Dunia haina usawa

Dunia haina usawa

Avatar yako tu unaonesha ni mtu wa kulia lia......., umebaki wewe tu kulalamikia mambo ya kuquote uzi wote, nitokee hapa
Unajua hiyo picha ni mtoto wa nchi gani unajua sijatumia jf kwa kipind gan unajua niliko unajua kazi nayofanya unadhan mm ni MTU wa kushinda kwenye mitandao all the time kujua kama kuna app mpya ... Subsidiary incontinecy makes the world incomprehensible ...
 
DUNIA HAINA USAWA

Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa nchini Uswisi, Bwana Henrik Kom alikuwa kwenye kikao kizito baadhi ya viongozi wa nchi hiyo akiwemo waziri mkuu, Bwana Stevenson Paul pamoja na mkurugenzi wa Benki ya Geneva, Bwana Anrik Morov aliyekuwa na asili ya Urusi.
Walikutana katika kikao hicho cha dharura kwa ajili ya kujadili matatizo yaliyokuwa yakiikumba Benki ya Geneva kwa pesa zake kutoka katika akaunti za wateja wao kuibwa na kuhamishwa katika benki nyingine nchini Marekani kabla ya kupelekwa katika akaunti nyingine.
Kwao, jambo lile lilionekana kuwa geni kabisa. Benki ilikuwa na ulinzi mkubwa, data base ililindwa saa ishirini na nne na watalaamu wa kompyuta lakini kitu kilichoshangaza kabisa, kulikuwa na mtu ambaye alifanikiwa kuingia katika akaunti hizo na kuhamisha pesa pasipo wao wenyewe kufahamu.
Walichanganyikiwa, waliona kuwa na uhitaji wa kupambana na mtu huyo kwani kama alikuwa na uwezo wa kuhamisha benki kutoka katika akaunti ya watu wawili, basi angekuwa na uwezo wa kuhamisha pesa kutokana hata kwa viongozi wengine na kuendelea kuichafua akaunti hiyo na kupoteza wateja zaidi kwa kuonekana hawakuwa na ulinzi wowowte ule.
Hawakutaka kuona aibu hiyo ikiwakuta, ilikuwa ni lazima kupambana na ndiyo maana aliweka kikao hicho cha dharura kwa ajili ya kuangalia ni kwa jinsi gani wangeweza kupambana na mtu huyo ambaye alikuwa nchini Tanzania.
“Ulisema ulituma vijana lakini walishindwa kumkamata?” aliuliza Bwana Stevenson.
“Ndiyo!” alijibu Kom na kuanza kumuhadithia namna vijana wake walivyosafiri kwenda nchini Tanzania, walivyodukua namba yake kwa kutumia picha waliyoituma katika Mtandao wa Kijamii wa WhatsApp lakini mwisho wa siku walimpata kijana mmoja aliyeitwa Ally ambaye alidai kwamba simu ile alikuwa ameuziwa na kibaka.
“Ulijuaje kama si yeye huyo mliyemkamata?” aliendelea kuuliza.
“Ni kwa sababu wakati tukiwa naye mikononi mwetu, akaunti ya pili ikaibiwa pesa.”
“Ooh! Sawa. Kwa hiyo mnataka kuniambia kwamba mmeshindwa kupambana naye?”
“Si kwamba tumeshindwa.”
“Bali?”
“Tutapambana naye na ndiyo maana nimeita kikao hiki kwa ajili ya kujadiliana kwani mtu ambaye tunadili naye ni mtaalamu wa masuala ya kompyuta. Mtu aliweza kufungua akaunti katika Benki ya America na hakukuwa na mtu aliyejua. Huyo mtu si mchezo,” alisema Bwana Kom.
Kikao kilikuwa kizito mno, hawakujua ni kwa namna gani wangeweza kumpata mtu huyo aliyeonekana kuwa hatari sana. Maofisa wa Usalama wa Taifa nchini humo, FIS walikuwa wakihangaika kila siku kumtafuta katika mitambo yao lakini hawakufanikiwa.
Waliambiwa kwamba mtu huyo ndiye alikuwa mmilikiwa akaunti ya Mabadiliko ya Kweli iliyokuwa Instagram, waliitumia akaunti hiyo kumtafuta na kujua mahali alipokuwa lakini hawakufanikiwa hata kidogo.
Walikwishawasiliana na Instagram wenyewe na kuwaambia juu ya uhitaji wa mtu huyo, waliwaambia kuwapa taarifa mahali alipokuwa lakini wao wenyewe walikataa kutoa ushirikiano wowote ule kwani kwa kuingilia kitu kama hicho ilikuwa ni sawa na kuvunja sheria ya kimtandao ya mtu kuingilia mambo ya mtu binafsi, tena kwa akaunti kama hiyo ambayo ilikuwa ikiongoza kuwa na wafuasi wengi barani Afrika, ilikuwa ikiwaingizia pesa nyingi tu.
“Wamekataa kushirikiana nasi?” aliuliza Bwana Stevenson.
“Ndiyo! Instagram wamekuwa wagumu sana, kama Apple kipindi kile walipotakiwa kutoa taarifa za ugaidi kwa mtumiaji wao wa iPhone, wamekataa kabisa,” alisema Kom.
“Cha msingi fanyeni kitu kimoja. Tumeni tena watu kwenda huko!”
“Unamaanisha maofisa wa FIS?”
“Ndiyo. Mnasema kwamba huyo mtu mlimpta jijini Dar es Salaam?”
“Ndiyo!”
“NA eneo linajulikana?””Ndiyo!”
“Basi mtumieni msichana wa kwenda huko. Awe mmoja, msichana mweusi, mrembo ambaye atakwenda huko kwa ajili ya kufanya kazi moja tu, kumtafuta na kumpata,” alishauri Stevenson.
“Kivipi?”
“Waafrika wanapenda sana ngono kuliko kazi!”
“Najua!”
“Mtumieni msichana mrembo tu. Akienda huko afanye kazi ya kumtafuta mwanaume huyo, akimpata, aanze kujilainisha kwake, itakuwa kazi nyepesi sana. Hata asipompata, yule mtu ambaye atakuwa akimuhofia ndiye aanze kujenga naye ukaribu na kumwambia kuhusu siri zake, hata kama si yeye, inawezekana kuna mtu hapo atakuwa anamfahamu,” alisema Stevenson.
“Sawa.”
“Tuna Mtanzania yeyote FIS?”
“Ndiyo! Lakini yupo nchini Somalia akiendelea kudadisi kuhusu Al Shaabab!”
“Mtoeni huko, mwambieni aende Tanzania.”
“Sawa bosi!”
“Anaitwa nani?”
“Halima!”
“Basi mtumeni aende huko mpaka katika mtaa ambao simu hiyo ilipopatikana, nina uhakika tutampata tu,” alisema Stevenson.
“Haina shida.”
Hakukuwa na la kuchelewa, haraka sana simu ikapigwa mpaka nchini Somalia na msichana huyo mrembo, Halima kupewa taarifa kwamba ilikuwa ni lazima asafiri mpaka nchini Tanzania, kwenye Jiji la Dar es Salaam katika Mtaa wa Tandale ambapo ndipo simu hiyo ilipopatikana kwa ajili ya kumtafuta mwanaume huyo.
Hilo halikuwa tatizo kwa Halima, kwa kuwa alikuwa msichana mrembo aliyekubuhu katika kuwatafuta watu wengi barani Afrika, akaondoka kuelekea nchini Tanzania huku kichwani mwake kukiwa na jambo moja tu, kumpata mwanaume huyo ambaye hakuijua hata sura yake, na hakujua alikuwa na muonekano gani, ila alichokuwa akikitaka ni kumpata na kumkamata kwa ajili ya kuirudishia sifa Uswisi.
***
Rais Bokasa hakuwa sawa, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria Godwin ambaye alikuwa tishio katika maisha yake. Moyo wake ulimuuma, hakuwa radhi kuona akiachia madaraka, aliupenda urais aliokuwa nao, kwake, alikuwa tayari kupoteza kila kitu lakinis si urais.
Hakujua mwanaume huyo alikuwa wapi, aliwatuma maofisa wa Usalama wa Taifa kwa ajili ya kumtafuta mwanaume huyo lakini hawakuweza kumpata, alichanganyikiwa, mawasiliano yake ya simu yalidukuliwa, hilo lilimchanganya na wakati mwingine alihisi kwamba hata watu wa mitandao ya simu walikuwa wakihusika lakini baada ya kupewa taarifa kwamba hata Usalama wa Taifa wa Uswisi walishindwa kumpata mwanaume huyo, akaona kulikuwa na kazi kubwa sana mbele yake.
Watu mitandaoni walizidi kulijadili suala lake, hakukuwa na mtu aliyemuonea huruma, wengi walikuwa wakijadili kwenye mitandao hali iliyokuwa ikiendelea nchini Tanzania, kila mmoja alikuwa akimuunga mkono mmiliki wa Akaunti ya Mabadiliko ya Kweli kwamba alikuwa mtu sahihi ambaye alitakiwa kuwakomboa Watanzania kutoka katika hali ngumu ya maisha waliyokuwa nayo.
Wakati yeye akihangaika kuhakikisha kwamba anaibakiza nafasi yake, upande wa pili Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania National, Bwana Elius Kambili aliendelea kuwaambia wenzake kwamba huo ndiyo ulikuwa muda wa kupambana, walikuwa na miezi miwili kuwaweka watu sawa kabla ya kuingia madarakani.
“Mkuu! Unaamini vipi uvumi wa mitandaoni?” aliuliza katibu wa chama hicho, Bwana Golden Kumba.
“Nimepigiwa simu na huyo jamaa,” alisema Bwana Kambili.
“Amekupigia simu? Hebu tuone namba yake.”
“Hii hapa!”
Kumba hakuwa akiamini, aliona kila alichokuwa akiambiwa kilikuwa ni uongo, akaipiga namba ile kwa lengo la kuhakikisha kama kweli ilikuwa ni ya huyo mwanaume lakini namba haikuwa ikipatikana. Kila mtu akaonekana kutokumuamini, ni kweli walikuwa wakipitia kila posti iliyokuwa imewekwa, hawakujua mwanaume huyo angefanya njia gani kumuondoa madarakani Rais Bokasa kwa kuwa alikuwa na kila kitu, alikuwa na jeshi, Usalama wa Taifa, je, angetumia kitu gani na wakati vyote hivyo vilikuwa vikimuunga mkono?
“Sidhani kama ni kweli! Huyu mtu anataka kucheza na akili zetu,” alisema Kumba maneno yaliyoungwa mkono na kila mmoja.
Kambili hakurudishwa nyuma, aliamini kwamba mwanaume huyo aliyempigia simu alikuwa na uwezo wa kubadilisha kitu chochote kile, aliwaambia wazi kwamba imani yake kubwa ilikuwa kwa mwanaume huyo hivyo kila mmoja alitakiwa kuamini kwamba kweli ndani ya miezi miwili rais huyo angachia madaraka.
Alichokifanya ni kuandaa mikutano ya kisiasa, aliwaeleza wananchi hisia zake, aliwaambia ukweli kwamba ndani ya miezi hiyo rais aliyekuwa madarakani alitakiwa kujiuzulu au nchi kupinduliwa. Watu wengi, hasa wanachama wamuunga mkono japokuwa viongozi wenzake ndani ya chama hakukuwa na mtu yeyote aliyekubaliana naye.
“Hivi nyie mtu anafanya mikutano ya kunichafua mnaangalia tu!” alisema Rais Bokasa huku akiwa na hasira.
Alikuwa akiongea na IGP, Gabriel Ng’osha, hakutaka kumuona Kambili akisimama jukwaani hasa katika kipindi cha hatari kama hicho, haraka sana akaagiza mwanaume huyo akamatwe, kazi ikafanyika, huku Kambili akiwa jukwaani, akavamiwa na polisi na kukamatwa.
Hali hiyo ndiyo iliyoibua zogo kila kona nchini Tanzania, ilikuwaje mtu akamatwe kwenye mkutano wa siasa kwa kuelezea kile kitu kilichokuwa kikiendelea katika mitandao ya kijamii na kila mtu alikuwa akijua ukweli?
Akapelekwa kituoni, maagizo kutoka juu yakaagiza Kambili ahojiwe na kusema mahali alipokuwa Godwin kwani kama alipigiwa simu na kuambiwa hivyo, alikuwa na uhakika kwamba alikuwa akimfahamu mwanaume huyo na alijua mahali alipokuwa.
“Alinipigia simu tu! Sijui yupo wapi,” alisema Kambili.
“Utakuwa unajua! Sasa subiri, leo utatuambia ukweli tu,” alisema polisi mmoja aliyekuwa na mwili mkakamavu.
Wakamchukua na kumuingiza katika chumba kimoja kilichoandikwa Sobibor mlangoni, kilikuwa chumba cha mateso ambacho waliingizwa watu waliokuwa jeuri kuzungumza kitu chochote kile. Humo kulikuwa na ng’e, nyoka, nyigu, maji machafu, mbu wengi na mateso ya kila aina.
Akatupwa, maji machafu yakamchafua, alibaki akilalamika kama mtoto, akaanza kuumwa, akaanza kutambaliwa na nyoka ambao walitolewa meno, hao walitumika kama kumtisha. Muda wote alikuwa akipiga kelele, alitakiwa kukaa humo mpaka pale ambapo angekuwa tayari kuzungumza ukweli juu ya mahali alipokuwa Godwin.
Muda wote IGP Ng’osha alikuwa akipiga simu kuulizia kilichokuwa kikiendelea. Pamoja na mateso hayo yote lakini Kambili alisema vilevile kwamba hakuwa akimfahamu Godwin na hakujua alikuwa mahali gani.
“Hivi kweli nyie mnatesa au mnambembeleza?” aliuliza IGP huku akionekana kukasirika kwani nyuma yake alikuwa rais, kama Kambili asingesema ukweli ilimaanisha naye kibarua chake kingekuwa matatani kwa kuonekana hafanyi kazi.
“Mkuu! Tunafanya kazi! Bado hasemi.”
“Mwacheni huko kwa siku tatu mfululizo.”
Hayo yalikuwa maagizo, IGP alivimba kwa hasira, muda wote alikuwa mtu aliyekuwa akitamani kufanya jambo fulani ili apokee sifa kutoka kwa Rais Bokasa. Polisi wake waliendelea kumsikilizia Kambili ili awaambie ukweli juu ya mahali alipokuwa Godwin lakini jibu lake lilikuwa lilelile kwamba hakuwa akifahamu mahali alipokuwa mwanaume huyo.
“Ngoja nije mimi mwenyewe. Nadhani nyie mnamshikashika tu,” alisema IGP, akatoka nyumbani kwake, akaingia stoo na kuchukua jenereta, akalipakiza ndani ya gari, akachukua nyaya mbili na kuondoka nazo, alikuwa amepania kukumbushia enzi zake jinsi alivyokuwa akiwatesa wahalifu wakubwa ambao hawakutaka kusema kilichokuwa kikihitaji mpaka kufikia hatua ya kusema.
Hakuchukua muda mrefu akafika kituoni hapo, akaagiza polisi wawili washushe jenereta na zile nyaya na kuzipeleka katika chumba kingine na kuwaambia wamchukue Kambili na kumpeleka katika hicho chumba kilichowekwa jenereta.
“Nasikia umekataa kuwaambia vijana wangu ukweli!” alisema Ng’osha huku akimwangalia Kambili aliyekuwa hoi.
“S..ij..u..i..ch..oc..ho..t..e,” alisema Kambili huku akimwangalia Ng’osha aliyekuwa akivua shati lake.
“Basi sawa! Tuingie kazini,” alisema Ng’osha na kuwaagiza vijana wake wawashe jenereta.
Kilichofuata kilikuwa ni mateso makali, Ng’osha hakuonekana kukubali, alitaka kuhakikisha mwanaume huyo anasema mahali Godwin alipokuwa na hivyo wao kumfuata.
Alimpiga kwa shoti ya umeme huku akiwa mtupu kabisa lakini bado mwanaume huyo aliendelea kusema kwamba hakujua mahali alipokuwa mwanaume huyo. Alishangaa, aliwahi kukutana na wanaume waliokuwa na viburi lakini kwa Kambili alionekana kuwa ni zaidi ya watu hao wote.
Alipitia mateso makali sana lakini bado msimamo wake ulikuwa uleule. Baada ya dakika ishirini za mateso mfululizo, Kambili akashindwa kuzungumza, hakuweza hata kuufumbua mdomo wake, yote hayo yaliyokuwa yametokea yalikuwa ni kwa ajili ya Godwin, kitendo cha kupokea simu ya mwanaume huyo lilionekana kuwa tatizo.
Wakati akiendelea kumtesa Kambili ndani ya chumba kile, akaanza kusikia simu yake ikianza kuita kwa kutetemeka, haraka sana akaichukua kutoka mfukoni kwani alijua kwamba alikuwa rais ambaye alitaka kujua kilichokuwa kikiendelea. Hakukuwa na namba, aliona neno lililosomeka unknown likiwa na maana kwamba mtu aliyekuwa akipiga simu hakuwa akijulikana. Akaipeleka sikioni.
“Kila kitu kinachotokea kina gharama, je utakuwa tayari kulipia gharama?” lilikuwa swali la kwanza alilokutana nalo.
“Wewe nani?”
“Godwin!”
“Godwin?”
“Jiandae kulipia gharama. Baada ya dakika tano ingia kwenye akaunti ya Mabadiliko ya Kweli! Kuna mengi utayaona, siri zako nyingi zitakuwa huko kwa kuwa ulihisi hakuna anayejua. Hizo ni gharama, kama Biblia kwenye Kitabu cha Malaki kinasema Bwana angezipaka nyuso zao mavi, basi nakwambia kwamba nami nitakupaka mavi, kila mtu atakayekuangalia atauona uchafu wako,” alisema Godwin huku Ng’osha akiwa makini kusikiliza.
“Hahah! Unatakiwa uingie kwenye vikundi vya vichekesho, uwe unaigiza na sisi tuwe tunacheka. Unadhani naogopa!” alisema Ng’osha huku simu ikiwa sikioni.
“Sawa. Unawakumbuka wale majambazi waliokwenda kuvamia Benki ya Wananchi? Unakumbuka wale watu waliouawa katika Msitu wa Pande akiwemo mtoto wa Bilionea Ngolisho? Unakumbuka kuhusu wale wanaume waliokamatwa na madawa ya kulevya yenye gharama ya bilioni moja? Unakumbuka ule wizi wa mafuta yanayotokea bandarini? Unamkumbuka msichana Yunus na dada yake jinsi walivyouawa kinyama na mpaka leo muuaji hajulikani? Ng’osha, ninakwenda kukupaka mavi, kila mtu atakayekuangalia, atauona uchafu wako. Tukutane mtandaoni kwa picha za sauti yako na watu hao,” alisema Godwin na hapohapo kukata simu.
“Halo...halo..Godwin halo...Godwin usifanye hivyo...Godwin haloooo....” aliita IGP Ng’osha huku akitetemeka, kijasho kikaanza kumtoka, mapigo ya moyo yakapanda, mdomo ukaanza kuchezacheza kama mtu aliyekuwa akisikia baridi kali.
“I am finished,” (nimekwisha) alisema IGP Ng’osha huku akikaa chini na kunyoosha miguu.
***
Ndege ya Shirika la Kenyan Airlines ilikuwa ikitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. Bila kupoteza muda, Halima na abiria wengine wakaanza kuteremka na moja kwa moja kuelekea katika jengo la uwanjani hapo na kwenda sehemu ya kusubiriwa mizigo ambayo ilikuwa ikipita katika sehemu ya kuchunguziwa.
Baada ya dakika kadhaa, akachukua begi lake na kuondoka mahali hapo. Alikuwa mzuri mno, kila mwanaume aliyekuwa akipishana naye ilikuwa ni lazima kugeuka na kumwangalia. Alivalia suruali, miwani na blauzi iliyomfanya kutoka chicha.
Alitembea kwa mwendo wa mikogo kama mwanamke aliyekuwa akiringa sana, alipofika nje ya jengo lile, akaifuata teksi moja na kusimama karibu yake, dereva mmoja akamuona, akamfuata na kumtaka kuingia.
Hakuzungumza kitu, alichokuwa akikihitaji ni kupelekwa katika Hoteli ya Tasmania iliyokuwa Posta Mpya ambapo baada ya kupewa chumba na kupumzika, asubuhi iliyofuata akaanza kuelekea Tandale Sokoni kwa ajili ya kununua nguo za mitumba ambazo aliamini zingemfanya kuwa na muonekano wa mwanamke wa Dar es Salaam, hasa uswahili ili asiweze kushtukiwa.
Alinunua nguo nyingi na siku hiyohiyo akaelekea mpaka Tandale sehemu iitwayo Fogo iliyokuwa Tandale kwa Tumbo ambapo kwa kumtumia dalali wa chapchap akapata chumba alichotakiwa kulipia shilingi elfu thelathini kwa miezi kumi kitu ambacho hakikuwa tatizo lolote lile.
“Ni chumba kizuri sana. Nimekipenda,” alisema Halima huku akikiangalia chumba hicho.
“Umeolewa?” aliuliza mwenye nyumba.
“Hapana! Nipo singo.”
“Basi humu kuna wanaume wengi tu. Unaweza kuchagua yeyote,” alisema baba mwenye nyumba kiutani huku akiachia tabasamuu pana.
“Nashukuru. Nadhani nitampata mmoja,” alisema Halima huku naye akirudisha tabasamu pana. Hakukuwa na mtu aliyejua kwamba msichana huyo alikuwa mpelelezi aliyefika kwa kazi maalumu.
***
Ilikuwa ni Andrew afanye kile alichokuwa ameambiwa vinginevyo asingeweza kuiona familia yake tena. Alipewa siku tatu na tangu alipoambiwa kwamba ana siku hizo za kufanya kazi hiyo vinginevyo familia yake ingeuawa, akaona mshale wa dakika ukienda kasi kupita kawaida.
Kichwa chake kilikuwa kikiifikiria familia yake tu, alikuwa mjanja, aliyeweza kupambana na watu wengi kisiri au hata kuwatuma Usalama wa Taifa kumtafuta mtu yeyote yule aliyekuwa amejificha lakini kwa kuipata familia yake aliona jambo gumu mno kutokana na siku chache alizokuwa amepewa.
Akarudi mpaka nyumbani kwa bosi wake, Noel. Hakuonekana kuwa sawa, alipokuwa akiwaona vijana wake wakiendelea kulinda mahali pale alijua kabisa kwamba walitakiwa kufanya jambo fulani kuhusu familia ya bosi wake huyo vinginevyo asingeweza kuiona familia yake katika maisha yake yote.
Hiyo ilikuwa kazi kubwa ambayo asingeweza kuifanya peke yake, ilikuwa ni lazima kushirikiana na wenzake mpaka kufanikisha suala hilo. Hakujua ni nani alitakiwa kushirikiana naye katika suala hilo ambalo lilihitaji usiri mkubwa mno.
“Selemani Kijogoo anaweza kweli?” alijiuliza.
“Sidhani!” akajijibu.
Kila mtu aliyekuwa akijaribu kumchekecha kichwani mwake hakuona kama alikuwa na moyo wa kutunza siri kwa kile alichotaka kukifanya. Jambo moja kubwa ambalo lilimjia kichwani mwake haraka ni kumshirikisha mtu aliyekuwa amemwambia afanye lile alilotakiwa kulifanya. Hapohapo akampigia simu Godwin.
“Naomba unisaidie kitu kimoja,” alisema Andrew mara baada ya simu kupokelewa na Godwin.
“Nikusaidie nini?”
“Simuamini mtu yeyote mahali hapa, ninatamani niifanye kazi hii peke yangu! Niifanye vipi? Naomba unisaidie, sitaki kuiona familia yangu ikiangamia, naomba unisaidie ili niweze kuifanya peke yangu,” alisema Andrew huku machozi yakimtoka, moyoni mwake alikuwa akisikia maumivu makali mno kwani aliamini kwa kushindwa vile ilimaanisha kwamba asingeweza kuiona familia yake tena.
“Sawa. Subiri! Baada ya dakika kumi, mwanamke huyo ataomba kuondoka kuelekea Magomeni Usalama kwenda kumuona rafiki yake, hakikisha haondoki na mtu kwenda huko. Akiondoka, wewe mfuatilie, huko ndipo utakapomteka yeye na mtoto wake,” alisema Godwin.
“Sawa!” aliitikia Andrew kwa heshima zote.
****
Godwin alikuwa akifahamu mambo mengi, kwa kutumia ujuzi wake wa kudukua namba za watu mbalimbali aliweza kujua siri nyingi mno. Alijua mawaziri waliokuwa wakitembea nje ya ndoa, alijua mtu aliyetakiwa kuuawa siku fulani, kila kitu kilichokuwa kikiendelea aliweza kunasa mawasiliano kwa haraka sana kuliko hata mitandao ya simu ambayo ilikuwa na kazi hiyo.
Katika kufuatilia mawasiliano ya mke wa Noel, akagundua kwamba kulikuwa na mwanamke mwingine aliyekuwa akiwasiliana naye sana, huyo aliitwa Amina na alikuwa akiishi Magomeni Usalama karibu kabisa na Tanesco.
Alifuatilia mawasiliano hayo zaidi na kugundua kwamba kulikuwa na mchezo hatari uliokuwa ukichezwa na mwanamke huyo. Japokuwa alikuwa na mume, familia lakini bado alikuwa akitembea na kijana aliyeitwa Masalu aliyekuwa akiishi Magomeni Usalama.
Ilikuwa siri kubwa, huyo alikuwa mwanaume wake aliyeunganishiwa na Amina ambaye alitokea kumuelewa sana. Yakaanza mazoea ya kuonana na kijana huyo katika chumba cha Amina huko Magomeni na mwisho wa siku kuzama katika penzi zito lililoanza kuiyumbisha ndoa yake ila kwa kuwa Noel alimpenda sana mkewe, hakuwa na la kufanya.
Godwin alinasa mazungumzo yao, alisikia kila kitu kilichokuwa kikiendelea, akafuma meseji za siri, picha walizokuwa wakitumiana kwa siri ambazo hazikuwa zikistahili hata kuchapishwa magazetini. Baada ya kugundua hilo, hapo ndipo alipoanza kuona kwamba kulikuwa na kazi nyepesi ya kumnasa mwanamke huyo, tena kwa urahisi sana.
Akachukua simu yake na kumpigia, akajitambulisha kama mwanaume aliyekuwa akiitwa Lukonge na alikuwa na taarifa zake nyingi kuhusu uhusiano wa siri uliokuwa ukiendelea baina yake na Masalu kitu kilichoonekana kumchanganya sana.
“Unasemaje?” aliuliza mwanamke huyo, kwa jinsi alivyoambiwa kila kitu kilichotokea, picha zake, akachanganyikiwa mno.
“Picha zako zote zipo. Ni picha chafu sana. Hivi mwanamke kama wewe mwenye familia yako, umewezaje kupiga picha kama zile. Hivi huyo mtoto wako, Vanessa atajifunza nini? Mwanamke mchafu sana wewe. Sasa kwa taarifa yako nazipeleka Facebook na WhatAapp. Tena kwa yule jamaa wa Mabadiliko ya Kweli,” alisema Godwin kwa kujiamini kabisa, tena wakati akizungumza na mwanamke huyo kwenye simu, mguu aliweka mezani, alikuwa na uhakika na kazi yake.
“Kaka yangu naomba usifanye hivyo, nakuomba usifanye hivyo nipo tayari kukupa kitu chochote kile,” alisema mwanamke huyo, tena kwa kuonyeshewa mfano, akatumiwa picha yake moja aliyokuwa mtupu kabisa ambayo alipiga chumbani kwa Masalu.
“Huna uwezo wa kunipa ninachohitaji!”
“Nina uwezo huo. Naomba nikupe chochote unachokihitaji!”
Mwanamke huyo alijiweka tayari kwa kila kitu, hakutaka kujali kuhusu heshima yake, alibanwa, alikuwa maji ya shingo. Aliongea kwa kutetemeka huku akisema kwamba alikuwa radhi kutoa kitu chochote kile, hata kama angeombwa penzi, kwa wakati huo alikuwa tayari lakini ilimradi tu picha zile zisiwekwe katika mitandao ya kijamii.
“Njoo Magomeni Usalama huku karibu na jengo la Tanesco, tena ukiwa wewe na mtoto wako tu. Nakupa dakika ishirini, ukichelewa naziweka haraka sana. Pia njoo na milioni tano, hizo ni kwa ajili ya kununua picha hizo, huwezi kuzipata bure,” alisema Godwin.
“Nashukuru baba! Nashukuru sana!” alisema huku akitamani hata kupiga magoti.
Hakutaka kuchelewa, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuchukua kadi yake ya benki kwa lengo la kuondoka kuelekea huko. Kwa kuwa kwenye simu yake alikuwa na milioni mbili, aliamini kwamba angeweza kutoa milioni tatu katika mashine ya ATM na kuwa na milioni tano na kwenda kumpa kijana huyo.
Aliifahamu mitandao ya kijamii, ilikuwa na nguvu sana, picha yako inapowekwa, ndani ya dakika kumi ilisambaa dunia nzima, kila mtu aliiona. Hakutaka kuona akipata aibu, alitaka kuona akiwa salama kabisa mpaka siku atakapoingia kaburini.
“Natoka!” aliwaambia walinzi ambao ni maofisa wa Usalama wa Taifa.
“Abdul! Twende naye!” alisema kijana mmoja.
“Hapana! Sitaki kwenda na mtu. Ninakwenda kwenye mambo ya kifamilia,” alisema huku akionekana kuwaka si kidogo.
Kila mmoja akatulia, haikuwa mara ya kwanza kwa mwanamke huyo kutaka kwenda sehemu peke yake kwani hata alipokuwa akienda kuonana na Masalu alikuwa akienda peke yake. Walinzi wote wakatulia, wakabaki wakimwangalia mwanamke huyo akiingia ndani ya gari na kuondoka zake.
Andrew alishangaa, hakujua mwanaume yule aliongea nini na mwanamke huyo. Hiyo ilikuwa nafasi yake na ilikuwa ni lazima afanye kile alichotakiwa kufanya. Alipoona mwanamke huyo ameeondoka, naye akaaga na kuanza kumfuatilia huku akiwa ndani ya gari lake.
“Umemuona?” aliulizwa na Godwin mara baada ya kupigiwa simu.
“Ndiyo! Nifanye nini?”
“Umteke. Nimekusaidia sana, bado unahitaji msaada wangu?”
“Naomba unisaidie! Nimechanganyikiwa, kichwa changu hakipo sawa. Naomba unisaidie, nakuomba sana mkuu,” alisema Andrew, kwa jinsi alivyokuwa akiongea ilikuwa vigumu kuamini kama mwanaume huyo alikuwa ofisa wa Usalama wa Taifa aliyekuwa mbabe.
Aliendelea kulifuatilia, gari lilipofika pembezoni mwa mahali kulipokuwa na nyumba za kota Magomeni Usalama nyuma ya jengo la Tanesco, akaambiwa na Godwin asimame na atulie kwani angefika mahali hapo muda si mrefu.
“Nimemsimamisha. Mfuate, ziba uso wako, mchukue na kuondoka naye, nenda kamfiche sehemu fulani salama kwani utakaa naye huko kwa siku kadhaa,” alisema Godwin.
“Sawa.”
Wakati mke wa Noel akiwa ndani ya gari, akashtukia mlango wa gari lake ukifunguliwa na mwanaume aliyekuwa kifua wazi huku akiwa ameziba uso wake kininja kwa kutumia kaoshi aliyokuwa ameivaa. Akamwambia mwanamke huyo akae nyumba ya gari na mtoto wake ili yeye aendeshe kuelekea sehemu.
“Naomba usiziweke picha zangu mitandaoni kaka! Nakuomba sana,” alisema huku akionekana kutetemeka, Andrew akaitikia kwa kutingisha kichwa,juu chini, chini juu.
Akaliwasha gari na kuondoka mahali hapo huku akimuweka mwanamke huyo katika walakini, ishu ilikuwa ni picha, kilikuwa kitendo cha kupewa na yeye kukabidhi pesa, ila kwa nini alikuwa akiondoka naye? Kila alichokiuliza, akakosa jibu.
***
Bi Sandra, mke wa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Noel alikuwa akishangaa, hakujua kilichokuwa kikiendelea mpaka mwanaume huyo kuingia ndani ya gari na kuanza kuondoka naye. Alitamani kuuliza lakini kwa jinsi mwanaume huyo alivyokuwa amevaa, hakuthubutu hata kuufumbua mdomo wake na kumuuliza mahali walipokuwa wakielekea.
Gari liliendeshwa mpaka Kinondoni B na kuingizwa katika jumba moja kubwa na kuingizwa humo. Lilionekana kutokukaliwa na mtu kwani hata geti lenyewe alilifungua mwanaume huyo na kuliingiza ndani. Haraka sana akamfuata na kumfungulia mlango kisha kumwambia aelekee ndani pamoja naye.
“Jamani kaka yangu kuna nini? Mbona umenileta hapa na wakati uliniambia nije na pesa yako?” aliuliza Bi Sandra lakini Andrew hakujibu kitu.
Akawachukua wote wawili, yaani yeye na mtoto wake na kuwaingiza ndani. Alibadilika, hakutaka kuleta urafiki, alikuwa akiyafanya hayo kwa ajili ya familia yake ambayo wakati huo hakujua ilikuwa mahali gani. Akawapeleka ndani ya chumba kimoja kilichokuwa na mwanga hafifu na kuwahifadhi humo, akafunga mlango na kuondoka mahali hapo pasipo kuongea jambo lolote lile.
Bi Sandra alikuwa akilia na mwanaye, hawakujua kama mwanaume yule alikuwa Andrew, kijana waliyekuwa wakimpenda kutokana na utendaji wake mzuri wa kazi. Alitamani kumpigia simu mume wake na kumwambia kile kilichokuwa kimetokea lakini alishindwa kwani mwanaume yule alipowaacha chumbani, aliichukua simu yake na kuondoka nayo.
Andrew hakutaka kubaki mahali hapo, akaingia ndani ya gari na kuondoka mahali hapo. Moyo wake ulimuuma mno, hakuamini kama ingetokea siku angekuwa mtekaji kama alivyokuwa. Alikuwa tayari kufanya lolote kwa wakati huo kwa familia yake, hakutaka kuona ikiuawa na wakati alitakiwa kufanya jambo ambalo alikuwa na uwezo nalo.
“Nimefanya kama ulivyoniambia! Familia yangu ipo wapi?” aliuliza Andrew alipompigia simu Godwin.
“Utaipata tu. Kuwa mpole,” alijibu Godwin huku akitoa tabasamu pana.
Upande wa pili alichokifanya Godwin kilikuwa ni kumpigai simu Noel na kuanza kuzungumza naye. Alimuanzia mbali lakini mwisho wa siku akamwambia kwamba kulikuwa na ktu alichotaka kumwambia hivyo amsikilize kwa makini kabisa.
“Kwanza wewe nani?” aliuliza Noel huku akionekana kuwa na hamu ya kusikia jibu kutoka kwa mwanaume huyo.
“Huna haja ya kunifahamu mimi ni nani! Ila ninataka ufanye jambo moja tu. Kusimama hadharani na kumshauri rais kwamba anatakiwa kuachia madaraka haraka iwezekanavyo,” alisema Godwin maneno yaliyomfanya Noel kushangaa, kwanza akacheka kwani kile alichoambiwa kilikuwa ni kitu kisichowezekana hata kidogo.
“Hahaha! Unanichekesha sana rafiki yangu!” alisema Noel huku akicheka kwa dharau.
“Sawa. Mpigie simu mke wako uzungumze naye,” alisema Godwin na kisha kukata simu.
Hilo likamchanganya Noel, hakutaka kuchelewa, kama alivyoambiwa ndivyo alivyofanya, akapiga namba za mke wake, simu haikuwa ikipatikana, hakujua kulikuwa na kitu gani na kitendo hicho kilianza kumpa shaka kwamba inawezekana jamaa huyo alikuwa amefanya jambo fulani kwa mkewe.
Akapiga simu nyumbani, akapokea mfanyakazi wa ndani ambaye alimwambia kwamba Bi Sandra hakuwepo, aliondoka kwenda mahali fulani, hakuaga, aliondoka ghafla sana.
“Hujui alipoondoka?”
“Ndiyo!”
“Hebu subiri!”
Akakata simu, alichanganyikiwa kwa kuhisi kwamba kweli kulikuwa na tatizo lililokuwa limetokea. Haraka sana akampigia Andrew ili kujua mahali alipokuwa mke wake. Alipompigia, mwanaume huyo alimwambia kwamba mke wake aliondoka, alipoondoka, hakukuwa na mtu aliyekuwa akijua kwani alisema kwamba angerudi kama siku nyingine.
“Kwa nini hukuwaambia vijana kwenda naye?” aliuliza Noel.
“Alikataa katakata! Tukaona haina shida kiongozi, tukafanya kama alivyotaka. Kwani kuna tatizo lolote mkuu?” alisema Andrew na kuuliza kana kwamba hakujua kilichokuwa kimetokea.
Noel hakujibu swali hilo, akakata simu na kuondoka ofisini kwake kuelekea nyumbani. Alichanganyikiwa, alihisi kaibisa kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea, ilikuwaje apigiwe simu na mwanaume huyo na kuambiwa kuhusu mke wake na wakati aliondoka nyumbani na hakukuwa na mtu aliyejua?
Wakati akiwa njiani, akasikia simu yake ikilia mlio ulioashiria kwamba kulikuwa na ujumbe umeingia, haraka sana akaichukua simu yake na kuangalia ujumbe huo, ulikuwa uliosomeka ‘mkeo ametwekwa. Usijisumbue sana kumtafuta. Fanya nilichokwambia, vinginevyo nitawaua wote wawili, yeye na mtoto wako. Kingine cha msingi, hatakiwi mtu yeyote afahamu kama wametekwa, kitendo cha kufahamu tu kinamanisha kwamba utazikuta maiti zao baharini hapo kesho’.
“Wewe ni nani?” aliuliza baada ya kupiga simu.
“Mshikaji wako! Unatakiwa kufanya kila kitu nilichokwambia kwenye meseji na mara ya kwanza nilipokupigia simu. Una siku tatu tu za kufanya hivyo,” alisema Godwin na kisha kukata simu.
Ulikuwa ni mtihani ambao hakufikiria kama ingetokea siku moja angekuja kukutana nao. Akasimamisha gari pembeni na kuegemea usukani. Alikuwa na mwazo mengi kichwani mwake, ni kweli aliipenda familia yake lakini kuzungumza hadharani kwamba Rais Bokasa alitakiwa kujiuzulu lilikuwa jambo gumu mno.
Alimfikiria rais huyo, alikuwa mtu muhimu kwake, alikuwa akishirikiana naye kwenye kila kitu, hakuona kama kulikuwa na sababu ya kufanya mambo hayo yote, alipambana kila siku na alimuhakikishia kwamba kila kitu kilichokuwa kimeharibika kingewekwa sawa lakini kitu cha ajabu hata kabla hajaweka sawa mambo yake, tayari alitakiwa kumkana.
Hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya. Kwa siku tatu alizokuwa amepewa zilikuwa chache sana hivyo alichokifanya ni kuelekea nyumbani kwake, alipofika tu, hakumuuliza mtu yeyote juu ya mke wake, alikumbuka kwamba aliambiwa hakutakiwa mtu yeyote afahamu kilichokuwa kimetokea.
Akaingia chumbani kwake na kulia sana, alishindwa kujua ni kitu gani alitakiwa kufanya lakini baada ya kulia sana, akaamua kusimama, kichwani mwake ulikuja uamuzi mmoja tu, kufanya kile alichoambiwa na mwanaume yule, kumtaka Rais Bokasa aachie madaraka haraka sana kwani nchi haikuwa ikielekea mahali pazuri.
“Nitazungumza kwa ajili ya familia yangu!”
Huo ndiyo uamuzi aliokuwa ameuchukua, hakutaka kuchelewa, huku akilia, akachukua simu yake na kumpigia rais kwa lengo la kuzungumza naye na kumwambia kwamba kuna kitu alikuwa njiani kwenda kukifanya hivyo asishangazwe na uamuzi huo, alikuwa akifanya hivyo kwa ajili ya familia yake tu.
“Kitu gani?” aliuliza Rais Bokasa, katika siku zote alizokuwa akimfahamu Andrew, hakukuwa na siku aliyosikia au kumuona akilia kama siku hiyo.
“Ni uamuzi mgumu sana, utakuumiza lakini nakuomba unielewe kwamba ninafanya haya kwa ajili ya familia yangu. Ninaipenda, ni kila kitu kwangu, siwezi kuiona ikiangamia na wakati nina uwezo wa kufanya jambo lolote lile kuiokoa,” alisema Andrew.
“Kuna nini tena?” alisikia rais akiuliza.
“Naomba unisamehe!”
“Nikusamehe kwa lipi? Niambie! Unataka kujiuzulu?”
“Hapana!”
“Kumbe?”
“Naomba unisamehe mheshimiwa rais, ninafanya hivi kwa ajili ya familia yangu,” alisema Andrew na kukata simu.
Hakuacha kulia, alikuwa akijifikiria ni kwa namna gani angelifanya jambo hilo. Alijua ni kwa jinsi gani watu wangeshtuka, alijua kwamba kila kona angezungumziwa yeye kwa kile alichokuwa akitaka kukifanya lakini hakutaka kujali, ilibidi kufanya vile kwa ajili ya familia yake tu.
Rais Bokasa alichanganyikiwa, hakujua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea, alimpigia simu Andrew kwa lengo la kuzungumza naye na kugundua tatizo alilokuwa nalo lakini mwanaume huyo hakutaka kupokea simu tena.
Alichokifanya ni kufunga safari na kumfuata nyumbani kwake, Masaki. Alitaka kujua kila kitu kilichokuwa kimetokea mpaka kutaka kufanya uamuzi huo ambao aliamini kwamba ungekuwa ni wa kumuumiza kupita kawaida.
Alipofika nyumbani kwake, hakumkuta mwanaume huyo, aliambiwa kwamba alitoka kwenda kuzungumza na waandishi wa habari kwani alikuwa na jambo zito alilotaka kulizungumza.
“Amekwenda kukutana na waandishi wa habari?” aliuliza Rais Bokasa.
“Ndiyo mkuu! Ana press na waandishi!”
“Wapi?”
“Habari Maelezo!”
Hakutaka kuchelewa, ilikuwa ni lazima kwenda huko haraka sana. Wakati akiwa njiani, akafungua redio ya Taifa kwa lengo la kusikia kilichokuwa kikiendelea huko. Mtangazaji alitangaza kwamba kulikuwa na mkutano uliotarajiwa kuanza muda mfupi ujao kwani Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Bwana Noel alikuwa na mambo ya kutaka kuzungumza na waandishi wa habari Tanzania nzima.
“Wahini kabla hajaanza kuzungumza,” alisem Rais Bokasa huku akionekana kuchanganyikiwa, aliamini kwamba kwa lolote ambalo mwanaume huyo angelizungumza kwa waandishi hao lilikuwa jambo la kumuumiza tu kitu ambacho hakutaka kabisa kuona kikitokea.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumanne ijayo hapa
 
Jackal tisha sana. Ila hujatuambia kuwa ni lini tena mzigo unawekwa. Asante sana
 
Shunie, shunie, shunie tafadhsli huyo Halima ashindwe kwa jina la Y na Godwin wetu afanye mambo. Bwana Noel Fanya kitu roho ipende na Bokasa asifanikiwe kufika huko mapema.!!
 
Story hii ingekuwa mfumo wa movie ..ingekuwa ya kusisimua saana
Sema tatizo serikari haisupport saan zetu
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom