HADITHI YA KUSISIMUWA VITA YA WACHAWI-9
ILIPOISHIA:
Atuganile hakukata tamaa, aliendelea kumuandaa mpenzi wake mpaka jasho likamtoka japokuwa kulikuwa na hali ya baridi. Lakini
ilikuwa hali ileile sehemu kuendelea kusinyaa badala ya kunyanyuka kitu kilichowashtua wote.
Amba umekuwaje leo mpenzi?
Yaani leo nashangaa toka nizaliwe sijawahi kutokewa na hali hii.
Sasa hii ni nini?
Labda uchovu wa Safari, Ambakisye alijitetea.
Si kweli mbona uliniambia kuna siku ulikwenda na baba yako Isaki na wewe ndiye uliendesha kwenda na kurudi lakini jioni
tulipokutana ulikuwa kwenye hali ya kawaida.
SASA ENDELEA
Sasa hii sijui nini? Ambakisye alishangaa.
Kwanza mbona sehemu zako zimezidi kusinyaa.
Mmh! Hili litakuwa tatizo, Ambakisye aliingiwa wasiwasi.
Sasa tutafanyaje?
Acha nikusindikize kwenu ili niangalie hali hii mpaka kesho.
Mmh! Sawa, Atuganile alikubali kwa shingo upande.
Walikubaliana kusindikizana baada ya kila mmoja kuvaa nguo zake, walikwenda hadi nyumbani kwa Atuganile na kuagana kwa shingo
upande. Ambakisye alirudi nyumbani na kuingia chumbani kwake, hakuamini hali iliyomtokea, alisogeza taa kujiangalia.
Maumbile yake yalikuwa madogo tofauti na umbile lake halisi la kuzaliwa.
Hakutaka kuwa na haraka, alilala ili kesho ajitazame hali yake, kama itaendelea kuwa vile basi angemueleza baba yake. Upande
wa pili, Atuganile alishtushwa sana na hali ya mpenzi wake Ambakisye, akawa na wasiwasi na dawa aliyopewa na wazazi wake
ampake sehemu za siri huenda ndiyo iliyokuwa imemfanya awe vile.
Alipanga asubuhi kumuuliza mama yake hali iliyomtokea mpenzi wake, ili amsaidie kwani aliogopa kama ile hali itaendelea
lazima mapenzi yao yataingia dosari. Baada ya kuwaza sana alipitiwa na usingizi. Usiku wa manane tumbo lilianza kumsokota na
kufanya asikie maumivu makali.
Baada ya kuvumilia labda ile hali itapoa lakini kila dakika maumivu yalizidi, ilibidi anyanyuke ili akafie kwa wazazi wake.
Aliponyanyuka damu nzito nyeusi zilianza kutoka sehemu za siri. Alitembea kwa kupepesuka huku akijitahidi kuwaita wazazi wake
kwa sauti ya juu.
Mamaaa nakufa
.Nakufa mie jamani.
Sauti ile iliwaamsha wazazi wake ambao walitoka mbio nje walishtuka kumuona Atuganile ameanguka karibu na mlango wao.
Mungu wangu mwanangu, mama Atuganile alisema kwa sauti huku akimkimbilia mwanaye aliyekuwa amekata kauli wakati huo.
Walimnyanyua na kumuingiza ndani na kumlaza kwenye mkeka, walishangaa kuona amejaa damu nyeusi miguuni. Wakati huo Atuganile
alikuwa amepoteza fahamu kitu kilichoongeza taharuki kwa wazazi wake.
Mmh! Hii nini? Mzee Andendekisye alichanganyikiwa.
Mume wangu tuwe makini la sivyo tutampoteza mtoto hivihivi .
Walianza kazi ya kuhakikisha wanaokoa uhai wa Atuganile aliyekuwa bado amepoteza fahamu huku akionesha amepoteza damu nyingi.
Walijitahidi kumrudisha katika hali yake ya kawaida, ilionekana kama inashindikana kwani hakukuwa na dalili zozote za
Atuganile kuamka.
Mume wangu hii hali inatisha.
Tufanyeje? mzee Andendekisye alichanganyikiwa kwa hali ya mwanaye.
Hebu kimbia haraka kwa bibi Tumwambilile, ilibidi atafute msaada baada ya wao kuchemsha.
Mzee Andendekisye alitoka mbio kwenda kwa bibi Tumwambilile japokuwa usiku ulikuwa mzito uliokuwa na kiza cha kutisha kutokana na kutokuwa na mwezi angani. Alipofika aligonga mlango wa bibi Tumwambilile.
Nani tena usiku huu? bibi aliuliza.
Mimi Andendekisye.
Baba Atu?
Ndiyo bibi.
Vipi mbona usiku?
Mjukuu wako anakufa huko.
Kafanya nini?
Tumesikia usiku huu akituita akisema anakufa alipotoka tulimkuta ameanguka chini huku akitoka damu nzito nyeusi katikati ya miguu akiwa tayari kapoteza fahamu.
Mmh! Isiwe ametoa mimba? bibi aliuliza.
Hatujui kwa vile toka tulipomkuta ameanguka haongei na pumzi zake zipo mbali.
Mmh! Hebu subiri.
Bibi Tumwambilile alirudi ndani na kutoka baada muda na kusema:
Mmh! Wajanja wamewawahi.
Una maana gani? Ina maana Atu ndiyo amekufa? mzee Andendekisye alishtuka.
Sina maana hiyo kuna kitu mtoto wenu alitegewa na kuruka ndicho kilichosababisha tatizo lile.
Tatizo gani?
Ujauzito umetoka?
Kautoa nani?
Kwanza twende tukamhudumie mtoto.
Waliongozana usiku ule kuelekea nyumbani, uani kwake bibi Tumwambilile alichuma majani mabichi na kwenda nayo. Walipofika walimkuta mama Atuganile bado amemuinamia mwanaye huku akilia.
Bibi Tumwambilile alipofika pale alimkemea kwa kitendo cha kumlilia mwanaye aliye hai.
Unalia nini wakati wewe ndiye bingwa wa kuwalipua watu, leo umewahiwa badala ya kupambana unalia, kweli vita ikitokea utaiweza? bibi Tumwambilile alimuuliza akiwa amemkazia macho.
Hapana Tumwambilile, sijui mwanangu amepatwa na nini, kila tulivyojitahidi kumrudisha katika hali yake ya kawaida ilishindikana, mama alisema kwa sauti ya kilio.
Siku zote nilikueleza ukijua kupiga ujue na kupigwa, hivyo ujue kukwepa na kujikinga. Umewahiwa unatakiwa kujua utafanyaje kumuokoa mtoto na si kulia.
Mpaka nalia uwezo wangu umefikia mwisho.
Basi tuache maneno tumsaidie mtoto, lete maji kwenye beseni.
Walifanya vile mara moja na kumletea maji kwenye beseni , bibi Tumwambilile alimuomba mzee Andendekisye aondoke kwa vile ilitakiwa kufanyika kazi ya wanawake.
Baada ya kuondoka walimvua Atuganile nguo zote na kumlaza chali kwenye mkeka.
Walichukua majani mabichi na kuyaweka kwenye maji na kuyachikicha mpaka maji yote yakabadilika rangi na kuwa ya kijani.
Msugue sehemu zake mpaka ndani, bibi Tumwambilile alimuelekeza mama Atuganile. Naye alifanya kama alivyoelekezwa baada ya zoezi lile, alielezwa aendelee kumsugua mwili wote na kufanya hivyo kisha walimwosha maji yaliyobakia. Pamoja na zoezi lile
kufanyika hakukuwa na mabadiliko yoyote kwa Atuganile alikuwa amelala vilevile hali iliyozidi kumtisha mama yake.
Tumwambilile mbona hakuna mabadiliko yoyote?
Kwani nimemaliza kazi yangu, mama Atu unataka kuniudhi, bibi Tumwambilile alikuja juu.
Basi bibi nisamehe nimechanganyikiwa mwenzio.
Wewe ulipotoa uhai wa mtoto wa mwenzio hukuchanganyikiwa lakini ugonjwa wa mwanao ukuchanganye.
Bibi eeh! Si nimekubali nimekosa.
Bibi Tumwambilile hakusema kitu alichukua kichupa kidogo alichokuja nacho na kukiweka puani kwa Atuganile kwa muda kisha alikitoa. Walitulia kwa muda ghafla Atuganile alipiga chafya mfululizo na kutulia akiwa bado amejilaza chini.
Atu, bibi Tumwambilile alimwita.
Abee, aliitikia.
Vipi?
Mmh!
Alifumbua macho na kushtuka kumuona bibi Tumwambilile na mama yake wakiwa wamesimama pembeni yake kingine kilichomshtua ubaridi wa usiku ule.
Jamani kwani vipi? alisema huku akikaa na kujishangaa kukaa kwenye mkeka akiwa hana nguo mwilini huku sehemu ya mwili wake zikiwa na vipande vya majani mabichi.
Unajisikiaje? bibi Tumwambilile alimuuliza huku mama yake akiwa kimya kuogopa kumuudhi bibi.
Kwani kuna nini? bado Atuganilie hakuelewa kumemtokea nini.
Kwani nini kimekutokea?
Atuganile alitulia na kukumbuka kilichomtokea wakati amelala, alikumbuka tatizo lilivyoanza wakati alipofuatwa na Ambakisye.
Lakini hakutaka kusema chanzo bali tatizo lilivyompata usiku kwa kuhofia kuingiza imani za kishirikina kutoka kwa wazazi wa mpenzi wake na kuleta mzozo wa familia mbili wakati wazazi wake waliisha mhakikishia Ambakisye hawezi kuoa mwanamke mwingine.
Itaendelea Kesho wakati kama huu.