HADITHI: KIZUIZI.
SEHEMU YA KUMI NA TANO
****
Hakuna chozi linaloweza kubadili msiba kuwa sherehe, na hakuna kilio kinachoweza kumbadili aliyekufa aweze kurejea.
Kilio huwa ishara ya uchungu, kisha maisha yanaendelea katika hali ya utofauti kwa muda mrefu kisha huzoeleka.
Emmy hakupata mtu sahihi wa kumtuliza, kila aliyejaribu kumtuliza ni sawasawa alikuwa anampigia Kondoo zeze ili akate mauno, jambo lisilowezekanika.
Mama yake alikuwa amekufa kwa kushambuliwa na sumu kali iuayo mara moja baada ya kupenya katika ngozi.
Mtu aliyejaribu kwa kiasi fulani kumtuliza Emmy japokuwa sio sana alikuwa ni mwanaume shujaa aliyeyakabidhi maisha yake kutetea wengine na kuwalinda.
Mwanajeshi kamili Lameck John Sulube.
Emmy alitulia kwa sababu hakuwa na taarifa ya marejeo ya mwanajeshi huyo, na pia ile hatia ya kuzini nje ya ndoa ikaibuka upya. Akausahau msiba kwa sekunde kadhaa. Maneno ya Lameck yalikuwa yaleyale Ni mipango ya Mungu!! Usilie sana utakufuru!!, Bwana ametoa na bwana ametwaa!!. Maneno ambayo huwa hayana maana kwa mfiwa.
Ukaribu wa Emmy na Lameck Sulube haukumshtua mtu yeyote ambaye aliijua kwa uchache familia ile. Waliwatambua hawa kuwa ni mtu na baba yake mdogo.
Hata James mumewe hakutilia mashaka yoyote. Alikuwa anamjua vyema Lameck, anamfahamu fika kwani wakati anamrandiarandia Emmy aliwahi kukunjana mashati na huyu bwana. Lakini hakuchoka hadi alipofanikiwa kumuoa na sasa ni mjamzito.
Ila jicho moja lilikuwa na mashaka na ukaribu ule.
Akiwa amejivika suti nyeusi iliyomkaa vyema kijana huyu anayekimbilia miaka ishirini na mbili, kichwa chake kikiwa na nywele fupi zilizopakwa mafuta ya kungara, kiatu cha bei ghali kikiuvaa mguu wake. Kijana huyu alikuwa mtulivu sana, leso yake mkononi akipambana na jasho ambalo linataka kumharibia mwonekano wake. Mkono mmoja alikuwa na funguo zilizofanana na za gari.nani anajua huenda nayeye alikuwa ameegesha gari lake nje ya nyumba.
Kwa kumtazama usingeweza kudhania yupo katika dunia nyingine, akijadili mambo yake tofauti kabisa na msiba unaoendelea.
Zilipigwa nyimbo za kusihi watu waandae nyoyo zao kwa sababu hatujui saa wala dakika ya mwisho wetu, yeye hakuzisikia bali alihisi anapigiwa makelele na wachina wanaoimba nyimbo zao kwa lugha yao ngumu.
Hatimaye ukafika wakati wa kutoa heshima za mwisho kwa marehemu.
Kutokana na uwingi wa watu katika msiba huu, ilibidi mwongozaji atoe utaratibu maalumu kabisa wa kuuaga mwili wa marehemu Devotha.
Alianza kwa kuiita familia ya marehemu, hapa akawaita watoto na baba. Wakaaga.
Dada, mawifi, shangazi, mama wadogo. Wakaaga.
Baba wadogo, baba wakubwa, mashemeji, wajomba, kaka. Nao wakajongea waweze kuaga.
Yule kijana aliyekuwa amejikita katika kujipangusa jasho akasitisha zoezi lile, akaiacha jasho itiririke, akajisahau kuwa alikuwa amevaa suti, akaanza kuhaha huku na huko.
Akazidi kujiuliza ile sura kwa nini inamvutia.
Mwanzoni alidhani kuwa ni mteja mmojawapo aliyewahi kufika katika banda lake kwa ajili ya huduma za kuweka na kutoa pesa.
Lakini sasa akili ikamruka hakutaka kuamini kuwa yule ni kama anavyomdhani.
Samahani kaka mambo vipi. U mwenyeji wa maeneo haya. Aliuliza kwa sauti tulivu, akiwa amelitoa koti la suti na kulitupia begani.
Jose B waukweli anaingia kazini.
Kiasi fulani kwani vipi?.
Hivi yule jamaa aliyevaa kadeti ndiye Thomas, mdogo wake na marehemu? alihoji kiujanja Jose B.
Mngaro wake na mavazi yake yakamfanya aheshimike.
Yule bwana hakuwa anajua sana juu ya ile familia. Lakini alimuita mwenye ukaribu na familia ile.
Jose B akauliza swali lilelile. Akapatiwa jibu kuwa yule anaitwa Lameck, ni shemeji wa marehemu.
Na yule mwanamke waliyekuwanaye ni kama mtoto wake. Alijibu hata ambayo hajaulizwa.
Na hivyo ndivyo Jose B alikuwa anapenda. Ili ajue mengi.
Kuna jambo hapa!! Si bure. Aliwazua Jose, huku akijituliza na kujiuliza inakuwaje amhisi vibaya yule bwana.
Baada ya ndugu wa karibu kumaliza kuaga. Wasindikizaji wengine nao waliaga.
Jose B hakwenda kuaga, akabaki kumfuatilia Lameck na nyendo zake.
Mara Lameck akakutana na kipande cha mtu, kilikuwa kinampa pole.
Jose B akashtuka, kile kipande alikuwa anakifahamu vyema. Aliwahi kukiona maeneo fulani jijini Dar es salaam.
Ubungo. Zamzam guest house.
Kipande kile cha mtu kilikuja kumpokea Emmy, kikamuingiza ndani kisha kikatoka nje.
Sasa ikajengeka picha ya mwisho ya kumaliza utata kwa Jose B waukweli mshakunaku wa kimataifa. Yule aliyebaki ndani pamoja na Emmy ndiye huyu anayeitwa baba mdogo.
Jose B akacheka kisha akamshukuru Mungu kwa kumbariki na kipaji hicho cha kipekee.
Kwa hiyo baba na mwana wanamahusiano ya kimapenzi....eeh!! Mungu ameumba dunia na maajabu yake, ndo maana nikashangaa kivipi napewa malipo makubwa hivyo.
Kumbe ni baba na mwana. Jose B akamaliza kwa kicheko kifupi.
Safari ya kuelekea kuzika ikafuata.
Jose B alikuwa amekuja na gari ndogo, ilikuwa ngumu kujua iwapo ni yake ama amekodi, aliingia katika gari na kumuamuru dereva aondoe.
Alifungulia mziki wa taratibu kwa sauti ya chini.
Wakati mziki ukiendelea, Jose B akaanza kumfikiria upya Emmy, akajisahaul,isha kuwa mwanamama huyu kwa sasa yupo katika machungu makubwa ya kumpoteza mama yake mpenzi.
Jose B akamuwaza kama mwanamke ambaye amejaribu kumtapeli ama wamefanya biashara isiyokuwa sahihi.
Mimi nilielewana naye kuwa anipe milioni saba ama nyumba nikidhani kuwa alikuwa na mtu wa kawaida tu wakimsaliti James, lakini kumbe alikuwa na baba mdogo? Hii biashara kamwe nisingeweza kuifanya kwa milioni saba au kinyumba kile, hii ni hasara tena hasara kubwa tu. Yaani mtu na baba yake niiuze kwa milioni saba? Si bora hata nisingeiuza kabisa. Mtu na baba yake unadhani mchezo!! Yaani hapa sikubali kudhulumiwa kiwepesi wepesi. Lazima haki itendeke hapa. Aliwaza Jose B kwa hisia kali sana kama mtu aliyewekeza mahali kisha akadhulumiwa pesa yake halali.
Jose B hakuwekeza chochote!! Cha ajabu analalamika.
Au huyo baba mdogo amsaidie huu mzigo, kweli ngoja nimtwike na yeye mzigo wa kulipia hasara niliyoingia. Alibadili mawazo yake Jose B, akaugeuzia upepo kwa Lameck Sulube.
****
Laiti usingekuwa ukakamavu wa jeshi, huenda Lameck angeweza kuanguka wakati wa kutupia mchanga wa mwisho katika kaburi la Devotha, mama yake Emmy.
Ama hakika damu ni nzito kushinda maji.
Lameck kwa mkono wake alikuwa ameteketeza maadui wengi waliothubutu kukatiza mbele yake katika vita huko Sudani.
Wengine aliwalipua vichwani na wengine aliwapasua matumbo kwa bunduki. Hayo yote yalikuwa ya kawaida kwake, iweje kifo cha mtu huyu kimguse kwa kiasi hicho.
Alikuwa nyumbani kwake wakati akiwaza haya.
Lakini ni ubishi wake..
Lameck aliyakumbuka mazungumzo yake ya mwisho na mama yake Emmy katika hoteli iliyopo pembebi kidogo ya jiji. Mazungumzo nyororo yaliyoishia pabaya baada ya mada mpya kuletwa mezani.
Mtu na shemeji yake wakaanza kulumbana baada ya Lameck kumgusia mama Emmy kuwa anampenda mwanaye sana.
Kumpenda halikuwa tatizo, Lameck akaleta hoja ya nyongeza kuwa wamewahi kuwa na mahusiano ya kimapenzi tangu wakiwa watoto.
Mnaendelea hadi sasa? Devotha alimuuliza.
Lameck akapinga. Devotha akashusha pumzi kali.
Lameck akaendelea kuikaribia maana aliyoitaka.
Akamgusia Devotha kuwa Emmy ameolewa akiwa si bikra.
Acha upumbavu wewe...mbona mumewe alileta shukrani ngombe mbili nyumbani kwa kumkuta Emmy akiwa mzima na usichana wake huko Uganda? Alijibu kwa kebehi kiasi fulani huku taharuki ikianza kuchukua mkondo.
Lameck akashtuka, hakutegemea kusikia hayo kutoka kwa yule mama. Kumbe James alienda kujisifu. Kujisifu kwa Bikra feki iliyotengenezwa na daktari mashuhuri Lameck John Sulube, kwa kutumia Shabu, Ndimu na kisha kuiweka makini zaidi ikawekewa dondoo za sabuni aina ya KAISIKI. James akadanganyika na kutoa ngombe mbili.
Au nimpigie James simu hapa akuumbue?? aliongezea yule mama Lameck akiwa bado kimya.
Haina maana shemeji kufanya hivyo Lameck aliweka nidhamu mbele.
Kumbe ulichoniitia.
Kuna jambo la ziada....
Lipi? aliuliza kisharishari.
Ni kuhusu Emmy na mimi, nimeamua nianze kujadili na wewe kiutu uzima kisha tutamuita Emmy.......
kabla hajaendelea yule mama mweupe ambaye uso wake ulikuwa umeanza kuwa mwekundu kutokana na hasira alimkatisha, Shem Lameck naomba tusivunjiane heshima, yaani mimi wewe na mwanangu tukae kuzungumzia bikra mara sijui mlikuwa na mahusiano utotoni, unamshutumu mwanangu hana bikra, hiyo bikra uliitoa wewe mpuuzi mkubwa, na kwa taarifa yako ni kwamba Emmy ni mama mtarajiwa, ana kitoto kinaimba kwa furaha tumboni, sitaki kabisa umkere mwanangu, nenda ukapambane na wanajeshi wenzako huko si mwanangu....jitu zima hata aibu huna na nitaenda kumwambia mume wake....mshenzi wewe....yaani umekosa wanawake mtaani huko unakuja kujishebedua kwa mtoto wako loooh aibu kweli na nitakushtaki ukiendelea nasema nitakushtaki Lameck...ukome, umkome mwanangu mama alipaza sauti, ikawa kazi ya Lameck kumsihi mama huyu asiongee sauti ya juu.
Mara akasimama aweze kuondoka. Lameck akamdaka mkono, akaanza kumlaghai kuwa alikuwa anatania, lakini yule mama alikubali kinafiki tu kuwa hawezi kuyafikisha mahali popote maneno yale.
Lameck kwa kumsoma macho yake akaugundua unafiki wake. Lameck alikuwa amechukizwa sana na maneno makali kutoka kwa yule mama, hasahasa maneno ya mwisho ya kumtishia kumshtaki. Lameck akaongozwa na hasira, na kwa kujilinda siri ile isitoke mapema.
Akatumia msemo wa heri mmoja afe wengi wapone.
Kitendo cha sekunde kadhaa kutoka kwa mwanajeshi huyu.
Sumu ikaugusa mwili wa mama Emmy.
Yeye akanawa upesi upesi.
Akarejea nyumbani, taarifa aliyoitegemea ndiyo ambayo aliipata kuwa mama Emmy alikufa akiwa katika gari iliyokuwa inamrudisha nyumbani akitokea hotelini. Bila kujulikana na nini alikuwa anafanya.
Sasa amezikwa tayari na ni usiku mwingine Lameck anawaza yaliyotokea.
Lameck ameua.
*************
***LAMECK amemuua DEVOTHA ili kujilinda asichafuliwe...amemuua kabla hajamwambia ni kipi alichomwitia wajadili.
***JOSE B anapata kitu kipya kabisa msibani, kumbe LAMECK na EMMY ni ndugu wa karibu. Dili jingine!!
ITAENDELEA