Hisia Zangu – 11
ILIPOISHIA...
LILIAN alikuwa akimsifia msichana aliyekuwa ndani ya kioo mbele yake. Alikuwa akiangalia taswira yake mwenyewe kwenye kioo. Hakuwa na shaka kuwa, eneo lote la Mlimani City, jioni hiyo kusingekuwa na mwanamke mzuri aliyependeza kama yeye!
Mara simu ikaita!
Ni Pam alikuwa anampigia!
Akapokea...
"Nimeshafika mama, upo tayari?" Pam akamwuliza.
"Bila shaka, dakika mbili tu nitakuwa hapo barabarani," akasema Lilian kisha akakata simu.
Mara moja akatumbukiza miguu yake kwenye viatu virefu kiasi. Akachukua mkoba na kuubamiza mlango!
Akatembea kama Twiga!
Sasa endelea...
Ni saa 10:00 alasiri, muda ambao kipindi kilikuwa kimemalizika. Kama walioambiana, Lucy na Latifa walitoka kwa pamoja darasani. Wakashuka ngazi taratibu wakianza kutembea kuelekea hosteli.
Tangu wanatoka darasani mpaka wanafika barabara kubwa ya lami, hakuna cha maana walichozungumza zaidi ya stori za hapa na pale.
Lakini baadaye, Latifa akaamua kuvunja ukimya. Akaanza kumzungumzia Lilian...
"Vipi mwenzangu, ulimuona Lilian alivyotoka darasani?" akauliza akionekana kuwa na shauku ya kusikia jibu kutoka upande wa pili.
"Nilimuona sana."
"Unadhani ana nini?"
"Anajua mwenyewe lakini kwa vyovyote vile, mapenzi ya Pam yatakuwa yameshaanza kumkolea. Unafanya mchezo na pesa?"
"Lakini kweli..."
"Si unamuona Leila, si alijifanya mjanja na mwenye msimamo, yuko wapi sasa? Si aling'ang'ania kuondoka na Big jana. Kuna mjanja kwenye pesa?" akasema.
Wote wakacheka!
Ilikuwa dili!
Kwao ilikuwa furaha, maana fedha ilikuwa inaingia kama kawaida.
"Lakini Pam amenitumia ujumbe nikiwa darasani," Lucy akasema.
"Amesemaje?"
"Mambo mazuri, leo ana mtoko na Lilian. Watajuana wenyewe. Unajua ninachompendea Pam, hana papara na anajua anachokifanya."
"Kweli kabisa."
"We subiri, siku mbili hizi usikie kama utamsikia Lilian akizungumza habari za Edo tena. Kila kitu kitafunikwa na fedha za Pam, niamini mimi."
"Kwa nini nisiamini wakati dalili zinaonekana wazi?"
"Umeanza kuwa mjanja sasa, unaona maneno hayo?"
"Wewe! Kwani tangu lini nikawa mshamba?"
"Haya bwana, ratiba ya leo vipi?"
"Kiukweli sitaki hata kujichosha sana. Tukapumzike, usiku twende tu hapo Udasa tukale mbuzi choma na ndizi, kisha tushushie na wine, nadhani itakuwa poa!"
"Sawa."
Wazo likapita!
Fedha kwa wasichana hao ilikuwa jambo dogo sana. Walikuwa na uhakika wa kufanya chochote bila kutegemea fedha zinazoingizwa kwenye akaunti zao na serikali kwa ajili ya matumuzi ya kawaida.
Walitumia usichana wao kujipatia fedha na kufanya kila aina ya anasa za mjini. Ni jambo moja tu walijua, pamoja na yote hayo, vichwani mwao walikuwa na madini ya ajabu.
Walikuwa wakifanya vizuri sana kiasi kwamba, wengine waliamini walikuwa wakitoa rushwa ya ngono kwa wahadhiri ili wawafaulishe. Haikuwa hivyo.
Ukweli ni kwamba, walijua vizuri kujisomea na kujadiliana katika kundi lao. Cha kushangaza ni kwamba, hawakutaka mtu yoyote aungane nao kwenye kundi zaidi ya wao wanne tu; Leila, Lucy, Latifa na Lilian.
Ndivyo msimamo wao ulivyokuwa!
***
Hakutaka lakini alijishangaa akitaka kuingia kwenye anwani pepe yake. Hiyo ni baada ya kuamua kujisomea kwa nguvu na kuachana kabisa na mawazo ya Lilian.
Edo alishaamua kuachana na mambo ya mapenzi. Kichwani mwake aliamini kuwa, Lilian hakuwa mwanamke sahihi kwake, hivyo alijipa muda kutafakari na pengine kutafuta mwingine ambaye angekuwa na penzi la dhati.
Lakini sasa uamuzi huo aliupinga ghafla. Kuna kitu alihisi kikizunguka kichwani mwake. Alitakiwa kujiridhisha tena kupitia maandiko yale kwenye email yake.
"Lilian anaweza kunitusi mimi? Anaweza kunikejeli? Napata shaka na jambo hili. Kuna kitu kipo nyuma kinafanyika. Kipo, naamini kipo," akawaza.
Muda huo huo akafungua email yake, kisha akaenda kwenye ujumbe wa mwisho kutoka kwa Lilian. Kwa uchungu moyoni, akarudia tena kuusoma. Sasa aliamua kusoma kwa sauti kabisa.
Hakuna kilichobadilika. Maneno yalikuwa ni yaleyale. Alihisi kupasuka kichwa kwa mawazo. Akapata wazo lingine la haraka. Alitakiwa kuzungumza na Lilian muda uleule ili amwulize vizuri kuhusu email alizokuwa akimtumia.
Ni Lilian pekee ndiye angemaliza utata uliokuwa umemzunguka kichwani mwake. Akachukua simu yake mezani kisha akampigia. Simu ikaita kwa muda mrefu sana, lakini haikupokelewa!
Akarudia kupiga kwa mara nyingine, bado haikupokelewa!
"Shiiiiit!" akasema kwa sauti na kuishusha simu hiyo kwa hasira.
Hakuweza tena kuendelea kusoma, alibadilisha nguo, akavaa suti za michezo, akatoka na kwenda uwanjani kwa ajili ya mazoezi ya viungo.
***
Alifungua mlango na kuingia ndani ya gari. Alikutana na tabasamu pana lililodhihirisha fedha kutoka kwa Pam. Lilian akakaa, huku akijishangaa namna woga ulivyoanza kumuondoka kwa kasi.
"Karibu mrembo!" Pam akasema.
"Ahsante. Pole na kazi."
"Nashukuru, nawe pole kwa masomo."
"Ahsante sana. Siku yangu haijawa nzuri sana leo, kichwa kimekuwa kizito sana."
"Usijali, amini kwamba utaimaliza siku vizuri sana."
"Nashukuru Pam."
Gari likaungurumishwa!
Walikuwa wanaelekea Mlimani City. Hapakuwa mbali, dakika tatu tu Pam alikuwa anaegesha gari kwenye maegesho eneo hilo. Akashuka, kisha akazunguka upande wa pili haraka na kumfungulia mlango Lilian.
Akashuka!
Wakaongozana hadi Samaki Samaki. Wakapata chakula cha jioni kisha vinywaji vikafuata. Kwa mara ya pili Lilian alikunywa mvinyo. Kidogo alianza kuuzoeazoea!
Hawakukaa sana, saa nne usiku, Pam alimrudisha Lilian chuoni. Akiwa ameegesha gari nje ya jengo la hosteli anayoishi, Pam alitoa bahasha na kuchomoa maburungutu matatu ya fedha na kumkabidhi.
Zilikuwa milioni tatu!
Lilian akasita kupokea.
"Chukua tu!"
"Hapana Pam. Kwa nini unanifanyia yote haya? Hebu niambie ukweli, unataka nini kwangu?" Lilian akamwuliza.
"Unataka kujua ukweli?" Pam akamwuliza akiwa amemkazia macho.
"Ndiyo niambie ukweli Pam, kuwa wazi..." akasema Lilian akionekana kukolea kwa kilevi kidogo.
Itaendelea ...