ILIPOISHIA:
"Mungu ni mwema."
"Karibuni," alikwenda kitandani kumwangalia Cecy ambaye muda huo alikuwa amepitiwa usingizi.
"Vipi anaendeleaje?"
"Tutazungumza nyumbani, vipi Colin naye anaendeleaje?"
"Kweli Mungu ni mwema anaendelea vizuri."
SASA ENDELEA...
Kwa vile alikuwa amekuja na gari aina ya Toyota Noah aliyoelezwa ndiyo inayotakiwa kumpokelea mgonjwa, walimweka kwenye gari na kuelekea nyumbani kwa mama Cecy ambako siku ile kulifanyika usafi na kuiweka nyumba katika hali nzuri.
Hivyo walikuta nyumba ipo vizuri pamoja na msichana wa kazi aliyeachwa kwa ajili ya kuangalia nyumba kwa muda wote ambao hakuwepo.Baada ya kufikishwa nyumbani aliingizwa chumbani na kulazwa kitandani, muda wote mama Colin alimfuatilia Cecy na kuonesha hakuwa na dalili zozote za kupona.
Pamoja na huruma kumjia lakini bado aliamini kama Cecy atakufa basi Mage ndiye mbadala wake.
Baada ya kumlaza kitandani daktari aliyekwenda na Cecy India alikaa na wazazi wawili na kuwaeleza:
"Jamani nina imani maelezo tuliyopewa India unayakumbuka, lakini kwa kuongezea ninataka kuwaeleza, mgonjwa hali yake bado japo kuna mabadiliko makubwa sana tofauti na alivyokwenda. Ugonjwa wa Cecy umekuwa tofauti na ugonjwa mwingine ambao madaktari bingwa wamekutana nayo huu kidogo umewala akili.
"Inaonekana mwili wa Cecy unajenga mawasiliano taratibu sana inaweza kuchukua muda mrefu sana kunyanyuka kitandani. Hivyo anatakiwa uangalizi wa karibu sana, kama kuna uwezekano aajiriwe mtu kwa kazi hii ili kumpumzisha mama yangu hapa kwani namhurumia amefanya kazi kubwa usiku na mchana kwa ajili ya kumwangalia mwanaye japo nilimsaidia bado muda wote alikuwa halali.
"Mgonjwa ataendelea kupata huduma ya kuchukuwa kila siku mwili mzima ili kusisimua misuli ya mwili. Nina imani kwa uwezo wa Mungu anaweza kupata nafuu upesi kwa vile mwisho wa akili ya mwanadamu ndipo uwezo wa Mungu huchukua nafasi yake," dokta Mariamu Shaka aliwapa moyo kwa maneno ya hekima.
"Nina imani mpaka leo yupo hivi lazima turudishe shukrani zetu kwa Mungu wetu," mama Colin alisema.
"Kingine mama, huoni maajabu pamoja na mwili kukosa mawasiliano lakini vitu vyote vya ndani vinafanya kazi hata kuweza kula japo chakula laini kitu ambacho kimewashangaza hata madaktari bingwa."
"Ni kweli tuna kila sababu ya kumshukuru alichotupa si haba, kama leo katupa kidogo na kurudisha shukurani kwake basi hatasita kutupa kikubwa, nina imani mwanangu siku moja atasimama," alisema mama Cecy kwa hisia kali.
"Amina, Mungu wetu ni msikivu," alijibu dokta Mariamu.
Kwa vile muda ulikuwa umekwenda mama Colin aliaga kurudi nyumbani na kumwacha mama Cecy mgonjwa na daktari ambaye alilala pale ili kesho yake baada ya kumpatia mgonjwa huduma arudi nyumbani kwake.
Kutokana na hali aliyomuona nayo Cecy, hakutaka kumweleza mwanaye kwa kujua atamshtua hata kukosa raha na kumuongezea matatizo kwa vile alimpenda sana mchumba wake. Lakini alijiuliza mwanaye akijua lazima atamwelewa vibaya, alipanga kumwambia baadaye kuwa Cecy amerudi.
Aliamua kukaa kimya huku wiki ikikatika bila kumweleza kitu chochote mwanaye juu ya Cecy kurudi toka India. Siku zote alitoka peke yake kwenda kumwona Cecy na kuonesha kuguswa na hali ile huku akimlipa daktari aliyekwenda naye India pesa nyingi ili kumpatia huduma ya kumchua na kumwangalia kila siku baada ya kazi.
Wema wake ulikuwa wa mamba wa kutoka machozi lakini alikuwa na siri moyoni mwake kujionesha anamjali mgonjwa. Lakini aliamini kupona kwa Cecy ni ndoto, kila alipoulizwa na mama Cecy kuhusu hali ya Colin alisema hajambo kiasi.
"Hawezi kutembea?"
"Mmh! Kwa sasa amekatazwa kutembea."
"Kwa nini basi usimlete aje amwone mchumba wake?"
"Atakuja hali yake ikitulia.""Kwa hiyo hali yake inaonekana bado."
"Ni kweli."
"Mmh! Mpe pole isingekuwa hali ya Cecy ningekuja kumwona mkwe wangu."
"Mungu atawapa afya na kuweza kunyanyuka.""Mungu atasikia dua zetu, kila jambo la heri Mungu ulishika mkono nina imani Cecy na Colin watasimama na siku moja kusherehekea harusi yao."
"Amen," mama Colin aliitikia huku moyoni akijisemea "Labda harusi aliyosema mwanaye ya kufunga ndoa na maiti ya Cecy, lakini harusi ya sherehe ukumbini itakuwa muujiza."
Mama Cecy aliamini hali ya Colin ni mbaya ila mama yake anampa moyo, alipanga siku akipata nafasi afike kumwona kwani haikuwa vizuri mzazi mwenzie kuja kumuona mwanaye na yeye kutokwenda kumuona Colin. Kwa vile hali ya mwanaye alijua alipanga siku moja baada ya kumpatia chakula akilala atoke mara moja kwenda kumwona Colin na kuwahi kurudi.
Siku ya tatu ambayo mama Colin alipiga simu kuwa hatakwenda kwa vile kuna sehemu ambapo angerudi usiku. Siku hiyo mama Cecy aliitumia kumwandaa Cecy ambaye alishangaa kuona mabadiliko madogo baadhi ya sehemu kupata joto kama miguuni ambako kulikuwa na ubaridi kwa muda mrefu.
Baada ya kumpatia chakula chepesi na dawa alimwacha apumzike na yeye kukodi gari mpaka kwa mama Colin kumjulia hali mgonjwa. Wakati huo Mage alikuwa akiendelea kuwa karibu na Colin ili kujivuta karibu kwa kuamini baada ya kifo cha Cecy basi nafasi ile ni yake.
"Colin nina imani sasa hivi afya yako ni nzuri unaweza hata kuendesha gari."
"Namshukuru Mungu, pia nashukuru kwa msaada wako kwangu kwa muda wote wa kuniangalia."
"Usijali nipo kwa ajili yako, nitapigania afya yako hata kwa gharama yoyote."
"Usiwe na wasi nina imani sasa hivi sijambo na wiki ijayo nitakwenda India kumwangalia Cecy."
"Lakini hali yako si bado kwa nini usisubiri upone kabisa.""Mage, mimi sijambo sasa hivi naweza kufanya lolote, lakini afya ya mpenzi wangu siijui. Mpaka leo bado yupo hospitali huenda yupo kwenye hali mbaya lazima niende nikajue hali yake."