MAISHA YANGU NYUMA YA PAZIA JEUSI
SEHEMU YA 11
Ilipoishia….
"Sikiliza barry, najua huwezi kukubali ila mi najua kila kitu. Tafadhali sana nakuomba siku ikifika nikuone na wewe. Ukiamua kujitenga sana na hata walimu nao watakutenga pia, watakuchukulia kuwa una kiburi. Kumbuka ulishawahi kufukuzwa ukaja siku ya mtihani wa taifa, hapa juzijuzi ukaharibu tena lakini nasikia mkuu wa shule alilimaliza kimya kimya na hapa kama ukigomea hii safari hakuna mtu mwingine atajishughulisha na wewe tena. Unaweza ona ni kitu kidogo lakini kitakuharibia sana. Anyway unaweza acha kwenda lakini kitakachokuja kukutokea huko mbeleni, utayakumbuka maneno yangu. Unaweza kwenda darasani" alisema mwalimu akiwa hana hata chembe ya utani. nilipata kigugumizi kidogo kuondoka, lakini nikafanya hivyo huku nikiwa nayatafakari maneno ya mwalimu Tricia.
nilipokaa na kufikiria zaidi niliona kuna ukweli flani hivi ndani yake na nikaona si vyema kama sitoenda. Siku zikasogea, mimi na wenzangu tukaanza kujiandaa na safari ya kwenda kutalii. Lakini kuna kitu kimoja ilikuwa kinanipa shida sana. Nilikuwa nawaza itakuwaje mimi na jennifer. maana kwa uchache ule ni lazima kuna mahali kungekuwa na muungano wa moja kwa moja na yeye lakini yeye tangu ile siku nimeomba msamaha darasani alionekana kuwa bado alikuwa na hasira na mimi japokuwa chanzo cha yale yote ni yeye. Sikujua ingekuwaje.
Endelea….
Ilikuwa ni siku ya jumatatu, saa kumi usiku tulipoanza safari ya kwenda kutalii. Ilikuwa inatulazimu twende kwanza kwenye kituo cha mabasi cha mkoa halafu tuchukue gari kutupeleka mkoa ambao mbuga hiyo ilikuwepo, halafu safari ya kwenda mbugani ndipo ingeendelea. Mwalimu aliyekuwa nasi alikuwa ni mwalimu Tricia. Safari ilianza, tukafika katika kituo cha mabasi mkoa tukapanda gari ambapo tiketi zetu zilikuwa zimekatwa siku kadhaa kabla siku ya safari. Kwenye gari nilikaa siti ya watu wawili pamoja na mwanafunzi mwenzangu aliyeitwa Jonas, mimi nikikaa upande wa karibu na njia ya katikati ya gari. Na upande wangu wa kulia baada ya kale kanjia alikuwapo Jennifer. Jennifer hakuwa na muda na mimi, nami sikuwa na muda na yeye.
safari iliendelea, wakati wote wa safari nilijitahidi sana kuonyesha kuwa sikujali kabisa uwepo wa Jennifer, pia hata yeye niliona alijitahidi kufanya hivyo. Saa nane na dakika zake tulifika mkoa tuliokuwa tunaelekea. Bila kuchelewa mwalimu Tricia alitafuta gari ambalo lingetupeleka kwenye eneo mbuga hiyo ilikuwepo.
Baada ya kufika eneo ambapo mbuga hiyo ya wanyama ilipokuwapo, tulipotiliza moja kwa moja kwenye hoteli iliyokuwa jirani na tulitafutiwa vyumba ambapo kila chumba kimoja kilichukuliwa na watu wawili isipokuwa mwalimu ambaye yeye alichukua chumba cha kwake peke yake. Na kwa kuwa tulikuwa wavulana sita na wasichana wanne, haikuwa ngumu kugawana vyumba.
Kwa kuwa tulikuwa tumechoka na safari, mwalimu alituambia kuwa kila mtu alitakiwa aende kujipumzisha ili kujiweka sawa na siku iliyokuwa inafuata. Mimi pamoja wavulana wenzangu tuliamua kwenda kupumzika sehemu ya nje ya hoteli tukipiga story za hapa na pale. Muda kidogo baadaye tulikula chakula cha usiku kisha tukapiga story kidogo kisha tukaenda kulala tukiisubiri kwa hamu kubwa siku iliyofuata.
Asubuhi na mapema tuliamshana ili kujiandaa na safari hiyo ya kutalii. Kila mtu alikuwa na shauku kubwa ya kuona wanyama na vitu mbalimbali kwenye mbuga hiyo. Hata mimi niliyekuwa sina mpango na safari ile niliingiwa na hamu kubwa kujionea yale tuliyokuwa tukitarajia kuyaona. Mara zote nilikuwa nawaona wanyama kwenye picha mnato na picha za video lakini saa chache ambazo zingefuata ningewaona live, shauku ilikuwa kubwa mno. Tulijiandaa kisha tukapata kifungua kinywa kwenye mkahawa uliokuwa ndani ya hoteli na baada ya hapo tukiongozwa na mwalimu wetu tukachukuliwa na kwenda moja kwa moja kwenda mbugani na tulipofika tulikaribishwa vizuri na wahusika kwa kutuelezea baadhi ya vitu vizuri ambavyo tungeviona katika mbuga hiyo.
Baada ya hayo taratibu za malipo zilifanyika. Baada ya malipo kukamilika, Mwalimu Tricia aliwauliza wahusika kama tungeruhusiwa kupiga picha eneo lile kabla hatujaanza safari ya kutalii, wakamjibu kuwa hakukuwa na tatizo, tungeweza kupiga picha kadri tupendavyo. Basi Madam Tricia alituambia tukusanyike ili tupige picha kwa kutumia simu janja yake. katika hili nilipaga kuhakikisha nakaa mbali na Jennifer katika kila picha ili kuepusha matatizo yasiyokuwa ya lazima.
Picha ya kwanza tulipiga katika mtindo wa selfie, ambapo mwalimu Tricia ndiye aliyekuwa kashika simu. Katika hiyo picha mimi nilikuwa nyuma kabisa huku Jennifer alikuwa mbele jirani kabisa na mwalimu. Baada ya picha kadhaa za selfie, tulipiga picha ya pamoja katika mtindo wa kawaida ambapo mmoja wa wafanyakazi wa hapo mbugani ndiye aliyetupiga hiyo picha.
“sasa nataka nipige picha na wale top three wangu kwanza halafu ndo picha nyingine zitafuata. Nadhani wanajijua” alisema mwalimu Tricia huku akionyesha uso wa tabasamu. Wanafunzi wengine walianza kusogea pembeni ili watuache sisi top three tupige picha na mwalimu. Tuliokuwa katika top three tulikuwa ni mimi, Jennifer na Karim. Lakini cha kushangaza nilimwona Jennifer pia akisogea pembeni pamoja na wanafunzi wengine kama vile naye pia hakutakiwa kuwepo katika hiyo picha.
“Jennifer, unaenda wapi? njoo tupige picha” alisikika mwalimu Tricia akimwambia Jennifer.
“samahani madam, siwezi kupiga hiyo picha” alisema Jennifer huku akiwa anakunja mikono yake kifuani. Ilikuwa ni asubuhi na mapema lakini niliona kuwa hali ya hewa ingeenda kuchafuka na huenda kuharibu safari hiyo ambayo ilikuwa na lengo la kutufanya tufurahie na kuburudika.
“kwa nini?”aliuliza madam Tricia.
“basi tu sitaki, labda barry atoke.” Alisema Jennifer kwa kujiamini kabisa. Japo nilikuwa namfahamu vema Jennifer kuwa alikuwa ni mtu wa kisirani lakini sikuwahi kutegemea kuwa angeweza kuonyesha chuki yake kwangu waziwazi katika eneo kama lile, eneo la ugenini ambapo tulikwenda kwa ajili ya kufurahia na kujifunza pia. Si mimi tu niliyeshangazwa na kauli yake, karibu kila mtu aliyekuwa pale alishangazwa, hasa madam Tricia na wale wafanyakazi wengine wa hifadhi.
“kwani ninyi watu mna shida gani? Eti barry kuna nini mbona siwaelewi” aliuliza mwalimu Tricia akiwa anageuza shingo yake kunitazama mimi.
“umeona madam, sikutaka kuja huku kwa sababu ya mambo kama haya.” nilimwambia mwalimu Tricia kwa sauti ya chini kidogo.
“kwa nini lakini nyinyi watu mnafanya hivi? Tumekuja huku kwa lengo la kufurahia uwepo wa raslimali adhimu katika nchi yetu lakini ninyi mnataka kuvuruga kila kitu! Jennifer hebu acha hayo mambo bwana. Lengo lako ni kutuaibisha sisi walimu huku ugenini ili tuonekane hatuwafundishi maadili mazuri? Ndivyo mnavyotaka tuonekane?” alisema mwalimu Tricia. Aliongea kwa sauti iliyobeba hisia za kukerwa na lile tukio.
“vijana, mmekuja kutoka huko kuja kufurahia na kujifunza vitu muhimu kuhusu utajiri wa raslimali ambazo nchi yetu imebarikiwa, tafadhalini sana msilivuruge hili. Hii ni sehemu ya kuonyeshana upendo na sio chuki, mmenielewa? Tafadhalini msimsumbue mwalimu wenu.” alisema mzee mmoja aliyekuwa moja ya watu waliotupokea.
“kweli kabisa, hii siyo sawa kabisa. Jennifer njoo tupige picha. Kuwa na staha japo kidogo tu.” alisema mwalimu katika kumuunga mkono Yule mzee. Jennifer ni kama hakuwa amesikia chochote. Aliendelea kusimama huku akiwa amekunja mikono yake kifuani huku uso wake ukionyesha sura iliyojaa kisirani kikali. Kiukweli jambo lile halikuleta picha nzuri kabisa.
“madam, samahani kwa hili lililotokea, lakini naweza kusema kitu kama ukiniruhusu” nilimwambia mwalimu. Tayari nilikuwa nimepata wazo ambalo niliamini kuwa lingeweza kutoa suluhisho la tatizo lililokuwa mbele yetu.
“unataka kusema nini barry?” aliniuliza mwalimu huku uso wake ukionyesha shauku kubwa ya kutaka kujua, shauku iliyochanganyika na kuchanganyikiwa.
“inaonekana uwepo wangu hapa unasababisha watu wengine wasijisikie vizuri. Kwa kuzingatia kuwa eneo hili ni eneo kwa ajili ya kuburudika, si vyema mtu mwingine akawa chanzo cha watu wengine kukosa furaha. Kwa hiyo madam, kwa ruhusa yako naomba nirudi hotelini ili wale wasiofurahia uwepo wangu wabaki na amani” nilitoa wazo langu ambalo niliamini lingetoa suluhisho.
“unasema nini wewe! Yaani mambo yenu binafsi yanataka kuharibu maana nzima ya safari hii. Barry, hauendi popote. Tutaambatana sote kwenda kutalii. Hakuna mtu yeyote atakayekosa kushiriki katika hili, nimemaliza” alisema mwalimu huku akiwa anaonyesha uso wa kukasirika. Sikumlaumu, kwa kile kilichokuwa kinaendelea alikuwa na haki ya kukasirika.
Wenyeji wetu ambao walitupokea na pia ambao ndio wangetutembeza katika mbuga hiyo ya wanyama walizidi kushangazwa na lile tamasha la bure ambalo lilikuwa likiendeea. Tamasha lile lilifanya tuonekane watalii kituko kabisa.
“kweli kabisa, hakuna mtu atarudi hotelini. Wote tutakwenda kutalii, sivyo jamani?” alisema dada mwingine ambaye naye alikuwa ni moja wa watu waliotupokea mahali hapo.
“ndiyo” wanafunzi baadhi walijibu kwa sauti ya wastani.
“hebu oneni, ndo kwanza hata safari haijaanza hali iko hivi, hakuna ajuaye ni nini kitatokea mbele. Ili kuepusha lolote baya, naomba nirudi nikapumzike hotelini” nilisema kwa kujiamini kabisa.
“oya mzee baba we potezea tu mwanangu, tumekuja ku’enjoy hapa sasa wewe ukirudi tena hotelini hiii tour itakuwa haina maana tena. We twende tu mzee” alisema Rashid, mwanafunzi mwenzangu ambaye tulikuwa wote kwenye tour hiyo.
“nakuelewa sana mzee baba, ila mwenyewe si unaona mzee. Ni wazi Jennifer hafurahii kabisa mimi nikiwepo. Wacha nigeuke hotelini, mtanisimulia nilichokiona pindi mtakaporudi. Mi sija’mind wala nini” Nilisema huku nikimpa tano Rashid na wanafunzi wenzangu wengine wa kiume kama ishara ya kuwaaga. Nilipomaliza nikamsogelea madam Tricia “madam naomba unisamehe sana kwa kutia doa tour hii, wacha nirudi hotelini ili angalau madoa zaidi yasijitokeze”.
Nilipomaliza kusema hayo sikusubiri jibu lake lolote, nilianza kupiga hatua kurudi hotelini. Palikuwa ni umbali mrefu kidogo ila sikujali. Nilitembea umbali wa mita kama thelathini hivi kisha nikageuka nyuma, niliona watu wote wakiwa wananitizama mimi, sikujali..niliendelea na safari.
Nilipofika hotelini eneo la mapokezi nikaomba funguo ya chumba. Yule mhudumu aliniuliza ni kwa nini nilirudi mapema namna hiyo nikamjibu kuwa sikuwa najisikia vizuri hivyo nilirudi kumpumzika, alinipa funguo kisha nikaondoka kuelekea chumbani kwangu. Nilipofika chumbani, bila kufikiria chochote nilijitupa kitandani. Akili yangu yote ilianza kulifikiria tukio lilitokea muda mchache uliopita, nikajikuta najilaumu sana kwa kukubali kushiriki katika ile safari kwa maana kama nisingesafiri kama nilivyokuwa nimeazimia mwanzo, hayo yote yasingejitokeza.
Pia nilimfikiria sana Jennifer, msichana aliyekuwa na hulka ya ajabu sana. Msichana ambaye angeweza kufanya chochote kile ambacho alijisikia bila kujali ni nani alikuwa mbele yake. japokuwa mimi nilikuwa sitaki tena matatizo yoyote na yeye, lakini ilikuwa si chochote maana nilikuwa bado nashuhudia tabia zake za ajabu ambazo sikuwahi kudhani kuwa binadamu yeyote wa kawaida angeweza kuwa nazo.
Niliendelea kubadili kila aina ya pozi pale kitandani lakini hiyo haikusaidia kuniondolea mawazo niliyokuwa nayo. Dakika na masaa yalienda taratibu sana, taaratiibu saana. Nikatamani ningekuwa na uwezo nikimbize muda mbele ili muda wa kukaa huko uishe mapema kwa maana hakuna jambo lolote la maana ambalo niliona kuwa ningweza kulipata.
Kwa tabu sana jioni ilifika, nikatoka nje kupunga upepo. Baada ya dakika kama ishirini hivi, nikawaona wanafunzi wenzangu pamoja na mwalimu wakirudi hotelini. Walipofika tulisalimiana na wote kasoro Jennifer ambaye yeye alipitiliza moja kwa moja ndani ya hoteli. Tulipiga stori za hapa na pale wakinisimulia walichokiona huku nikijitahidi kukwepesha story za tukio lililotokea asubuhi. Baada ya dakika kama 45 hivi tulianza kutawanyika mmoja baada ya mwingine kwenda kuoga. Baada ya hapo tulipata chakula cha jioni, haya yote yalifanyika huku mimi nikijitahidi kujiweka mbali Jennifer kadri nilivyoweza.
Baada ya kupata chakula cha jioni tulienda kupiga stori na ‘wanangu’ eneo la nje ya hoteli hiyo. Katika kundi hilo tulikuwa watu wote isipokuwa jennifer, madam Tricia na msichana mwingine aliyeitwa Najma. hali hii ilinifanya niwe huru kidogo kwa maana jennifer hakuwepo. Wakati tukiwa tunaendelea na kupiga gumzo nilimuona Najma akija mahali ambapo tulikuwa tumekaa. Alikuja akatusalimia kisha bila ya kuchelewa aliniambia kuwa madam Tricia alikuwa akinihitaji. nilipatwa na mshangao kidogo, nikamuuliza kwani kulikuwa na nini, Najma alisema hata yeye hajui. Nilimwambia twende wote lakini alisema yeye harudi tena huko ila alinielekeza mahali ambapo madam alikuwa amekaa. Nikaona isiwe shida, nikachanganya miguu yangu kuelekea mahali ambapo najma alikuwa amenielekeza.
Wakati nafika mahali hapo nilimuona mwalimu akiwa amekaa na jennifer, kitu ambacho kilinipa shida sana wakati nasogea pale. Nilifika pale nikamsalimia madam pekee. Sikutaka kumsalimia Jennifer maana yawezekana hata asingejibu salamu yangu halafu ingeleta picha mbaya mbele ya mwalimu na kumfanya mwalimu azidi kutukasirikia. Nilimtupia jennifer jicho la wizi nikamwona na na yeye akiniangalia kwa jicho la wizi vilevile. Wezi tulikuwa tumekutana sasa.
"madam, nimesikia kuwa unaniita" nilimwambia madam ili aongee haraka niende, nipate nafasi ya kumuepa jennifer.
"ndiyo" alijibu madam.
"nakusikiliza madam"
"kaa kabisa maana hautoondoka sasa hivi” alisema madamu Tricia. Kauli ile ilinishtua si kidogo. Nikiwa sijui nini kinaendelea madam Tricia akaendelea “nilichokuitia hapa ni kuhusu mahusiano yako na jennifer. Kuna nini kinaendelea kati yenu? Ni nini chanzo cha ugomvi wenu?”
"sidhani kama ni ugomvi, ni kutokuelewana kwa kawaida tu madam. mimi sina ugomvi na jennifer" nilijibu kwa jinsi yakufanya mambo yaonekane madogo.
“barry, Jennifer..hebu oneni jinsi mlivyotutia aibu leo asubuhi. Mmefanya sisi sote tuonekane na watu wa ajabu kabisa. Hivi nini nini kinawasumbua nyinyi wawili?,eeh eti Jennifer, nini tatizo.? Je, ni masuala ya mapenzi? Eeh?” Aliuliza mwalimu Tricia.
“hapana madam, ila huyu mkaka huwa ananifuatilia sana, kila siku ananichokonoa chokonoa tu ili tu anikere, sijui ananitafuta nini. Kiukweli namchukia sana, silipendi kama nini” alisema Jennifer akionyesha ni wazi alikuwa anamaanisha kile alichokuwa anakisema. Kauli ya Jennifer ililenga kunibebesha zigo la lawama ili nionekane imi ndiye chanzo cha matatizo yote. Japokuwa nilitaka kujitetea mbele ya mwalimu ila nikaona ni bora kukaa kimya.
“Jennifer, kwani yeye alikufanya nini hadi unamchukia hivyo?” aliuliza mwalimu kwa sauti ya upole.
“anajua yeye alichokifanya” alijibu Jennifer kwa mkato. Jibu la Jennifer lilifanywa mwalimu Tricia anigeukie mimi.
“eti barry, ulimfanyaje Jennifer?” walimu aliniuliza.
“madam, binafsi sioni kama kuna umuhimu wowote wa kuzungumza mambo mwengi kuhusu hili jambo. Sikatai kuwa kulikuwa na kutokuelewana kati yangu na yeye, lakini kwa sasa mimi sina tatizo na yeye na wala sihitaji matatizo zaidi na yeye na ndiyo maana niliweza hata kumuomba msamaha mbele ya darasa zima lakini yeye hakutaka tuyamalize. Sasa kwa hali kama hiyo unadhani mimi nitafanyaje madam” nilisema kwa sauti iliyojaa utulivu mkubwa.
“Jennifer, barry alishawahi kukuomba msamaha mbele ya darasa? Kwa nini hukumsamehe? Kwa nini msimalize tofauti zenu?” mwalimu alimuuliza Jennifer maswali matatu mfululizo. Jennifer hakujibu chochote bali uso wake ulizidi kubadilika na kuonyesha hasira na chuki za wazi alizokuwa nazo juu yangu. “Jennifer, msamehe barry yaishe. Sijui ni nini kimetokea kati yenu lakini sidhani kama ni jambo kubwa kiasi kwamba hamuwezi kulimaliza. Jennifer, ninyi ni wanafunzi, tena wanafunzi wenye uwezo mkubwa sana darasani, ninyi mnatakiwa mshirikiane ili kuongeza chachu kwa wengine katika kuporesha taaluma yenu na ya wanafnzi wenzenu wengine.”
“pia hata hivyo, kuna maisha baada ya shule. Mkitoka hapa mnaweza kukutana tena huko kwingine nje ya shule, sasa kama mtashindwa kusaidiana katika shida mbalimbali huko mtaani. Tafadhali Jennifer, ni wazi naona barry yuko tayari kumaliza tofauti ambazo zipo kati yenu basi hebu msamehe yaishe” alisema mwalimu Tricia kwa sauti iliyojaa hisia za upendo na kujali. Alimtizama Jennifer huku usoni wake ukionyesha matumaini kuwa huenda Jennifer angeuelewa ujumbe huo na kuufanyia kazi haraka.
Kinyume na matarajio ya mwalimu na hata mimi pia, Jennifer alinyanyuka na kuondoka pasipo kusema kitu chochote. Mwalimu alijaribu kumuita lakini hakugeuka, aliendelea kupiga hatua hadi alipopotea mbele ya macho yetu.
Huo ulikuwa ni mwendelezo mwingine wa tabia za kushangaza za jennifer. Nilijikuta nacheka kwa sauti hali iliyomfanya mwalimu anishangae. Si kwamba nilicheka kwakufurahia tukio lile bali nilipatwa namshangao mkubwa kiasi kwamba nikajikuta nacheka pasipo kutarajia.
“ni kipi kilichokufurahisha hapo?” aliniuliza mwalimu.
“hakuna chochote cha kufurahisha, ila nadhani utakuwa umeiona rangi halisi ya Jennifer. Yeye si msikivu kabisa” nilimwambia mwalimu.
“nilitaka kujaribu kuwawekeni sawa ila mtajua wenyewe, sitojishughulisha tena na lolote kuwahusu ninyi wawili” alisema mwalimu huku akinyanyuka na kuondoka. Sauti ya mwalimu ilionyesha ni wazi alikuwa amekasirika. Hata mimi nilijisikia vibaya kwa kile Jennifer alichokifanya.
Asubuhi iliyofuata ilikuwa ni siku ya pili ya ya kwenda kutalii. Siku hii sikupanga kujishughulisha na chochote kuhusu kwenda kutalii, nilipanga kutumia siku zangu zote hapo hotelini tu kwa kuwa sikutaka kuwa sababu ya kuharibu furaha ya Jennifer. Kuna wakati nilikuwa nafikiri ni vyema kama ningeachana na mambo ya kutalii na kurudi shule ila niliona jambo hilo lingeleta maswali mengi. Kwa kuwa sikuwa nimepanga kuandamana na wenzangu kwenda kutalii, nilichelewa sana kuamka. Niliamka kama saa tatu na dakika zake.
Niliswaki kisha nikaoga, baada ya hayo nikaanza kwenda kwenye mkahawa uliokuwa ndani ya hoteli hiyo ili nipate kifungua kinywa. Kwa kuwa watu wengi muda huo walikuwa wameenda kutalii hapakuwa na watu wengi. Wakulikuwa na watu watatu tu waliokuwapo ndani ya mkahawa. Na kati ya watatu hao nilimwoona mtu ambaye sikutarajia kumwona eneo hilo. Alikuwa Jennifer, ndiyo Jennifer.
Jennifer alikuwa amekaa akipata kifungua kinywa. Lilikuwa ni jambo la kustua mimi kumwona yeye pale kwa kuwa niliamini kuwa kwa wakati huo angetakiwa kuwa na wenzake kwenye kutalii huko, sasa ni nini kilimfanya abaki? sikupata jibu.
Wakati nikipiga hatua kuingia ndani ya mkahawa, akili yangu kuna kitu ilikifikiria nikifanye. Nami sikutaka kuipinga, nikaridhia kufanya kulingana na matakwa yake. nilienda mahali ambapo mhudumu wa alikuwepo, nikaagiza chai na chapati tatu. Nikampa pesa yake kisha nikabeba kifungua kinywa changu na nikaanza kupiga hatua kutafuta sehemu ya kukaa. Nilichagua meza iliyokuwa inafuatana na meza aliyokaa Jennifer na zaidi nikachagua kukaa kiti ambacho mimi na yeye tulikuwa tunatizamana.
Nilianza kunywa chai huku nikimuangalia Jennifer kwa chinichini, yeye alijifanya yuko bize kutafuna machapati yake. nami bila kuchelewa nikaanza kufanya kile ambacho akili yangu ilitaka nikifanye.
“mbona yeye yuko hapa! Alitakiwa kuwa na wenzake, sivyo? Nini kimemzuia yeye kwenda?” niliongea kwa sauti ambayo nilikuwa na uhakika Jennifer alikuwa anaisikia vyema kabisa. Nilimwangalia kwa jicho la wizi, alionekana kama hakuwa amesikia chochote. Nikaamua kuendelea kuongea. “labda jana hakuvutiwa na wanyama aliowaona hivyo leo ameamua asiende kabisa. Lakini mbona mbuga hii ni moja ya mbuga kubwa na yenye wanyama wengi wa kuvutia! Ina maaana yeye hakuvutiwa na mnyama hata mmoja! Hapana haiwezekani, lazima kuna sababu nyingine” niliongea huku nikimtupia jicho la wizi. Niliona kasi yake ya kula inapungua. Ni wazi alikuwa anasikiliza kile ambacho nilikuwa nakiongea. Nilipata nguvu ya kuendelea zaidi.
“au itakuwa ameogopa wanyama wa mwituni kwa kudhani kuwa wangemla yeye. Lakini hata hivyo, yeye muda wote amenuna, ana hasira na visasi. Ni wazi hata nyama yake itakuwa mbaya sana, itakuwa chungu mno. Hakuna mnyama anaweza kujisumbua kumla yeye. Hata wanyama wa porini wanapenda na kuvitambua vitu vizuri bwana. Lakini pia, yeye siyo muoga. Yeye anaweza kupambana na kitu chochote, anaweza kupambana na moyo wake mwenyewe, nini samba.! Ni wazi kuna sababu nyingine.” niliendelea kuongea huku nikimtupia jicho la wizi,mara hii aliacha kula kabisa, ila hakunyanyua macho kuniangalia, ni kama alikuwa anatafakari kile ambacho alikiwa aikisikia nikikisema. Kwa upande wangu, nilikuwa nimebaki na silaha moja ya maangamizi. Bila kuchelewa nikaamua kuitumia.
“anhaa nimekumbuka, jana kuna kijana hakwenda kutalii sasa inawezekana yeye anampenda sana huyo mvulana kiasi kwamba ameshindwa kwenda kutalii ili tu amuone hotelini huyo mvulana ambaye ni kipenzi cha roho yake kwa sasa. Kweli kabisa, hili ni jibu sahihi maana mapenzi yana ngu…..” kabla sijamaliza kuongea nilistuka kimiminika cha moto kikitua sehemu za usoni, kifuani na baadhi ya sehemu za tumboni. Kimiminika hicho kiliniunguza katika ni mwili wangu. Alikuwa ni Jennifer, Jennifer aliniwagia chai, kisha akasimama na kuanza kupiga hatua kutoka katika eneo lile. Na mimi bila kufikiri mara mbili nikanyanyuka na kuanza kumfuata kwa nyuma kwa kasi kubwa. Baada ya muda mchache nilimfikia kisha nikampita na kumzuia kwa kusimama mbele huku nikiwa nimemkazia jicho isivyo kawaida. Jennifer naye alisimama huku akinitizama kwa jicho hasira.
Itaendelea….