Hadithi: Wakili wa moyo

Hadithi: Wakili wa moyo

Yan mapenz haya jaman!! Mage naye hajielew maskn. Hv hans aktoka jela atamfuata atamwambia Nakupenda.
 
ILIPOISHIA:
“Lakini hali yako si bado kwa nini usisubiri upone kabisa.”
“Mage, mimi sijambo sasa hivi naweza kufanya lolote, lakini afya ya mpenzi wangu siijui. Mpaka leo bado yupo hospitali huenda yupo kwenye hali mbaya lazima niende nikajue hali yake.”
SASA ENDELEA...

“Mmh! Sawa,” Mage aliogopa kutia neno kwa kuhofia kukorofishana na Colin ambaye alionekana bado ana mapenzi mazito na Cecy. Alijua msimamo wake ni kwa vile hajamwona lakini akimwona hali yake aliamini lazima angebadili mawazo na nafasi ile kumpa yeye.
Wakiwa katikati ya mazungumzo walishtuliwa na hodi, waliponyanyua macho Colin hakuamini kumwona mama Cecy aliyejua yupo India na mpenzi wake, lakini afya yake ilionekana imedhoofu sana.
“Ha! Mama ni wewe?” Colin alisema huku akinyanyuka na kwenda kumpokea mama mkwe.

“Ni mimi mwanangu, unaendeleaje na wewe?”
“Namshukuru Mungu, hali yangu sijambo. Sasa hivi nilikuwa nasema wiki ijayo nakuja India kumwona mchumba wangu. Ha..ha..lafu mbona uko huku Cecy umemwacha na nani hospitali?”
“Kwani mama yako hajakwambia?”
“Kuhusu nini?”

“Kurudi kwetu, nimemuulizia ameniambia hali yako bado si nzuri, hivyo nikaona nije nikujulie hali baba yangu na kumwacha mchumba wako na msichana wa kazi.”
“Mama unataka kuniambia Cecy yupo Tanzania?” Colin alishtuka huku macho yamemtoka pima.
“Colin unauliza ukweli au unatania?”

“Mama mimi na wewe hutujawahi kutaniana, hata muulize Mage muda si mrefu nilikuwa namwambia lazima nije India kumjulia mchumba wangu hali yake baada ya mimi kuamini nimepona.”
“Siamini unachokisema najua unaumwa hivyo hukuwa na uwezo wa kuja kumpokea mchumba wako, lakini sikubali kauli yako kuwa huna taarifa yoyote kuwa mimi na Cecy tupo nchini kwa wiki sasa.”
“Wiki!?” Colin alishtuka.

“Colin hebu acha kujitoa akili, ina maana mama yako hajakwambia?”
“Hajaniambia, ina maana mama anajua?”
“Mbona ndiye aliyetupokea na kila siku lazima afike kumuona mgonjwa kasoro leo.”
“Mmh! Unamaanisha mama yangu, mama Colin?”
“Ndiye huyohuyo, inamaana hajakwambia?”

“Haki ya Mungu sijui kitu, sikuwa mgonjwa wa kushindwa kuja kumpokea mpenzi wangu, kwa nini mama kanificha hivi, Cecy mpenzi wangu atanielewa vipi?” Colin alisema kwa uchungu.
“Sijui, labda muda wake wa kukueleza bado, lakini namshukuru sana amejitolea kwa hali na mali ili kuhakikisha afya ya mpenzi wako inatengemaa.”
“Vipi hali ya mpenzi wangu?”

“Bado, lakini ana afadhali kwa mbali.”
Colin alinyanyuka na kumwomba mama Cecy aende akamwone mpenzi wake.
“Mama naomba nikamwone mpenzi wangu.”

“Colin pumzika kwanza hujapona vizuri, nilikuja kukuona tu.”
“Hapana...kama Cecy ana wiki hapa mama kanitendea unyama mkubwa sana,” Colin alisema huku akionekana kuchanganywa na taarifa zile ambazo hakutegemea kusikia kwa kuamini Cecy bado yupo India.

Colin hakusema kitu alikwenda ndani na kuchukua ufunguo wa gari na kutoka.
“Mama naomba twende,” Colin alipagawa na kusahau muda mfupi alikuwa na Mage alitoka bila hata kumuaga na kumfanya Mage aumie moyoni kuona ana kazi kubwa ya kuubadili moyo wa Colin. Lakini aliamini kifo cha Cecy ndiyo tiketi yake ya kuwa na Colin, aliendeleza dua za kuomba kifo cha Cecy.

Colin japo alikuwa hajaruhusiwa kuendesha gari, alikwenda kuchukua gari na kumwomba mama Cecy waondoke. Waliongozana hadi kwenye gari na kuondoka kuelekea kwa Cecy. Wakiwa ndani ya gari, Colin alimdodosa mama Cecy.
“Mama kwanza vipi hali ya mchumba wangu?”
“Hajambo, lakini bado.”“Bado nini kinamsumbua?”
“Siwezi kukueleza kwa vile unakwenda mwenyewe kila kitu utakiona.”
“Mmh! Sawa.”

Colin aliendesha gari huku akiwa na mawazo mengi juu ya mama yake kukaa kimya huku kila siku anakwenda kumwona mgonjwa bila kumwambia alijiuliza alikuwa na maana gani na mchumba wake angemwelewa vipi kama amerudi bila kwenda kumwona.
Walipofika walikwenda hadi ndani, Colin alionekana mwenye kimuhemuhe cha kumwona mpenzi wake. Kwa vile alikuwa akikijua chumba cha Cecy, aliingia moja kwa moja. Lakini chumbani kwake hakuwemo alitoka na kukutana na mama Cecy.
“Mama mpenzi wangu yupo wapi?” Colin aliuliza macho yamemtoka pima na presha juu.
“Colin taratibu umefika utamuona, subiri,” mama Colin alisema huku akielekea chumba alicholazwa Cecy.
Alipogusa mlango alishtuka kusikia Cecy akimwita sauti ambayo ilipotea toka alipopata ajali.
“Mama...mama.”

Alisogea haraka kitandani na kuitikia.
“Abee mwanangu.”“Nigeuze nimechoka kulala hivi?”

Nini kilitokea? Usikose wiki ijayo.
 
Duuuh naombea collin lisimpate baya lolote la sivyo kitamnukia mama secy
 
ILIPOISHIA:
"Colin taratibu umefika utamuona, subiri," mama Cecy alisema huku akielekea chumba alicholazwa Cecy.
Alipakaribia alipogusa mlango alishtuka kusikia Cecy akimwita sauti ambayo ilipotea toka alipopata ajali iliyokuwa ikimwita.

"Mama...mama."
Alisogea haraka kitandani na kuitikia.
"Abee mwanangu."
"Nigeuze nimechoka kulala hivi?"
SASA ENDELEA...

Mama Cecy aliona ule ni muujiza mkubwa kwake kwa vile siku zote mgonjwa alikuwa wa kulala bila kujitikisa wala kusema neno zaidi ya kutumbua macho tu bila kuyapepesa. Alimgeuza na kumlaza vizuri.
"Niwekee mto chini."
Mama yake haraka alichukua mto na kumwekea mwanaye.
"Mama ulikuwa wapi?"
"Nilikuwepo nje."

"Mbona dada alisema ulitoka?"
"Nilifika dukani."
"Mume wangu Colin yupo wapi?"
"Yupo sebuleni."
"Anafanya nini?"
"Ndiyo amefika sasa hivi."
"Alikuwa wapi?"

"Kwao."
Cecy kusikia Colin yupo sebuleni alitaka kunyanyuka na kuishia kukaa kitako na kurudi tena chini. Kitendo cha kujinyanyua peke yake yalikuwa maajabu mengine kwa mama Cecy ambaye alipiga ishara ya msalaba na kumshukuru Mungu kwa kile alichokionyesha muda ule mbele yake.
"Asante Mungu... Asante baba... Asante kwa kila akifanyacho mbele ya macho yangu."
"Mama," Cecy alimwita mama yake.

"Abee."
"Naomba niende kwa Colin."
"Subiri."
Mama Colin alitoka hadi sebuleni ambapo Colin alikuwa akizungumza na dada wa kazi juu ya hali ya Cecy. Alimdodosa na kuelezwa yote toka alipofika na hali aliyokuwa nayo na maajabu ya siku ile alipokuwa akimtengeneza kitandani na kushtuka kumsikia akiita jina la Colin na baadaye aliita mama yake.

Dada wa kazi alimweleza ametoka, ndipo alipoanza kumuuliza maswali ambayo alimjibu kwa vile mambo mengi alikuwa akiyaelewa. Baada ya mazungumzo ya dakika ishirini Cecy aliomba kugeuzwa tofauti na siku za nyuma alikuwa wa kulala tu na kugeuzwa kwa kipindi.
"Kwa hiyo toka apate ajali ndiyo kazungumza leo?"
"Ndiyo najua hata mama ataona muujiza."

"Mmh!" Colin aliguna na kujiuliza nini hatima ya mpenzi wake ikiwa sehemu inayotegemewa na watu wote imeshindwa. Ile kwake ilikuwa picha mbaya sana na kukiona kifo cha Cecy kipo mbele. Aliamini yote aliyasababisha yeye alijikuta akitokwa na machozi ya uchungu.
"Colin baba," Colin alishtuliwa na mama Cecy.

"Naam mama," Colin aliitikia huku akinyanyua kichwa.
"Ha! Unalia nini tena?" mama Cecy alishtushwa na machozi ya Colin.
"Inauma."
"Cecy anakuita."

Colin bila kujibu alinyanyuka na kuelekea chumbani ambako alimkuta Cecy amelala kitandani mwili ukiwa umepururuka kwa ugonjwa.
"Cecy," aliita kwa sauti huku akisogea kitandani na kumkumbatia mpenzi wake.
"Colin mume wangu," Cecy alisema huku akijitahidi kumkumbatia mpenzi wake.
Ilikuwa ajabu nyingine Cecy kuweza kumkumbatia Colin kwa mwili uliobakia mifupa mitupu.
"Ni mimi Cecy mke wa maisha yangu."

"Colin nimefurahi kukuona mpenzi wangu japokuwa nina muda mrefu nilikuwa siwezi kuzungumza wala kujigeuza. Lakini kuja kwako kumekuwa dawa ya kupona kwangu. Hata nikifa sasa hivi moyo wangu utakuwa na furaha kwa vile nimekuona chakula cha nafsi yangu," Cecy alisema kwa sauti ya chini.
"Ni kweli naamini Mungu alituumba kwa ajili yetu, siamini niliyoyasikia na niliyokutana nayo leo," Colin bado alikuwa kama yupo ndotoni.
"Ni Mungu tu mpenzi wangu."

Siku ile Colin alishinda pale mpaka jioni pembeni ya Cecy, pamoja na yeye hali yake kuwa katika uangalizi lakini hali aliyomkuta nayo mpenzi wake aliamini amepona kabisa. Jioni daktari aliyempeleka India alipopitia kuangalia hali ya mgonjwa wake alishikwa na mshangao baada ya kukuta hali ya Cecy ina mabadiliko makubwa.
"Mungu mkubwa siamini ninachokiona leo," mama Cecy alisema huku akifuta machozi kwa kiganja cha mkono.
"Ni kweli Mungu katenda muujiza wake,"Colin alisema huku naye akifuta machozi."
"Jamani msinililie tena, kama nilikuwa nusu mfu kwa muda mrefu na leo nipo hivi, basi aminini nimepona," Cecy alisema kwa kujiamini.

Siku ile kazi ya masaji aliifanya Colin huku akimpa moyo mpenzi wake kuwa atapona.
"Kweli nitaweza kutembea, maana kwa hali ya kulala kitandani kama nyoka nitapona?"
"Utapona tena na kusimama, nakuahidi baada ya kupona nakufanyia bonge la surprise."
"Colin nawe kwa kunipa moyo, je nisipopona?"
"Ugonjwa utakuwa wetu sote."

"Hutafuti mwanamke mwingine?"
"Cecy baada ya kukufungia moyoni mwangu ufunguo niliutupia baharini, mimi ni kipofu mbele yako. Wewe ndiye uliyekuwa mwanamke wa mwisho kuonwa na macho yangu. Siamini kama nitapenda tena katika maisha yangu kama tutatengana. "Nakupenda Cecy zaidi ya kupenda. Amini usiamini muda si mrefu utasimama na kutimiza ndoto yetu ya kuwa mke na mume."

Itaendelea wiki ijayo.
 
Duuuh yan hawa watu wanapendana hadi naona wivu lol
 
ILIPOISHIA:

"Cecy baada ya kukufungia moyoni mwangu ufunguo niliutupia baharini, mimi ni kipofu mbele yako. Wewe ndiye uliyekuwa mwanamke wa mwisho kuonwa na macho yangu. Siamini kama nitapenda tena katika maisha yangu kama tutatengana. "Nakupenda Cecy zaidi ya kupenda. Amini usiamini muda si mrefu utasimama na kutimiza ndoto yetu ya kuwa mke na mume."

SASA ENDELEA...

"Colin sikuwahi kumwamini mtu katika maisha yangu lakini wewe kwangu sina la kuongeza nakuamini mpenzi wangu. Mungu ana maajabu yake amini kila litendekalo lina makusudio yake."

"Cecy Mungu wa ajabu wewe ni yule wa jana leo na kesho, Mungu alikupa azina ya busara na hekima ni mtaji mkubwa katika maisha yetu."

"Asante kwa kulitambua hilo."

Pamoja na Cecy kuwa mgonjwa aliweza kuzungumza mengi na mpenzi wake mpaka ulipofika muda wa kumwacha apumzike. Colin hakutoka alilala pembeni ya mpenzi wake. Mpaka muda daktari alipofika kumjulia hali Cecy. Alishangazwa na hali aliyomkuta nayo Cecy ulikuwa muujiza mkubwa maishani mwake.

"Kweli Mungu mkubwa hutenda pasipo mtu kutegemea, siamini... siamini kuna kila sababu ya kumshukuru Mungu wetu," dokta Mariam Shaka alichanganyikiwa na hali aliyomkuta nayo Cecy.

Dokta Mariam alisema baada ya kumwona Cecy akijigeuza kitandani na kumwita mpenzi wake.

"Colin."

"Naam mpenzi."

"Nataka kwenda msalani."

Colin alimnyanyua na kumkalisha kisha aliomba chombo cha kujisaidia na kupewa, kazi yote ya kumhudumia mpenzi wake alifanya mwenyewe. Baada ya kumwogesha alimrudisha kitandani. Baada ya huduma zote dokta Mariam alimchunguza ilionesha kila kiungo kimepata ufahamu.

Kila alipominywa kwa nguvu alipiga kelele, ile ilikuwa dalili nzuri kuonesha mwili mzima umesharudisha mawasiliano. Baada ya kufanyiwa uchunguzi alikalishwa kitako na kuelezwa aliyekuwepo mbele yake ni dokta Mariam Shaka aliyekwenda naye India kwa siku zote alizokuwa naye huko katika kumchua mwili.

"Asante dada yangu Mungu atakulipa," Cecy alisema huku machozi yakimtoka.

"Usijali, Mungu mkubwa naamini muda si mrefu utasimama tena, hatua ya leo ni kubwa kweli kila lililo zito kwa mwanadamu kwa Mungu ni jepesi."

"Hakika," alisema mama Cecy.

Colin alikuwa karibu muda wote kuonesha jinsi gani anavyomjali mpenzi wake ambaye aliamini ni mwanamke wa maisha yake. Siku hiyo kila kitu Colin aliomba amfanyie mpenzi wake. Ilikuwa faraja kubwa kwa Cecy ambaye pamoja na kuwa bado mgonjwa lakini ukaribu wa kipenzi chake uliongeza faraja moyoni mwake.

***

Upande wa pili baada ya Colin kuondoka na mama Cecy, Mage hakuondoka alibakia kumsubiri Colin kwa kuamini kutokana na maelezo ya mama yake Cecy alikuwa nusu mfu mtu wa kulala tu. Hivyo asingekaa muda mrefu angerudi mapema na kumkuta, alitumia muda mwingi kuangalia mikanda ya video.

Mama Colin alirudi saa mbili kasoro usiku na kumkuta Mage peke yake amejaa tele sebuleni. Mage alipomwona mama mkwe zilipendwa alinyanyuka na kumpokea.

"Wawooo, karibu mama."

"Asante mwanangu, za kushinda?"

"Mmh! Nzuri."

"Mbona kwanza umeguna kabla ya kujibu."

"Hamna mama."

"Mwenzio yupo wapi?"

"Ametoka."

"Ametoka! Kaenda wapi?"

"Kumwona mgonjwa."

"Mgonjwa! Mgonjwa gani?"

"Cecy."

"Cecy! Nani kamwambia kama Cecy yupo?" mama Colin alishtuka kusikia habari zile.

"Mama yake alikuja."

"Mama yake nani?"

"Colin."

"Mama Colin ndiye nani?"

"Ooh! Sorry mama Cecy."

"Mama Cecy alikuja hapa?"

"Ndiyo."

"Jamani huyu mwanamke vipi, si nilimkataza pia nilimwambia Colin bado mgonjwa? Kwa nini amemchukua yule mama ananitafuta nini?"

"Kwa hilo namtetea mama Cecy, Colin ndiye aliyeng'ang'ania baada ya kujua Cecy yupo nchini."

"Hata hivyo, nani kamwambia aje hapa? Mimi nilikuwa na maana yangu ya kuchelewa kumwambia Colin. Nilijua hali ile itamchanganya sana."

"Basi ndiyo hivyo mwanao kachanganyikiwa baada ya kuelezwa tu alikimbilia ndani na kuchukua funguo ya gari na kutoka. Hata mimi niliyekuwa naye muda wote kaondoka bila kuniaga."

"He! Na gari kaendesha?'

"Ndiyo."

" Huyu mama Mwanga! Anataka kuniulia mwanangu si nilimwambia anaumwa?"

Mage alikosa jibu kwa vile hakuona kosa la mama Cecy hivyo hakutia neno lolote.

"Mmh! Kwani kaondoka toka saa ngapi?"

"Saa tano asubuhi."

"Saa tano asubuhi mpaka sasa? Lazima atakuwa amezidiwa, Mage hebu twende tukamtazame. Utaendesha gari maana hapa nilipo hata nguvu sina sijui mwanangu yupo kwenye hali gani."

"Hakuna tatizo mama mkwe."

Mama Colin na Mage walitoka nje kwenda kwenye gari ili waelekee kwa mama Cecy kumwangalia Colin, waliamini Cecy bado yupo katika hali ya nusu mfu akisubiri muda wake wa kuigawa roho kwa mtoa roho japokuwa alionekana mbishi kuitoa kwa kipindi kirefu.

Walikwenda kwa mama Cecy ambako kulikuwa na nyumba ya kisasa iliyojengwa na Colin kwa ajili ya mpenzi wake.

Itaendelea wiki ijayo!
 
duuuuh...jumamosi mbali jamani..nice story mpaka nachanganyikiwa
 
Mr Rocky obh'eja sana...hongera kwa kupokea mkoba tulikuwa tumepoa.
 
Last edited by a moderator:
Dah! mama colin ana roho mbaya sana kuliko mbwa mwitu
 
Back
Top Bottom