Hadithi: Wakili wa moyo

Hadithi: Wakili wa moyo

ILIPOISHIA:
Aliwaeleza hatua walizochukua tokea mwanzo kwa
wagonjwa wote na kufanikiwa kwa mmoja na
sehemu walipokwama na kuhitaji msaada wa
matibabu zaidi kwa mmoja nje ya nchi.
SASA ENDELEA...
Waliulizia kama kuna uwezekano wa mgonjwa
kupona, walijibu upo wa hamsini kwa hamsini.
Waliuliza gharama ya matibabu yote walielezwa
milioni ishirini na tano kwa awali kama itazidi
watajulishwa kwa vile mgonjwa hakuwa wa kutoka
mapema.
Walikubali kugharamia matibabu ya Cecy mpaka
hatua ya mwisho. Baada ya makubaliano, zilifanywa
taratibu zote za kumsafirisha mgonjwa na mtu wake
wa karibu.
Siku ya tatu, Cecy alisafirishwa pamoja na mama
yake kwenda India kwa matibabu ambayo wengi
waliamini madaktari wa Tanzania waliona aibu
kusema ukweli kuwa Cecy ameisha kufa
anachosubiri kupoa tu. Baada ya safari ya angani
Cecy alitua katika jiji la Mumbay na kupelekwa
katika Hospitali ya Apolo.
Alipokelewa mara moja alianza kupatiwa matibabu
kwa kuchukuliwa vipimo vyote ili kuangalia tatizo
lipo wapi. Baada kurudi majibu ya vipimo ilionesha
Cecy atapona lakini itachukua muda kurudi katika
hali ya kawaida kutokana na kupoteza kumbukumbu
kutokana na ubongo wake kucheza kidogo, lakini
alikuwa na bahati nzuri ubongo haukuvia damu.
Hali ya Colin iliendelea vizuri kwa kuimarika kwa
kasi kubwa tofauti na walivyotegemea. Baada ya
wiki aliweza kuzungumza vizuri na kuanza
kumkumbuka mpenzi wake Cecy. Wakiwa wamekaa
kitandani Colin alimuuliza mama yake.
“Mama mbona simuoni Cecy wala mama yake leo
siku ya tatu?”
“Cecy alisafiri walifiwa na bibi yao kabla hujapata
ajali.”
“Mama ina maana nilipata ajali peke yangu?”
Swali lile lilimchanganya sana mama yake
aliyeamini mwanaye baada ya ajali alipoteza
kumbukumbu na hakutaka kumshtua kutokana na
hali na mchumba wake ambaye aliamini aliondoka
mfu kwa asilimia tisini na tano.
“Kwani unakumbuka nini?”
“Unajua mama nakumbuka wakati napata ajali
nilikuwa na Cecy tukitoka mazoezini na sababu ya
ajali ni Mage.”
“Mage?” mama yake alishtuka.
“Ndiyo mama.”
“Mage kasababisha kivipi?”
Colin alimweleza tukio zima la ajali ilivyotokea
mpaka kupata ajali, baada ya kumsikiliza aliguna na
kusema:
“Kwani Mage aliandika ujumbe gani?”
“Kwa kweli sikuuona bali usomaji wa Cecy
ulionesha ujumbe siyo mzuri.”
“Sasa wewe nini kilikupelekea kupata ajali.”
“Mama baada ya kumwangalia Cecy usoni moyo
ulishtuka na kujua hakuna tena usalama kwa vile
aliisha mshutumu Mage mapema baada ya hukumu
ya mchumba wake kabla ya simu na kutishia
kusitisha mkataba. Mage alinipigia simu na
kuzungumza maneno ambayo ni uchokonozi kwa
vile anajua kabisa nipo na nani.”
“Inaonekana alikuacha bado anakupenda ulikuwa
una hiyari kukubali au kukataa au hata kumfanya
spea taili.”“Mama Cecy ni kila kitu kwangu ndiye
mwanamke wa pekee moyoni mwangu sina nafasi
nyingine.”
“Lakini ulitakiwa kujua ameandika ujumbe gani
kabla ya kupagawa na kusababisha ajali mbaya.”
“Kwani gari limeharibika sana?”
“Limeungua lote na moto.”
“Mungu wangu na..na Cecy?”
“Naye alipata majeraha kama yako.”
“Yupo hapa hospitali?”
“Hapana yeye inaonekana alipata matatizo
makubwa na kukimbizwa India.”
“Maskini mpenzi wangu,” Colin alishika kichwa kwa
mshtuko.
“Lakini taarifa zinasema anaendelea vizuri,” mama
yake alimpa moyo.
“Hospitali natoka lini?”
“Wiki hii lakini utatakiwa kuja kila siku asubuhi
kufanya mazoezi ya viungo ili kuurudisha mwili
katika hali ya kawaida.”
“Nikijisikia vizuri kidogo nakwenda India kumwona
mpenzi wangu.”
“Hakuna tatizo tutakwenda wote,” mama Colin
alimkubalia mwanaye kumpa moyo lakini aliamini
kabisa Cecy hakuna kitu siku zake zilikuwa
zikihesabika walichosubiri taarifa za msiba wake.
***
Mama Mage na mwanaye walikuwa wakizungumza
kuhusiana na hali ya Colin na mchumba wake.
“Mama unafikiri mchumba wa Colin anaweza
kupona?”
“Mmh! Kwa kweli ni Mungu tu mwenye uwezo wa
kumponya, taarifa nilizopata kutoka kwenye
hospitali aliyokuwa anatibiwa kupona ni asilimia
ndogo na hata akipona bado hatakuwa sawa.”
“Kwa hiyo mama nina imani hii ni nafasi yangu ya
kurudi kwa Colin?”
“Ni nafasi yako kama ukiifanyia kazi bila hivyo
itakupita huku unaiona.”
“Sasa mama niifanyie kazi vipi au niende kwa
Karumanzila?”
“Si kwenda kwa Karumanzila bali kujipendekeza
muda huu wa matatizo kuonesha unamjali sana
Colin kwa kwenda asubuhi unarudi usiku
ikiwezekana ulale hukohuko.”
“Mama tena naondoka muda huu.”
“Mwanangu kijua ndicho hiki lazima uuanike sasa,
huenda Mungu alikuwa na kusudio lake la
kuirudisha ndoa yenu iliyoyeyuka kwa kifungo cha
Hans na kufa kwa Cecy.”
“Umeona eeh, mama utakuwa nabii kwa kuliona
hilo, japo siwezi kufurahi kwa matatizo ya Cecy
lakini kila kitu hupangwa na Mungu.”
“Halafu nimeambiwa Colin atatakiwa kila siku
asubuhi apelekwe hospitali kwa mazoezi, nataka
kazi hiyo uifanye wewe tena utachukua gari la
kifahari la kumpelekea hospitali.”
“Mama hilo si la kusema mbona kikohozi kimepata
mkohoaji nitahakikisha mahaba ninayompa
anamsahau marehemu wake(Cecy).”
Baada ya mazungumzo Mage alimuaga mama yake
kwenda kumwona Colin nyumbani kwao ili
aurudishe ukaribu wao kutokana na matatizo ya
mchumba wake Cecy. Mage maombi yake alitaka
Cecy afie India, Tanzania urudi mwili tu usio na

uhai, aliendesha gari hadi nyumbani.
Itaendelea wiki ijayo!
 
ILIPOISHIA:
Mage maombi yake alitaka Cecy afie India,
Tanzania urudi mwili tu usio na uhai, aliendesha gari
hadi nyumbani.
SASA ENDELEA...
Mama Colin alimpokea Mage aliyejionesha mwenye
huzuni kutokana na ugonjwa wa Colin.
“Karibu mkwe.”
“Asante mama, mume wangu anaendeleaje?”
“Mmh! Kiasi hajambo vipi nyumbani hamjambo.”
“Hatujambo kiasi.”
“Kuna anayeumwa?”
“Hapana ila huwezi kuamini toka Colin apate
matatizo nimekuwa sili wala silali vizuri utafikiri
naumwa mimi.”
“Pole, la muhimu kumuomba Mungu atapona tu.”
“Mama maombi yangu yote kila dakika ni kwa
Colin.”
“Mama yako hajambo?”
“Hajambo, mume wangu yupo wapi?” Mage
alijifanya ana shauku ya kumuona Colin.
“Yupo chumbani kwake amepumzika.”
Kwa vile chumba cha Colin alikuwa akikijua,
alikwenda moja kwa moja na kuingia ndani bila hodi.
Alimkuta amesinzia aliinama na kumpiga busu la
shavu lililomfanya Colin afumbue macho. Alishtuka
kukutana na Mage aliyekuwa amemchanulia
tabasamu pana amesimama pembeni ya kitanda.
“Colin mpenzi wangu pole sana,” Mage alisema
huku akikaa kitandani, lakini Colin hakumjibu
alikuwa kama anamshangaa.
“Vipi unaendeleaje mpenzi?” alimuuliza tena.
“Mage unatafuta nini hapa?” Colin alimuuliza akiwa
amemkunjia uso.
“Colin mpenzi wangu maswali gani hayo wakati
unajua wewe ni mgonjwa.”
“Hata kama mgonjwa sikukuita uje unione labda
ungekuja kuona jeneza langu na si mwili wangu.”
“Kwa nini unasema hivyo mpenzi wangu?” majibu
ya Colin yalimshtua Mage.
“Kwanza naomba jina la mpenzi lifutike mdomoni na
moyoni, mpenzi wako! Mpenzi wangu ni mmoja tu,
Cecy.”
“Kumbuka kabla ya Cecy nilikuwepo miye.”
“Kuna mtu aliye mpenzi wa moyo wako si mwingine
bali Hans si Colin.”
“Colin, Hans amefungwa siyo mpenzi wangu
mwenye nafasi hiyo ulibakia wewe peke yako.”
“Mimi ulinipenda lakini Hans ulimpenda zaidi kwa
hiyo ndiye chaguo sahihi la moyo wako si mimi.
Nami wewe nilikupenda lakini Cecy nilimpenda zaidi
naye ndiye aliyenipenda kuliko kiumbe chochote
kilichopo chini ya jua. Malaika sijawaona ninaamini
hata wao ningewaona wasingeuzidi uzuri wa Cecy.”
“Wewe Colin acha kukufuru Cecy ana uzuri gani
kumshinda malaika?”
“Malaika ulishamuona?”
“Sijamuona lakini nasikia mzuri sana.”
“Basi uzuri wao haufiki kwa Cecy, kwa vile
ulichokitaka kimefanikiwa naomba uachane na
mimi.”
“Colin nimefanya nini?” Mage aliuliza huku akilia.
“Unajua umeniumiza mara ya kwanza hukutosheka,
umeniumiza kwa mara ya pili bado hujaridhika
naona imebakia roho yangu tu.”
“Colin usiseme hivyo unaniumiza?”
“Ulitaka tufe sote lakini nakuhakikishia Cecy
atapona na atarudi tufunge ndoa hata kama Cecy
atakufa nitafunga ndoa na maiti ya Cecy si
mwanamke mwingine.”“Colin usiseme hivyo, Cecy
akifariki siyo mwisho wa dunia maisha yataendelea,
nina imani hakutakuwa na mwanamke mwingine
atakayechukua nafasi ya Cecy bali mimi.”
“Ninachokisema hakitafutika moyoni mwangu, Cecy
ndiye mwanamke wangu wa maisha nawe msubiri
Hans mfunge ndoa au nenda mkafungie ndoa
gerezani.”
“Kwa nini Colin unanichukia hivyo?”
“Sitakusamehe mpaka nakufa naomba utoke nje,”
Colin alisema kwa sauti ya juu.
“Colin ukikataa najiua.”
“Kajiue kwani ukifa mimi napungukiwa nini labda
muuaji mwenzio Hans.”
Maneno yale yaliuchoma moyo wa Mage ambaye
alikuwa na matumaini ya kuchukua nafasi ya Cecy
ambaye aliamini kupona kwake ni asilimia ndogo
sana na hata akipona hataweza kuwa sawa.
Kutokana na maelezo ya kidaktari aliyemfuata
baada ya Cecy kupelekwa India.
Alimueleza kuwa kama atapona angeweza kuwa na
tatizo la kusahau au kupoteza kumbukumbu
ambapo huwa sawa na kichaa cha kipindi kama
maji kupwa maji kujaa kuna wakati inakaa sawa
kuna wakati inahama.
Baada ya kuumizwa na maneno ya Colin
yaliyomkatisha tamaa alitoka nje akilia kilio cha
kwikwi kitu kilichomshtua mama Colin aliyekuwa
amekaa sebuleni akisoma Biblia.
“We, Mage unalia nini, Colin kazidiwa?”
“Ha..ha..pana mama, Colin kanifukuza eti hataki
kunioa.”
“He! Kwa sababu gani?”
“Hata sijui, yaani anasema yupo radhi kufunga ndoa
na maiti ya Cecy kuliko kunioa mimi. Eti mama,
siombi ila kwa bahati mbaya Cecy amekufa
mwanamke wa kuolewa na Colin kuna mwingine
zaidi yangu?”
“Hakuna.”
“Sasa kwa nini ananidhalilisha kwa maneno
makali?”
“Labda umemkuta leo hayupo vizuri.”
“Mama naomba kama Cecy atakufa basi nafasi
yake nipewe mimi kwa vile tunajuana vizuri,
inawezekana kufungwa kwa Hans na hii ajali ilikuwa
mpango wa Mungu kuirudisha harusi yetu
iliyofungwa mbinguni.”
“Mmh! Makubwa,” mama Colin aliguna maneno ya
Mage.
“Mama naomba ukazungumze na Colin, si ulisema
anatakiwa kupelekwa hospitali kila asubuhi, kazi
hiyo nitaifanya mimi hata kumpikia chakula na
kumfulia kipindi chote nitafanya mimi. Nipo tayari
kuhamia hapa kuhakikisha Colin hapati tatizo
lolote.”
“Basi tulia nitazungumza na Colin.”
Mama Colin alikwenda chumbani kwa Colin ili ajue
kimetokea nini mpaka apishane kauli na mpenzi
wake wa zamani.
Alimkuta Colin amejilaza macho kaangalia juu,
mlango ulipofunguliwa aligeuza shingo kuangalia
nani anayeingia alimkuta ni mama yake.
“Vipi baba?” mama yake alimuuliza.
“Safi tu,” alijibu akiwa bado ameangalia juu.
“Upo sawa baba?”
Itaendelea wiki ijayo!
 
Nataman Colin abak na msimamo wake asikubal kurudi kwa mage kabisa
 
ILIPOISHIA:
“Vipi baba ?” mama yake alimuuliza .
“Safi tu ,” alijibu akiwa bado ameangalia juu .
“Upo sawa baba ?”
“Sipo sawa,” alijibu akiwa bado macho yake yakiangalia darini.
SASA ENDELEA...
“Kwa nini tena mwanangu ?”
“Nani kampa ruhusa huyu shetani kuingia ndani?” aliuliza huku akigeuka kumtazama mama
yake.
“Colin ! Shetani nani ?”
“Mage , sitaki kumuona machoni mwangu, ” alisema kwa sauti ya juu kidogo.
“Kwa nini baba ?”
“Aliyonifanyia madogo , leo ni Mungu tu nipo hai lakini kifo changu angechangia yeye hata
mateso ya mpenzi wangu chanzo ni yeye . Kaniumiza mara ya kwanza hajafurahi karudia mara
ya pili kaniumiza na mpenzi wangu bado tu ananifuata anataka nini kama siyo uhai wangu?”
“Lakini kwa nini unamhukumu bila kujua ujumbe alioandika umeandikwaje ?”
“Mama , ulikuwa mbaya , Cecy hawezi kulia kwa ujumbe wa kawaida .”
“Colin bado hutakiwi kumhukumu kwa kitu usichojua , inawezekana ulikuwa wa kawaida lakini
kwa vile mpenzi wako alishajenga chuki kwa Mage huenda hakufurahia ujumbe ule .”
“Lakini mama hata kama , ni haki mtu kutuma ujumbe au kupiga simu akijua kabisa mimi ni
mchumba wa mtu na tupo katika hatua gani ?”
“Hapo anaweza kuwa amefanya makosa lakini hakuna adui wa maisha , adui wa leo rafiki wa
kesho , msamehe mwenzio nimemwacha analia kwa maneno yako makali .”
“Mama nitamsamehe Mage labda Cecy apone asipopona sitamsamehe mpaka nakufa. ”
“Sikiliza mwanangu , ni wazi Mage anakupenda sana hujui tu , kama Mungu anapitisha uamuzi
wake, Cecy anafariki Mage ndiye mwenye nafasi ya kuwa mkeo . ”
“Mama kwa nini unakimbilia kufa mpenzi wangu, nataka nikuambie kitu . Cecy akifa nitafunga
naye ndoa kabla ya kuzikwa .”
“Wee Colin umerogwa ? Yaani ufunge ndoa na maiti, ili iwe nini ?”
“Kutimiza ahadi niliyomuahidi Cecy ambayo ndiyo ndoto yake kubwa kwangu ya kuwa mke
na mume . Mama Cecy nampenda lakini yeye ni mwalimu wangu wa mapenzi ndiye wakili wa
moyo wangu kanipigania wakati wote kuonesha ana mapenzi ya kweli kwangu Cecy
hanipendei kitu bali mimi kama mimi . ”
“Mmh ! Na ukishamuoa ?”
“Nitaendelea kuwa muaminifu katika ndoa yangu mpaka mauti yatakaponichukua.”
“Kwa hiyo huoi tena ?”
“Mama ndoa ipo moja tu ikishafungwa duniani mpaka mbinguni haitafunguliwa .”
“Sasa kama amekufa si ndiyo mwisho wa ndoa yenu .”
“Kwangu itakuwa mwanzo kwa vile sijaitumikia ndoa yetu . ”
“Colin mwanangu upo sawa?”
“Tena akili zangu zipo timamu .”
“Hebu pumzika naona kama haupo sawa .”
“Mama wala usisumbuke kufikiria unavyotaka kufikiria sina jibu zaidi ya hilo nililokupa.”
“Kwa mfano Cecy atarudi hayupo sawa na ugonjwa wake hauponi au amepooza utafanya
nini ?”
“Kama nitaweza kufunga ndoa na mwili wake usiyo na pumzi sitabadilika, nitafunga ndoa na
Cecy katika hali yoyote. ”
”Mmh ! Sawa .”
Mama Colin alitoka bila kuongeza neno huku akijiuliza Mage kamfanya nini Colin mpaka
kufikia uamuzi mzito kama ule . Lakini aliamini zile ni hasira za kumwona Mage lakini baadaye
zitashuka na kuelewana.
Aliamini kabisa ugonjwa wa Cecy si wa kupona na kama akipona hatakuwa sawa hivyo
mwanamke aliyeona anamfaa mwanaye ni Mage kwa vile tayari walishakuwa wapenzi kabla ya
hapo.
Mage baada ya kutokeza , mama Colin alikaa mkao wa kutaka kujua amezungumza nini na
mwanaye .
“Vipi mama , Colin kasemaje ?”
“Hii kazi niachie mimi , najua bado ana hasira zikipoa atanielewa tu .”
“Yaani mama siamini maneno yake anataka kuoa maiti ya Cecy kwani wanawake
wamekwisha? Hata kama hanitaki mimi lakini bado wapo wazuri na wenye tabia nzuri kuliko
Cecy .”
“Hilo lisikutie presha, nammudu kwa vile ni mwanangu na wala hataoa mwanamke mwingine
zaidi yako. Ninyi mnafahamiana na vile mlikuwa mnapendana hivyo mtaendelea
mliposimamia.”
“Umeona eeh mama , yaani Colin namshangaa kweli .”
“Sasa sikiliza kesho anatakiwa kupelekwa hospitali kwa mazoezi njoo asubuhi umpeleke. ”
“Mamaa ! Kwa hali hii atakubali ?” Mage aliishangaa kauli ya mama Colin .
“Mage we njoo mimi nitajua nitafanya nini , nakuhakikishia lazima utaolewa na mwanangu .”
“Mmh ! Mama nitafurahi, bado naona kama nipo ndotoni.”
“Wala si ndotoni, amini Colin wewe ndiye mkewe .”
“Nashukuru sana mama , basi nikuache niwahi nyumbani . ”
“Hakuna tatizo msalimie mama yako .”
“Salamu zimefika.”
Mage aliagana na mama Colin na kurudi nyumbani kwao huku dua zake zikiwa kwa Cecy
asirudi hai ili aichukue nafasi ambayo aliamini ilikuwa yake hapo awali .
Je nini kitaendelea ? Usikose toleo lijalo
 
Hivi katika hii hadithi kuna mahali mwandishi alidokeza kuwa huyu mama collin ni mchawi?
 
Back
Top Bottom