Dunia haina usawa

Dunia haina usawa

DUNIA HAINA USAWA

“Halo! Nazungumza na bilionea Kizota hapo?” lilisikika swali kutoka kwenye simu ya bilionea mkubwa kuliko mabilionea wote nchini Tanzania, Gabriel Kizota.
“Ndiyo! Wewe nani?”
“Naitwa Godwin. Mmiliki wa Akaunti ya Mabadiliko ya Kweli,” alijibu Godwin jibu lililomfanya bilionea huyo kunyong’onyea, hapohapo akatulia kochini.
“Please!” (tafadhali) alisema, alimjua mtu huyo kupitia mitandao, alikuwa mtu hatari sana.
“Nina taarifa zako nyingi sana, nitaziweka hadharani kama ukitaka. Najua kwamba kila siku ya Alhamisi unafanya mapenzi na mama yako, najua huwezi kubisha hilo. Nina meseji zenu mlizokuwa mkitumiana huku mkiitana bebi. Huwezi kubisha hilo. Nataka nikutane na wewe Mlimani City baadaye mchana, fanya hivyo, vinginevyo utaujua moto wangu mtandaoni,” alisema Godwin.
“Hakuna shida. Nitakuja mkuu!”
“Peke yako. Kuja na polisi kunamaanisha kwamba umevujisha meseji na picha zako,” alisema Godwin.
“Sawa. Mkuu!”
“Iwe saa kumi na mbili jioni. Mlimani City, utaingia katika jumba la sinema, tukutanie huko,” alisema Godwin na kisha kukata simu na kumuacha mzee huyo akiwa kwenye presha kubwa.
***
Godwin alishtuka baada ya kusikia taarifa za Wazungu waliokuwa wamekwenda Tandale na kumkamata kijana mmoja na kuondoka naye. Hakujua kilichokuwa kikiendelea lakini akahusisha tukio hilo na kuibiwa kwake simu usiku uliopita, akawa na hofu kwamba inawezekana Wazungu hao walikuwa wamemfuatilia, walifuatilia mawasiliano yake na kujua mahali alipokuwa.
Akaona kabisa kwamba vita alivyokuwa akipigana havikuwa na Watanzania wenzake tu bali kulikuwa na Wazungu waliokuwa wakimtafuta ambapo hakupata tabu kujua sababu, alijua kwamba kwa kuwa alihamisha pesa zile, basi inawezekana ikawa sababu ya watu hao kumtafuta kila kona.
Hakutaka kuona akikamatwa, kwa kuwa alikoswakoswa alichokifanya ni kuongeza umakini katika matumizi yake ya simu na siku hiyohiyo akaenda kununua simu aina ya iPhone 7, lengo lake kubwa ni kuzuia kutafutwa kwani aliamini simu hizo zilikuwa na ulinzi mkubwa.
Kwa kuwa aliifahamu IMEI namba ya simu yake, kitu cha kwanza kabisa alichokifanya ni kuifunga, akafuta namba zake katika mtandao na data base ya kampuni iliyotengeneza simu ile, hakutaka kuona mtu yeyote akijua kitu chochote kilichokuwa kikiendelea, baada ya kuhakikisha kwamba simu yake ilikuwa salama na kusingekuwa na mtu ambaye angeweza kufanya lolote, akaanza kuingiza taarifa zake katika simu mpya aliyonunua.
Bado alikuwa na kazi kubwa na viongozi wa Tanzania, aliwachukia, maisha waliyokuwa wakiishi Watanzania masikini yalimuumiza, alitaka kubadilisha kila kitu, alijua kwamba kulikuwa na viongozi wengi waliokuwa na akaunti katika Benki ya Geneva, hivyo alitaka kuzihamisha pesa hizo zote kutoka kwenye akaunti zao.
Hakutaka kuchelewa, akaanza kuingia kwenye data base ya benki ya Geneva na kuanza kuangalia akaunti za viongozi hao. Kuingia katika data base ya benki kubwa kama hiyo halikuwa jambo jepesi, kulikuwa na ugumu mno kwa kuwa kulikuwa na watu wengi, wenye ujuzi wa kompyuta waliokuwa wakilinda kila kitu katika benki hiyo lakini kitu cha ajabu kabisa, Godwin alikuwa akiingia bila hofu yoyote ile.
Alianza na akaunti ya Rais Bokasa, alichokifanya baada ya hiyo ni kuanza kufuatilia akaunti ya mtu mwingine, Waziri Buberwa na kufanya kile alichotaka kukifanya. Akaingia kwenye akaunti ya mwanaume huyo na kugundua kwamba alikuwa na dola za Kimarekani, dola milioni themanini ambazo zilikuwa ni zaidi ya shilingi bilioni mia moja na sitini, alichokifanya ni kilekile, kuhamisha pesa hizo kwenda kwenye akaunti ya akaunti ya Hospitali ya St. Lucas ya nchini Marekani kisha kumtumia meseji Buberwa kwamba alishukuriwa kwa utu wake aliouonyesha wa kutuma pesa hizo kwenye akaunti ile.
Alipomaliza ndipo akapata taarifa kwamba mzee huyo alishikwa na presha, alianguka na baada ya saa chache kufariki dunia. Hakutaka kujali, alichokuwa akikiangalia ni kuhamisha pesa za viongozi hao wote ili hapo baadaye azirudishe kwa Watanzania wenyewe.
Alipoona kwamba akaunti ya hospitali ile haikutakiwa kutolewa pesa yoyote ile, akatengeneza akaunti nyingine kwenye Benki ya Marekani na kuzihamishia pesa hizo katika akaunti yake.
Hilo likawachanganya Wamarekani, hawakuamini kile walichokiona, kwanza kitendo cha akaunti kuanzishwa ghafla na kuhamishiwa kiasi kikubwa cha pesa kikawafanya kuwa na walakini, wakachapisha taarifa ya akaunti hiyo na kuanza kuifuatilia, kwanza wajue ilifunguliwa na nani na kwenye tawi gani la benki hiyo.
“Which branch?” (tawi gani?)
“I don’t find his name. Oh my God! How does he manage to open this account?” (silioni jina lake hapa. Oh Mungu wangu! Amewezaje kufungua akaunti hii?) alijibu jamaa na kuuliza swali lililoonyesha kushangazwa na kile kilichokuwa kimetokea.
Waliiona akaunti hiyo ikiwa imefunguliwa, ilikuwa ikifanya kazi lakini kitu cha ajabu haikuonyesha ilifunguliwa katika tawi gani hapo Marekani. Hilo liliwashangaza, kiasi kikubwa cha pesa kilikuwa kimeingizwa na kilichowashtua zaidi, jina la akaunti hilo lilikuwa People of Tanzania.
Hawakujua ilikuwaje. Walijaribu kuifunga akaunti hiyo, walishindwa kufanya hivyo, wakawasiliana na watu mbalimbali wa kompyuta na kwenda kufanya kazi hiyo lakini cha ajabu kabisa walishindwa kwani mbali na kufunguliwa kwa akaunti hiyo, pia kulikuwa na virusi vilivyokuwa vimewekwa, kama wangeendelea kulazimisha kuifunga akaunti hiyo, virusi vingeingia kwenye data base na kuharibu mafaili.
Wakaangalia taarifa za pesa hizo, waligundua kwamba mara ya kwanza pesa hizo ziliingizwa kwenye akaunti moja ndani ya benki yao na kisha kutolewa na kurudishwa katika Benki ya Geneva, kilichotokea, pesa hizo zikachukuliwa tena huko na kupelekwa kwenye akaunti hiyo, mbali na pesa hizo, pia kulikuwa na dola milioni themanini ambazo nazo zilihamishiwa humo.
“Make a call to Geneva Bank,” (wapigie simu Benki ya Geneva) alisema mkurugenzi wa benki hiyo huku akionekana kuchanganyikiwa.
Mawasiliano yakafanyika na walichoambiwa ni kwamba wao wenyewe walishindwa kabisa kufanya jambo lolote lile kwani mtu aliyekuwa akiwachezea mchezo huo alikuwa mtu hatari sana ila bahati nzuri ni kwamba walikuwa wamemkamata.
“He is very dangerous man!” (ni mtu hatari sana) alisikika jamaa kwenye simu.
Wakati wao wakiendelea kuhangaika, Godwin alikuwa Tandale akiendelea kuwaambia watu kilichokuwa kikiendelea, jinsi alivyokuwa akizihamisha pesa za viongozi mbalimbali kwenye akaunti zao kule Uswisi kwamba hata kama viongozi wengine wangejaribu kwenda kuchukua pesa zao, wasingeweza kwa kuwa alikuwa amezifunga akaunti hizo.
“Nimefunga akaunti zao, hakuna atakayeweza kutoa au kuingiza pesa. Si wao tu, bali hata benki yenyewe haiwezi kufanya hivyo,” aliandika Godwin kwenye akaunti yake ya Mabadiliko ya Kweli.
Kila Mtanzania alifurahi, waliibiwa sana pesa zao na viongozi wao, kitendo cha Godwin kuibuka na kucheza mchezo huo kila mtu alimsifia kwani alikuwa akiwasaidia kwa kuzificha pesa za kodi zao ambazo zilikuwa zikiibwa kila siku na viongozi hao.
Baada ya kufuatilia mazungumzo kwa njia ya simu, akagundua kwamba hata Jenerali Ojuku Abraham alikuwa akihusika katika kuihujumu nchi kwa kujilimbikizia mali na pesa nyingi katika benki tofautitofauti nchini Tanzania. Alitaka kumkomesha, alitaka kumuondoa katika nafasi aliyokuwa nayo, aibuke hadharani na kusema kwamba hakuwa na imani na rais hivyo kuachia cheo hicho cha ukubwa wa majeshi Tanzania, kitu pekee alichokifikiria Godwin ni kuiteka familia ya jenerali huyo.
“Nani anaweza kuifanya kazi hii?” alijiuliza.
Jina la bilionea Kizota likamjia kichwani mwake, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kufuatilia mawasiliano yake kwa njia ya simu na meseji, alichokigundua kilimshangaza, hakuamini alichokuwa akikiona kwamba mwanaume huyo alikuwa akifanya mapenzi na mama yake hali iliyomfanya kupata utajiri mkubwa, mbali na kufanya uchafu huo pia alikuwa akiua watu kama njia ya kuwatoa kafara.
Ilimshangaza, utajiri mkubwa aliokuwa nao mwanaume huyo ulikuwa ni utajiri wa damu, hivyo alichokifanya ni kumpigia simu na kumwambia uchafu wote na kutaka kuonana naye.
Bilionea huyo alikuwa akitetemeka, muda wa kuonana na Godwin ulipofika, akaingia ndani ya gari lake huku akiwa na kofia kubwa na miwani, hakutaka kugundulika, walinzi walimshangaa, dereva wake hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea mpaka bosi wake kukataa kwenda na mtu mwingine.
Hakuchukua muda mrefu akafika Mlimani City, akateremka na kuelekea kulipokuwa na mlango wa kuingilia kisha kwenda katika jumba la sinema alilokuwa ameambiwa. Alipofika, akachukua tiketi na kuingia ndani. Aliangalia huku na kule, hakumuona mtu yeyote yule, akakaa huku akiangalia macho yake huku na kule.
“Samahani mzee!” alisema kijana mmoja, alikuwa amemfuata mzee huyo. Akayainua macho yake na kumwangalia.
“Bila samahani!”
“Kuna mtu ameniambia nikuletee hii simu yako uliidondosha,” alisema kijana yule.
“Niliidondosha?”
“Kwa maelezo ya mtu huyo.”
“Sawa. Nashukuru!”
Alijua kilichokuwa kikiendelea, si kwamba aliidondosha bali iliwezekana Godwin alitaka kuzungumza naye. Wakati ameishika simu hiyo, ikaanza kuita, haraka sana kaipokea.
“Kuna maagizo tu ninataka kukupa,” alisikika Godwin kwenye simu.
“Niambie chochote kile nitafanya!” alisema mzee huyo huku akitetemeka.
“Ninahitaji uiteke familia ya Jenerali Ojuku.”
“Unasemaje?”
“Nadhani umenisikia. Una siku tatu za kufanya hivyo. Ukishindwa basi nitakwenda kutoa siri hiyo, tena haiishii hapo, bali nitasema mpaka mabasi yako yanavyoua watu na kuwatoa kafara,” alisema Godwin.
“Nitawezaje kuiteka familia ya Jenerali Ojuku?”
“Wewe ni bilionea. Utaweza tu. Kama ukishindwa basi picha zako na mama yako mkiwa kitandani zitakuwa mtandaoni. Kama hutaki kuziona picha hizo, basi fanya kazi yangu. Una siku tatu tu,” alisema Godwin na kukata simu.
“Halo..halo..halo..” aliita mzee huyo huku akikiangalia kioo cha simu hiyo.
Machozi yalikuwa yakibubujika mashavuni mwake, hakuamini alichokuwa ameambiwa, alitetemeka na muda wote alikuwa akilia kwa uchungu, kazi aliyokuwa amepewa ilikuwa ngumu, hakujua pa kuanzia, siku tatu alizokuwa amepewa zilionekana kuwa chache sana kuifanya kazi hiyo.
Kuiteka familia ya Jenerali Ojuku ilikuwa kazi kubwa, lakini kwa kuwa ilikuwa ni amri, hakuwa na jinsi, alitakiwa kuifanya kwa haraka sana vinginevyo angekwenda kudhalilika baada ya siku tatu pasipo kazi hiyo kufanyika.
“Why me? God why me?” (kwa nini mimi? Mungu kwa nini mimi?) aliuliza huku akiendelea kulia, japokuwa ndani ya ukumbi ule kulikuwa na kiyoyozi kilichokuwa kikipiga kiasi cha watu wengine kuingia na makoti kwa ajili ya baridi, lakini yeye ndiyo kwanza kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka.
***
Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa nchini Uswisi, Henrik Koma alikuwa amechanganyikiwa mno, hakuamini kile alichokuwa akikiona.
Aliwatuma vijana wake mpaka nchini Tanzania kwa ajili ya kumkamata mtu aliyekuwa akihamisha pesa kutoka katika Benki ya Geneva na kisha kutamba katika mitandao ya kijamii, vijana hao wakaondoka mpaka huko, wakafuatilia mawasiliano kwa njia ya simu na kumkamata kijana huyo.
Waliondoka naye mpaka nchuni Uswisi, walijua kwamba walikuwa wamemaliza kila kitu lakini kitu cha ajabu kabisa, akaunti ile iliendelea kuandikwa na la kushangaza, kukawa na akaunti nyingine benki ambayo ilichukuliwa pesa.
Hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya, kijana yule ambaye alipelekwa kwenye chumba cha mahojiano aliyejitambulisha kwa jina la Ally Mneke aliwaambia polisi kwamba hakuwa mtu waliyekuwa wakimtafuta na hakujua sababu iliyomfanya mpaka Thomas na Bruno kwenda kumkamata.
“Where did you find this phone?” (uliipata wapi simu hii?) aliuliza mwanaume mmoja aliyevalia suti nyeusi ambaye alikaa nyuma ya meza ya mahojiano.
“Someone came and gave me,” (kuna mtu alikuja na kunipa) alijibu Ally.
“Where did he get it?” (aliipata wapi?)
“He robbed someone,” (alimuibia mtu)
Kila alipokuwa akiulizwa, alijibu huku akionekana kuwa na uhakika na kile alichokuwa akikizungumza, hakujua kitu chochote kile, kila alichokuwa akiwaambia watu hao ndicho ambacho alikuwa na uhakika nacho.
Mtu aliyekwenda kumuuzia alikuwa mhuni wa mtaani, alipopelekewa, hakujua ni kwa namna gani mtu huyo aliipata ila alikuwa na uhakika kwamba aliiba sehemu fulani kwani bei yake ilikuwa tofauti na gharama yake.
Walikuwa na simu hiyo, walitaka kufuatilia kila kitu kilichokuwa kimetokea lakini jambo la ajabu kabisa, simu hiyo ilikuwa imefungwa. Walijitahidi kuifungua lakini wakashindwa, walichokifanya ni kuwasiliana na Kampuni ya Orange ambayo ndiyo iliyotengeneza simu ile kwa ajili ya kuwaambia waifungue lakini kitu kilichowastaajabisha ni kwamba namba ya simu hiyo haikuwa ikionekana katika data base yao.
“Unasemaje?” aliuliza Kom.
“Hatuna simu yenye IMEI hiyo. Iangalieni vizuri, ni Orange?” aliuliza mwanaume aliyesikika kutoka upande wa pili.
“Ni Orange!”
“Siyo Nokia au Samsung?”
“Hapana! Ni Orange!”
“Mbona hatuna simu yenye namba hiyo!”
Mpaka kufikia hapo Kom akawa na uhakika kwamba mwanaume huyo alikuwa amecheza mchezo mchafu wa kuifuta simu ile katika data base ya kampuni hiyo ya simu. Moyo wake ulimuuma mno, walionekana kuchezewa mchezo mchafu mno.
Aliwaangalia wenzake waliokuwa ndani ya chumba kile, aliwaona kama hawakuwa wakifanya kazi kwani kulikuwa na ugumu gani kumkamata mtu mmoja aliyekuwa akiwasumbua kwa kiasi kikubwa mno.
Malalamiko yalikuwa mengi, kwa jinsi pesa zilivyokuwa zikichukuliwa katika Benki ya Geneva ikawafanya watu wengi kuwa na mashaka na pesa zao huko hivyo wengi kutaka kujiondoa kwani kwa jinsi hali ilivyokuwa walihisi kwamba baada ya mtu huyo kuwaibia pesa watu hao, angehamia kwao.
Idadi ya wateja waliojiengua katika benki hiyo ikawa kubwa, mashirika mbalimbali yakajitoa, wafanyabiashara wengi wenye pesa nyingi nao wakajitoa, beki ikaingia hasara kubwa kwa kipindi kifupi sana hali iliyowafanya usalama wa taifa nchini humo, FIS kuwa na hasira zaidi ya kumtaka mtu huyo.
“Take him back,” (mrudisheni)
Hawakuwa na jinsi, Ally alitakiwa kurudishwa nchini Tanzania kwani hakuwa yule mtu waliyekuwa wakimuhitaji, walimkamata lakini cha ajabu bado pesa zilikuwa zikichukuliwa na mtu huyo hivyo kugundua kwamba huyo hakuwa mwenyewe.
****
Bilionea Kizota alichanganyikiwa lakini hakuwa na jinsi, kile alichoambiwa kilikuwa ni lazima kifanyike haraka sana. Mbele yake aliuona ugumu mkubwa lakini hakuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima afanye kile alichoambiwa kwa kuwa tu kama asingefanikiwa kufanya hivyo ilikuwa ni lazima picha zake akiwa na mama yake faragha kuchapishwa katika mitandao ya kijamii.
Akawapigia simu vijana wake, alitaka kazi ya kuiteka familia ya Jenerali Ojuku ifanyike sana kwani alikuwa na siku tatu tu, kama isingefanyika basi ingeonekana kwamba amefeli kile alichotakiwa kufanya.
Vijana wawili wakaelekea nyumbani kwake, hao ndiyo walikuwa vijana aliowatumia kwa ajili ya kufanya matukio mbalimbali hasa kwa watu waliokuwa wakimsumbua. Akawaambia kile kilichotakiwa kufanywa, kila mmoja alishangaa, hawakujua sababu iliyomfanya bosi wao huyo kuchukua uamuzi huo kwani kuiteka familia ya Jenerali Ojuku lilikuwa jambo la hatari sana.
“Kuna nini mkuu! Mbona ni uamuzi mgumu sana huo?” aliuliza Sao, alikuwa mmoja wa vijana wake.
“Nina kazi nao. Kuna kitu kimetokea, ninahitaji kazi ifanyike haraka sana,” aliagiza Kizota.
“Basi haina shida mkuu!”
“Tuna siku tatu. Naomba jambo hili lifanyike kati ya leo, kesho, keshokutwa mwisho,” alisema Bwana Kizota.
“Haina shida mkuu!” alisema kijana wake mwingine, Abdallaman na kisha kuondoka mahali hapo.
****
Bi Matilda alikuwa ndani ya gari lake na watoto wake wawili wakielekea Mlimani City kwa ajili ya kunuunua baadhi ya bidhaa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
Alikuwa makini barabarani, redioni aliweka wimbo wa Injili wa Utanitambuaje ulioimbwa na mwimbaji Bonny Mwaitege. Hakuwa na habari kwamba nyuma yake kulikuwa na gari lililokuwa likimfuatilia, alikuwa bize kuangalia mbele na hata wakati mwingine alipokuwa akiliona gari hilo kwa kupitia kioo cha mbele, hakuwa na hofu hata kidogo.
Japokuwa alikuwa mke wa mtu mkubwa nchini Tanzania lakini hakukuwa na kitu ambacho hakuwa akikipenda kama kutembea akiwa na ulinzi, alizungumza sana na mumewe kwamba hakutaka mlinzi kwa kuwa alimwamini Mungu wake kwamba angemlinda katika kila kona alipokuwa akienda.
Mumewe, Jenerali Ojuku hakutaka kukubaliana naye, alimwambia kabisa kwamba hakutakiwa kujiamini kwamba watu wangeweza kufanya jambo lolote lile tena wakati wowote ule lakini mwanamke huyo alikataa katakata.
Hakuwa na jinsi, alichokifanya ni kukubaliana naye tu. Miaka mingi ikapita, hakukuwa na jambo baya lolote lile lililotokea kitu kilichomfanya kuamini kwamba kweli hakukuwa na kitu kibaya chochote kile na kama angemuwekea ulinzi ingekuwa kama kumnyima uhuru wake.
Siku hiyo ambayo hakuwa akiitegemea alikuwa njiani kuelekea huko Mlimani City, hakuonekana kuwa na hofu mpaka alipoingia ndani ya eneo la jengo hilo kubwa. Bila kuwa na hofu, akateremka huku akiwa na watoto wake wawili mapacha wenye miaka kumi na mbili na kuanza kuelekea humo ndani.
Akafanya manunuzi yake yaliyochukua saa moja ndani ya jengo hilo kubwa na kutoka kuelekea sehemu alipopaki gari lake, alipofika, akafungua mlango wa nyuma, akaingiza vitu vyake kisha kufungua milango mingine kwa ajili ya kuondoka.
Wakati akiwa amewasha gari na kufunga kioo cha mlango wa mbele upande wake, akashtuka kumuona mwanaume mmoja mwenye sura yenye tabasamu pana akikigonga kioo chake kwa lengo la kukifungua.
Hakuona kama kulikuwa na tatizo, akashusha kioo chake tena huku akimrudishia tabasamu mwanaume huyo ambaye akamuuliza kuhusu kadi yake ya kuingilia ndani ya eneo hilo.
“Ulipewa kadi mama?” aliuliza mwanaume huyo.
“Ndiyo! Hii hapa.”
“Na lisiti ulipewa ndani baada ya kufanya manunuzi?” aliuliza.
“Ndiyo! Hizi hapa baba yangu!” alisema Bi Matilda huku akifungua mkoba wake na kutoa lisiti na kumuonyeshea kijana yule.
Wakati akizungumza naye pasipo kujua kama kijana huyo alikuwa mbaya wake, akatokea mwanaume mwingine, akamsogelea yule aliyekuwa akizungumza naye, akatoa bastola yake na kumuonyeshea mulemule garini huku akimtaka kutulia kabisa.
“Tunaomba utulie, ila fanya hivyo kama tu utatamani kuiona siku ya kesho,” alisema kijana huyo aliyefika mahali hapo, na yule mwingine naye akatoa bastola.
“Naomba msiniue...” alisema Bi Matilda huku akitetemeka.
“Hatuna mpango wa kukua, ila ukitaka, tutakuua tu kwani hiyo ndiyo kazi yetu kubwa. Kakae kiti kile kule,” alisema jamaa huyo, haraka sana mwanamke huyo akasogea katika kiti kile kingine na kutulia, kijama mmoja akaingia ndani, akashikilia usukani huku mwingine akipanda nyuma kukaa na watoto.
“Relax mama! Ukionyesha kutetemeka, nakuapia kwa Muungu wangu, nakuua,” alisema kijana aliyeshikilia usukani na kuanza kuliondoa gari hilo mahali hapo ambapo mbele kidogo dereva akatakiwa kutoa kadi, akatoa na kisha kuruhusiwa.
Watoto wake ambao walikuwa wakishuhudia kila kitu kilichokuwa kikiendelea nao walikuwa wakitetemeka, mbele yao waliviona vifo vyao, wanaume waliokuwa wameingia ndani ya gari lao walionekana kuwa watu hatari wasiokuwa na mchezo hata kidogo.
Wakati wakiwa njiani, wakawafunga vitambaa machoni na kisha kueendelea nasafari yao mpaka Tegeta, gari likasimama ndani ya eneo la jumba moja kubwa na kisha kuteremkshwa na kuanza kupelekwa ndani.
“Naomba msituue...naomba msituue,” alisema mwanamke huyo huku akiwa ameshikwa kwa nyuma na watoto wake.
“Wala msijali! Mtakuwa hai kabisa, ila mume wako asipofanya kile tunachokitaka, kesho atakuta maiti zenu ufukweni,” alisema Abdallahman huku wakiwaingiza ndani ya chumba kimoja ambacho kwa muonekano wake tu kilionekana kuwa chumba kilichojaa mateso makubwa.
“Jamani naomba msituue,” aliendelea kusema mwanamke huyo, wakatolewa vitambaa na kisha mlango kufungwa huku wakiwaacha watatu hao wakiwa wamekumbatiana, kwa jinsi hali ya chumba ilivyokuwa, ilionyesha kabisa kwamba kama wangetoka salama, basi ilikuwa ni bahati yao.
***
Bilionea Kizota akapigiwa simu na vijana wake na kuambiwa kwamba kile alichokitaka kilikuwa kimefanyika, familia ya Jenerali Ojuku ilikuwa imetekwa na kuhifadhiwa sehemu salama kabisa.
Hilo lilimfurahisha, hakutaka kuchelewa, hapohapo akampigia simu Godwin na kumwambia kwamba kazi kubwa aliyokuwa amempa ilikamilika kwa asilimia mia moja hivyo alikuwa na wajibu wa kunyamaza na kutokuzisambaza picha hizo.
Godwin akafurahi, kitu pekee alichomwambia ni kwamba alitakiwa kuishikilia familia hiyo zaidi na hakutakiwa kuiachia huru mpaka pale ambapo angemwambia kwamba alitakiwa kufanya hivyo.
“Hilo halina tatizo. Ila naomba usiziweke picha hizo kwenye mitandao ya kijamii,” alisema Bilionea Kizota huku akizungumza kwa njia ya simu na Godwin.
“Wala usijali! Nitumie picha za watu hao.”
Hilo nalo halikuwa tatizo hata kidogo, akawapigia simu vijana wake na kuwaambia waipige picha familia hiyo na kisha kumtumia Godwin ambaye akazichukua na kuzihifadhi katika kompyuta yake. Hakutaka kuchelewa, hapohapo akaiunganisha simu yake kwa kupitia simu ya kibandani ya mitaani ambayo moja kwa moja ilipiga mpaka katika namba ya Jenerali Ojuku kwa lengo la kuzungumza naye.
Mwanaume huyo alipopigiwa simu hiyo, akakiangalia kioo cha simu yake, alishangaa kuona akipigiwa na namba ngeni, tena simu ya mtaani iliyokuwa katika mabanda ambayo ilikuwa ikitumika kipindi cha nyuma. Haraka sana akapokea.
“Nadhani utakuwa umeshangazwa na simu hii. Kwa kifupi ni kwamba ninataka ujue kwamba nina familia yako, na muda wowote ule ninaiteketeza na maiti zao kuzitupa baharini,” alisema Godwin maneno ambayo yalimfanya Jenerali Ojuku kushtuka.
“Wewe nani?”
“Si lazima unijue. Ila jua familia yako ninayo. Nakutumia picha zao wakiwa chimbo wakisubiri vifo vyao,” alisema Godwin na kukata simu.
Ojuku akachanganyikiwa, hakuamini kile alichokisikia, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumpigia simu mke wake, simu haikuwa ikipatikana, akampigia simu dada wa nyumbani ambaye alimwambia kwamba mama aliondoka kuelekea Mlimani City kufanya manunuzi ya chakula huku akiwa na watoto.
“Waliondoka muda gani?” aliuliza.
“Tangu saa tano asubuhi!” alijibu msichana huyo, Ojuku alipoangalia simu yake, ilikuwa saa kumi jioni.
Akachanganyikiwa zaidi, hakuamini alichokuwa ameambiwa, hapohapo akashtukia simu yake ikiwa imeingia ujumbe mfupi, akafungua, ujumbe huo ulikuwa ni kwenye akaunti yake ya WhatsApp ambapo alipoifungua, akakutana na picha za familia yake, mke wake na watoto wake wakiwa wamefungwa katika chumba kimoja kilichokuwa na mwanga hafifu huku wakilia na tena wakiwa wamekumbatiana.
“Nimekutumia picha zao kuona sura zao za mwisho,” aliandika Godwin kwenye mtandao uleule. Hapohapo Ojuku akampigia simu kwa lengo la kuongea naye, amwambie alikuwa akitaka nini lakini si kuiangamiza familia yake.
“Niambie unataka nini!” alisema Ojuku.
Ilikuwa vigumu kuamini kama mwanaume huyo alikuwa Jenerali nchini Tanzania, pale alipokuwa amesimama alikuwa akitoka jasho jingi, mwili wake ulikuwa ukitetemeka na alionekana kuogopa mno.
Hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya, ujasiri wote aliokuwa nao ukapotea, aliishiwa nguvu na kwa jinsi hali ilivyoonekana, kama angejifanya kiburi basi ilikuwa ni lazima familia yake iuawe kama zilivyouawa familia za watu wengine.
Hakutaka kuona hulo likitokea, alikuwa tayari kufanya kitu chochote kile kuiokoa familia yake. Alimuomba sana Godwin aiache familia yake kwani ndiyo ilikuwa kila kitu maishani mwake lakini mwanaume huyo hakutaka kukubaliana naye hata kidogo, alisisitiza kwamba ilikuwa ni lazima aiangamize na kamwe asingeweza kujua mahali familia hiyo ilipokuwa.
“Nakuomba kaka yangu....nakuomba sana,” alisema Ojuku huku akitetemeka, alihisi presha ikianza kupanda.
“Nakupa saa mbili za kuifikiria familia yako, umuhimu wake kuwa pamoja nawe, baada ya hapo, nitaimaliza. Mtu yeyote akijua kama familia yako imetekwa, ni lazima niiue tena haraka sana,” alisema Godwin na kukata simu.
***
Bilionea Kizota akapigiwa simu na vijana wake na kuambiwa kwamba kile alichokitaka kilikuwa kimefanyika, familia ya Jenerali Ojuku ilikuwa imetekwa na kuhifadhiwa sehemu salama kabisa.
Hilo lilimfurahisha, hakutaka kuchelewa, hapohapo akampigia simu Godwin na kumwambia kwamba kazi kubwa aliyokuwa amempa ilikamilika kwa asilimia mia moja hivyo alikuwa na wajibu wa kunyamaza na kutokuzisambaza picha hizo.
Godwin akafurahi, kitu pekee alichomwambia ni kwamba alitakiwa kuishikilia familia hiyo zaidi na hakutakiwa kuiachia huru mpaka pale ambapo angemwambia kwamba alitakiwa kufanya hivyo.
“Hilo halina tatizo. Ila naomba usiziweke picha hizo kwenye mitandao ya kijamii,” alisema Bilionea Kizota huku akizungumza kwa njia ya simu na Godwin.
“Wala usijali! Nitumie picha za watu hao.”
Hilo nalo halikuwa tatizo hata kidogo, akawapigia simu vijana wake na kuwaambia waipige picha familia hiyo na kisha kumtumia Godwin ambaye akazichukua na kuzihifadhi katika kompyuta yake.
Hakutaka kuchelewa, hapohapo akaiunganisha simu yake kwa kupitia simu ya kibandani ya mitaani ambayo moja kwa moja ilipiga mpaka katika namba ya Jenerali Ojuku kwa lengo la kuzungumza naye.
Mwanaume huyo alipopigiwa simu hiyo, akakiangalia kioo cha simu yake, alishangaa kuona akipigiwa na namba ngeni, tena simu ya mtaani iliyokuwa katika mabanda ambayo ilikuwa ikitumika kipindi cha nyuma. Haraka sana akapokea.
“Nadhani utakuwa umeshangazwa na simu hii. Kwa kifupi ni kwamba ninataka ujue kwamba nina familia yako, na muda wowote ule ninaiteketeza na maiti zao kuzitupa baharini,” alisema Godwin maneno ambayo yalimfanya Jenerali Ojuku kushtuka.
“Wewe nani?”
“Si lazima unijue. Ila jua familia yako ninayo. Nakutumia picha zao wakiwa chimbo wakisubiri vifo vyao,” alisema Godwin na kukata simu.
Ojuku akachanganyikiwa, hakuamini kile alichokisikia, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumpigia simu mke wake, simu haikuwa ikipatikana, akampigia simu dada wa nyumbani ambaye alimwambia kwamba mama aliondoka kuelekea Mlimani City kufanya manunuzi ya chakula huku akiwa na watoto.
“Waliondoka muda gani?” aliuliza.
“Tangu saa tano asubuhi!” alijibu msichana huyo, Ojuku alipoangalia simu yake, ilikuwa saa kumi jioni. Akachanganyikiwa zaidi, hakuamini alichokuwa ameambiwa, hapohapo akashtukia simu yake ikiwa imeingia ujumbe mfupi, akafungua, ujumbe huo ulikuwa ni kwenye akaunti yake ya WhatsApp ambapo alipoifungua, akakutana na picha za familia yake, mke wake na watoto wake wakiwa wamefungwa katika chumba kimoja kilichokuwa na mwanga hafifu huku wakilia na tena wakiwa wamekumbatiana.
“Nimekutumia picha zao kuona sura zao za mwisho,” aliandika Godwin kwenye mtandao uleule. Hapohapo Ojuku akampigia simu kwa lengo la kuongea naye, amwambie alikuwa akitaka nini lakini si kuiangamiza familia yake.
“Niambie unataka nini!” alisema Ojuku. Ilikuwa vigumu kuamini kama mwanaume huyo alikuwa Jenerali nchini Tanzania, pale alipokuwa amesimama alikuwa akitoka jasho jingi, mwili wake ulikuwa ukitetemeka na alionekana kuogopa mno.
Hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya, ujasiri wote aliokuwa nao ukapotea, aliishiwa nguvu na kwa jinsi hali ilivyoonekana, kama angejifanya kiburi basi ilikuwa ni lazima familia yake iuawe kama zilivyouawa familia za watu wengine.
Hakutaka kuona hulo likitokea, alikuwa tayari kufanya kitu chochote kile kuiokoa familia yake. Alimuomba sana Godwin aiache familia yake kwani ndiyo ilikuwa kila kitu maishani mwake lakini mwanaume huyo hakutaka kukubaliana naye hata kidogo, alisisitiza kwamba ilikuwa ni lazima aiangamize na kamwe asingeweza kujua mahali familia hiyo ilipokuwa.
“Nakuomba kaka yangu....nakuomba sana,” alisema Ojuku huku akitetemeka, alihisi presha ikianza kupanda.
“Nakupa saa mbili za kuifikiria familia yako, umuhimu wake kuwa pamoja nawe, baada ya hapo, nitaimaliza. Mtu yeyote akijua kama familia yako imetekwa, ni lazima niiue tena haraka sana,” alisema Godwin na kukata simu.
Ojuku alikuwa akitetemeka, hakuamini kile alichokuwa ameambiwa, alipewa saa mbili za kuifikiria familia yake, aliifikiria kwa kina na baada ya muda huo akapigiwa simu na mwanaume huyo na kuambiwa kwamba kulikuwa na kazi alitakiwa kuifanya kwa nguvu zote vinginevyo angeishuhudia familia yake ikiteketezwa na miili yao kutiupwa baharini.
“Nipo tayari kufanya lolote lile. Nipo tayari kwa ajili ya familia yangu,” alisema Ojuku kiasi kwamba ilikuwa vigumu kuamini kama alikuwa Jenerali wa Jeshi la Wananchi.
Alichoambiwa ni kwamba kulikuwa na kazi kubwa alitakiwa kuifanya, kazi ya kuiteka familia ya Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Bwana Noel. Alitakiwa kujipanga vilivyo na kuifanya kazi hiyo haraka sana.
Ilikuwa kazi ngumu na kubwa kuifanya, hakujua kama angeweza kufanya hivyo kwani aliijua familia hiyo, ilikuwa ikilindwa na maofisa wengi wa usalama wa taifa. Alichoambiwa ni kwamba alitakiwa kuifanya kwa nguvu zote na hakutakiwa kutoa sababu zozote zile kwani kama angefanya hivyo ilikuwa ni lazima kuishuhudia familia yake ikiuawa na kutumiwa video.
“Nitafanya hivyo!”
“Una siku tatu tu!” alisema Godwin na kukata simu.
****
Moyo wa Godwin ukaridhika, hakuamini kama alifanikiwa kupanga mipango yake ambayo mpaka muda huo ilionekana ikienda kutimia. Kitu alichokifanya kwa haraka sana ni kuchukua simu yake na kisha kuandika posti katika akaunti yake ya Mabadiliko ya Kweli na kuwaeleza watu kwamba hatimaye Rais Bokasa alikuwa njiani kupinduliwa kitu ambacho kilimfanya kila mtu kuwa na furaha tele.
Hiyo ndiyo ilikuwa habari ya jiji, kila mtu aliyeisoma posti hiyo kwenye akaunti hiyo akaenda kuandika katika akaunti yake kwamba hatimaye rais huyo alikuwa njiani kupinduliwa kitu ambacho watu wengi kiliwafurahisha kwani tangu walipoanza kuifuatilia akaunti hiyo, hakukuwa na taarifa yoyote ya uongo ambayo iliwahi kuandikwa.
“Kama kweli huyu kiumbe atakwenda kupinduliwa, ni lazima nitachinja kuku,” alisema jamaa mmoja huku akionekanna kuwa na furaha tele.
“Hunishindi mimi. Nafikiri nitakunywa sana pombe, nilewe mpaka nivue nguo,” alisema jamaa mwingine huku akiwa ameshika simu yake akiisoma mara kwa posti ile iliyokuwa imeandikwa.
“Ila wewe si umeokoka!”
“Kuokoka ndiyo nini kwa jambo kama hili? Mama yangu alikufa hospitalini kwa sababu hakukuwa na dawa. Yaani nina hasira naye huyu,” alisema jamaa huyo.
Mara baada ya Rais Bokasa kupata ujumbe kuhusu posti ile iliyokuwa imeandikwa katika akaunti ile akachanganyikiwa, akapewa simu na kuiangalia kwa macho yake, hakuamini kile alichokuwa akikiona, alijua fika kwamba kila kitu kilichokuwa kikiendelea Godwin alikuwa akikifahamu, kwa sababu alikuwa na akaunti iliyokuwa na watu wengi, akahisi kabisa kwamba kulikuwa na watu alikuwa akiwapanga kwa ajili ya kumpindua.
Hakutaka kuona hilo likitokea, haraka sana akawasiliana na Jenerali Ojuku, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Noel, Jaji mkuu, spika wa bunge na waziri mkuu. Alitaka kuzungumza nao juu ya kile kilichokuwa kimeandikwa, kama jeshi la Tanzania, Ojuku alitakiwa kuweka ulinzi wa nguvu kuhakikisha hakuna majeshi mengine yatakayoingia kwa ajili ya kumpindua.
“Haiwezekani! Ni lazima tusimame kuitetea nchi yetu na kunitetea Amiri Jeshi Mkuu! Ni lazima ulinzi uongezeke. Waziri mkuu zungumza na jeshi la polisi, waambie ulinzi usambazwe kila kona,” alisema Rais Bokasa huku akiwaangalia watu aliokuwa amewaita.
Akili yake ilimwambia kwamba kupinduliwa kwa jeshi ilikuwa ni lazima jeshi moja litoke nchi nyingine na kwenda kuvamia na kumtoa madarakani, hakuhisi kwamba jeshi lake hilohilo lingetumika kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.
Ojuku alikuwa kimya, kichwa chake kilikuwa kikiifikiria familia yake, alichanganyikiwa, ilikuwa ni lazima aiteke familia ya Noel na kuificha sehemu ili kuikoa familia yake isiweze kuuawa na mwanaume huyo ambaye alionekana kuwa mbaya wake.
Kikao cha dharura kilipomalizika, haraka sana Ojuku akarudi nyumbani ambapo aliendelea kupanga mipango yake. Aliipenda sana familia yake, hakutaka kuona ikiuawa hivyo ilikuwa ni lazima kufanya kile alichoambiwa akifanye, tena haraka sana.
Akawaita wanajeshi watatu, makomandoo na kuwapa kazi hiyo. Alipewa onyo kwamba kazi ilitakiwa kufanyika pasipo mtu yeyote kujua kama familia hiyo ilitekwa na kufichwa, hivyo alitakiwa kuwa makini kabisa.
“Ila nyumba yake ina ulinzi, tutaiteka vipi?” aliuliza komando mmoja.
“Hapa ndipo kwenye ugumu. Hebu subiri,” alisema Ojuku na kuondoka kuelekea chumbani.
Hakuwa sawa hata kidogo, kule chumbani akachukua simu na kumpigia Godwin, akamuuliza kwamba iliwezekanaje wafanye tukio la utekaji pasipo mtu yeyote kugundua kama familia hiyo ilikuwa imetekwa?
“Ni jambo rahisi sana. Nyumbani kwake kuna ulinzi wa Usalama wa Taifa. Msimamizi mkubwa wa ulinzi ni Andrew Carlos, unachotakiwa, iteke familia ya Andrew kwanza,” alisema Godwin, alikuwa akimpampango kabambe mwanaume huyo.
“Sawa. Halafu?”
“Baada ya hapo, niambie nimpigie simu aruhusu mchezo fulani uchezwe nyumbani hapo,” alisema Godwin.
“Mchezo gani?”
“Fanya hilo kwanza!”
“Sawa mkuu!” aliitikia Jenerali Ojuku kiheshima kwani alijua kwamba mtu huyo alikuwa na familia yake, hivyo ilikuwa ni lazima kumuheshimu.
***
Jenerali Ojuku akawapanga vijana wake kwamba ilikuwa ni lazima kuhakikisha familia ya Andrew inatekwa kwani yeye ndiye aliyekuwa kiongozi wa ulinzi na usalama katika nyumba ya Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Noel.
Hilo halikuwa tatizo. Kitu cha kwanza kabisa walichotaka kukifahamu ni mahali alipokuwa akiishi Andrew, wakawasiliana na ofisa mmoja wa Usalama wa Taifa ambaye hakuwa akijua chochote kile kilichokuwa kimepangwa, alipoulizwa mahali alipokuwa akiishi, akawaambia kwamba alikuwa akiishi Masaki hivyo walitakiwa kwenda huko.
Lengo kubwa la kwenda huko lilikuwa ni kuonana na mke wake, kuzungumza naye huku wakionekana kama kulikuwa na jambo limetokea, na wakati wakiwa katika hilo, Godwin alikuwa na kazi ya kuifunga simu ya Andrew, isiweze kutumika kwa kuingiza simu wala kutoa.
Kupapata nyumbani kwake hakukuwa na ugumu wowote ule, walifanikiwa na kuingia huku wakitaka kuonana na mwanaume huyo. Kwa jinsi walivyovaa, gwanda za kijeshi na hata kofia zilizoonyesha kwamba walikuwa makomando, hakukuwa na mtu aliyekuwa na hofu nao.
“Hayupo, aliondoka kwenda kazini!” alijibu mke wake.
“Basi sawa.”
“Kuna tatizo?”
“Lipo lakini tunakwenda, tutarudi tena baadaye,” alisema komando mmoja na kuondoka mahali hapo.
Mkewe, Selena akabaki na walakini, akahisi kwamba kulikuwa na tatizo lakini wanaume wale hawakutaka kumwambia ukweli. Akachukua simu yake kwa lengo la kumpigia lakini kitu cha ajabu kabisa simu haikuwa ikipatikana.
Hiyo haikuwa kawaida, mumewe hakuwa mtu wa kuzima simu, muda wote simu yake ilikuwa hewani, kwa nini azime simu hiyo? Hilo likazidi kumuingizia hofu moyoni mwake na kuwa na uhakika kwamba kweli kulikuwa na tatizo.
Wakati makomando walipotoka, wakawasiliana na Ojuku na kumwambia kwamba waliondoka nyumbani kwa Andrew. Ojuku akachukua simu na kumpigia Godwin na kumwambia kwamba kile alichokitaka tayari kilikuwa kimefanyika.
“Sawa. Subiri nitakwambia nini cha kufanya,” alisikika Godwin.
Hapohapo Godwin akaiunganisha simu ya Andrew ambayo alikuwa ameifunga na kisha kumpigia Selena kwa ajili ya kuzungumza naye. Kule alipokuwa, Selena alipoona simu ya mumewe ikiingia, haraka sana akainyanyua kwa lengo la kuzungumza naye, alitaka kujua kilichokuwa kikiendelea kwani moyo wake haukuwa na amani hata kidogo.
“Mume wangu! Nini kinaendelea?” aliuliza Selena huku simu ikiwa sikioni.
“Huzungumzi na mumeo. Unazungumza na Dk. Amani wa Hospitali ya Mwananyamala,” alijibu Godwin kwa kupitia namba ileile ya Andrew.
“Dokta! Mungu wangu! Naomba usinipe habari mbaya. Niambie mume wangu yupo wapi,” alisema Selena huku akianza kulia kwani kitendo cha kusikia kwamba mtu aliyekuwa akizungumza naye upande wa pili alikuwa daktari, akachanganyikiwa.
“Mumeo alipata ajali ya gari, ameletwa hapa Mwananyamala kwa matibabu. Nimechukua simu yake na kuona ameliandika jina lako kama mkewe na ndiyo maana nimekupigia” alijibu Godwin.
“Nakuja...nakuja kumuona mume wangu,” alisema Selena huku akionekana kuchanganyikiwa.
Hapohapo Godwin akakata simu na kumpigia Ojuku na kumwambia kwamba kila kitu kilikuwa tayari na muda wowote mwanamke huyo angeondoka nyumbani kwake hivyo watu wake walitakiwa kumsubiri njiani.
Hilo halikuwa tatizo, akawapigia simu vijana wake na kuwaambia kwamba mwanamke huyo alikuwa akiondoka nyumbani hivyo ilikuwa ni lazima wamteke.
Mpango huo ukaandaliwa, wakati Selena akiondoka nyumbani kwake huku akiwa na watoto wake mapacha waliokuwa na miaka mitano, akaingia ndani ya gari na kuanza kuliendesha kuelekea hospitalini huku akiwa amechanganyikiwa.
Kutoka Masaki mpaka Mwananyamala hakukuwa mbali sana, wakati gari lake likiwa limekata Mwananyamala Vijana, akashangaa kuliona gari jingine likimpita na ghafla kusimama mbele yake, akalisimamisha gari lake.
Wanaume wawili walioshika bunduki wakateremka, miili yao ilikuwa imejazia, walivalia kaoshi za kijeshi, watu walisimama pembeni wakiliangalia tukio hilo, wanaume hao wakapiga risasi nne hewani, kila mtu aliyekuwa mahali hapo akakimbia kuyaokoa maisha yake.
Wakafungua mlango, wakamteremsha mwanamke huyo na watoto wake, wakawaingiza ndani ya gari lao na kuondoka huku mahali hapo kukiwa hakuna mtu hata mmoja, na hata wale waliokuwa baa walikimbia na kuziacha chupa za pombe mezani, kila mmoja alitaka kuyaokoa maisha yake.
Haraka sana wakampigia simu Ojuku na kumwambia kwamba watu aliokuwa akiwataka walikuwa mikononi mwao na walikuwa wakielekea sehemu kwenda kuwahifadhi, Ojuku alipoambiwa hilo, haraka sana akampigia simu Godwin na kumwambia kwamba kile alichokuwa akikitaka tayari kilifanyika na hivyo aliihitaji familia yake.
“Wala usijali! Familia yako ipo salama sehemu. Hatujamaliza kazi. Itunze hiyo familia mpaka nitakapokwambia uiachie. Umenielewa?” alisema Godwin na kuuliza.
“Ndiyo! Lakini....”
“Kwenye hili hakuna lakini. Fanya nilichokwambia. Au unataka baadaye uende ukazione maiti za familia yako ufukweni?” aliuliza Godwin kwa mikwara mizito.
“Hapana! Hapana mkuu!”
“Basi sawa. Ngoja niwasiliane na Andrew,” alisema Godwin na kukata simu.
***
Andrew ndiye aliyekuwa akihakikisha ulinzi unakuwa wa kutosha nyumbani kwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Bwana Noel Joseph. Kila siku kazi yake ilikuwa ni kuwapanga maofisa ambao walitakiwa kuwa nyumbani hapo kwa zamu huku akihakikisha kwamba kila kitu kinakuwa salama kabisa.
Yeye ndiye aliyeamua nani alitakiwa kukaa na nani alitakiwa kupumzika. Hiyo ndiyo ilikuwa kazi yake ya kila siku, aliifanya kwa nguvu kubwa, kitendo cha kuiacha familia hiyo ikipata tatizo basi ingekuwa hatari sana kwake, hivyo ilikuwa ni lazima kuona akiwahimiza maofisa wa Usalama wa Taifa wailinde nyumba hiyo kuliko kitu chochote kile.
Siku ambayo tukio la utekaji wa familia yake ulikuwa ukifanyika alikuwa nyumbani huko. Moyo wake ulikuwa na hamu na kukaa na familia yake, alihitaji kupata mapumziko na tayari aliandika barua ya likizo ya mwezi mmoja na wakati huo alikuwa akifikiria ni kwa jinsi gani angekwenda Visiwani Zanzibar kula raha na familia yake.
Aliikumbuka sana, alikuwa karibu nayo kupita kiasi, aliipenda na wakati mwingine alikuwa radhi kupoteza kila kitu lakini si familia hiyo. Wakati akiwa hapo ndipo akakumbuka kumpigia simu mke wake, Selena japo azungumze naye na kumjulia hali.
Cha ajabu, simu yake haikuwa ikitoka, alishangaa mno, alijaribu kupiga zaidi na zaidi lakini simu hiyo haikuwa ikitoka kabisa. Akawaambia wenzake wajaribu kumpigia na kumtumia meseji matokeo yalikuwa yaleyale, hakukuwa na simu iliyoingia wala kutoka jambo ambalo likamfanya kuhisi kulikuwa na tatizo.
“Hii mitandao ya simu inazingua sana,” alisema Andrew huku akionekana kukasirika.
Akawasiliana na huduma kwa wateja kwa kupitia simu ya rafiki yake na kuambiwa kwamba ombi lake lingepatiwa ufafanuzi haraka sana. Akatakiwa kusubiri, alisubiri na kusubiri, dakika ziliendelea kwenda mbele na baada ya saa moja, akaona simu yake ikianza kuita, haraka sana akaipokea, akafurahi kwamba hatimaye kulikuwa na uwezekano wa simu yake kufanya kazi kama mwanzo.
“Halo!”
“Halo Andrew Carlos,” alisikika Godwin, Andrew akashtuka.
“Nazungumza na nani?” aliuliza.
“Kunijua si suluhisho. Sikiliza. Nina familia yako. Nimeiteka kwa ajili ya kazi moja tu. Kuimaliza kwa kuitumbukiza katika pipa la tindikali,” alisikika Godwin akiongea kwa msisitizo kabisa uliomfanya Andrew kutetemeka mno.
“Unasemaje?”
“Nadhani umenisikia. Nakupa mtihani mdogo sana, ukiweza, utaiona familia yako tena, ila ukishindwa, utaiona ahera,” alisema Godwin maneno yaliyomfanya Andrew kuogopa.
“Familia yangu imefanya nini mpaka uiteke? Hivi unanijua mimi? Hivi unajua adhabu nitakayokupa mwanaizaya wewe?” alisema Godwin huku akionekana kupaniki.
“Kwa kuwa unapaniki na kutoa vitisho, baadaye saa kumi na moja jioni nitakupigia simu kukwambia maiti za familia yako zipo wapi,” alisema Godwin na kukata simu.
Andrew akachanganyikiwa, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumpigia simu mke wake, simu haikuwa ikipatikana, alichanganyikiwa, haraka sana akaondoka nyumbani kwa bosi wake na kuelekea nyumbani kwake. Machozi yalikuwa yakimtoka, hakuamini kilichokuwa kimetokea. Hakuchukua muda mrefu kufika Masaki, akaingia ndani, akaita na kuita lakini hakukuwa na mtu aliyeitikia zaidi ya mfanyakazi wake.
“Wifi yako yupo wapi?” aliuliza Andrew huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Eeh! Kaka! Mbona wifi aliondoka kwenda hospitalini!” alisema mfanyakazi huyo.
“Aliondoka kwenda hospitalini? Nani anaumwa? Watoto?”
“Hapana! Aliambiwa wewe umepata ajali ndiyo amekwenda huko,” alijibu mfanyakazi huyo.
“Mimi nimepata ajali? Muda gani?” aliuliza Andrew lakini hata kabla hajajibiwa maswali yake, akatoka ndani na kurudi kwenye gari kuelekea katika Hospitali ya Mwananyamala.
Aliendesha gari kwa kuchanganyikiwa, hakuchukua muda mrefu akafika hospitalini huko ambapo moja kwa moja akaanza kuzunguka huku na kule kumtafuta mkewe kwa kuamini kwamba alifika mahali hapo kwa ajili ya kumuona baada ya kupewa taarifa kwamba alikwenda huko kwa kuwa aliambiwa kwamba alipata ajali mbaya ya gari.
Alikaa huko kwa dakika arobaini na tano akimtafuta, alishindwa kumuona, alikuwa akilia, moyo wake uliumia, alikuwa tayari kupoteza kila kitu katika maisha yake lakini si kuipoteza familia yake. Wakati akiwa anaifikiria ndipo akakumbuka kwamba alipigiwa simu na mwanaume mmoja na kumwambia kwamba alikuwa njiani kuimaliza familia yake, haraka sana akachukua simu yake na kumpigia.
“Halo! Halo! Naomba usiiue familia yangu, nitakupa kiasi chochote cha pesa unachokitaka,” alisema Andrew huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Unatania sana, sasa nitataka nikuonyeshee mfano ili iwe adabu kwa watu wengine,” alisema Godwin kwa mikwara ili kumtia presha.
“Naomba usiiue familia yangu! Nakuomba sana.”
“Sawa. Una bahati kwa kuwa umeomba msamaha! Nahitaji ufanye mambo mawili tu, ukishindwa, naimaliza familia yako,” alisema Godwin.
“Niambie kitu chochote kile, nitafanya.”
“Sawa. Kwanza hatakiwi mtu yeyote kufahamu kama familia yako imetekwa, hata polisi hawatakiwi kufahamu hilo,” alisema Godwin.
“Sawa. Nitaficha siri.”
“Cha pili nataka ukaiteke familia ya mkurugenzi wake, Noel,” alisema Godwin.
“Unasemaje?”
“Najua umenielewa. Ninakupa siku tatu kufanya mambo hayo mawili.”
“Siwezi kuiteka, sijui nitaiteka vipi!”
“Basi kama hujui, subiri niwaue watoto wako kwanza ndiyo utajua jinsi ya kuiteka,” alisema Godwin na kukata simu.
“Halo..halo...halo...” aliita Andrew.
Akachanganyikiwa, akajua kabisa kwamba mwanaume huyo angeweza kuimaliza familia yake, akampigia simu, ilipopokelewa, akamuomba sana, akamwambia kwamba angefanya kama alivyotakiwa kufanya pasipo pingamizi lolote lile.
“Una bahati! Ndiyo pipa lililetwa hapa kwa ajili ya kutumbukizwa. Kama upo tayari. Kafanye kazi kisha nipe taarifa,” alisema Godwin na kukata simu.
Andrew akabaki akishusha pumzi ndefu huku akijifikiria ni kwa namna gani angeweza kuifanya kazi hiyo aliyopewa ndani ya siku tatu tu.
***
Mipango ya Godwin ilikuwa ikienda kama ilivyotakiwa kwenda, hakuona ugumu wa kazi hiyo mbele yake, alihisi kwamba angefanikiwa kwa kuwa kazi kubwa ilikuwa ni kwa watu ambao aliwapa kazi hiyo lakini si yeye.
Hakutaka kumteka mtu yeyote yule, alitaka kuwatumia wenyewe kwa wenyewe kufanikisha mambo yake kitu kilichoonekana kuwa rahisi kupita kawaida.
Hakutaka kuiweka mipango hiyo katika mitandao ya kijamii, kitu pekee ambacho aliwaambia watu ni kwamba ndani ya miezi miwili ilikuwa ni lazima Rais Bokasa apinduliwe kama tu hatoweza kuachia madaraka kwa hiari.
Watu wakawa na hamu ya kuona rais huyo akijiuzulu, lilionekana kuwa jambo gumu kwa kuwa hata Jenerali Ojuku alionekana kuwa upande wake kwa asilimia mia moja kwani hata kwenye mikutano aliyokuwa akiweka rais huyo, yeye alikuwa pembeni na kumuahidi rais huyo kwamba angepambana na wabaya wake kwa asilimia mia moja.
Si huyo tu bali hata Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Noel alionekana kuwa upande wake, aliwatuma vijana wake kuwatafuta wabaya wa rais huyo, wengine walikuwa wakitumia akaunti feki katika mitandao ya kijamii kuhakikisha rais hachafuliwi, kama Godwin alisema ndani ya miezi miwili rais Bokasa alitakiwa kujiuzulu vinginevyo angepinduliwa, ni kwa jeshi gani lingetumia kumpindua?
Wengi waliiamini akaunti ya Mabadiliko ya Kweli iliyokuwa kwenye Mtandao wa Kijamii wa Instagram, hakukuwa na habari ya uongo iliyokuwa ikiandikwa, kila kitu ambacho kilisemwa, kilitokea, sasa ilikuwaje jambo hilo litokee na wakati kila mtu aliyetakiwa kufanya hivyo alikuwa upande wa rais huyo? Hakukuwa na mtu aliyekuwa na majibu.
“Yaani kauli ya Mabadiliko ya Kweli inanishangaza sana,” alisema jamaa mmoja, alikuwa miongoni mwa wafuasi milioni thelathini na tano waliokuwa wakiifuatilia akaunti hiyo.
“Kila mtu anashangaa, si wewe tu, hata mimi mwenyewe nashangaa, hivi huyu jamaa ni mtu wa aina gani aisee, au ofisa wa Usalama wa Taifa?” alisema jamaa mwingine na kuuliza swali.
“Inawezekana! Ila kama ni ofisa wa Usalama wa Taifa, mbona mkurugenzi wake yupo upande wa dikteta? Itawezekana kweli?”
“Hatujui! Ngoja tusubiri!”
Hilo ndilo lililobaki, hawakujua mtu yule aliyekuwa akiiendesha akaunti ile angefanya jambo gani kumuondoa rais huyo madarakani. Kila mtu mtaani alizungumza lake, hakukuwa na mtu aliyependa kumuona rais huyo akiendelea kuwa madarakani kwani hakuwa mtu mzuri, aliifinya katiba, alivunja baadhi ya vipengele na mbaya zaidi alibadilisha kifungu muhimu kilichomtaka rais akae madarakani miaka mitano na yeye kuweka kwamba alitakiwa kutawala mpaka kifo chake.
Kwa kuwa alikuwa na mkakati wa kumuondoa madaakan rais huyo, alichokifanya ni kuwasiliana na mwenyekiti wa Chama cha Upinzani cha Tanzania National Party, Bwana Elius Kambili na kumwambia kwamba alikuwa katika mpango mkubwa wa kumuondoa Rais Bokasa madarakani hivyo alitakiwa kujipanga na watu wake kwa ajili ya kuichukua Tanzania.
“Sisi tuichukue Tanzania?” aliuliza Kambili, hakuamini alichokisikia.
“Ndiyo! Mpo tayari?” aliuliza.
“Ndiyo! Ila itawezekana vipi? Kwanza nazungumza na nani?” aliuliza, hakuonekana kujiamini hata kidogo. Walihangaika kwa miaka ishirini kuichukua Tanzania lakini wakashindwa mpaka pale katiba ilipobadilishwa na kumfanya rais huyo atawale mpaka kifo chake.
“Mabadiliko ya Kweli!”
“Aiseee! Hivi matukio yote unayapata wapi? Nimesoma ulivyoandika kwamba ndani ya miezi miwili unataka Rais Bokasa ajiuzulu au atapinduliwa, itawezekana vipi?” aliuliza Kambili.
“Niachie mimi. Cha msingi fanya kile nilichokwambia. Anza kupanga nani atakuwa makamu wa rais kama wewe utakuwa rais, nani atakuwa waziri mkuu na vyeo vingine,” alisema Godwin.
“Basi hakuna shida. Ngoja nifanye hivyo!”
“Ila kumbuka kitu kimoja. Iwe siri kubwa, ishu ya kumtoa madarakani huyu dikteta niachie mimi,” alisema Godwin.
“Sawa bosi.”
Godwin akakata simu, hakutaka kujulikana mahali alipokuwa, kila kitu kilichokuwa kikiendelea kilikuwa siri kubwa. Hakutaka kumwamini mtu yeyote yule na ndiyo maana hata kuwasiliana na Kambili alitumia simu yake na si kuonana ana kwa ana.
Alipomaliza, akampigia simu Andrew na kumuuliza kama alikuwa amekamilisha ule mpango aliokuwa amempa wa kuiteka familia ya Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Bwana Noel.
“Umefikia wapi?” aliuliza Godwin.”
“Mkuu! Bado! Ndiyo nataka kujipanga!”
“Unakumbuka kwamba una siku mbili tu?”
“Nakumbuka mkuu! Naomba usiiue familia yangu,” alisema Andrew.
“Ikimalizika siku ya tatu, hautoiona tena familia yako,” alisema Godwin na kukata simu.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumanne hapahapa
 
Godwin nouma, nahisi akimaliza mipango yake atajitokeza hadharani
 
Anachofanya Godwin kinafana na kwenye Movie fulani inaitwa S.A.W. (SAW)

Mambo ya puzzle, tasks, missions...


Cc: mahondaw
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom