ILIPOISHIA...
Kutoka Masaki mpaka chuoni tayari walishakuwa wapenzi! Lilikuwa tukio jipya kwa Lilian. Bado aliendelea kuwaza kuhusu burungutu la pesa alizopewa na Pam! Big akaondoa gari Leila akiwa pembeni yake.
Range Rover ya Pam ikaunguruma, akaingiza gia namba moja, akakanyaga mafuta!
Ikapepea!
SASA ENDELEA...
GIZA nene lililokuwepo lilizimwa na mwanga wa taa zilizokuwa katika majengo mbalimbali chuoni hapo. Pembeni ya kituo cha daladala, kulikuwa na Hosteli za Hall 5 chuoni hapo, jengo hilo lilikuwa na taa nyingi zilizowaka kwa mwanga mkali.
Sinema ya Leila ni kama ilikuwa imekwisha. Leila aliondoka zake na Big, likiwa jambo jipya kabisa kwa Lilian aliyebaki anakodoa macho.
Sasa walibaki watatu; Lilian, Latifa na Lucy. Latifa ndiye aliyekuwa kwenye gari la Big pamoja na Leila. Yeye ndiye aliyekuwa na majibu ya maswali ya Lilian.
Vipi tena mwenzetu? Lilian akamwuliza Latifa.
Mwenzangu hata mimi nashangaa.
Unashangaa nini?
Mi niliwaona wanazungumza muda wote, kuna wakati Leila alikuwa akimlalia sana Big, tulipofika hapa akakataa kushuka. Sasa huwezi kubishana na mtu mzima mwenye akili zake, akasema.
Wote wakaungana naye.
Kwa hiyo amekwenda kulala naye? Lilian akauliza.
Unauliza swali gani hilo la kitoto?
Poa, tuondokeni, akasema Lucy.
Lilian hakujua kuwa wenzake walikuwa wakimshangaa yeye kwa kuwa kila kilichofanyika, hapakuwa na jambo la ajabu. Yalikuwa mambo ya kawaida sana kwao.
Waliongozana hadi chumbani mwao, wakaingia na kufunga mlango. Hapo sasa ndipo Lucy alipomwuliza kuhusu bahasha aliyokuwa amebeba...
Vipi? Lucy akamwuliza huku akiangalia ile bahasha kwa uchu.
Amenipa, amesema zitanisaidia lakini nina wasiwasi sana kwa kweli. Hawezi kuwa anatumia gia hiyo kunishawishi kimapenzi? Lilian akamwuliza Lucy.
Wasiwasi wako tu, hawa ndiyo watu wa mjini wenye fedha zao, jifunze kula na kipofu, acha ushamba bwana!
Mh! Haya bwana.
Pamoja na kwamba mvinyo aliokunywa ulikuwa ukimpeleka puta, akili yake ilikuwa ikifanya kazi kama kawaida. Kuna taa nyekundu ziliwaka kichwani mwake juu ya Pam.
Nitaona mwisho wake! akawaza.
***
Mlio wa meseji ndiyo uliomshutua Lilian usingizini. Akaamka na kuichukua simu yake haraka. Akafungua ujumbe na kuusoma. Ulitoka kwa Pam.
Nilifurahi sana kupata wakati mzuri na wewe jana. Vipi umeamka salama?
Ilikuwa saa 2:30 asubuhi!
Mh! Mapema yote hii? Ina maana hana mke? Au labda ameshakwenda kazini. Lakini kwa nini anakuwa na spidi kiasi hiki? akawaza kabla ya kumjibu:
Nami pia. Ahsante kwa fedha kaka Pam.
Zile ni pesa ndogo sana kwa ajili ya kukusaidia, usiwe na wasiwasi kuwa huru kwangu. Nimekuambia nataka uishi kama malkia, sitaki uteseke!
Nashukuru kusikia hivyo Pam, ahsante sana.
Masomo mema.
Lilian hakuwa na kipindi cha asubuhi ya siku hiyo, alitakiwa darasani saa 8:00 mchana, hivyo hakuwa na sababu ya kuamka haraka hasa ukizingatia kuwa alikuwa na uchovu wa pombe wa jana yake.
Akaendelea kulala!
Simu ilimwamsha tena Lilian. Ilikuwa imeshafika saa 5 za asubuhi. Akajinyoosha pale kitandani kisha akaamka. Chumba chote kilikuwa tupu.
Lucy na Latifa walishaondoka chumbani hapo tangu saa tatu. Walielekea Baa ya UDASA kupata supu kwa lengo la kupooza mninginio. Hilo halikumshtua sana Lilian.
Alipochukua simu yake, alishangazwa na namba zilizoonekana kupitia kioo cha simu yake. Hazikuwa namba za kawaida. Zilionekana wazi kuwa za nje ya nchi.
Simu ilikatika akiwa bado anashangaa. Sekunde chache mbele, simu ikaanza tena kuita kwa mara nyingine. Mara moja Lilian akapokea...
Haloo, sauti ya Lilian ilitoka ikionyesha wazi mashaka aliyokuwa nayo.
Haloo! sauti ya upande wa pili ikasikika.
Hapakuhitaji akili nyingi kwa Lilian kugundua kuwa aliyekuwa akizungumza simuni alikuwa ni mpenzi wake Edo aliyepo Malaysia. Alishtuka sana lakini moyoni alifurahi.
Waooo baby, vipi za huko? Mbona umenisusa mpenzi? akasema Lilian akionekana kuwa na furaha sana.
Tena uishie hapohapo. Nilikuambia nini? Nilisema nikiondoka utabadilika na kweli hata wiki mbili hazijaisha tayari. Nashukuru sana kwa ujumbe wako. Naomba nikuhakikishie kuwa nimepata ujumbe wako na nimekubaliana na wewe.
Siwezi kulazimisha mapenzi mahali nisipopendwa. Najua umekutana na mwanaume mwenye fedha, lakini tambua kuwa, mapenzi ya kweli yapo moyoni na siyo mfukoni kama unavyofikiri. Nashukuru sana kwa kunipotezea muda wangu, lakini nakuahidi sitakutafuta tena.
Endelea na maisha yako na huyo unayemuona ana maana kwako. Ni vile tu hujajua. Ni vile hujafahamu maumivu ya mapenzi, lakini nataka kukuambia kuwa, moyoni mwangu nina maumivu makali sana. Moyo wangu unavuja damu, akasema Edo kwa sauti iliyoonyesha kujawa na maumivu makali moyoni.
Mbona sikuelewi Edo mpenzi wangu? Ujumbe wangu upi ambao nimekutumia? Sijakutumia ujumbe wowote mbaya!
Acha ujinga wewe, email zako zote nimesoma.
Email? Nimekutumia email ya namna gani hadi unaniambia maneno makali ya namna hiyo mpenzi wangu?
Nimemaliza na sitaki maswali wala mawasiliano na wewe tena. Acha nisome. Kwa heri, akasema Edo kisha akakata simu.
Lilian akachanganyikiwa! Akajiuliza sana kuhusu email anayosema Edo lakini hakukumbuka kitu. Alihisi kuchanganyikiwa. Alipojaribu kumpigia tena Edo, hakupokea.
Alirudia mara nyingi, bado hakupokea. Alishinda akilia mpaka muda wa kwenda darasani ulipofika. Alikaa kwenye kiti chake, macho yake yakiangalia mbele alipokuwa mhadhiri akifundisha, lakini hakuelewa chochote!
Mhadhiri aliyekuwa mbele yake, alikuwa kama kopo. Hakuelewa chochote. Kichwa kilimuuma mno. Mawazo yake yalikuwa kwa Edo tu. Hakuwa tayari kumpoteza mwanaume wa maisha yake!
Alijaribu kufikiri labda huenda kuna mtu amevujisha kuwa ameanza kutoka usiku na alirudishwa na mwanaume, lakini jambo hilo halikumwingia akilini mwake maana ilikuwa ndiyo mara ya kwanza, tena siku ya kwanza tu!
Aliwaza zaidi kuhusu email. Hilo ndilo lililomkosesha raha!
Kuna kitu kimejificha hapa, nitakijua tu! akajipa moyo.
Itaendelea....