ILIPOISHIA...
Hipsi zilikuwa kivutio kingine, mwisho ni milima ya haja iliyokuwa nyuma ya viuno yao! Hakika walifungasha. Kufungashia huko hakukuwa na maana kuwa walifanana na majimama, la hasha!
Milima yao iliendana kabisa na maumbo yao. Kwa mifanano ya maumbo walikuwa sawa, tatizo likawa kwenye tabia. Hasa kwenye maisha yao ya kimapenzi.
Leila na Lilian walikuwa na misimamo inayofanana. Leila alikuwa na mpenzi wake mmoja anayejulikana aliyeitwa Michael, maarufu zaidi kama Mike, Lilian yeye alitoka na Edo ambaye awali alikuwa akisoma naye chuoni hapo.
Latifa na Lucy wao habari zao zilikuwa nyingi! Hawakutulia na wanaume kabisa. Mikesha na kwenda klabu ilikuwa ndiyo michezo yao. Pamoja na yote hayo, bado wote kwa pamoja walikuwa na juhudi sana darasani na walikimbiza wenzao katika masomo yote.
Lilian alikuwa akitembea kwa pozi kama vile alikuwa akizionea huruma ngazi alizokuwa akitembea. Bado alishindwa kuondoa Edo kichwani mwake.
SASA ENDELEA...
ILIKUWA ndiyo kwanza siku ya pili inakatika baada ya kuagana na Edo. Hadi muda huo hakuwa na mawasiliano yoyote na Edo ingawa alimtumia waraka pepe tatu na zote hakujibu. Kwa mbali akawaona rafiki zake akina L wakiwa wamekaa kivulini wanajisomea.
Ni palepale pa siku zote!
Kwa kawaida walizoea kusomea sehemu moja. Lilian alikazana na kuwafikia. Lilikuwa kundi zuri sana la majadiliano kutokana na namna wote walivyokuwa na mtazamo mkubwa na uwezo wa kuelewa.
"Mambo zenu warembo?" Lilian akasalimia.
"Poa Lilian, vipi mwenzetu?" Leila alikuwa wa kwanza kuitikia salamu.
"Safi tu."
"Karibu mrembo, tunatengeneza maisha hapa, hatupo tayari kuendelea kunyanyaswa na wanaume, elimu ndiyo mkombozi wetu wa kweli," Latifa naye akasema.
"Kweli kabisa," akajibu Lilian kisha akaketi na kutoa vitabu vyake.
Jambo lililomshangaza ni kwamba, muda wote aliofika hapo, Lucy hakusema kitu chochote! Lilian hakumfikiria vibaya, aliamini ni masomo ndiyo yaliyokuwa yamembana. Akanyamaza kimya na kuanza kupiga kitabu.
Wote wakawa kimya!
Dakika tano baadaye, Lucy alionekana kuchukua bahasha kwenye begi lake la vitabu na kumkabidhi Lilian. Alipokea kwa mshangao. Ilikuwa bahasha ndogo kiasi lakini iliyonona. Ilionekana ndani yake kuwa na makabrasha muhimu ila yaliyojaa.
"Ni nini?"
"Utafungua baadaye."
"Kama ni bomu je?"
"Mh! Wewe naye, nani wa kukuwekea bomu sasa mtoto wa kike?"
"Niambie ni nini basi?"
"Mtoto una haraka sana wewe. Haya fungua!" akasema Lucy.
Lilian akafungua. Alikutana na burungutu la noti za elfu kumikumi!
Bahasha ilikuwa imejaa kiasi kwamba haikuwa rahisi kufungika vizuri.
"Zimetoka wapi?"
"Hapo sasa tutazungumza baadaye."
"Hapana Lucy, chukua pesa zako."
"Acha upuuzi wewe, lini utakuwa na akili? Huyo Edo unayemn'ang'ania, unajuaje kuwa naye hakusaliti? Kwanza sasa hivi hayupo nchini, una wasiwasi gani? Tumia urembo wako vizuri mtoto, la sivyo utabaki unang'aa macho tu mjini hapa," akasema Lucy kwa msisitizo.
Lilian hakuwa mtoto, alishajua kuwa zile fedha zilitoka kwa mwanaume. Kwa Lucy na Latifa, kubadilisha wanaume lilikuwa jambo la kawaida kabisa.
"Lucy tunaheshimiana sana mimi na wewe, kumbuka kinachotukutanisha hapa ni masomo tena ni kwa vile hili ni kundi letu la kujisomea na ni zuri. Tuishi kwa kuelewana na kuheshimiana.
"Ni vyema kila mmoja akaheshimu hisia za mwenzake. Kwanini unataka kunilazimisha nifanye kitu ambacho sikipendi? Chukua pesa zako," Lilian akasema kwa ukali sana.
"Sitaki, kama unaweza kuzichoma labda ufanye hivyo. Huo ushamba utakutoka lini? Kwani kula pesa ya mtu ndiyo kumkubali? Acha ujinga, kula maisha hayo, mambo mengine baadaye," akasema Lucy akijiandaa kuinuka.
Ni kweli aliinuka.
Alikusanya vitabu vyake na makabrasha mengine, akaondoka zake. Pale akawaacha Latifa, Leila na Lilian wakimshangaa.
Ama kweli alishangaza!
"Sikia shosti, kwani wewe umeomba hela?" akasema Leila.
"Ndiyo nashangaa!"
"Sasa huna haja ya kushangaa, chukua mzigo utumie. Ni nani anaweza kukufuata kukudai? Kwani umekopeshwa? Tumia lakini akikuambia mambo ya wanaume kataa," akasema Leila na kuungwa mkono na Latifa:
"Kweli kabisa, sioni tatizo."
"Wewe na yeye ni walewale tu!" akasema Leila.
"Jamani hebu tusomeni basi, kwani Lilian ni mtoto? Kwanini tunatofautina kwa mambo binafsi? Yeye ni mtu mzima na anaweza kuamua chochote kwa utashi wake," akasema Latifa.
Lilian alikuwa kwenye mzigo mzito wa mawazo lakini alipotafakari sana, hakuona sababu ya kukataa hizo fedha. Akaziweka kwenye mkoba wake na kuendelea kujisomea.
"Kibaya ni kumsaliti Edo, kama ni pesa sioni tatizo lake," akajisemea moyoni mwake akiendelea kujisomea.
***
Edo alifika jijini Kuala Lumpur, nchini Malaysia salama kabisa. Alikuwa na maelekezo yote, hivyo haikuwa vigumu kwake kufika chuoni. Alipokelewa vizuri na kuelekezwa chumbani kwake kisha taratibu nyingine zikafuata.
Alikuwa mchovu sana kutokana na safari ndefu ya kutoka Tanzania hadi Malaysia. Siku tatu baadaye ndipo alipopata utulivu wa akili kidogo. Akiwa chumbani kwake, akakumbuka kuwasiliana na mpenzi wake.
Bado hakuwa na mawasiliano ya simu ya mkononi, simu alikuwa nayo lakini alikuwa bado hajapata usajili wa namba kutoka moja ya kampuni za simu nchini humo.
Alifungua laptop yake na kuingia kwenye akaunti yake ya waraka pepe. Alikutana na ujumbe kutoka kwa watu wengi sana, akiwemo Lilian ambaye alimwandikia mara tatu. Akaanza kusoma mmoja baada ya mwingine.
Hello,
Edo. Najua umefika salama mpenzi wangu. Pole na safari baba. Napenda kukuhakikishia kuwa, moyoni mwangu umejaa wewe pekee na hakuna nafasi ya mwingine zaidi yako. Nakupenda sana.
Ukipata ujumbe wangu, tafadhali unijibu.
Lilian.
Edo akavuta pumzi ndefu sana kisha akazishusha taratibu kabisa. Akatulia kwa muda. Baadaye kidogo akafungua ujumbe unaoufuata.
Ujumbe huo ndiyo uliomshtua sana moyo wake. Aliuma meno kwa nguvu, akarudi kuangalia jina na anwani ya mtu aliyemtumia ili ajiridhishe kuwa Lilian ndiye aliyemtumia.
Ni kweli alikuwa ni Lilian!
Akazidi kuchanganyikiwa!
Itaendelea…