ILIPOISHIA:
Mage hakutaka kuuliza swali lingine alinyanyuka na kutoka kuelekea kwa mama Colin kutaka kujua sababu ya safari yake ya Afrika ya Kusini na kwa sababu gani hakurudi na Colin. Alitoka hadi kwenye gari na kuchukua aina ya Toyota Harrier na kuelekea kwa mama Colin, aliendesha kwa kasi ili kuwahi kupata taarifa.
SASA ENDELEA...
Alipofika alipaki gari kwenye maegesho, kwa shauku ya kuyajua ya Afrika Kusini hakufunga hata mlango wa gari. Alitembea mwendo wa haraka hadi mlango wa kuingia ndani. Alibisha hodi na kukaribishwa na mama Colin aliyekuwa amekaa na mama Cecy wakiangalia mkanda wa video huku wakinywa vinywaji.
"Karibu ma mkwe," mama Colin alisema.
"A..a..sa.."
Alishindwa kumalizia sentesi ambayo ilikatikia njiani baada ya jicho lake kutua kwenye kioo cha runinga alichokiona mbele yake.
Alimuona Cecy katika vazi la harusi akiwa na Colin katika suti ya gharama, alikaza macho kama yanataka kudondoka.
"Maa..a..ma."
"Vipi mkwe?"
"Huyu si Colin?" alisema huku akinyoosha kidole.
"Ndiyo."
"Na..na..huyu si Cecy?"
"Ndiyo."
"Hii si..si..harusi?"
"Ndiyo."
"Wameoana lini?"
"Leo ni siku ya nne toka waoane na sisi tumerudi jana usiku kutoka huko."
"Mmh! Si kweli, haya ni maigizo tu ili kuniumiza roho."
"Kukuumiza roho ili iweje? Na picha zao hizi hapa."
Mage alizichukua albamu akiwa haamini anachoambiwa, aliifungua na kuanza kuangalia picha mojamoja huku mapigo ya moyo yakimwenda mbio. Kila ukurasa alioufunua uliupasua moyo wake alijikuta machozi yamefunika macho na kushindwa kuona picha.
Alihisi mapigo ya moyo yakiongeza kasi pumzi zikamjaa na kutoka kwa shida, kiza kizito kilitanda mbele yake kilichoendelea hakukijua. Mage alianguka kama mzigo akiwa amepoteza fahamu, kitendo kile kiliwashtua sana. Walijikuta wakitaharuki ilibidi wamchukue na kumkimbiza hospitali kisha kumjulisha mama yake.
Kwa vile huduma ile haikuwepo alitakiwa kupelekwa Afrika Kusini haraka kwani walisema ugonjwa ule ikiwa atapata matibabu ya haraka anaweza kupona.
***
Mage alisafiri na mama yake mpaka Afrika Kusini katika Hospitali ya Milpark iliyopo katika Jiji la Johannesburg. Alipokelewa na kuanzishiwa matibabu mara moja, madaktari walifanikiwa kufanya upasuaji uliochukua saa tatu kuondoa damu zilizovuja baada ya mshipa kupasuka.
Baada ya upasuaji kwenda vizuri alirudishwa kwenye chumba maalumu chini ya uangalizi ya madaktari bingwa. Taarifa za Mage kuumwa zilimfikia Colin aliyekuwa katika mji wa Port Elizabeth.
"Mpenzi nasikia Mage anaumwa ameletwa hospitali ya Milpark, Johannesburg," Colin alimwambia Cecy aliyekuwa akicheza game kwenye Ipad.
"Maskini mke mwenzangu nini kimemsibu?"
"Nasikia kapata mshtuko baada ya kuona video na picha zetu za harusi."
"Maskini, Mage alikuwa kama fisi aliyeamini siku moja mwanadamu atadondosha mkono."
"Namshangaa kutaka kufa wakati anajua mimi ni wa nani."
"Wa Cecy."
"Najiuliza bila Cecy, Colin leo ningekuwa wapi?"
"Anajua Mungu si sisi wanadamu ambao hupokea matokeo."
"Asante mpenzi wangu kwa kuyaokoa maisha yangu, huwezi kuamini baada ya kuachwa ghafla na Mage nilijawa na mawazo mengi na kujiona nina mapungufu."
"Asante niseme mimi uliyoyapa majibu maswali yangu kama kuna siku maji yatapanda mlima."
"Nina imani huu ni muda muafaka wa ku-renew mkataba wako na makapuni yote ya mavazi ya majarida. Waliniuliza afya yako nikawaambia hujambo kabisa hivyo wameomba tupange siku ya wao kuja ili uendelee na kazi yako."
"Mpenzi moyoni mwangu nimepanga kwanza nikae na mume wangu kwa mwaka mzima ndipo nifanye kazi nyingine.""Cecy si tumeshafunga ndoa wasiwasi wako nini?"
"Sijaifaidi raha ya ndoa kazi ipo tu, kama wameweza kunisubiri muda wote waendelee kusubiri."
"Makubaliano ya awali ni kwamba tutakuwa tupo pamoja katika kazi zako zote kwa vile mimi ndiye meneja wako."
"Mmh! Kama hivyo sawa."
"Mmh! Bado tu una wasiwasi wa kuibiwa?" Colin alimtania.
"Si umesikia mtu kataka kufa baada ya kusikia umeoa, vipi niwe mbali nawe? Nikisikia upo na Mage ningekufa mimi."
***
Baada ya kuwajulisha siku ya kuonana na Kampuni ya Ebony walifika katika Hoteli ya The Beach na kuingia mkataba mpya wa miaka miwili. Pia kampuni ya maonesho ya mavazi na urembo nayo iliingia mkataba mpya na makubaliano ya kuanza kazi baada ya miezi mitatu.
Mage naye alitoka hospitali akiwa na afya njema, mama yake alipotaka kujua sababu ya mshtuko ule, alimweleza ukweli kuwa baada ya kuona harusi ya Colin na Cecy alipata mshtuko wa ajabu kilichoendelea hakujua mpaka alipozindukia Hospitali ya Muhimbili akiwa amepooza upande mmoja.
"Unasema nani kaoa? Sijakuelewa vizuri," mama Mage alishtuka kusikia Colin kaoa.
"Colin, mama."
"Kama ni kweli basi mwanangu achana na mawazo ya Colin, Mungu atakupa mume wa kweli."
"Mama hata mimi nimejifikiria hivyo lakini Colin nilimpenda sana."
"Si kweli, ulimpenda Hans, Colin anapendwa na Cecy kwa hiyo waache na ndoa yao."
"Ndiyo mama, japo nilikuwa na nia mbaya kwa Cecy, lakini kuanzia sasa sitashughulika na Colin wala Cecy nami nasubiri ndoa yangu."
"Hilo ndilo neno la kijasiri mwanangu."
Baada ya Cecy kumaliza mapumziko alianza kazi rasmi, mwaka mmoja baadaye alishika ujauzito na kusubiri muda wa kujifungua. Mage naye alipata mchumba na mambo yalikwenda kama yalivyopangwa.
Siku ya harusi akiwa anajiandaa kwenda kanisani anapata habari zilizomshtua moyo na kufanya apoteze fahamu kuwa mpenzi wake Hans yupo huru baada ya kushinda rufaa yake.
*****************************************MWISHO***********************************
Baada ya kuwa safari ndefu hatimaye chombo kinatia nanga, mambo ya kujifunza kutokana na simulizi hii yako mengi ngoja nianishe machache tu, 1. mapenzi ya kweli hayaangalii hali ya mtu awe na pesa asiwe na pesa, 2. tuthamini hisia za mtu anayekupenda, 3.usimfanyie unyama mwenzio hasa wa kimapenzi aliyoyafanya Mage kwa coliny ndo yaliyomtesa mpaka mwisho. Mwisho wa yote mpende akupendae asiye kupenda chapa lapa