HADITHI YA KUSISIMUWA VITA YA WACHAWI-23
ILIPOISHIA:
Mzee Andendekisye aliondoka Matipa alifajiri na kufika mpakani saa moja asubuhi alivuka na kwenda kuchukua baiskeli yake alipoicha na kurudi kijijini kwake kuendelea na maandalizi ya mazishi ya mwanaye kipenzi. Wakati akirudi jirani yake Amangise alikuwa safarini kuelekea kwa jamaa yake ambaye alisoma na kuingia kwenye utaalamu wa miti shamba.
Walitoka vizuri na mwanaye kwa kupakiana kwenye baiskeli na kuelekea boda ili wavuke kwenda Karonga ili wakamzime mzee Andendekisye. Kama kawaida Ambakisye ndiye alikuwa akimuendesha baba yake.
SASA ENDELEA...
Baada ya mwendo wa saa mbili Ambakisye alisimamisha baiskeli na kufanya baba yake kumuuliza.
Vipi umechoka nikusaidie.
Hapana baba kichwa kimenishika ghafla.
Mmh! Mbona unanitisha,
Mara Ambakisye alishika kichwa na kuanza kupiga kelele za maumivu.
Baba kichwa, nakufa mimi kichwa kinapasuka kinapasuka
.Mungu wangu nakufa..baba nakufa kichwa kinapasuka, Ambakisye alisema huku ameshikilia kichwa kama kinataka kutoka.
Ni nini mwanangu? baba yake alishtuka.Baba nina wasiwasi na familia ya kina Atuganile wamelipa kisasi, kama ni wao naamini siponi, Ambakisye alisema kwa shida.
Hapana utapona tu mwanangu, mbona mimi sijafanya lolote kwa kifo cha mpenzi wako kisasi hicho kitokane na nini? Wacha niendeshe mimi nikuwahishe kwa mganga,
Baba
niagie kwa mama nakufa bila kumuaga, Ambakisye alisema kwa sauti ya kukata tamaa.
Huwezi kufa mwanangu, mzee Amangise alisema huku akimshika mwanaye aliyetaka kuanguka na kumdaka na na kumkalisha kwenye miguu yake.
Ba..ba..ba.. Ambakisye alimwita baba yake kwa shida kwa sauti ya chini.
Na..na..am mwanangu, baba yake aliitikia huku hofu kubwa ikiwa imemtawala.
U..u..naona ubishi wako?
Mbona mwanangu nilikubaliana na wewe.
Alichelewa tayari cheche imeisha unguza msitu na moto hakuna wa kuuzima.
La..la..kini..
Ba..ba, suluhu ya hili ka..ka..ma ..Mu..mungu watanichukua usilipe kisasi, ukilipa patabakia ma..ma..ma..go..fu..
Ambakisye hakumalizia, ghafla alibadilika na damu zilianza kumtoa mdomoni, puani, masikioni na machoni huku macho yakiongezeka ukubwa. Taratibu alifumba macho na kutulia.
Amba..Ambakisye
Ambaaaa, alimtikisa kwa nguvu lakini hakukuwa na jibu lolote. Alimshika mapigo ya moyo yalikuwa yametulia, mzee mzima aliangua kilio kumlilia mwanaye ambaye alijua amechelewa kumpeleka kwenye kinga .
Wapita njia walishtuka kumkuta mtu wanayemfahamu kampakatia mtu huku akilia.
Vipi mzee Amangise?
Jamani mwanangu, alijibu kwa sauti ya kilio.
Ha! Ni Ambakisye! Amefanya nini? walishtuka kumuona ni mtu wanayemjua katika hali ile.
Jamani mwanangu ameniacha ghafla.
Mungu wangu, alikuwa akiumwa?
Wala, tulikuwa na safari ya kuelekea Kilasilo lakini ghafla kichwa kimemuuma hata dakika kumi hazikuchukua amefariki dunia.
Mzee Amangise aliangua kilio kama mzazi wa kike akimlilia mwanaye, walimsaidia kuurudisha mwili wa Ambakisye kijijini. Watu wote njiani walishtuka kuwaona walivyobebwa Ambakisye kwenye baiskeli huku baba yake akilia kilio cha chini chini.
Jamani kuna nini?
Nimemkuta mzee Amangise akilia huku amemkumbatia mwanaye kwa kweli mpaka sasa hatujajua nini kimemsibu.
Eti mzee wangu kuna nini?
Wa..wa
, alishindwa kuzungumza kwani doge la uchungu lilimkaba kooni.
Walimsaidia kuufikisha mwili wa Ambakisye ambaye hakuwa na uhai wakati huo, ujaji ule ulimshtua mama Ambakisye aliyekuwa akifanya usafi uani. Alitulia akiwa amepigwa na butwaa na kujikuta vitu alivyoshikilia mkononi vikimdondoka na kuanguka chini.
Aliyekuwa ameshikiliwa kwenye baiskeli alikuwa mwanaye Ambakisye, walipofika waliuteremsha mwili wa mwanaye na kuingiza ndani.
Kafanya nini? mama Ambakisye aliuliza huku akisogea alipokuwa mumewe ameinama huku akilia kilio cha sauti ya chini.
Vipi mume wangu Amba kafanya nini? alimuuliza kwa sauti ya juu.
Wametuwahi.
Wametuwahi nini mume wangu?
Inaonekana walitangulia kabla hatajafika.
Una maanisha Amba anaumwa?
Ha..ha..p..
Hapana nini mume wangu, kwani kafanya nini? mama Ambakisye alimuuliza mumewe akiwa amemkwida shati na kumtikisa kwa nguvu.
A..a..me..ku..ku..u.
Kauli ile ilimfanya mama Ambakisye amuachie mumewe taratibu na kuteremka chini na kujitupa kama mzigo akiwa amepoteza fahamu baada ya kupata mshtuko kutokana na taarifa ile. Wakati huo wajirani walikuwa wamefika kutokana na kelele za mama Ambakisye kabla ya kupoteza fahamu.
Jamani kuna nini?
Ambakisye amefariki ghafla, alijibu mmoja wa watu walioleta mwili wa Ambakisye.
Wewee! msichana mmoja alishtuka na kuweka mikono kichwani.
Kweli Ambakisye hatunaye.
Mungu wangu mambo gani haya, mpenzi wake si amefariki juzi tu, mwanamke mmoja alisema huku ameshika mdomo.
Kina mama walimpa huduma ya kwanza mwanamke mwenzao huku wazee wa eneo lile wakimchukua mzee Amangise na kukaa naye pembeni kutaka kujua tatizo, pia wafanye nini baada ya kutokea kitu kama kile kwa ghafla.
Vipi mzee mwenzetu kulikoni?
Aliwaelezea hali iliyomtokea Ambakisye ghafla, aliongeza uongo walikuwa wakienda kuhani kwa mchumba wa mwanaye aliyefariki katika mazingira ya kutatanisha.
Sasa hii itakuwa nini, juzi mtoto wa Andendekisye, Atuganile na bibi Tumwambilile wamefariki katika mazingira hayahaya .
Itaendelea Kesho....