Hadithi: Kizuizi

Hadithi: Kizuizi

Hii simulizi ni kiboko, mweeeh
Kila siku mkanganyiko mpya, I can't wait for next episode
Rich Pol unapitwa huku
 
Last edited by a moderator:
HADITHI: KIZUIZI

SEHEMU YA KUMI NA SABA

Alipoanza kupiga mara likatokea jina. Jina katika simu ya
mkewe.
SAM WA PILI.......
James akataharuki, akakata ile simu mara moja.
Wasiwasi ukatanda, Sam wa Pili ndiye Jose B waukweli. Maajabu.
Na ameanza lini kuwasiliana na mkewe, na alimjuaje? Ina maana mkewe anajua juu ya KIZUIZI ambacho kiliondoka na roho za Bibiana na Deo.
James akahisi kijasho chembamba kikipenya katika uti wa mgongo wake.
Kisha akagundua kuwa alikuwa anatetemeka.
Hofu. Hofu kubwa ikatanda.
KIZUNGUMKUTI........


James akabaki katika sintofahamu, alitamani kumwamsha mkewe usiku huohuo aweze kumuuliza Sam wapili ni nani. Akakiendea chumba kwa mwendo mkali wa kisharishari.

James hakuwahi kufikiri kuwa ipo siku anaweza kukumbwa na hasira za kuwaza kumpiga mwanamke lakini siku hiyo alijihisi yupo katika jinamizi la kufanya kitu kama hicho.

Alipofungua mlango alikutanisha macho na kiwiliwili cha mkewe kikiwa hoi kwa usingizi.

Akataka kumuamsha, mara akasita. Akajiuliza swali moja tu.

Kipi kilikuwa bora kwake, mke na mtoto ama ukweli.

Akatumia sekunde kadhaa kuchambua majibu haya. Alifikiria jinsi anavyojisikia amani kuwa na mwanamke kama Emmy, amani inayozidishwa na kitoto kinachorukaruka kwa furaha tumboni. James akakiri kuwa vitu vile vilikuwa vinakamilisha furaha yake na hakuwa tayari kuvipoteza.

Akahamia upande wa pili. Akafikiria namna atakavyoukabili ukweli, ukweli asioufahamu juu ya ni kitu gani Emmy anajua juu ya Jose B.

Vipi kama anajua kuhusu Kizuizi? Huu utakuwa mwanzo wa maelewano kupotea na kisha kuachana. James akaumizwa na fikra hizo za kuachana na Emmy.

Akanywea, akaamua kuachana na ukweli, kizuizi cha kugombana na Emmy kikawa kimemzuia.
Siku iliyofuata asubuhi alimuaga Emmy, wakakumbatiana kisha akatoweka.

Kichwani akiwa amevurugwa kabisa bila kujua ni wapi mahali sahihi anataka kuelekea.

****

Jose B hakuwa mtulivu katika kijiwe chake, kila mara aliwaza juu ya tukio lililotokea baina yake na Emmy, lilikuwa tukio ambalo hakulitegemea hata siku moja lakini sasa lilikuwa limetokea na aliburudika.
Jose B akafumba macho na kumfikiria James. Akaanza kumuonea wivu kwa jinsi anavyofaidi kuchangia kitanda kila siku na msichana mrembo kama Emmy. Jose B akajiona kuwa na yeye alikuwa ana haki ya kufaidi ladha tamu kama ile.

Jose B akajiona kama ni mjinga kwa kutaka kuchangia penzi na mwanaume mwenzake tena ambaye amefunga ndoa kabisa.

Kwanini nisitafute msichana mwingine? Alijiuliza.

Ni hapo alipogundua kuwa licha ya kuwa mwongeaji sana na mjuaji wa mengi hakuwa na uwezo wa kumsimamisha msichana kwa ajili ya kumtaka kimapenzi. Mara yake ya mwisho kuwa katika mahusiano alisaidiwa na rafiki yake ambaye ndiye alikuwa mzungumzaji mkuu.

Sasa yupo jijini Dar na rafiki yule yupo Mwanza.

Jose B akaona hali hiyo inamtia katika kizuizi.

Ni kweli kuna wasichana wengi tu walikuwa wanamchekeachekea na yeye anawachekea, hakuzijua ishara za watoto wa mjini, akangoja msicha amfuate na kumwambia ‘Jose nakupenda....' jambo ambalo aliendelea kulingoja bila mafanikio hadi siku anayokutana kimwili na Emmy bila kutarajia.
Jose B akawa anataka tena mchezo huo ujirudie, lakini uzito wa mdomo wake angeanza vipi kumweleza mama yule mtarajiwa? Kamwe asingeweza.

Siku mbili zikakatika bila hali ile kutoweka katika kichwa chake.
Kila alipokuja msichana kutoa ama kuweka pesa Jose B alijikuta akimtamani. Tatizo hili likawa kero isiyostahimilika.

Hakufanya mawasiliano zaidi na Emmy, alijaribu kufanya hivyo ili aweze kusahau lile tukio lakini kumbe kufanya vile ndio kujitesa zaidi.

Uvumilivu ulipozidi. Akamtumia ujumbe mfupi wa kuhitaji kuonana naye.
Emmy aliupokea ujumbe huu majira ya mchana akiwa jikoni anapika. Siku hii hakwenda kazini, ilikuwa siku yake ya mapumziko.

Nyumbani alikuwa peke yake. Mdogo wake Jose na mdogo wake walikuwa wameenda shuleni.
Uvivu wa Emmy kumfuata Jose B alipo, na pia hali ya mumewe kuwa safarini akaamua kumuita Jose B nyumbani.

Jose B hakutegemea majibu yale.

Majibu yale hayakumfurahisha, kikubwa cha kwanza alichowaza ni fumanizi ama kuabishwa mbele ya mume wa Emmy.

Jose akajiuliza mara kadhaa kisha akamuona Emmy kama msichana -------- anayetaka kuiharibu ndoa yake kirahisi namna ile.

"Akiniumbua natibua kila kitu tena nasema kabisa alifanya mapenzi na ndugu yake...hawezi kunifanya mimi mjinga namna hii." Aliapa Jose B.

Baada ya saa zima, kijana mtanashati, ndani ya mavazi ya kisasa alitinga katika nyumba ya Emmy.
Emmy ambaye bado alikuwa katika mapishi, alikuwa amevalia kanga moja pekee, kanga iliyoonyesha vyema maungo yake.

Alikuwa ameumbika haswaa. Jose B akafanya kukohoa kidogo.

"Sam....kuna nini?" Emmy aliuliza huku akionyesha waziwazi kuwa hajaupenda ujio wa Jose.

"Tunaongea huku tukiwa tumesimama ama...."

Emmy akashusha pumzi kwa nguvu kisha akamkaribisha Jose B sebuleni.
Jose akajilazimisha kuizoea ile nyumba akachukua rimoti akabadilisha chaneli katika luninga.

"Sam....." Emmy akaita.

Jose akamtazama kwa makini akiwa amejiandaa kumsikiliza.

"Naomba tusahau yale yaliyotokea na ya siwe chanzo cha wewe kuwa karibu yangu zaidi ya awali. Nakuomba sana Sam, nina ndoa yangu na nimekulipa tayari ulichotaka. Au kuna kipi kingine Sam. Nakuomba Sam kuwa na utu kidogo, nyumba nimetimiza, nimekufungulia lile banda na kodi nimelipia ya mwaka mzima....." Emmy akashindwa kuendelea kuongea midomo ikawa inamtetemeka, na machozi yakaanza kumtoka baada ya kugundua kuwa ndoa yake ipo hatarini.

Akanyanyua upande wa kanga aweze kujifuta machozi, akiwa amesahau kuwa amevaa hiyo kanga pekee.
Jicho la Jose B likakutana na paja lililonona. Midadi ikampanda.

Hakuwa tayari kuikosa ladha aliyoonjeshwa.

"Emmy, kwani nimewahi kuitikisa ndoa yako."

"Hapana, sasa hapa umekuja kufanya nini?"

"Ni wewe umeniita hapa...."

"Baada ya wewe kuhitaji kuonana na mimi." Emmyu alijibu kwa hasira.

Jose B akiwa katika matamanio alijikuta anapata ujasiri. Akazungumza.

"Nina kesi na wewe Emmy. Kubwa kuliko ya awali."

"Kesi?"

"Na malipo yake ni ya kawaida tu, kwa sasa sio nyumba tena. Wala sihitaji banda jingine la kutoa na kuweka pesa. Kwa kifupi sihitaji chochote kitakachokufanya uwaze mara mbili."

"Sam acha kunichanganya tafadhali."

"Ninahitaji ulichonipa siku ile nyumbani kwangu."

"Sam unasemaje? Sam....unasema...sikiliza, naomba usimame na uiache nyumba hii katika utulivu ulioukuta awali."

Jose B akasimama, akaanza kutoka nje, akitembea kwa majivuno.
Emmy alikuwa ameiva kwa hasira, alijisikia msaliti mkubwa kwa jambo alilofanya na Jose B ambaye alimtambua kwa jina la Sam wa pili.

Jose B alipoufikia mlango aligeuka kisha akakiruhusu kinywa chake kuzungumza.

"Nadhani unaikumbuka vizuri biashara yetu ilikuwa inahusiana na wewe kumsaliti Jose kwa mwanaume mwingine huko uswazi Zamzam guest house. Hilo tumelimaliza, lakini kumbe yule mwanaume anaitwa Lameck....na kama hiyo haitoshi ni baba yako mdogo. Emmy una hatari wewe. Yaani na baba mdogo? Ujue hata siamini. Ila sawa ni maamuzi, kama uliweza kumpa baba mdogo Lameck ambaye mnafahamiana na mnachangia damu, sijui kinakushinda nini kunipa mimi mtu usiyenifahamu. Lakini bado unaweza kuamua, aidha niiuze siri hii kwa jamaa mwingine ama utimize nilichokuomba kistaarabu.

Halafu kuna jambo pia nimesahau, umemsaliti James kwa kijana fulani hivi juzi kati...anaitwa Sam wa pili. Biashara nyingine hiyo tunaweza pia kuizungumza ukipenda. Au la nitaiuza mamilioni mengi.
Usiku mwema mama kijacho..." Jose B alimaliza huku akitabasamu.
Emmy alitamani kumzuia asiondoke lakini akagundua kuwa miguu yake ilikuwa haina nguvu tena. Alijaribu kusema neno, mdomo ukawa mzito.

Geti likasikika likibamizwa kwa nguvu, Jose B hakuwa pale tena.
Mshikemshike.

****

Miji miwili katika mikoa tofauti ilikuwa imebeba viumbe wawili wa jinsia tofauti kila mmoja na harakati zake.

Jiji la la Mwanza lilikuwa limemtunza mwanaume jasiri ambaye alikuwa ameamua kuzirudia enzi zake kwa ajili ya kuokoa kile alichokuwa anakipenda kwa dhati.

Huyu alikuwa ni James.

Hakumtaarifu mtu yeyote juu ya uwepo wake katika jiji la Mwanza.

James alikuwa anafanya msako wa kimya kimya. Harufu ya kuua ilinukia katika pua zake.
Aliitamani roho moja baada ya nyingine ili kuuficha ukweli.

James alihitaji kumkabili Jose B ambane ili auseme ukweli wote ambao ameuropoka kwa mkewe kisha amuue ili kuondoa ushahidi.

James aliamini kuwa siri ambayo mke wake anaimiliki haitakamilika bila kuwa na ushahidi. Na kama hapatakuwa na ushahidi atakuwa na uwezo wa kumruka Jose B na kudai kuwa alikuwa anamsingizia.
Na endapo Jose B atatafutwa ili aweze kutoa ushahidi, mwili wake utakuwa ukiendelea kuoza katika aidha ardhi ama utakuwa umeliwa na samaki. Inategemeana kifo atakachokufa.

Uamuzi huu James akauona kuwa ni uamuzi sahihi zaidi.

Sasa yupo katika jiji la Mwanza kumsaka Jose B waukweli aweze kuiondoa roho hii inayoushikilia ukweli.

Jiji la Dar es salaam, lilikuwa limetembelewa na mwanamke wa makamo, akiwa na pete katika kidole chake cha shahada.

Hasira yake ilikuwa imepungua kwa kiasi fulani japo alikuwa hajaridhika.
Hii ilikuwa safari yake kubwa ya mwisho katika mlolongo wa safari zake za siri tangu alipodhaniwa kuwa ni mfu.

Hakuna aliyedhania roho hii ilikuwa inaishi, japo suala la kifo chake lilibakia kuwa katika mabano. Hakuna aliyeweza kukielezea.

Hata baba yake alibaki katika sintofahamu. Akishindwa kumtupia mtu yeyote lawama juu ya kifo hicho.
Akaufuga uchungu wake, uchungu uliokuwa unamtesa.

Hatimaye ule uchungu ukamkondesha kisha ukazalisha magonjwa ya ajabu ajabu katika mwili wake.
Akaiaga dunia huku akiwa haamini kama mwanaye amekufa. Lakini hakuyasema hadharani.
Akazikwa huku ile roho aliyoamini kuwa bado inaishi ikibaki duniani.

Na sasa roho hii ipo katika jiji la Dar es salaam. Roho yenye chuki kali. Chuki ya miaka kadhaa iliyopita, chuki kali, na aliamini kuwa yu hai ili aweze kufanya mambo mawili tu. Kulipa kisasi na kuuweka ukweli wazi kwa kila mwenye mashaka.

Kisasi cha damu ndiyo kisasi pekee alichoamini kuwa ni sahihi kwa majina hayo.
Roho hii ya mwanamke iliyojihifadhi katika mwili dhaifu ilikuwa katika chumba namba kumi na nane katika nyumba ya kulala wageni pembeni kidogo ya jiji.

Majina kadhaa yalipangana katika kichwa chake.

Kindo, Keto na Kakele.

Aliwahitaji kwa hali na mali.

Na aliamini kuwa kwa kumpata mmoja wao lazima atampata na mwingine, kisha huyo mwingine naye lazima atamtaja mwenzake.

Kazi ikapangwa kuanza rasmi siku inayofuata.
Katika jiji hilohilo la Dar es salaam.


****************
**KIZUIZI kimezua balaa..JOSE B ananogewa na penzi, anaongeza kizuizi ili aendelee kuburudika. JAMES yu jijini Mwanza akimsaka Jose B ili aujue ukweli kisha amuondoe duniani....LAMECK na kizuizi cha undugu lakini anamtaka mtoto ambaye anaamini kuwa ni damu yake.

***MWANAMAMA yu katika jiji la Dar anazisaka roho tatu..KETO, KINDO na KAKELE....ni akina nani hawa........

***Kuna siri gani imejificha katika KIZUIZI.......
 
Lol utamu njoo utamu kolea....hii kama series ya 24...kila episode tamu....hongera sanaa mtunzi
 
HADITH: KIZUIZI

SEHEMU YA KUMI NA NANE


Akaiaga dunia huku akiwa haamini kama mwanaye amekufa. Lakini hakuyasema hadharani.
Akazikwa huku ile roho aliyoamini kuwa bado inaishi ikibaki duniani.
Na sasa roho hii ipo katika jiji la Dar es salaam. Roho yenye chuki kali. Chuki ya miaka kadhaa iliyopita, chuki kali, na aliamini kuwa yu hai ili aweze kufanya mambo mawili tu. Kulipa kisasi na kuuweka ukweli wazi kwa kila mwenye mashaka.
Kisasi cha damu ndiyo kisasi pekee alichoamini kuwa ni sahihi kwa majina hayo.
Roho hii ya mwanamke iliyojihifadhi katika mwili dhaifu ilikuwa katika chumba namba kumi na nane katika nyumba ya kulala wageni pembeni kidogo ya jiji.
Majina kadhaa yalipangana katika kichwa chake.
Kindo, Keto na Kakele.
Aliwahitaji kwa hali na mali.
Na aliamini kuwa kwa kumpata mmoja wao lazima atampata na mwingine, kisha huyo mwingine naye lazima atamtaja mwenzake.
Kazi ikapangwa kuanza rasmi siku inayofuata.


****
ENDELEA...........


Emmy alipatwa na maumivu ya kichwa, makali kuliko yoyote ambayo aliwahi kuyapata katika maisha yake.
Licha ya kichwa chake kumiliki elimu ya chuo kikuu kwa hili tatizo aliamini elimu ya darasani sio tiba ya kila tatizo.

Hali ilikuwa tete. Baada ya kuhimili milima na mabonde ya kuvikwepa vishawishi vya wanaume walaghai katika ngazi mbalimbali akiwa shuleni hadi kazini, mwisho akaangukia kwa baba yake mdogo, Lameck, akafuatia mume wake wa ndoa James, sasa yupo katika sintofahamu ya nini kimemsibu hadi akajirahisisha kwa Jose B wa ukweli ambaye anatambulika kama Sam wapili.

Licha ya kujirahisisha sasa kuna mzigo mwingine wa hatari.

Jose B anataka apewe penzi kama malipo ya kuificha siri ya Emmy kufanya uzinifu na baba yake mdogo.
Emmy aliliona sharti hili kama dharau na kejeli iliyopitiliza akamtolea nje mara moja Jose B kisha akamtimua nyumbani kwake.

Lakini maneno makali kutoka katika kinywa kipana cha Jose B yakamwachia simanzi na kumrejesha katika kushika makali huku mpini wa kisu ukikamatwa ipasavyo na Jose B.

Maamuzi yakawa mawili tu, aidha avutane na Jose aliyekamata mpini jambo ambalo lingemletea jeraha na kumwacha Jose B akiwa mshindi, ama la amwachie Jose B ushindi mapema kwa kukubaliana na masharti hayo.
Emmy alijilazimisha kuamini kuwa hii ni ndoto anaota na akishaamka itasahaulika na kuondoka zake.

Lakini la haikuwa ndoto. Lilikuwa tukio halisi. Na Jose B alikuwa ametamka maneno yale akiwa hana utani hata kidogo.

Emmy akamkumbuka marehemu mama yake, akatamani angekuwa hai angemweleza ukweli wote na angeweza kupata ushauri wa kiutu uzima. Hakuonekana mtu mwingine ambaye angeweza kumpatia ushauri wa kumwokoa katika hili, alijaribu kuwawaza marafiki mmoja baada ya mwingine akawachambua hakupata hata mmoja wa kumshirikisha.

Aliamini kwa kufanya hivyo angejichafulia jina lake mapema na ungekuwa mwanzo wa kufanana na yule mwanamke -------- anayeivunja nyumba yake kwa mikono yake mwenyewe.

Emmy hakuwa tayari kuwa mwanamke --------.

Akayafumba macho yake kwa kutumia viganja vya mikono yake. Alipoyaacha wazi akakutana na picha kubwa ukutani. James na msichana fulani wakiwa wanacheka kwa furaha, James alikuwa amevaa suti na mwanamke alikuwa amevaa shela.

Ilikuwa siku ya ndoa yao takatifu.

Emmy akaona aibu. Akamtazama James kama mwanaume jasiri tena mvumilivu na mwerevu asiyekuwa na papara katika maisha yake, na pia anatimiza kile ambacho anakuwa ameahidi.

James alivumilia kwa miaka kadhaa bila kufanya zinaa na Emmy, alimfanyia kila kitu na wala upendo haukupungua hadi wamefunga ndoa, akaishia kupewa bikra feki.

Dharau ya hali ya juu.

Emmy alikiri kimya kimya kuwa ana tabia mbaya tena anafaa kuitwa malaya aliyekubuhu lakini amevikwa vazi la utukufu.

Emmy akaamua moja, kulipigania penzi lake ili asiwe mwanamke -------- ambaye jamii itamdharau kila kukicha.

Akaitwaa simu yake akabofya jina alilolinitaji. Akaanza kungoja simu iweze kuita.

Jose B aliondoka na usafiri wa bajaji, iliyomuwahisha nyumbani kwake. Alijihisi anaonewa sana kwa kunyimwa kile alichokihitaji.

Jose aliamini kabisa kuwa Emmy ana dharau tena dharau iliyopitiliza. Jose B akahisi ni haki yake kupewa kila anachohitaji kwa kuwa tu anamiliki siri.

Alikifikia kitanda chake, akakirukia bila hata kuvua viatu. Akagalagala kidogo na kujihisi ameaibishwa sana kwa kukataliwa kwake.

Simu ilimkatisha vurugu alizokuwa anafanya kitandani pale.

Akaitazama. Alikuwa Emmy.

Akaipokea upesiupesi. Hakusema neno akamsikiliza Emmy.

“Sam...nisamehe kwa yaliyotokea rafiki yangu. Ni hasira tu na sijui zilitoka wapi. Sikia Sam sahau yaliyotokea. Nakuomba unisikilize....”

Akiwa anaendelea kuongea mara simu ilikatwa. Akajaribu kupiga ikakatwa tena, mara nne hali hiyo hiyo.
Emmy akapagawa Jose B akawa anacheka kwa kutambua ni kiasi gani alikuwa anamchanganya mtoto huyu wa kike.

Emmy alipoona jitihada za kupiga simu zinashindikana.

Akafanya kosa kubwa kupindukia.

Kosa la kumtumia ujumbe Jose B. Ujumbe wa kukubaliana naye katika kuwa mtumwa wa ngono lakini kwa malipo ya kumtunzia siri yake.Katika ujumbe huo majina ya Lameck na James yaliambatanishwa.

Emmy hakujua madhara ya ujumbe.

Ujumbe ni ushahidi tosha unaoweza kukufunga.

Jose B aliupokea kwa shangwe ushindi ule.

Akajitwalia medali ya dhahabu na mkongojo wa utawala. Akaanza kuiongoza nchi ya Emmy kadri alivyotaka.
Emmy akawa mtumwa wa ngono kwa Jose B.

Walau mara moja kwa juma. Hayo yakawa makubaliano ambayo yangedumu hadi mimba ikifikisha miezi saba.
Makubaliano ambayo yalitakiwa kuanza rasmi. Siku mbili baadaye.

Emmy hakuwa na ujanja akakubaliana na Jose B.

Siku ya miadi ilifika, siku iliyomfanya Emmy ajitambue kama msichana changudoa ambaye yupo katika ndoa. Alikuwa ameomba ruhusa kazini siku hiyo maalumu kwa ajili ya kujiuza kwa kijana machachari Jose B waukweli.

Akiwa katika kuwaza na kuwazua juu ya jambo analoenda kulifanya alijikuta anatokwa machozi na wala hakuweza kumsikia mtu aliyeingia uani baada ya kulipita geti akiwa amegonga kwa muda mrefu sana.
Emmy aliyasugua macho yake ili kuyaweka sawa na kuyapa mwangaza. Akakutana na mwanaume mbele yake. Alikuwa anatabasamu.

Emmy badala ya kulijibu tabasamu lile akapigwa na butwaa.

“Lameck.....” akaita, mwanaume akasogea karibu.

“Nambie Mama James..”

“Sijui hata la kusema lakini afadhali kama umekuja.”

“Nami pia niseme kuwa afadhali nimekukuta. Huenda nakuhitaji zaidi kuliko wewe unavyonihitaji.” Lameck aliketi baada ya kuhakikishiwa kuwa James alikuwa safarini.

Lameck hakutaka kupoteza muda. Wala kuishusha hali aliyokuwanayo.

Emmy akawa mtulivu kumsikiliza bwana huyu. Mada ikaanza rasmi.

Lameck akaelezea utata wake juu ya mimba aliyobeba Emmy. Wasiwasi huu ukamshangaza Emmy.

“Una maana gani sasa. Nina mimba mimi wewe wasiwasi wa nini Lameck.”

“Sio mimba ya James hii...” Lameck akasema huku akimtazama Emmy usoni.

Emmy akaduwaa. Lameck hakutetereka akajieleza juu ya kukutana kwao kimapenzi mara ya kwanza na kisha mara ya pili.

“Kile kichefuchefu ulichosema, mimba ilikuwa tayari imeingia. Sasa vipi useme kuwa ni ya James.” Lameck akasisitiza.

Hapa Emmy akajisikia kupasuka vipandevipande kisha dunia imsahau. Maisha yake yakajawa na changamoto lukuki.

Akapingana na Lameck kwa ukali mkubwa, akatoa matusi jambo ambalo hakuwahi kulifanya hapo awali. Matusi haya yakamkera mwanajeshi huyu aliyepoteza kizazi katika nchi ya Sudani.
Mwanajeshi akasimama imara. Hakutaka kumdhuru Emmy. Lakini alikereka.

“Emmy nisikilize...huyo mtoto uliyembeba ni damu yangu. Tena damu yangu halali. Usijidanganye kuwa ni wa James. Ni vyema tukae mimi na wewe tuzungumze namna ya kufanya.”

“Yaani mimi nikae na wewe tuzungumze juu ya mimba niliyoipata ndani hya ndoa,bamdogo

umechanganyikiwa?? Jeshi limekuchanganya baba yangu.....hivi kumbe walikuwa sahihi waliosema ukitaka kuwa mjeshi lazima akili zako zipunguzwe.” Emmy alikaripia. Huku akitetemeka. Lameck alikuwa mkimya akiwa wima, Emmy akaendelea kuzungumza kwa jazba, “wewe ni mjinga tena -------- sana nasema. Mjinga wa mwisho kabisa...unikome nasema Lameck unikome nisije nikakushushia heshima yako.”

Lameck alimtazama huku hasira ikimkabili na kujikuta akitokwa na neno baya kabisa lisilopaswa kutamkwa hasahasa ukiwa na hasira.

“Emiliana Emiliana...TUTAONA NANI MJANJA...” Alimaliza akaondoka.

Emmy akasonya. Alikuwa ametaharuki.

Wakati Lameck anatoweka kwa kupitia getini akiwa ametaharuki. Majira ya saa kumi na moja jionisimu ya Emmy ikaita. Alikuwa Sam wapili.

Akaipokea kwa shingo upande. Jose b akamuita nyumbani.

Emmy akakubali. Alipomaliza kuzungumza na Jose b.

Akampigia simu James na kumwambia kuwa anatoka anaelekea kwa rafiki yake.
James akatoa ruhusa akiwa jijini Mwanza.

Ruhusa ya mkewe kwenda kumgawia mwili, Jose B waukweli ambaye James alikuwa ameenda kumsaka jijini Mwanza.

Emmy akajiandaa akatoka majira ya saa kumi na mbili.

Aliondoka kwa kutumia taksi tofauti tofauti tatu. Akafika nyumbani kwa Jose B waukweli.

Majira ya saa tatu usiku. Kiwiliwili kimoja kilitangulia katika nyumba ya James. Kisha viwiliwili vingine viwili vikafuatia kwa nyuma.

Mlango ukagongwa kwa muda mrefu. Hatimaye ukafunguliwa.
Kiwiliwili kimoja kikatangulia ndani kisha kikafuatiwa na vile vingine.
Aliyefungua mlango alikuwa amepigwa kabali ya nguvu na aliongoza njia kuelekea ndani.

Mchuano huu ulienda kimya kimya.

Hakuna kelele iliyopigwa.

Emmy aliporejea majira ya saa tatu usiku alikuta geti likiwa limerudishiwa.
Akasukuma likafunguka.

Akaanza kugomba kuanzia nje huku akielekea ndani, hasira kali za kuchezewa mwili wake na Jose B zilikuwa zinamkabili.

Akaamua kuzihamishia kwa yeyote aliyeliacha geti lile wazi.
Alipofika ndani akagundua kuwa alikuwa anagombezana na hewa. Hakuna aliyemjibu.

“Haya matoto yamelala wakati geti lipo wazi..naua mtu leo.” Akawatukania mama zao kikabila huku akiifunga vyema kanga kiunoni, akaenda mbiombio katika vyumba vyao, akafungua huku akiporomosha matusi mazito. Kimya akakutana na kitanda tupu.

“Ina maana wameanza kwenda disko hawa watoto.” Alijiuliza huku akimuwazia mdogo wake James kama kiongozi wa mambo hayo. Aliamini kabisa kuwa binamu yake kamwe asingeweza kuwa na mambo hayo.
Emmy mwenye hasira akaingia jikoni.

Huko ndipo aliposhindwa kuvumilia. Ujasii pembeni akalainika, akaanguka chini.
Lakini hakuzimia.

Alikutana na mwili wa shemeji yake (mdogo wake James) ukiwa umefungwa kamba zilizokazwa haswa. Lakini alikuwa anapumua.

Binamu yake atakuwa wapi? Lilikuwa swali la kwanza.

Baada ya nguvu kumrejea kidogo akausogelea ule mwili.

Akakutana na karatasi kubwa kiasi ikiwa imeandikwa kwa kalamu ya wino mzito.

“TUTAONA NANI MJANJA”

“Mungu wangu...Lameck Lameck.....” Emmy alipatwa na nguvu akatokwa maneno hayo.

Aliyakumbuka kuwa aliwahi kuyasikia mahali, na yalitamkwa na Lameck masaa kadhaa yaliyopita baada ya kukataliwa juu ya suala la mimba anayobeba.

Emmy akataharuki zaidi alipomkosa binamu yake. Akamuweka Lameck katika hatia ya kutenda yale.
Akachukua simu aweze kutoa taarifa polisi. Akasita.

Kama akitoa taarifa kuhusu Lameckm, katika ushahidi lazima aseme nini kilitokea hadi wakakwazana na baba yake mdogo. Na kisha kufikia hatua ya kuambiana maneno yale makali.

Emmy akagaili, akampigia simu jirani yake. Kisha baada ya jirani kufika akamweleza kilichojiri na kumwomba awasiliane na mume wake jijini Mwanza.

Ilikuwa sasa sita usiku James alipoona namba ya mkewe ikipiga.
Akapuuzia simu ya kwanza, mara ikaita tena. Haukuwa utaratibu wa Emmy kupiga simu mara mbili kwa mumewe. Jambo hili likamfanya James ahisi kuna tatizo.

Akakaa kitako akapokea.

Hakuwa Emmy ilikuwa sauti ya kiume.

Mchomo wa wivu ukapenya katika masikio ya James kisha ukaunguza moyo wake.
Akahisi Emmy ameamua kuwa na mwanaume mwingine kama ishara ya kulipa kisasi baada ya kuambiwa siri zote za James.

Lakini haikuwa hivyo. Kulikuwa na tatizo. Mpigaji ambaye hakukumbuka kujitambulisha alisema kila kitu juu ya kilichotokea.

Kisha akalikumbuka neno “TUTAONA NANI MJANJA”

James akakata simu baada ya kusikia maelezo hayo. Neno la mwisho likamchanganya. Ni kama halikuwa neno analolisikia kwa mara ya kwanza. Alikuwa amewahi kulisikia hapo kabla.

Hofu ikatanda. Akajaribu bahati yake kwa kuwapigia wahusika wa tiketi za ndege anaofahamiana nao.
Pesa ikazungumza. Tiketi ikapatikana kwa gharama za juu sana.

James ambaye alikuwa ameweka mipango yake madhubuti ya kuishambulia familia ya Jose B ili kijana huyo aweze kuonekana kiwepesi. Mipango ambayo iliangukia kwa kumtoa muhanga mama yake Jose B ambaye anapatikana kwa wepesi zaidi ikaishia hapohapo.

Ikawa ngekewa kwa roho ya mama Jose B asiyekuwa na hatia na asiyejua lolote kuhusu mchezo unaoendelea kutanuka kwa kasi.

Siku iliyofuata mapema sana. James anayekaribia kuchanganyikiwa alikwea ndege. Katika sarari nzima aliyawaza maneno yaliyoachwa na mtekaji katika nyumba yake.

“TUTAONA NANI MJANJA.”


*****************

**UTATA mpya....maneno yaliyoachwa katika tafrani yanamuhusu EMMY na JAMES naye anadhani aliwahi kuambiwa......ni nani hasa muhusika.

***EMMY anazidiwa ukubwa na matatizo.....anaiokoa ndoa yake kwa gharama za kuuacha mwili wake utumike hovyo.....JOSE B naye anatafutwa jijini Mwanza ilhali yupo Dar es salaam.

***KIZUIZI kimesambaa sasa na ni muda wa kulipuka...KIZUIZI kitaondoka iwapo tu UKWELI utafunguliwa kutoka katika minyororo....
PESA na MAPENZI vinauchelewesha UKWELI huu......

ITAENDELEA.......[/B]
 
Mmmh, nimeishia kuguna tu
Pole emmy kwa mapito unayopitia sometimes nakuona kama mjinga hivi but nakuonea huruma
Ahsante mizambwa kwa story hii, ni bonge la story aisee
 
Last edited by a moderator:
Kweli adithi hii imenikosha sana, it has taken my whole day, sema boss wangu kila mara anakuja na kuniharribia uhondo kwani inabida kufunga na kufungua tena, big up
 
Back
Top Bottom