Ambokile juu ya tukio lile.
"Jamani nimejitahidi kadri ya uwezo wangu, lakini nilikuwa napambana na jeshi la watu wengi. Bila hilo ningeweza kumtoa hai. Sasa baada ya tukio hilo kama wazazi mlikuwa mnasemaje?"
"Tunakusikiliza wewe."
"Mnamuachia Mungu au na nyinyi mnataka kurudisha kombora lilipotoka?"
"Kwa vile wamemkata binti yangu hivihivi na mimi nataka aliyefanya hivi basi naye akatike kama mwanangu," alisema mama Bupe kwa uchungu.
"Basi kazi hiyo kwangu ndogo sana," alisema mganga Msioka.
"Unasema wameshiriki zaidi ya mtu mmoja wote utawafyeka?"
"Kila aliyehusika hatabaki hai hata awe nani kwa dawa nitakayoifanya utaniambia, hata uwe ukoo mzima utapukutika ila kwa aliyehusika tu."
"Majibu lini?"
"Narudi leo Malawi, leo usiku silali nitakesha na kazi hiyo, asubuhi nalituma kombora, mpaka jioni mtasikia majibu ya kazi mliyonituma, kwa vile sehemu yenyewe mbali unaweza kwenda kusikilizia kumetokea nini."
"Tutashukuru maana wametuchukulia jicho letu, kama ikiwezekana fagia ukoo mzima."
"Ninyi si mmenipa kazi, basi kaeni kimya muuone moto wangu, mimi ndiye Msioka," mganga alijitapa.
Baada ya makubaliano, mganga Msioka aliondoka kurudi Malawi ili kurudisha kombora kwa mtu aliyeshiriki kumuua Bupe.
KIJIJINI IBUNGU
Siku iliyofuta taarifa zilifika kijijini Ibungu juu ya msiba wa mchumba wa Ambakisye aliyetolewa na mganga toka Malawi akiwa amefariki na mazishi kufanyika haraka siku iliyofuata kutokana na kuogopa mwili kuharibika.
Taarifa ile ilikuwa kama shubiri kwa mzee Amangise baada ya kusikia mazingira ya kifo cha mkwewe mtarajiwa, aliamini kabisa waliofanya hivyo ni familia ya mpenzi wa mwanaye.
Lakini hakuwa na jinsi zaidi ya kuzipokea habari zile na kuziacha kama zilivyo kutokana na maneno mazito aliyoyatoa mwanaye juu ya familia ya mpenzi wake kama kingewatokea chochote basi yeye angechukua uamuzi mzito juu ya familia yake.
Taarifa za kuonekana kwa Bupe akiwa amekufa zilimfikia Ambakisye ambaye alifurahia moyoni kwa kujua ndoa na Atuganile ipo karibu hasa baada ya familia yake kuonesha kubadilika na uamuzi wao mzito juu ya wazazi wenzao.
Alitoka na furaha hadi kwa mpenzi, Atuganile alipomuona alijawa na shauku ya kutaka kujua jana yake mpenzi wake kazungumza nini na wazazi wake.
"Karibu mpenzi wangu, yaani uso wako unaonesha kuna dalili njema."
"Ni kweli, hebu nipe kwanza kwenu ilikuwaje ili nami nikujuze yaliyojiri."
Atuganile alimweleza mpenzi wake jinsi alivyowachachafya wazazi wake mpaka wakabadili uamuzi na kufuata anachokitaka yeye.
Ambakisye naye alimueleza mtiti aliouanzisha kwao baada ya mpenzi wake kumsikiliza alimuuliza.
"Sasa Amba kama baba yako angeendelea kusimamia msimamo wake ungeondoka kweli?"
"Nilikuwa sitanii ningejua mbele ya safari lakini si kukaa nyumba ya wauaji wale."
"Sasa tutafanyaje ili familia zikae pamoja na kumaliza tatizo?"
"Si bibi Tumwambilile alisema atakaa nao kwa vile kazi kubwa tumemaliza itakuwa rahisi kulizungumza."
"Na kweli, unaonaje twende tukamwambie sasa hivi?"
"Poa, tena nina habari njema mpenzi wangu."
"Habari gani tena mpenzi?" Atuganile alishtuka.
"Bupe kapatikana..."
"Sasa hizo ndizo habari njema, yaani kumbe unanidanganya unanipenda kumbe mawazo yako yapo kwa Bupe?" Atuganile alimkata kauli mpenzi wake na kuliza wivu.
"Atu, mbona unanikata kauli kabla sijamaliza sentesi yangu."
"Kuna nini zaidi ya kunirusha roho, jana nimewakosea adabu wazazi wangu kwa ajili yako, kumbe kuna mtu unayempenda."
"Atu, tutakorofishana naomba uniache nimalize ninachotaka kukueleza."
"Haya sema."
"Bupe kapatikana juzi mtoni akiwa amekufa na kazikwa jana."
"Muongo unataka kuniongopee."
"Atu mpenzi wangu kipi utakachoniamini, kweli taarifa imefika nyumbani nasikia ametolewa ndani ya maji akiwa amenyolewa upande mmoja. Tena nasikia baba yake kasafiri mpaka Malawi kumfuata mganga kwani wa pale Kilasilo walichemka."
"Mmh! Unajua siamini."
"Ndiyo maana nikakuambia habari njema, sasa hivi ndoa nyeupe baada ya kuwatolea uvivu wazazi wetu."
Atuganile alifurahi kwa kurukaruka na kumkumbatia mpenzi wake baada ya kujua aliyekuwa akimpa presha amekufa.
"Sasa hivi nina uhakika wa kuitwa Mrs Amba," Atuganile alijishebedua.
"Basi tuwahi kwa bibi Tumwambilile."
Walikubaliana kwenda kwa bibi Tumwambilile kumwambia walipofikia na wazazi wao. Walikwenda taratibu huku wakizungumza:
"Mmh! Bado siamini kama utanioa."
"Kipi kitakachofanya nisikuoe ikiwa yule msichana amekufa."
Wakiwa wameacha barabara kuu na kuingia yenye majani ili kupita njia ya mkato, ghafla mbele yao alitokea nyoka mweusi walishtuka na kutaka kumkwepa kwa kuruka nyuma lakini nyoka yule aliruka na kutaka kumuuma Atuganile. Kwa vile alikuwa amemuelekea alijitahidi kumkwepa na kurudi nyuma lakini kwa bahati mbaya alijikwaa na kuanguka chini.
Nyoka yule alimgonga mguuni, alikuwa tofauti na nyoka wengine baada ya kumgonga Atuganile wakati akipiga kelele za kuomba msaada kwa maajabu yule nyoka, aliingia mdomoni na kuishia wote ndani ya mwili. Muda uleule Atuganile alibadilika rangi na kuwa mweusi, Ambakisye alichanganyikiwa na kushindwa kumsaidia mpenzi wake.


Itaendelea Kesho.............
 
Daaaaaahhh!!!!

Sasa itakuwaje hapa Atu amekufa.

Vita itakuwa kubwa, na kweli kutabaki magofu.


MIZAMBWA
INANIUMA SANA!!!
 
HADITHI YA KUSISIMUWA VITA YA WACHAWI-20

ILIPOISHIA:
Nyoka yule alimgonga mguuni, alikuwa tofauti na nyoka wengine baada ya kumgonga Atuganile wakati akipiga kelele za kuomba msaada kwa maajabu yule nyoka aliingia mdomoni. Muda uleule Atuganile alibadilika rangi na kuwa mweusi, Ambakisye alichanganyikiwa na kushindwa kumsaidia mpenzi wake.
SASA ENDELEA...


Alitoka mbio hadi kwa bibi Tumwambilile kuomba msaada, alipofika alikuta nyumba ipo kimya ila mlango ukiwa wazi, alimwita kwa sauti lakini hakukuwa na jibu lolote.
Aliingia ndani na kushtushwa na mkoromo mzito, aliposogea alishtuka kuona aliyelala pale chini kumbe ni bibi Tumwambilile bila nguo yoyote huku ndani kukiwa na harufu kali ya kinyesi, hali ile ilimtisha sana.
Alimsogelea akitetemeka huku ameziba pua kutokana na harufu kali, alijaribu kumwita hakukuwa na jibu lolote zaidi ya kuzidi kukoroma, baada ya muda alimsikia akivuta mkoromo mrefu na kutulia. Hali ile ilizidi kumchanganya Ambakisye aliyetoka mbio kurudi kwa mpenzi wake.
Alipofika alishangaa kukuta akiwa bado yupo palepale amelala chini mdomo ukiwa wazi, alipomsogelea karibu huku akitetemeka alishtuka kuona kitu mdomoni kwa mpenzi wake. Alipoangalia vizuri alikiona kichwa cha nyoka kikichungulia kuonesha yule nyoka alitaka kutoka.
Ghafla yule nyoka alitoka mdomoni kwa Atuganile na kutoweka bila kujua amekwenda wapi. Akiwa bado anatetemeka alimsogelea mpenzi wake aliyekuwa bado amelala chini ametulia kama amekufa kwa vile alikuwa hajigeuzi.
Kwenye jeraha la kuumwa na nyoka palianza kutoa funza kama kidonda cha muda mrefu, Ambakisye alizidi kuchanganyikiwa na kuanza kulia kwa sauti iliyofanya wapita njia kumfuata na kutaka kujua alitokewa na nini. Walipofika walishtuka kumuona Atuganile akiwa amelala huku mwili wake ukiwa mweusi kama kapakwa mkaa.
"Kafanya nini?"
"Tulikuwa tunapita ghafla katokea nyoka wa ajabu na kumgonga kisha kutoweka katika mazingira ya kutatanisha."
"Mmh! Watu wamesha anza, jamani watu wa kijiji hiki hawamuogopi Mungu kila kukicha kurogana?" alisema mama mmoja kwa uchungu.
"Mmh! Tumuwahishe kwao, hali ya Atu inatisha," mwingine alitoa wazo.
Walimbeba na kumpeleka kwao akiwa amepoteza fahamu, wazazi wake walishtuka kuwaona watu wamembeba Atuganile juujuu.
"Vipi jamani kulikoni?" mama Atuganile aliuliza kwa hofu.
"Amegongwa na nyoka."
"Nyoka?"
"Ndiyo tena nyoka mwenyewe wa mauzauza baada ya kumgonga amepotea."
Wazazi wa Atuganile walichanganyikiwa, walipomuangalia mtoto wao alikuwa na kila dalili za mfu, hakuwa na dalili za kupumua huku kidonda chake kikitoa harufu kali ya kuoza na wadudu kuendelea kutoka. Kilichowashangaza, mwili ule ulianza kuvimba na kuwa kama papai lililoiva.
"Amba, mwanangu umemfanyaje?" mama Atu alimuuliza Ambakisye huku akilia.
"Tulikuwa tunakwenda kwa bibi Tumwambilile akatokea nyoka ambaye alimgonga na baadaye kuingia mdomoni."
"Mungu wangu! Yaani nyoka kaingia mdomoni kwa mwanangu?" mama Atuganile alisema kwa sauti ya kilio.
"Lakini alitoka ."
"Mungu wangu! baba yako amemuua mwanangu," walipeleka tuhuma moja kwa moja katika familia ya mzee Amanyisye.
"Mume wangu wahi kwa bibi hali ni mbaya."
Ambakisye alishindwa kuwaeleza alichokikuta kwa bibi kwa kuogopa kuongezewa tuhuma kwa kuonekana tatizo alilomkuta nalo bibi Tumwambilile familia yao inahusika. Alikaa kimya ili kusubiri jibu atakalorudi nalo baba Atuganile.
Mzee Andendekisye alikimbilia kwa bibi Tumwambile kumweleza tatizo lililomtokea mwanaye. Alipofika mlangoni alishtuka kukutana na nyoka mkubwa, alisita kuingia mara yule nyoka alitoka na kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
Kwa vile alikuwa akijua michezo ya bibi hakushtuka sana na kuingia ndani huku akiita. Nyumba ilikuwa kimya kama hakuna mtu, aliingia ndani huku akiita jina la bibi,akakutana na harufu kali ya kinyesi. Alitoka nje kutokana na harufu ile kuwa kali, alizuguka nyuma ya nyumba labda atamkuta lakini hakukuwa na jibu.
Alitaka kuondoka kurudi nyumbani lakini moyo ulisita, aliamua kuingia ndani ili ajue kama amelala ili amuamshe kwa vile asingerudi bila kumuona. Pamoja na harufu kali aliingia ndani alipokaribia mlango wa chumbani alimuona mtu amelala chini akiwa hana nguo mwilini. Alishtuka sana na kumsogelea huku harufu ya kinyesi ikiwa kali. Alimwita kwa sauti ya chini labda ataamka pale chini alikuwa amejitapakaza kinyesi.
Alijipa moyo na kumgeuza ili amuondoe kwenye kinyesi kile na kumfanyia usafi, kwa vile alikuwa amelala kifudifudi alimgeuza na kushtuka kumuona hana jicho moja, sehemu ya jicho ilikuwa ikivuja damu na kuonesha bibi Tumwambilile alikuwa amekufa kifo kibaya sana.
Alitoka mbio kwa hofu na kujikuta akijikwaa na kuanguka kwenye vumbi na mwili wote kujaa vumbi kama alikuwa akiogelea kwenye vumbi. Alirudi nyumbani mbio kama mtu anayefukuzwa na simba, mke wake na watu waliokuwepo walishtuka na kumuuliza:
"Vipi mbona hivyo?"
"Wametumaliza."
"Una maanisha nini?"
"Tegemeo letu wamelimaliza."
"Una maanisha nini hebu kuwa muwazi."
"Bi...bi...bi...a...a...me...ku.."
"Amefanya nini?"
"Amekufa kwa...kwa...kutolewa roho kikatili."
"Mungu wangu nisaidie mimi! Jamani kijijini kwetu kumeingia nini?" jirani mmoja alisema kwa uchungu huku mikono ikiwa kichwani.
"Yaani kama mwanangu akifa aliyekula mbuzi wangu atanilipia ng'ombe kumi," mzee Andendesye alisema kwa uchungu.
"Sasa mume wangu tutafanyaje?"
"Labda tumfuate Kigugu nasikia na yeye ni mtaalamu wa mambo haya."
"Nina wasiwasi na mwanangu maana sioni dalili zozote za kuwepo mtu hapa," mama alisema kwa kukata tamaa.

Itaendelea Kesho.............
 
Back
Top Bottom