MAISHA YANGU NYUMA YA PAZIA JEUSI
SEHEMU YA 12
Ilipoishia….
“anhaa nimekumbuka, jana kuna kijana hakwenda kutalii sasa inawezekana yeye anampenda sana huyo mvulana kiasi kwamba ameshindwa kwenda kutalii ili tu amuone hotelini huyo mvulana ambaye ni kipenzi cha roho yake kwa sasa. Kweli kabisa, hili ni jibu sahihi maana mapenzi yana ngu…..” kabla sijamaliza kuongea nilistuka kimiminika cha moto kikitua sehemu za usoni, kifuani na baadhi ya sehemu za tumboni. Kimiminika hicho kiliniunguza katika ni mwili wangu. Alikuwa ni Jennifer, Jennifer aliniwagia chai, kisha akasimama na kuanza kupiga hatua kutoka katika eneo lile. Na mimi bila kufikiri mara mbili nikanyanyuka na kuanza kumfuata kwa nyuma kwa kasi kubwa. Baada ya muda mchache nilimfikia kisha nikampita na kumzuia kwa kusimama mbele huku nikiwa nimemkazia jicho isivyo kawaida. Jennifer naye alisimama huku akinitizama kwa jicho hasira.
Endelea……
“Jennifer, a.k.a. malkia wa nguvu. Msichana jasiri kuliko wote, lakini imekuwaje leo unanikimbia?” nilimwambia Jennifer kwa sauti ya chini lakini ambayo ilikuwa inasikika vyema. Jennifer alitaka kuondoka kwa kujaribu kupita pembeni yangu lakini nikamzuia “ngoja kwanza wewe, jibu maswali yangu. Inakuwaje leo unanikimbia? Au wewe si jasiri tena?” niliendelea kumzonga. Eneo ambalo tulisimama lilikuwa ni kwenye korido iliyotenganisha vyumba hivyo niliamini kuwa watu wasingetuona kirahisi ikizingatiwa kuwa watu wengi hawakuwepo vyumbani mwao, hili lilinipa kujiamini zaidi.
“barry usitake kunivuruga, naomba uniache niende” alisema Jennifer kwa sauti iliyojaa mamlaka pamoja na vimelea vya hasira akidhani kuwa angefanikiwa kunitisha. Kitu ambacho hakujua kuwa siku hiyo nilikuwa Barry tofauti, siyo Yule Barry aliyemzoea.
“Funga domo lako wewe mtoto wa kike. Hivi unadhani unaweza kunifokea eeh!, sivyo? Mimi niliacha kwenda kutalii jana na leo ili nikuachie uhuru wewe. Sasa kwa kuwa leo umeamua kutokwennda na kubaki hapa hotelini basi ujue uko kwenye himaya yangu mimi. Hivyo, acha hicho kidomodomo na ukae kwa kutulia” nilionngea kwa madaha na kujiamini sana, nilikuwa najiona ni kama nyota wa kwenye filamu. “Kwanza hebu niambie, ni kwa nini hujaenda kutalii leo?” nilimuuliza.
“hayakuhusu” alijibu Jennifer huku akiwa amenikazia macho.
“hayanihusu!? Ubongo wako utakuwa umeshaanza kuoza ndiyo maana unasahau upesi sana. Nimeshakwambia kuwa hapa upo katika himaya yangu hivyo unatakiwa uwe mpole na ujibu maswali yangu kadri inavyotakiwa. Nambie, ulinimiss sana eeh, kiasi ukashindwa kuvumilia kutokuniona leo eeh, ndiyo maana ukaamua ubaki hotelini. Usione aibu bwana” niliamini hili lingemchokoza vya kutosha Jennifer.
Nikiwa bado nafikiri ni jinsi gani maneno yangu yalimgusa Jennifer, nilistuka napigwa makofi mawili mfululizo kwenye mashavu yote mawili. Nilipigwa na bumbuwazi, macho yakawa yanaona nyota nyota na vitu vingine visivyoeleweka. Wakati nikiendelea kusikilizia maumivu ya yale makofi, Jennifer aliondoka na kuanza kwenda chumbani kwake. Ghafla nilizinduka na kuamua kumfuata, kwa kuwa nilihisi kile nilichokuwa nataka kukifanya hakikuwa kimekamilika.
Nilitembea kwa kasi na kwenda kumzuia tena kwa kusimama mbele yake, mara hii nikimangalia kwa tabasamu mwnana. Nilipanga kumvuruga kiakili kwa kutumia mbinu zangu adhimu ambazo nilikuwa nikizitumia katika mazingira kama yale.
“sijali hata unipige makofi mangapi ila hadi unijibu hili. Jennifer, nambie…kwa nini umemua kubaki hotelini leo. Kum’miss mtu hakijawahi kuwa kitu kigeni bwana. Sema tu kama ulinimiss” nilimwambia Jennifer nikiamini ningechochea moto wa hasira zake, na ndicho nilichokuwa nakitaka.
“nikumiss wewe kama nani! Sijaenda kwa sababu wewe na madam Tricia mlinikera jana na vikao vyenu visivyo na maana. Vipi kuna kingine unataka kujua?” alinijibu Jennifer. Nadhani aliamua kunijibu ili kuondoa usumbufu. Baada ya kusikia hayo, nilisogea pembeni kuashiria kupisha aendelee na safari yake kwa kuwa niliridhika na kile alichokijibu. Kumpisha aende haikumaanisha kuwa kazi yangu ilikuwa imekamilika, ila ilikuwa inakaribia kukamilika.
Jennifer alianza kupiga hatua kwa mwendo wa wastani huku mimi nikimwangalia. Nilikuwa natafakari ni kwa jinsi gani ningeumaliza mchezo ule kiufundi zaidi. Baada ya sekunde chache za kufikiri nikapata suluhisho.
“jana ulikataa kupiga picha mimi nikiwepo kwa kuwa pengine unaamini huwa nakukera, nikaamua kuondoka na kukuachia uhuru na furaha yako. Leo umebaki hapa kwa madai kuwa mwalimu Tricia na yeye kakukera pia. Vipi kuhusu kesho, kesho kutwa, mwezi ujao, miaka mitano ijayo? Pengine utakuwa na kundi kubwa la watu ambao utakuwa unadai kuwa wanakukera. Utawezaje kuishi huku una watu wengi unawachukia? Na kwa nini wakukere wewe tu? Wewe ni nani hasa? Una nini cha ajabu hadi ujione wewe ni maalum kiasi hicho? Ni upumbavu mkubwa kumchukia mtu kisa tu hapendi kile unachokipenda wewe, au akiwa yupo tofauti na mtazamo wako. Maisha hayaendi hivyo Jennifer.” Nilisema basipo kumtazama. Lakini japo nilikuwa simtazami niliweza kutambua kuwa alikuwa amesimama akinisikiliza. Nilitambua hilo kwa kuwa sauti za viatu zilikoma wakati naongea. Niligeuka taratibu kutazama kama kweli alikuwa amesimama, ni kweli Jennifer alikuwa amesimama,na ni wazi alikuwa ananisikiliza.
Nilianza kupiga hatua taratibu kumfuata mahala alipokuwa amesimama, nikamfikia, nikasimama sambamba naye.
“Jennifer, unatakiwa kujifunza kuishi na watu walio kinyume na wewe kwa sababu kwenye hii dunia hatufanani. Ukiendelea na misimamo yako hiyo ya kijingajinga utapata tabu sana, saana. Mimi siyo mhuburi, ila hili ni neno langu kwako. Ukipenda lichukue na ukatafakari na kama hujalipenda fanya vile roho yako inapenda, kama kunizaba makofi mengine, kunitemea mate au vyovyote vile” nilihitimisha.
Baada ya mimi kumaliza kusema hayo, Jennifer alianza kupiga hatua kuelekea chumbani kwake. Alipofika alifungua mlango kwa kasi na kuufunga kwa spidi hiyo hiyo. Nilisimama mahala pale kwa muda kisha nami nikaenda chumbani kwangu. Baada ya kufika chumbani nilipitiliza moja kwa moja kitandani huku nikijaribu kutafakari tukio la siku hiyo kati yangu na Jennifer. Nilikuwa najaribu kung’amua ni kwa namna gani Jennifer aliuchukulia ujumbe wangu. Je, aliuona ni wa maana au aliuchukulia takataka kama alivyozoea. Ila baadaye nikahitimisha kuwa muda ungenipa majibu. Niliendelea kujilaza pale kitandani na jambo la kushangaza nikajikuta napitiwa na usingizi.
Nilikuja kustushwa na sauti aliyekuwa anagonga mlango. Nilijizoazoa na kwenda kuangalia ni nani alikuwa anagonga. Akili yangu ilinambia kuwa huenda alikuwa ni moja ya wahudumu wa hoteli alikuwa akihitaji kitu Fulani. Lakini makisio yangu yalikuwa tofauti kabisa kwa sababu yalikuwa tofauti na kile ambacho mimi nilikitarajia. Nilitoa macho kwa mshangao, sikuamini kile nilichokuwa nakiona.
“Jennifer, ni wewe!?” nilisema nikiwa namwangalia Jennifer usoni. Jennifer aliitikia kwa kutingisha kichwa. Alikuwa amesimama kwa utulivu sana. Baada ya muda kidogo, mshangao wangu ulipungua na nikarudi katika hali yangu ya kawaida. “nini tena kingine?, unataka kunipiga makofi mengine? Nambie” alimuuliza swali la kichokozi.
“samahani barry, naweza kuongea na wewe” alisema Jennifer katika sauti ambayo sikuwahi kuisikia kabla. Sauti ya utulivu na unyenyekevu.
“kweli maajabu hayawezi kwisha, leo Jennifer unaweza kusema samahani….hahahaha, ok sawa. Unataka kuongea kuhusu nini?” nilimuuliza.
“nataka kuongea kuhusu mimi na wewe” alisema Jennifer.
“kuhusu mimi na wewe!?....maajabu kabisa haya, lakini…ok, nikukute nje huko. Nakuja” nilimjibu Jennifer. Jennifer aligeuka na kuelekea kwenye korido iliyokuwa inaelekea nje kwa mwendo wa wastani. Nilibaki pale mlangoni nikimtazama huku nikitafakari jambo lile. alitembea hatua kadhaa, kisha akageuka, akanitazama, kwa kuwa hata mimi pia nilikuwa namtazama macho yetu yaligongana. Tulitizamana kwa sekunde kadhaa, kisha Jennifer akageuka na kuendelea kwenda. Niliendelea kumtizama hadi pale alipopotea kwenye macho yangu, nikafunga mlango na kurudi chumbani.
Kwa jinsi Jennifer alivyokuwa amevaa sura ya utulivu iliniwia viggumu kuelewa ni nini hasa kilikuwa kimempata. Msichana ambaye alitenda jeuri kadri ya vile alivyojisikia leo alikuwa anaomba kuonana na mimi kwa lugha ya kistaarabu kabisa. Moyoni mwangu nilianza kujiona mshindi kwa kufikiri kuwa huenda maneno yangu yalimchoma moyoni na kumfanya ahisi kuwa alihitajika kubadilika. Wazo hili lilikuwa na nguvu sana japo sikuweza kijihesabia kufanikiwa moja kwa moja kwa maana Jennifer alikuwa ni mtu ambaye haikuwa rahisi kumtabiri.
Nilitoka chumbani baada ya dakika kadhaa za tafakari, nikapiga hatua kuelekea nje ya jingo la hotel hiyo ambapo kulikuwa na sehemu za kupumzika ambapo kimsingi ndipo ambapo nilimwambia Jennifer anisubiri huko. Kila hatua niliyokuwa napiga ilinifanya nizidi kuwa na shauku zaidi ya kufahamu ni nini hasa alitaka kuniambia.
Nilifika kwenye lango kuu la kuingilia na kutokea kwenye hoteli hiyo, nikaangaza macho yangu huku na kule ili niweze kuoa ni wapi alipokuwa amekaa Jennifer. Baada ya sekunde chache za kuangaza nilifanikiwa kumwona. Nikaanza kupiga hatua kwa mwendo wa wastani huku kichwa changu kikijaribu kuandaa maneno ya kuongea kulingana na hali ambazo zingeweza kutokea katika maongezi yangu mimi na Jennifer.
Nilipofika nikakaa pembeni yake huku nikiwa namtizama. Nilifanya hivyo ili angalau niweze kung’amua ni nini hasa pengine alipanga kuniambia. Jennifer alikuwa bado katika uso ule ule ambao nilimwona wakati alipokuja kunigongea chumbani kwangu, uso uliojaa unyenyekevu na utulivu.
Baada ya kukaa nilisubiri yeye aanza kuongea alichokitaka, lakini cha kuchangaza alibaki kimya. Ukimwa ulitawala kiasi nikaona ni bora nianzishe mazungumzo mimi mwenyewe, japo sikupenda iwe hivyo.
“nakusikiliza” nilitamka neno hilo moja ili kumpa nafasi yeye aanze kuongea alichokitaka. Tofauti na matarajio yangu, Jennifer bado aliendelea kuwa kimya pia hakuwa akiiangalia. Muda wote macho yake yaliangalia mbele ambako hakukuwa na kitu chochote cha maaana kiasi cha kuvuta makini yake. “kama huwezi kuongea niambie mimi niondoke” nilisema baada ya kuona kuwa alikuwa bado kimya licha kumpa nafasi ya kuongea.
“barry sijui hata nianzie wapi?” alisema Jennifer pasipo kuniangalia. Ni kama nilianza kumwelewa ni nini hasa pengine alitaka kukisema ila alishindwa. Kwa kuwa sasa nilikuwa na uhakika kwa asilimia nyingi juu ya mawazo yake kwa wakati huo, niliamua kutumia mbinu mbadala ili kuharakisha mambo.
“sawa, ngoja mimi nirudi chumbani, ukishapata pa kuazia njoo, Nitakusikiliza” nilitamka maneno hayo huku nikianza kunyanyuka na kurudi tena ndani ya hoteli. Nilifanya vile si kwa kuwa nilitaka kurudi chumbani badi ilikuwa ni nja ya kumfanya yeye aonngee upesi. Nilianza kutembea kuelekea lango la kuu la hoteli huku masikio yangu yakiwa yanatarajia kusikia sauti ya Jennifer ikinizuia kuwa nisiende. Nilizidi kupiga hatua ila sikusikia chochote. Nilitaka kugeuka kumwangalia ili nione ni nini alikuwa anakifanya lakini nikaona kuwa kufanya hivyo kungefanya nionekane kuwa hata mimi nilikuwa najali sana kuhusu mazungumzo hayo. Kwa hiyo ili nionekane sikuwa najali chochote kuhusu yeye niliendelea kukaza shingo yangu ukelekea mbele huku nikiwa na shauku kubwa ya kugeuka.
Nilizidi kupiga hatua huku nikianza kuona kuwa plan yangu ilikuwa inaelekea kushindwa, maana Jennifer alikuwa kimya bado. Nilianza kujilaumu ni kwa nini nilitumia mpango huo kwa msichana kama Jennifer, msichana ambaye hakuwa akitabirika kwa lolote.
Baada kulikaribia lango kuu la hoteli masikio yangu yalisikia kitu ambacho kilifufua matumaini yangu tena. Nilisikia vishindo vya mtu akikimbia kuja katika uelekeo wangu. Nilihisi moja kwa moja huyo alikuwa ni Jennifer. Japo nilitaka kujiridhisha kama kweli alikuwa ni yeye, ila nikaendelea kushikilia kanuni yangu ya kutokujionyesha kuwa nilikuwa najali hivyo nilijikaza nisigeuke.
Kadri sekunde zilivyokuwa zinasogea ndivyo vishindo navyo vilizidi kunikaribia na hatimaye nikashikwa bega, nikasimama lakini bado sikutaka kugeuka. Nilisimama huku kichwa changu kikiwa kinatazama mbele bila kutetereka.
“barry, naomba unisamehe” alisikika akisema mtu aliyekuwa amesomama nyuma yangu. Kwa sauti yake niweza kumtambua. Kauli ile ilinishangaza sana. Ilinishangaza si kwa sababu ilikuwa ni kauli ya ajabu, bali ni kauli ambayo ilitoka kutoka katika kinywa cha mtu ambaye hakuwa na haiba ya kuweza kutamka kauli kama hiyo. Lakini licha ya mshangao wangu mkubwa nilioupata, nilijitahidi kuuficha ili usigundulike.
“kwa lipi?” nilimjibu pasipo mimi kugeuka.
“kwa yote ambayo yametokea kati yetu. Maneno yako ya leo yamenifungua mengi. Nimegundua ni wapi nilikuwa nakosea. Barry nisamehe” alisema Jennifer akiwa bado amesimama nyuma yangu.
“nilishakusamehe zamani sana, wala hukuwa na haja ya kuniomba msamaha” nilimjibu.
“kweli barry?” aliuliza jeniifer huku akisogea na kusimama mbele yangu na kufanya tusimame katika namna ambayo tulikuwa tunatazamana.
“kwani kuna gharama gani kumsamehe mtu? Mimi siyo kama wewe” nilimjibu huku nikimtazama. Baada ya kutamka sentensi hiyo, Jennifer aliruka na kunikumbatia kwa nguvu sana. Matukio yote haya yalinifanya nipigwe na bumbuwazi. Sikuwahi kufikiri kuwa ingetokea siku Jennifer angenikumbatia kama vile. Japo nilikuwa katika dimbwi laa mshangao, nilijitahidi kutoa ushirikiano kwa kuweka mikono yangu juu kwenye mgongo wake. Baada ya sekunde chache nilijitoa mikononi mwa Jennifer kwa kuwa eneo lile ilikuwa la wazi sana, tungeweza kuonwa na watu kirahisi kabisa.
“barry, shukrani sana, wewe ni mtu mwema sana. Kwa kuwa umenionyesha mapungufu yangu nakuahidi nitabadilika. Sitakuwa Yule wa zamani” alisema Jennifer akiniangalia usononi huku mikono yake ikiwa imeishika mikono yangu. Lilikuwa ni pozi ambalo lilifanya tuonekane I kama tuliokuwa katika penzi jipya.
“Hilo la kubadilika halinihusu, ubadilike, usibadilike, mimi sijali. Hilo ni juu yako mwenyewe hivyo huna haja ya kujiapiza mbele yangu” nilijibu jeniifer. Kauli hiyo ilikuwa ni mwendelezo kuwa kujifanya nionekane nilikuwa mgumu na sikuwa najali sana japokuwa nafsini mwangu nilikuwa na hisia tofauti kabisa, hisia za kufarijika kwa kuona juhudi zangu ngalau zilikuwa zimeanza kuzaa matunda.
“barry, ni lazima nijiapize mbele yako kwa kuwa wewe umekuwa muathirika mkubwa wa tabia zangu za ajabu. Hata hivyo nashukuru kwa kunionyesha nafasi sahihi kwa ajili yangu” alisema Jennifer.
“ok, vipi kuna lingine la ziada.? Maana nahitaji kwenda kupumzika” nilimwambia Jennifer huku nikijiandaa kuondoka. Nilifanya hayo yote kwa kuwa nilikuwa tayari nimehakikisha kuwa Jennifer alikuwa chini yangu kihisia, hivyo huo ulikuwa ni mpango wa kucheza na hisia zake ili azidi kujishusha zaidi.
“barry, huwezi kukaa na mimi japo dakika chache? Ningependa nitumie muda zaidi na wewe” alisema Jennifer. Na hicho ndicho hasa nilikuwa nakitarajia kutoka kwake. Alipita kwenye njia hiyohiyo ambayo mimi nilitaka apite.
“ni hivyo kumbe!, kwa hiyo mimi kukusamehe kunakufanya ujisikie una amri ya kuniamuru nifuate matakwa yako na niyaache yangu? Sivyo?” nilimuuliza swali la mtego kwa makusudi. Nilitaka azidi kuninyenyekea. Unajua katika haya maisha ukipata nafasi ya kutamba, tamba kweli kweli maana huwezi jua ni lini hiyo nafasi uliyonayo itakupotea. Hivyo kwa kuwa Jennifer kwa ridhaa yake mwenyewe aliamua kujiweka chini yangu, nilitaka kuitumia vyema nafasi hiyo.
“siyo hivyo barry, karibu muda wote ambao tumefahamiana hatujawahi kuwa na mawasiliano mazuri, hivyo nilikuwa napenda kama tutautumia muda huu kucheka na kufurahi pamoja ili kufuta kumbukumbu mbaya za nyuma zilizotokea kati yetu. Sio kama nakulazimisha barry, ni kama ukipenda na ukizingatia kuwa kwa kinywa chako mwenyewe umesema kuwa umenisamehe” alisema Jennifer. Ni kama na yeye aliniweka kwenye mtego wa kupima imani yangu juu yake. kitu ambacho alikuwa hakijui ni kuwa nilipanga kumshangaza.
Itaendelea…