Hadithi ya kusisimua: Vita ya wachawi

Hadithi ya kusisimua: Vita ya wachawi

HADITHI YA KUSISIMUWA VITA YA WACHAWI-11

ILIPOISHIA...
Kila mmoja alisema lake, mwenye jicho la tatu walijua ule ni mchezo umechezwa kwa kutumia uchawi wa Mamba ambao hutumika sana nchini Malawi. Ilibidi taarifa zipelekwe kwa wazazi wa Bupe waliokuwa shamba. Mama Bupe alipatwa na mshtuko uliofanya apoteze fahamu baada ya kuzipata taarifa za mwanaye Bupe na kufanya watu waliopeleka taarifa wapate kazi ya kumbeba kumkimbiza hospitali.
Sasa endelea…


Taarifa za Bupe kuchukuliwa na mamba zilizagaa kijijini haraka kama moto kwenye majani makavu. Kwa vile upoteaji wake ulikuwa wa utata watu walimshauri mzee Andendekisye aende upande wa pili (Tiba asili). Alielekezwa Kijiji cha Kanjumjumere ambako kulikuwa na mganga aliyekuwa maarufu eneo lile aliyetambulika kwa jina la Mpalapala (aliyeshindikana).
Siku ya pili walifunga safari na wenyeji wa eneo lile, baada ya kufika walikwenda kwa mganga (Mpalapala) aliyekuwa na nyumba ya majani iliyozungukwa na zingine ndogo. Walipokelewa na kukutana naye. Baada ya kukutana na mganga Mpalapala kuangalia ramli yake alisema:
“Hili tukio siyo la kawaida, mamba aliyemchukua mtoto wenu si wa kawaida ila wa kichawi. Mpaka sasa mtoto wenu bado amefichwa pembeni ya mto. Wanasikilizia mpaka kesho kama hakutafanyika kitu chochote cha kumrudisha basi wataondoka naye.”
Kama kuna uwezekano wa tiba ifanyike usiku wa leo ili kumrudisha zaidi ya hapo tutamkosa kabisa au kuokota maiti yake pembezoni mwa mto. Kwa vile kazi ni nzito inatakiwa apatikane mbuzi mweupe asiye na doa ambaye tutamchinja na kumwaga damu yake kwenye maji ili kuweka mwanga wa kumpata alipofichwa.”
“Kama hatutapata mbuzi mweupe?” mtu aliyempeleka mzee Andendekisye kwa mganga aliuliza.
“Mbuzi yoyote anafaa lakini mweupe atasaidia kuondoa kiza. Mbuzi mweusi au mwekundu hafai kwani ataongeza giza ila mwenye rangi mbili nyeusi na weupe au wa kijivu wanaweza kusaidia lakini itabidi ifanyike kazi ya ziada.”
“Umesema usiku, je tunaweza kuondoka sasa hivi ili tuwahi muda?” mzee Andendekisye aliuliza.
“Hakuna tatizo cha muhimu ni huyo mbuzi mweupe.”
“Tutajitahidi apatikane.”
Waliondoka Kijiji cha Kanjumjumere na kurudi Kilasilo na kufika saa nne usiku, mara moja ulianza msako wa kutafuta mbuzi mweupe. Walikwenda kwa mzee Mwangibile aliyekuwa na mbuzi na kubahatika kupata mbuzi mweupe lakini mwenye baka jeusi mgongoni.
Mganga alisema atafaa, majira ya saa sita usiku waliongozana hadi mto Kiwira, ambako ndipo alipokamatwa Bupe na mamba. Walipofika eneo lile mbuzi alichinjwa na damu yake kumwagwa mtoni kisha alichovya usinga wake kwenye damu ya mbuzi iliyochanganywa na dawa na kuanza kurusha ndani ya maji huku mganga akiliita jina la Bupe kwa sauti kubwa.
“Bupeee….Bupeee….Bupeee.”
Aliendelea kufanya vile huku akitembea kwenye maji na kusogea sehemu aliyoamini ndipo alipofichwa. Aliendelea kumwita huku akiendelea kuzunguka ndani ya maji, ghafla wote walishtuka baada ya kutokea mamba ambaye alimkamata mganga na kuzama naye chini ya maji na kufanya waliongozana naye kutimua mbio.
Wasaidizi wa mganga walirudi eneo lile ambalo lilikuwa tulivu bila kuonesha kuna tukio lolote lililotokea. Walijiuliza alikokuwepo, waliita jina lake lakini hali ya ukimya ilitawala.
Hali ile ilizidi kumtisha mzee Andendekisye na kujiuliza kama mganga naye kachukuliwa itakuwaje.
Kwa vile ulikuwa usiku mkubwa walirudi nyumbani kulala kwa ajili ya kumtafuta siku iliyofuata. Wasaidizi wa mganga walipanga kuamka alfajiri kwenda kuangalia mtoni.
Mzee Andendekisye na mkewe walikosa usingizi kwa tatizo lile zito ambalo hawakujua hatima ya mtoto wao kwa vile mganga alisema usiku wa siku ile ukipita hawatampata tena na kama watampata hatakuwa hai.
“Mume wangu tumewakosea nini walimwengu, kibaya zaidi muoaji anatoka mbali,” mama Bupe alilalamika.
“Labda vijana wa hapa, si ulisema mtoto wa Mwandambo alikuwa akitaka kumuoa na kumkatalia huenda ndiye aliyefanya mchezo huo,” mzee Andendekisye alisema.
“Mmh! Yule mtoto mbona alishakwenda Mwanza kwa mjomba wake muda,” mama Bupe alimtetea.
“Sasa atakuwa amefanya nani?”
“Mtaalamu amepotea sijui itakuwaje?”
“Hebu ngoja alfajiri tukienda mtoni tutapata jibu labda ndiyo amekwenda kumsaka,” alijipa moyo.
Usiku wa siku ile mzee Andendekisye alikesha macho na saa kumi na nusu aliwaamsha wasaidizi wa mganga na kuelekea mtoni.
Waliongozana hadi mtoni walipofika walipigwa na butwaa baada ya kumkuta mganga akielea pembeni ya mto akiwa amekufa. Kilichowashtua kumkuta akiwa hana nguo huku baadhi ya sehemu zake za mwili zikiwa zimechukuliwa. Sehemu za siri, kucha, ulimi na kunyolewa pembeni ya kichwa.
Hali ilizidi kutisha, lilikuwa jambo la ajabu kutokea sehemu ile kwa mganga kuchukuliwa kichawi na kukatwa sehemu za mwili kisha kuonekana akielea pembeni ya mto. Kilichowashangaza zaidi, mwili wa mganga uliwahi kuonekana wakati wa mtoto wao Bupe haukuonekana wakati mamba aliyemchukua ni yuleyule.
Ilibidi mwili wa mganga uchukuliwe na kusafirishwa kwenda kijijini kwake Kanjumjumere kwa ajili ya maziko na kumuacha mzee Andendekisye asijue la kufanya juu ya kutoweka kwa binti yao kwani mganga aliwaambia kama ungepita usiku bila Bupe kupatika angepatikana akiwa maiti.
Aliamini kwa kauli ya mganga mtoto wao asingepatikana tena.
Lakini majirani walimpa moyo kuwa asikate tamaa, wengine walimshauri avuke boda kuingia Malawi ambako kulisifika kwa uchawi na waganga.
Wengi waliamini uchawi ule mtu aliufuata Malawi. Alielekezwa kijiji kinachosifika kwa uchawi na waganga cha Mwakawenge katika mji wa Chitipa. Mzee Andendekisye alipanga kwenda Malawi kufuatilia kupotea kwa mwanaye. ***
Atuganile aliamka siku ya pili akiwa mzima wa afya njema lakini ujauzito hakuwa nao, wazazi wake walimuweka chini ili kutaka kujua kipi kilimsibu na alikwenda wapi.
“Atu.”
“Abee baba.”
“Jana ulikula nini kwa kina Ambakisye?”
“Sikula kitu.”
“Usifiche kwa vile mchezo waliokufanyia ni mbaya sana, bila bi Tumwambilile tungekupoteza.”
“Kama ni wao wamepata faida gani?”
“Ndiyo maana tunataka kukupa dawa ili ukampake mpenzi wako kabla ya kukutana naye ili kuhakikisha unashika ujauzito haraka.”
“Mama haraka ya nini kushika ujauzito kama imetoka kwa bahati mbaya niacheni nipumzike japo moyo unaniuma kumpoteza mwanangu.”
“Kwa hiyo humpendi Amba?”
“Nampenda, lakini kuna kitu kimenishtua jana.”
“Kitu gani?”
“Siwezi kukisema mbele ya baba,” Atuganile alisema kwa aibu.
Ilibidi baba yake aondoke ili kumwacha azungumze na mama yake, baada ya kutoka mama yake alitaka kujua kilichomshtua mwanaye.
“Ehe, niambie mwanangu, kipi kimekushtua?”
Alimueleza hali iliyomtokea mpenzi wake jana yake walipokutana faragha.
“Mama hali ile haijawahi kutokea hata siku moja nina wasiwasi na dawa mliyoniambia nikampake.”
“Si dawa niliyokupa labda ana tatizo lingine,” mama yake alijitetea.
“Hapana mama dawa uliyonipa jana ndiyo iliyosababisha yote yale.”
“Sasa mimi nifanye hivyo ili iweje, shida yangu nataka kuhakikisha unaolewa naye.”
“Mmh! Sawa.”
“Sawa nini?”
“Nimekubali, lakini nitampakaje bila yeye kujua kwa ajili ya nini?”
“Inatakiwa umpake kwa siri asijue.”
“Hapo ndipo penye tatizo, angekuwa mzima ningeweza kafanya zoezi hilo bila tatizo.”
“Kuna dawa ya kunywa nitakupa ukampe kisha tuangalie ili ufanye zoezi lako.”
“Kama hivyo nitakuwa sawa.”


Usikose kufuatilia Kesho....
 
Uchawi wa wazazi wake na Amba ni wa kurithi, wakijua mrembo wa mwana wao amechukuliwa na mamba pamoja mganga mtifuano mkali utaibuka! Na hasa wakijua kijana wao hashegedui kwa sasa!
 
da itabidi nifanye mpango niende kwa bibi tumwambilile,maana kuna mtu ananisumbua sana...
 
HADITHI YA KUSISIMUWA VITA YA WACHAWI-12

ILIPOISHIA:

“Hapo ndipo penye tatizo, angekuwa mzima ningeweza kufanya zoezi hilo bila tatizo.”
“Kuna dawa ya kunywa nitakupa ukampe kisha tuangalie ili ufanye zoezi lako.”
“Kama hivyo nitakuwa sawa.”
SASA ENDELEA…


Atuganile alimkubalia mama yake huku akipanga kwenda kwa bibi Tumwambilile kumweleza hali ya mpenzi wake pia tatizo la kupoteza ujauzito limetokana na nini.
Mama yake alimpa dawa ya kunywa kwa siku tatu kwenye maji ya vuguvugu. Baada ya kuchukua dawa aliiweka ndani na kupanga kumpelekea akitoka kwa bibi.
Aliachana na wazazi wake na kwenda kufanya shughuli za usafi kisha aliondoka bila kuaga. Alikwenda mpaka kwa bibi Tumwambilile, alizunguka na kutokea nyuma ya nyumba uani. Lakini alishangaa kukuta pako kimya, ilibidi aite kwa sauti.
“Bibiiii….Bibiiii.”
Lakini hakukuwa na jibu, aliamua kuingia ndani huku akimwita kwa sauti.
“Bibiii….Bibiiiii Tumwaa.”
“A..a..be,” ilisikika sauti ya chini ikitokea chumbani.
Atuganile alishtuka na kwenda chumbani kwa bibi Tumwambilile, alikuta amelala kitandani.
“Vipi bibi unaumwa?” Atuganile alishtuka.
“Kiasi, afadhali umekuja maana leo asingekuja mtu kwangu ningekufa.”
“Kwa nini bibi?”
“Kwanza kafunue kwenye mtungi wangu sebuleni kuna kifurushi cheusi, fungua toa dawa kidogo nichanganyie na maji uninyweshe,” Bibi Tumwambilile alisema akiwa bado amelala kitandani.
Atuganile alifanya kama alivyoelekezwa na bibi Tumwambilile, alikwenda kwenye mtungi mkubwa uliokuwa nyuma ya mlango wa kuingilia na kufunua ungo uliokuwa juu yake. Alipotaka kuingiza mkono alishtuka kuona kuna joka kubwa limo mule, alishtuka na kupiga kelele.
“Mamaaa! Nakufa!” Atuganile alipiga kelele za woga zilizomfanya bibi Tumwambilile kuuliza kwa sauti ya shida.
“Nini mjukuu wangu?”
“Bibi joka!”
“Hebu njoo.”
Atuganile alikwenda chumbani kwa bibi akitweta kwa hofu huku akitetemeka.
“Unasema umeona nini?”
“Joka kubwa bibi”
“Pole mjukuu wangu.”
“A..a..sante.”
“Mbona hakuna kitu kwenye chungu ni wasiwasi wako, hebu rudi ukaangalie hakuna joka.”
“Hapana bibi siendi kuna joka litaning’ata.”
“Yule ni mlinzi, nilisahau kukujulisha ila sasa hayupo kanichukulie dawa nitakufa mjukuu wangu.”
“Mmh! Sawa bibi kwa vile wewe ni mtu wangu muhimu, la sivyo nisingekwenda.”
“Sawa mjukuu wangu.”
Atuganile alirudi kwenye mtungi mkubwa ambao wakati huo ulikuwa wazi, alisogelea kwa tahadhari kubwa. Alichungulia kabla ya kuingiza mkono ili kuona kama kweli hakuna lile joka kubwa. Lakini ajabu hakukuwa na joka zaidi ya tunguli.
Aliingiza mkono na kutoa kifurushi cheusi na kukifungua na kukuta dawa ya rangi ya njano. Alichukua bakuli na kuweka ile dawa kwenye maji na kumpelekea bibi Tumwambilile.
Kabla ya kumpa alimkalisha kitandani na kumsaidia kumnyesha kwani hata nguvu za kushika bakuli hakuwa nazo. Alimnywesha yote kisha alimrudisha kitandani ili asubiri atamwambia nini.
“Bibi nifanye kitu gani tena?”
“Zunguka nyuma ya nyumba kuna mti mmoja mfupi una majani mapana, chuma matatu kisha yaweke kwenye maji ya kuoga kisha njoo unisaidie kunitoa nje ili nikaoge.”
Atuganile alifanya kama alivyoelekezwa, akaenda nyuma ya nyumba na kuchuma majani matatu na kuyaweka katika beseni la maji na kupeleka bafuni ambako alimuwekea na kigoda cha kukalia.
Alimfuata ndani na kumsaidia kumshika mkono mpaka nje na kumpeleka bafuni, alimkalisha kwenye kigoda na kuanza kumuosha huku akimsugua yale majani kila kona ya mwili.
Baada ya zoezi lile, bibi Tumwambilile alimuomba Atuganile atoke nje, alitoka na kwenda kukaa kwenye gogo lililokuwa uani.
Alijikuta akijiuliza kuhusu lile joka ambalo bibi alisema ni mlinzi. Alijiuliza bila ruhusa yake lingemfanya nini.
“Atu,” sauti ya bibi ilimshtua.
“A..a..bee bibi,” Atu aliitikia huku akishangaa kumuona bibi Tumwambilile akitokea ndani akiwa amejifunga kaniki wakati alimuacha bafuni na hakumuona kupita kwenda ndani.
Alitaka kumuuliza lakini aliachana nayo na kufuata yake.
“Njoo ndani.”
Atu alinyanyuka na kuingia ndani, waliingia chumbani na kumwambia akae kwenye kitanda, naye alikaa pembeni yake.
“Atu mjukuu wangu nashukuru kwa kuja kunisaidia bila hivyo ningekufa.”
“Pole bibi ugonjwa umekuanza saa ngapi wakati uliondoka salama?”
“Jana nilikuwa na vita nzito, bila ujuzi wa ziada nilikuwa nakufa, kwanza nilitaka kukujulisha ile kazi yako jana ilikamilika.”
“Usiniambie!” Atuganile alishtuka kwa furaha.
“Sasa hivi Kilasilo ni vilio, yule msichana kapotea katika mazingira tata na akionekana atakuwa marehemu.”
“Duh! Bibi asante,” Atuganile alimshukuru bibi Tumwambilile kwa kuondoa kizingiti cha ndoa yake na Ambakisye.
“Ila jana kuna mganga alitaka kumtoa kabla hajatoka uhai, hali ilianza kuwa mbaya kwa kunivuta na nguvu zake. Lakini washirika walinisaidia na kuweza kunivuta kisha tulimuangamiza.”
“Kivipi?”
“Tulituma mamba aliyemkamata na kumzamisha, alipotoka alikuwa marehemu.”
“Mmh! Kwa hiyo vita ni kali?”
“Tena kubwa, lakini wala isikuogopeshe nimeisha izoea nilijisahau kidogo ndiyo maana aliniwahi. Mpaka narudi hali ilikuwa mbaya, ugumu wangu ndiyo ulionifikisha asubuhi bila hivyo nilikuwa nakufa najiona.”
“Pole bibi, sasa utafanyeje wakija tena?”
“Kuanzia sasa hivi najipanga, sikai kizembe tena.”
“Sasa bibi kuna kitu kimenileta.”
“Kitu gani?”
“Nina imani unajua kilichonipata jana?”
“Ndiyo.”
“Eti nani aliyefanya vile?”
“Kwa vile umepona achana nayo.”
“Bibi niambie eti wazazi wa Ambakisye wanahusika?”
“Mjukuu wangu ukifukua jalala lazima utakutana na uvundo, nisikilize mimi achana nayo.”
“Kingine bibi majuzi nilipewa dawa na mama nikampake mpenzi wangu...
Itaendelea wiki ijayo.
ili asiniache, lakini ajabu jana nilipokutana naye hakuwa na nguvu za kiume kilichonitisha zaidi sehemu zake za siri zilizidi kusinyaa. Nimemwambia mama labda sababu ni ile dawa lakini alikataa ila amesema atanipa dawa ya kunywa nimpelekee mpenzi wangu anywe kwa siku tatu kisha atanipa dawa nikampake.
“Bibi hebu nieleze tatizo la mpenzi wangu linatokana na nini?”
Bibi Tumwambilile alitulia kwa muda kisha alichukua ugoro na kunusa kisha alipiga chafya na kusema:
“Mjukuu siku zote chanzo cha moto mkubwa cheche.”
“Una maanisha nini?”
“Dawa ya kunywa mpelekee mpenzi wako, ila ya kumpaka usimpake.”
“Ina nini?”
“La muhimu kufuata niliyokueleza mengine achana nayo, dawa yoyote utakayopewa na mama yako juu ya Ambakisye usiitumie bila kuniambia.”
“Sawa bibi.”
“Hebu nenda kwa mzee Mwangibile kaniletee chimpumu nizimue kwani nilikuwanakufa.”
Atuganile alipitia kikopo cha lita moja na kuelekea kwenye kilabu cha Mwangibile kununua chimpumu.


Itaendelea Jumatano jioni
 
HADITHI YA KUSISIMUWA VITA YA WACHAWI-12
"Hebu nenda kwa mzee Mwangibile kaniletee chimpumu nizimue kwani nilikuwanakufa."
Hahahahaaaaa, hadithi yako mkuu tamu kweli na inasisimua kweli! Nimesisimka sana na nilipofika kwenye mstari huu nikatabasamu baada ya bibi kunusurika kifo yeye anaomba kimpumu tu! Hii inaonyesha ni kwa sababu gani wachawi wana uwezo mkubwa kabisa lakini ni maskini wa kutupwa!
 
Hii vita ni kali.

Hadi mganga naye anakufa????????


MIZAMBWA
INANIUMA SANA!!!
 
We mzizimkavu leta no yako nikutumie credit naona unatuchekewesha video yetu.
 
HADITHI YA KUSISIMUWA VITA YA WACHAWI-13

ILIPOISHIA:
"Bibi hebu nieleze tatizo la mpenzi wangu linatokana na nini?"
Bibi Tumwambilile alitulia kwa muda kisha alichukua ugoro na kunusa kisha alipiga chafya na kusema:
"Mjukuu wangu siku zote chanzo cha moto mkubwa ni cheche."
"Una maanisha nini?"
"Dawa ya kunywa mpelekee mpenzi wako, ila ya kumpaka usimpake."
"Ina nini?"
SASA ENDELEA


"La muhimu kufuata niliyokueleza, mengine achana nayo, dawa yoyote utakayopewa na mama yako juu ya Ambakisye usiitumie bila kuniambia."
"Sawa bibi."
"Hebu nenda kwa mzee Mwangibile kaniletee chimpumu nizimue kwani nilikuwa nakufa."
Atuganile alipitia kikopo cha lita moja na kuelekea kwenye klabu cha Mwangibile kununua chimpumu. Baada ya kununua, alimpelekea kisha aliondoka kurudi nyumbani ili baadaye aende kwa mpenzi wake kumpelekea dawa.
Siku ya pili, Ambakisye aliamka asubuhi kama kawaida na kujiangalia kutokana na mabadiko wakati akitaka kufanya mapenzi na mpenzi wake usiku. Aligundua mabadiliko sehemu zake za siri kutokana na maiki kuwa dolo kitu ambacho si cha kawaida kwani lazima aamke na kujikuta amesisimkwa sehemu zake.
Hali ile ilimshtua sana na kumfanya ajiulize inatokana na nini, hali ile ilimtisha na kutaka kwenda kumueleza baba yake. Lakini alitaka kwanza aiache siku ile ipite ili ajiangalizie jioni akikutana tena na mpenzi wake. Akiwa bado hajapata jibu alisikia hodi. Ilikuwa sauti ya mpenzi wake Atuganile, alimkaribisha:
"Karibu pita ndani."
Baada ya kuingia ndani alimsalimia mpenzi wake.
"Vipi mpenzi unaendeleaje?"
"Mpaka sasa sijielewi maana nimeamka asubuhi mtalimbo umekuwa dolo."
"Inaweza kuwa tatizo kubwa?"
"Ndiyo wasiwasi wangu mkubwa."
"Hebu nione."
Ambakisye alimuonesha rafiki yake sehemu zake nyeti ambazo zilionesha kunywea.
"Mmh! Sasa tatizo nini?"
"Hata najua! Sasa nijaribu tena ili nione." Walikubaliana kujaribu asubuhi ile hali ilikuwa ileile mtalimbo uliendelea kulala dolo.
"Amba una nini mpenzi wangu?"
"Najua yaani sijui nani kanifanya hii, lazima utakuwa mkono wa mtu."
"Ambakisye au yule mwanamke ana mpenzi wake ndiye aliyekufanya."
"Sasa anifanye hivi kwa kosa gani? Si angewafanyia waliomnyang'anya mke!"
"Amba kuna dawa nimekuletea ili ujaribu kutumia."
"Dawa ya nini?"
"Ya kurudisha nguvu za kiume."
"Umetoa wapi."
"Kwa..kwa…"
Alihofia kusema kapewa na mama yake kuhofia kukataliwa, ilibidi aseme uongo.
"Ni..nimepewa na bibi Tumwambilile."
"Halafu umejuana naye vipi yule bibi nasikia wanasema kigagula (mchawi)?"
"Mimi nitajuaje ikiwa hajaniroga."
"Nasikia wanasema anatisha."
"Kama angekuwa mchawi jana angenisaidia."
"Kakusaidia nini?"
"Basi jana nilipotoka hapa usiku tumbo liliniuma, maumivu niliyosikia nilimuona mtoa roho kanisimamia mbele yangu. Nilijitahidi kwenda kwa wazazi ilishindikana na nilitokwa na damu nyingi kisha nilianguka na kupoteza fahamu."
"Mungu wangu unasema umetoa damu nyingi?"
"Ndiyo mpenzi wangu."
"Mmh! Mwanangu ana usalama?"
"Autoe wapi, bibi Tumwambilile alifuatwa na kuja kunusuru roho yangu."
"Kwa hili familia yako inahusika."
"Ihusike nini?"
"Kutoka kwa ujauzito wa mwanangu."
"Utaionea lakini hata wao wamesikitika sana."
Wakiwa katikati ya mazungumzo walisikia sauti ya juu ikimwita Ambakisye.
"Ambakisye."
"Naam mama."
"Njoo mara moja."
Alitoka nje na kwenda kwa wazazi wake, alipofika alishtuka kuwaona katika sura za huzuni. Pia walikuwepo wageni ambao aliwafahamu ni ndugu wa mchumba wake Bupe.
"Naam mama, ooh! Wageni karibuni, za Kilasilo?"
"Nzu..nzuri," walijibu kwa kigugumizi.
"Mke wangu Bupe hajambo?"
Swali lile lilikuwa kama kaa la moto mdomoni, walishindwa kulijibu moja kwa moja na kubaki wakitazamana. Hali ile ilifanya baba yake aingilie kati na kusema:
"Hebu kaa kwanza tuzugumze kilichotokea."
"Sawa," alijibu na kusima ili asikie alichoitiwa.
Baada ya ukimya mfupi kila mmoja akiwa ameinamisha kichwa chini, mzee Andendekisye alisema kwa sauti ya upole:
"Kuna taarifa tata zimefika toka kwa mchumba wako kuwa ametoweka katika mazingira ya kutatanisha."
"Mkisema mazingira ya kutatanisha mnamaanisha nini?"
Alielezewa yaliyotokea Kilasilo yaliyomhusu mpenzi wake kuchukuliwa kichawi na mamba ambaye alimchagua yeye peke yake katika kundi la watu."
"Mungu wangu, ina maana ule mto una mamba?"
"Hauna, juzi ilikuwa ajabu ya mwaka, kibaya kingine mganga aliyesema atamrudisha alishikwa na mamba na kuzamishwa ndani ya maji na kuokotwa siku iliyofuata akiwa amekufa na kunyofolewa baadhi ya sehemu za mwili.""Mmh! Kazi ipo, nani aliyefanya hivyo?"


Itaendelea kesho jioni......
 
HADITHI YA KUSISIMUWA VITA YA WACHAWI-14

ILIPOISHIA:
Alielezewa yaliyotokea Kilasilo ya mpenzi wake kuchukuliwa kichawi na mamba ambaye alimchagua yeye peke yake katika kundi la watu.”
“Mungu wangu, inamaana ule mto una mamba?”“Hauna juzi ilikuwa ajabu ya mwaka, kibaya kingine mganga aliyesema atamrudisha alishikwa na mamba na kuzamishwa ndani ya maji na kuokotwa siku iliyofuata akiwa amekufa na kunyofolewa baadhi ya sehemu za mwili.”
“Mmh! Kazi ipo, nani aliyefanya hivyo?”
SASA ENDELEA…


“Hajajua, ila nitaingia kazini kuangalia nani kafanya vile, nikimjua nitakachomfanya Mungu anajua,” alijiapiza mzee Amanyisye.
“Kwa hiyo nini kinaendelea?”
“Baba amesafiri leo kwenda Malawi kutafuta tiba kwa vile wanasema uchawi ule unatumika sana huko,” alisema mmoja wa vijana waliokuja kuleta taarifa za kupotea kwa Bupe mchumba wa Ambakisye.
“Nami nitamtafuta aliyefanya vile nikimjua nitamaliza familia nzima,” alizidi kujiapiza mzee Amanyisye.
“Sawa nimesikia,” alisema Ambakisye kwa unyonge huku moyoni akifurahi kupotea kwa yule msichana lakini hakupenda afe.
“Kuna kauli iliyotukatisha tamaa, mganga aliyekufa maji alisema kuwa siku ya jana ikipita hatutampata tena na tukimpata atakuwa ameishakufa,” alisema kaka yake huku akitokwa machozi ya uchungu.
“Wee waache si wameanza sisi tutamaliza,” mzee Amanyisye aliendelea kujitapa kwa hasira.
Baada ya vijana walioleta taarifa za kupotea Bupe kuondoka, wazazi wa Ambakisye walikaa kikao cha faragha kulijadili lililotokea.
“Mke wangu mi nina wasiwasi na familia ya Andendekisye!”
“Hata mimi nilikuwa na wazo hilo, inawezekana kabisa kitendo cha Amba kumpatia ujauzito mtoto wao ndicho kilichosababisha wafanye hivyo,” mkewe aliunga mkono wazo la mumewe.
“Na ile dawa tuliyompa aitege aliitega kweli?”
“Hata mimi nashangaa leo siku ya ngapi hatujapata majibu.”
“Hebu mwite.”
Mama Ambakisye alimwita mwanaye kwa sauti ya juu.
“Ambaaa!”
“Naam mama.”
“Hebu njoo.”
Ambakisye aliyekuwa akimpa taarifa Atuganile aliyejifanya kushituka alimuacha na kwenda kumsikiliza mama yake.
“Mpenzi nakuja.”
“Dah! Pole sana nenda ukawasikilize.”
Atuganile alikuwa na hamu ya kujua familia ya mpenzi wake itapokea vipi kupotea kwa mchumba wa mtoto wao katika mazingira ya kutatanisha. Ambakisye alikwenda hadi kwa wazazi wake, alipofika alisimama mbele yao.
“Naam.”
“Eti ile dawa ulimtegea Atu?”
“Ndiyo jana, halafu kitu cha ajabu alipotoka na kuruka ile dawa alipiga kelele na kuinama chini akishika mikono chini ya kitovu. Usiku alipolala kwao ile hali ilijirudia tena safari ile ilisababisha atokwe damu nyingi na kusababisha kupoteza ujauzito wake,” Ambakisye alisema kwa masikitiko.
“Mmh!” waliguna wote.
“Sasa mbona haikusaidia kitu?”
“Tulikuambia wale si watu wema lazima wameutoa kwa hasira kabla ya kuitega ile dawa,” walitengeneza uongo.
“Ila hata mimi sikubali aliyemuua mwanangu naye nitamsafiria Malawi, haiwezekani waniulie mwanangu asiye na hatia.”
“Ambakisye usirogwe kushiriki uchawi, wewe bado kijana mdogo kazi hiyo tuachie sisi wazazi ndiyo tunaweza kukabiliana nao,” mzee Amanyisye aliwahi kumzima mwanaye kwa kujua bomu limetegewa ndani mwao.
“Mmh! Sawa lakini ungeniacha tu.”
“Vita ya kichawi inataka uzoefu, ukienda kichwakichwa utapotea. Sasa hivi uchawi wa bure. Kwa vile nimeahidi kupambana nao basi niachie mimi kazi hiyo.”
“Sawa baba.”
“Basi kaendelee na kazi yako.”
Ambakisye aliondoka na kuwaacha wazazi wake wakiendelea kuteta, alirudi hadi chumbani kwake na kupokewa na Atuganile aliyekuwa na hamu ya kujua mpenzi wake aliitiwa nini kwani hata uso wake ulijaa simanzi.
“Amba kuna nini, mbona hivyo?”
“Mchumba niliyetaka kumuoa kachukuliwa na mamba katika mazingira ya kutatanisha,” alimweleza mengine japo mwanzo hakumwambia.
“Mungu wangu pole sana,” Atuganile alijifanya kushtuka.
“Si bure lazima kuna mkono wa mtu.”
“Lakini mpenzi usisikitike sana mimi mpenzi wako wa damu si nipo?”
“Sawa, lakini huoni kama wanaweza kutufikiria vibaya labda tumepanga kumpoteza ili tuendelee kuwa pamoja. Japo tuko pamoja lazima kipindi hicho uhusiano wetu usiwe wa wazi sana kuonana kwetu iwe usiku tu.”
“Sawa, lakini sikubali utafutiwe mwanamke mwingine kama amepotea au amekufa nasubiri ndoa yangu.”
“Hakuna tatizo, kama hivyo sitakubali kuchaguliwa tena mwanamke,” Ambakisye alimuhakikishia mpenzi wake.
“Nimefurahi kusikia hivyo, basi naomba utumie hii dawa ili tujue tatizo nini.”
“Mmh! Sawa, lakini lazima nizungumze na baba ili nijue ataniambiaje.”
“Amba kwa nini usitumie tu ili tujue kitakuwa nini kuliko kuwapa presha wazazi wako?”
“Hapana lazima nimwambie baba kwa vile ni mtu wangu wa karibu ili nijue atanisaidia vipi kabla ya kutumia dawa.”
“Bibi Tumwambilile tatizo lako aliliona na kusema ukitumia dawa hii ndani ya siku tatu kila kitu kitaenda vizuri.”
“Sawa, lakini hili ni jambo zito kwa vile toka nizaliwe halijawahi kunitokea, jana nilijua ni uchovu wa safari lakini leo imenijulisha kuwa hili ni tatizo.”
“Kwa hiyo dawa hii niirudishe?”
“Hapana, niachie ila lazima nimwambie kwanza baba nisije sema hali imekuwa mbaya.”
“Mmh! Sawa.”
“Atu kuna kitu gani kati yetu?”
“Kipi?”
“Kwa nini matatizo yametutokea kwa siku moja, huoni hapo kuna mchezo fulani tuliochezewa?”
“Mmh! Kweli kabisa mpenzi wangu siku uliposhindwa kufanya kazi usiku wake ndipo niliharibu ujauzito wangu.”
“Unafikiri ni kwa amri ya Mungu?”
“Hapana lazima kuna mkono wa mtu.”
“Hujamuuliza bibi Tumwambilile tatizo lako linatokana na nini?”
“Aliniambia nikifukua sana uchafu nitakutana na uvundo na chanzo cha moto mkubwa ni cheche.”
“Alimaanisha nini?”
“Nilimuuliza, aliniambia kwa vile nimepona haina haja ya kuchimba sana.”
“Na mimi?”
“Kaniambia utumie dawa hii utapona kabisa.”
“Sasa fanya hivi nitakupitia kwenu ili twende tukamchimbe bibi Tumwambilile, nina senti kidogo najua atakubali kutueleza.”
“Sawa, basi mi nitakusubiri, muda mzuri jioni nitakuwa nimemaliza kazi.”

Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia Kesho....
 
Back
Top Bottom