ILIPOISHIA:
"Baba timiza ndoto yetu ya mimi kuwa mke halali wa Colin, Baba Mungu nashukuru kwa kunichagulia mume mwema mwenye mapenzi ya dhati, nami namwahidi kuwa mke mwema katika siku za pumzi zangu. Simamia ndoa yetu, ondoa kila jicho la husuda, roho chafu za chuki, uongo na uadui kwa jina la mwanao Yesu Kristo aliye hai, Ameni."
SASA ENDELEA...
"AMENI," waliitikia pamoja huku kila mmoja akifuta machozi kutokana na maombi mazito aliyoporomoshwa na Cecy. "Naombeni maji," Cecy aliomba maji baada ya kuomba kwa muda mrefu na kuvunjwa jasho kama maji, kutokwa na jasho jingi ulikuwa muujiza mwingine kwa mama Cecy baada ya kutotoka jasho jingi kwa zaidi ya miezi sita.
Alipatiwa maji na kuomba kupumzika, Colin alimpandisha kitandani na kumfunika shuka.
"Colin mpenzi napumzika kidogo ila usiondoke wewe ndiyo furaha yangu."
"Sawa mpenzi."
Walimwacha Cecy amelala na kutoka nje kwa ajili ya mazungumzo.
"Jamani kuna nini kimefanyika ambacho mimi sikijui?" mama Colin aliuliza.
"Hakuna kilichofanyika na muujiza wa Mungu, wakati narudi nilisikia Cecy ananiita, nilipoingia nilishtuka kumwona akiniita. Nilipomsogelea sikuamini kumwona mwanangu katika hali ile kwani niliisha kata tamaa."
"Kweli nimeamini muujiza wa Mungu upo," alisema mama Colin.
"Ni kweli."
"Sasa kwa vile nilikuwa nimekuja ghafla acha nikapumzike pia tumwache mgonjwa apumzike ili kesho tujue tutafanya nini."
"Dokta Mariam amesema lazima tumpeleke hospitali akafanyiwe vipimo."
"Hakuna tatizo, Colin baba," alimgeukia mwanaye.
"Naam mama"
"Itabidi tuondoke ili ukapumzike kwa vile nawe hali yako haijatengemaa vizuri."
"Mama mimi nimepona kabisa, mgonjwa ni Cecy na nipo hapa kwa ajili ya kumhudumia kwa kila kitu."
"Sawa, lakini twende nyumbani tutakuja kesho."
"Mama naomba unisamehe, leo siondoki nitalala na mpenzi wangu."
"Mmh! Sawa."
"Nikutakie usiku mwema."
Mama Colin alimkumbatia mwanaye kisha alimuaga kuelekea alipopaki gari. Alimkuta Mage amesinzia baada ya kumsubiri kwa muda mrefu, alipofika alimwamsha.
"Mage pole kwa kukuweka."
"Usijali mama mkwe, vipi mbona umechelewa Colin amesha ondoka?"
"Yupo."
"Mbona umemwacha?"
Mama Colin alimweleza Mage yote aliyoyakuta na kumfanya asindwe kuamini na kujikuta akiuliza:
"Mama unayosema ni kweli?" Mage hakuamini.
"Kweli kabisa, yaani nilichokiona mbele yangu ni muujiza, Cecy amenyanyuka tena anaonekana kama mtu aliyepata nafuu wiki nzima."
"Mmh! Nimekwisha!" Mage alisema kwa sauti ya kukata tamaa.
"Kwa nini unasema hivyo?" mama Colin alishtuka.
"Mama kweli Colin atanioa?"
"Sikudanganyi, Colin anampenda sana Cecy, hakuna kiumbe kitakachombadili mawazo, yaani nimemkuta kama mwendawazimu sijui Cecy angekufa mwanangu angekuwaje."
"Mmh! Sawa," Mage alisema huku nguvu zikimwisha na kujikuta akijilaza kwenye usukani badala ya kuondoa gari.
"Vipi mbona hivyo?"
"Mama kupona kwa Cecy ni pigo zito moyoni mwangu, hapa nilipo sina hata nguvu za kuendesha gari. Naomba mama yangu uendeshe naweza kugonga."
"Hakuna tatizo."
Mama Colin alizunguka upande wa pili ili kuendesha gari baada ya Mage kupatwa na mshtuko kutokana na Cecy kupona. Mama Colin alishangazwa na hali ya Mage kubadilika ghafla baada ya kupata taarifa ya kupata nafuu kwa Cecy.
"Mbona umekuwa hivyo?"
"Mama basi tena."
"Lakini Mage hukutakiwa kununua pilipili kwa shughuli ya mwenzio ile ilikuwa pata potea. Nafasi uliichezea mwenyewe huna wa kumlaumu."
"Mmh! Sawa."
Kutokana na kutokuwa kwenye hali nzuri, Mage alilala palepale ili kuitafuta siku ya pili, mama Colin naye alikuwa na maswali yasiyo na majibu juu ya hali ya Cecy kubadilika kabisa wakati alikuwa nusu mfu. Lakini upande mwingine alimshukuru Cecy kupona kama angekufa mwanaye angekuwa chizi kwa jinsi alivyopagawa kwa mpenzi wake kupona.
***
Siku ya pili, Cecy alichukuliwa na kupelekwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa afya yake, majibu yalionesha kila kitu kipo sawa. Majibu yale yalikuwa faraja tele kwa Colin na kwa mama Cecy ambao ndiyo walioteseka kipindi chote cha ugonjwa wa Cecy.
Alitakiwa kufanya mazoezi kutokana na viungo kukaa muda mrefu bila kufanya kazi, afya ya Colin ilikuwa imetengemaa. Aliomba kwenda kupumzika na mchumba wake Afrika Kusini kwa miezi miwili.
Wazazi hawakuwa na jinsi, walikubali watoto wao waende kupumzika na kuendelea kupata huduma za kiafya. Baada ya siku mbili, Colin na Cecy walielekea Afrika Kusini katika mji Port Elizabeth na kufikia kwenye Hotel ya The Beach kwa ajili ya mapumziko baada ya mateso ya muda mrefu.
Colin alichukua muda ule kuhakikisha anafuta machungu yote aliyoyapata mpenzi wake kutokana na ajali mbaya iliyowapata ili kurudisha imani kwake kwa vile Mage alionekana bado yupo karibu na familia yao hasa mama yake hivyo kutia doa upendo wake.
Muda mwingi walitumia kukaa wawili chumbani kila asubuhi na jioni walifanya mazoezi madogomadogo katika gym iliyokuwa kwenye hoteli hiyo waliofikia na majira ya saa moja walitembeatembea pembezoni mwa ufukwe.
Itaendelea Juma mosi..............