Dunia haina usawa

Dunia haina usawa

DUNIA HAINA USAWA

Godwin alikuwa ndani ya gari na wanaume wale, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea mahali hapo, aliwaangalia watu hao ndani ya gari lile, alijifanya kushangaa na wakati mwingine kuwauliza kilichokuwa kikiendelea mpaka yeye kukamatwa.
Hakukuwa na mtu aliyemjibu kitu chochote kile, kila mmoja alikuwa kimya huku akionekana kuwa bize na mambo yake. Godwin akaanza kujitetea kwamba yeye hakuwa mwizi, alikuwa mpiga debe na hata hakuwa akivuta bangi zaidi ya kuvuta sigara ambayo nyingine alikuwa nayo sikioni.
Gari liliendeshwa mpaka kufika Kibamba kwenye jumba moja kubwa. Likasimamishwa na kuingizwa ndani ya jumba hilo lililokuwa na eneo kubwa sana ambapo hapo akawakuta wanaume wengine wengi wakiwa humo.
Alishangaa, hakujua kilichokuwa kikiendelea. Kila mtu aliyemuona akiingia, alikuwa akimwangalia, watu hao waliokuwa humo waliendelea kujiuliza maswali juu ya sababu zilizowafanya kuwa mahali hapo.
“Tumefanya nini?” aliuliza jamaa mmoja.
“Sijui! Mimi nilikuwa nachoma mahindi! Washikaji wakaja na kunidaka,” alisema jamaa mmoja.
“Daah! Poapoa! Ngoja tusubiri! Tutajua ukweli. Naitwa nani?” alisema jamaa mmoja.
“Godwin!”
“Godwin?”
“Ndiyo!”
“Hata mimi naitwa Godwin!”
“Duuh! Kama bahati vile, jina hili huwa adimu sana,” alisema jamaa mmoja na mtu aliyekuwa pembeni akasikia na yeye kuwageukia wenzake.
“Kumbe na nyie mnaitwa Godwin! Hata mimi naitwa Godwin,” alisema mwanaume aliyekuwa akiwaangalia.
Mwanzo walihisi kama muujiza fulani lakini walipokuwa wakiwaulizana zaidi wakagundua kwamba kila mmoja aliyekuwa ndani ya jumba hilo alikuwa akiitwa Godwin.
Hapo ndipo wakapata jibu sababu ya kuwa ndani ya jumba hilo. Kulikuwa na mtu aliyekuwa akitafutwa ambaye waliamini kwamba kama wangewakamata watu waliokuwa na jina hilo basi ingekuwa rahisi kwao kusimamisha kile kilichokuwa kikiendelea mitandaoni.
Wakati watu hao wakiwa wamekamatwa na kupelekwa ndani ya jumba lile, huku nyuma maofisa wa usalama walikuwa wakiendelea kufuatilia kuona kama mtu aliyekuwa akitumia akaunti ile alikuwa akiendelea kufanya hivyo.
Siku ya kwanza ikapita, ya pili, ya tatu mpaka siku ya nne ambapo hawakumuachia mtu yeyote yule, bado akaunti hiyo haikuwa imetumiwa kuonyesha kwamba mtu waliyekuwa wakimuhitaji alikuwa ndani ya jumba lile.
“Tunahisi mtumiaji wa akaunti hii yupo ndani ya jumba hili,” alisema ofisa mmoja wa usalama wa taifa.
“Sawa. Ila ni nani? Tuna watu zaidi ya mia saba, tutajua yupi ni yupi?” alihoji jamaa mwingine.
“Ni rahisi sana! Tuwe tunaruhusu watu watano halafu tuwe tunaangalia ni kitu gani kitaendelea,” alisema jamaa mwingine na kukubaliana kufanya hivyo.
Wakati hayo yakiendelea, kila mtu aliyekuwa ndani ya jumba lile alijua sababu iliyowapelekea kuwa humo. Godwin alikuwa na wasiwasi tele, aliamini kwamba kama asingekuwa makini basi watu hao wangeweza kugundua kwamba mtu aliyekuwa akitafutwa alikuwa yeye.
Alikuwa muulizaji mkubwa, kila wakati alikuwa mtu wa kuwauliza watu waliokuwa wakiwalinda kwamba nini ilikuwa sababu ya kufika mahali hapo lakini hakukuwa na mtu aliyemjibu chochote kile.
Humo, walikuwa wakiishi vizuri, waliletewa vyakula kila siku, walipewa huduma zote muhimu, nguo na kila kitu walichokuwa wakikihitaji isipokuwa simu tu. Pamoja na kufanyiwa yote hayo lakini bado hakukuwa na mtu aliyekuwa na furaha hata kidogo, kila mmoja alihitaji sana kuwa huru na si kufungiwa humo kama kuku.
Baada ya siku ya tano kuingia ndipo hapo wakaanza kutolewa. Idadi ambayo walikuwa wakitakiwa kutoka ilikuwa ni watu watano. Kabla ya kutoka walikuwa wakipigwa picha na kisha kupelekwa mpaka nyumbani kwao halafu kuwasikilizia kwa siku mbili kuona kama akaunti ile ingeandikwa kitu chochote kile.
“Kwa watano wa kwanza, hakuna mhusika. Hebu tuoneni watano wengine,” alisema mkurugenzi wa usalama wa taifa.
Ilikuwa kazi kubwa na ngumu lakini hawakuwa na jinsi, walichokuwa wakisema ni kwamba walitaka kuiokoa nchi yao kutokana na hali iliyokuwa ikiendelea ambayo walihisi kwamba kama wasingefanya juu chini basi nchi hiyo ingeweza kuchafuka.
Watu walitolewa zaidi, waliendelea kutolewa na baada ya mwezi mmoja na nusu ndipo Godwin ikafika zamu yake na kutolewa ndani ya jumba hilo. Mara baada ya kupigwa picha, yeye na wenzake wanne wakapakizwa ndani ya gari na kuanza kurudishwa nyumbani.
Hakukuwa na aliyejua kama walitakiwa kufuatilia kila walipokuwa wakiondoka, Godwin hakulijua hilo, moyo wake ulikuwa umevimba, alikuwa na dukuduku kubwa moyoni mwake kwamba atakapofika nyumbani ilikuwa ni lazima kuchukua simu yake na kuandika posti ndefu kwa kuwakashifu maofisa wa usalama wa taifa kwamba hawakuwa wakimtisha na kamwe wasingeweza kumgundua hata kama wangefanya nini.
“Nitawaonyesha! Subiri nifike nyumbani.”
Akapelekwa mpaka katika Kidtuo cha Daladala cha Makumbusho alichokuwa amechukuliwa kabla. Washikaji zake wote walikuwa wakimwangalia kwa mshangao, walitaka kufahamu kilichokuwa kimeendelea huko alipochukuliwa na watu wale.
“Walitupeleka sehemu fulani hivi, wapuuzi sana wale,” alisema Godwin.
“Kwa nini walikuchukua wewe tu hapa?”
“Sijajua! Au kwa sababu naonekana navuta bangi!”
“Hapana! Mikono yenyewe laini kama demu, kwa nini wakuhisi hivyo?” aliuliza jamaa mmoja huku akimwangalia Godwin kwa mtazamo ulioonyesha kutamani kusikia ukweli juu ya kile kilichokuwa kimetokea huko.
“Sijajua! Niambieni, nimemisi nini kijiweni?” aliuliza Godwin huku akiwatoa watu hao kwenye ishu nzima ya kukamatwa.
“Demu wako alikuwa anakuja sana hapa!”
“Nani? Winfrida?”
“Ndiyo! Anasumbua kinoma, anasema kwenye simu hupatikani. Atakuja tu manake ndiyo mida yake hii,” alisema rafiki yake huyo.
Hakutaka kubaki mahali hapo, hakupenda kuonana na Winfrida na wakati moyo wake ulikuwa na dukuduku kubwa la kuandika kila kitu kilichokuwa kimetokea kule walipokuwa wamepelekwa.
Hakujua kwamba maofisa wale walikuwa wakifautilia kwenye akaunti ile ili kama wangeona posti yoyotesiku hiyo basi wajue kwamba miongoni mwa watu watano waliokuwa wamewaachia siku hiyo, mmojawapo ndiye alikuwa Godwin waliyekuwa wakimtafuta.
Hakuchukua muda mrefu akafika nyumbani, akaichukua simu yake, akaiwasha kisha kuingia Instagram ambapo huko akakutana na maoni mengi ya watu huku wengine wakiuliza maswali alikuwa wapi.
“Nimerudi!” alianza kuandika kwa kusindikizia na picha iliyoonyeshwa minyororo iliyofunga mikono ya watu ikiwa imekatika kumaanisha kwamba alikuwa huru.
Akaanza kuandika ujumbe mrefu hata kabla ya kuposti. Alielezea kila kitu kilichokuwa kimetokea huko, jinsi walivyokuwa wakiishi na hata uzembe waliokuwa nao usalama wa taifa. Alipomaliza, akaisoma posti ile na kujiandaa kuposti, akaifuata sehemu iliyoandikwa ‘share’ tayari kabisa kwa kuipost posti hiyo.
***
Hali ya Rais Bokasa iliendelea kuimarika kitandano alipokuwa, kila alipokumbuka sababu iliyomfanya kuwa kitandani hapo alibaki akilia, hakujua kama kiasi cha pesa kilichoondolewa katika akaunti yake kilirudishwa au la.
Alikuwa akilia, maishani mwake ilikuwa ni afadhali kukosa kitu chochote kile lakini si pesa alizokuwa ameibiwa. Aliiangalia familia yake, alikuwa akisikitika kwani alijua kwamba kama ingetokea siku ambayo angetoka madarakani, basi kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuzitumia pesa hizo na familia yake na ndiyo maana alikuwa ameziiba kwa kipindi kirefu.
Kupata ahueni kwa afya yake ilikuwa taarifa mbaya kwa Watanzania, hawakumpenda, walimchukia mno na katika kipindi chote alichokuwa nchini India, wengi walikuwa wakiombea afariki dunia kidogo ingeweza kuifanya Tanzania kuwa mpya, rushwa ipungue na hata pesa zipatikane kama kipindi cha nyuma.
Akapooza upande mmoja, akawa mtu wakusukumwa katika kibaskeli cha walemavu, hakuwa mzungumzaji sana kama zamani, alitia huruma, alisikitisha mno, yaani rais yule yule, mjanja, aliyekuwa akiwahujumu wananchi wake leo hii alikuwa kwenye kiti cha mataili.
Akaruhusiwa kurudi Tanzania, hakupokelewa kwa shangwe kama ilivyokuwa kwa marais wengine waliopita, alipokelewa kwa manenoo ya kejeli kwenye mitandao ya kijamii huku wengine wakiweka wazi hisia zao kwamba kama ingewezekana basi rais huyo afe hukohuko alipokuwa, ila wengine wakaibuka na kusema kwamba kwa kitendo cha kupooza mwili wake kilionyesha ni kwa jinsi gani Mungu alikuwa amewalipia.
“Bora! Manake alituonea sana, mnapoona Mungu yupo kimya msifikiri ni kiziwi hasikii au kipofu haoni,” aliandika jamaa mmoja pasipo kusema wazi kile kilichokuwa kimetokea, aliandika hivyo kama kuweka utata ili asichukuliwe hatua na sheria za mitandaoni.
Rais Bokasa hakuwa na amani hata kidogo, mawazo yalimtesa na muda mwingi alikuwa akizifikiria pesa zake, zilikuwa nyingi mno na aliamini ili kuzipata tena basi ingemchukua miaka na miaka.
Akaendelea kuwa rais wa Tanzania, kila siku akawa anawasiliana na vijana wake juu ya mahali walipofikia kumtafuta mwanaume aliyemfanya kukosa amani, mwanaume aliyemuibia pesa na kumsababishia matatizo aliyokuwa nayo.
“Yupo wapi?” aliuliza rais huyo.
“Bado hatujampata ila tumefanya jambo moja kubwa sana,” alisikika mkurugenzi wa usalama wa taifa.
“Jambo gani?”
“Tumewakamata wakina Godwin wote Dar es Salaam, na kweli tumefanikiwa kwani mpaka sasa hakuna kitu chochote kilichoandikwa katika ile akaunti,” alisema mkurugenzi huyo.
“Kwa hiyo huyo mwenyewe yupo humo?” aliuliza.
“Tunahisi. Sasa tunataka tuwaruhusu watano kwa siku kadhaa tuone kundi lipi likitoka posti itaandikwa ili tujue cha kuwafanya,” alisema mkurugenzi huyo.
“Wazo zuri! Hakikisheni mnafanya hivyo. Jamani huyo mtu akikamatwa, nitazungumza na majaji anyongwe tu,” alisema Rais Bokasa huku akionekana kuwa na hasira na mwanaume huyo.
Hilo ndilo lililofanyika, kwa kila kundi walilokuwa wakilitoa kazi yao kubwa ilikuwa ni kuangalia kwenye akaunti ile ili kama wataona kuna posti imeandikwa basi wajue kwamba ni kundi hilo ndilo lililohusika na hivyo kuwakamata tena.
Wakati wakiendelea kusikilizia, Godwin alikuwa amemaliza kuandika posti hiyo katika akaunti ya Mabadiliko ya Kweli ya Instagram na kilichokuwa kikifuatilia ni kuposti posti hiyo.
Alikwishakwenda sehemu iliyoandikwa share lakini hata kabla ya kuposti, akaanza kuingiwa na hofu, akaanza kujiuliza maswali mengi kwamba kwa nini walikuwa wakiruhusiwa watanowatano kwa siku kadhaa, akahisi kitu, akajua kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea, tena akahisi kabisa kwamba kama siku hiyo angeandika kwamba ni leoleo basi wangeweza kufuatiliwa, hivyo harakaharaka akabadilisha posti nzima na kuandika ‘Wakina Godwin wengi tulitekwa na watu wanaojidai usalama wa taifa, wiki iliyopita siku ya Jumatatu tukaruhusiwa, nimerudi uswahili pasipo kugundulika, sasa naanza tena kazi’ aliandika na kisha kuposti katika akaunti hiyo.
Kila mtu aliyeiona posti hiyo akafurahia, wengi wakamkaribisha kwa mbwembwe na kumshukuru Mungu kwa kumrudisha tena uraiani na hivyo kuendelea kupambana.
Godwin hakuishia kuandika posti hiyo tu bali alichokifanya ni kuifungua akaunti yake ya WhatsApp, akaona ametumiwa picha kwa namba ngeni, harakaharaka akaifungua na kuanza kuiangalia, ilikuwa picha iliyotoka katika namba ngeni ambayo hakujua kama ilikuwa ni namba ya wale wapelelezi, Thomas First na Bruno Mendez waliotoka nchini Uswisi ambao walitaka kujua alikuwa Tandale sehemu gani.
Usalama wa taifa waliokuwa wakifuatilia walipoiona posti hiyo, haraka sana wakawasiliana na wenzao na kuwaambia kwamba mtu waliyekuwa wamemshikiria na kumuachia alikuwa ameibuka tena na alikuwa katika kundi la watu walioondoka siku ya Jumatano wiki iliyopita.
Hawakutaka kuchelewa, haraka sana wakawasiliana na wenzao na kuwaambia kwamba ilikuwa ni lazima kuwatafuta watu wote waliowaruhusu siku ya Jumatano kwa ajili ya kuwarudisha tena na kubaki nao pasipo kugundua kwamba mtu aliyekuwa ameandika posti hiyo alitolewa siku hiyo kule walipokuwa wamehifadhiwa.
“Hakikisheni wote mnawapata. Si mnazo picha zao?” aliuliza mkurugenzi.
“Ndiyo!”
“Na wote mnajua wanapoishi au vijiwe vyao?”
“Ndiyo!”
“Basi watafuteni,” aliagiza na kisha kukata simu.
****
Moyo wa Winifrida uliendelea kuuma, aliumia kupita kawaida, kila siku alikuwa akienda katika Kituo cha Daladala cha Makumbusho kwa ajili ya kumuona mwanaume wa ndoto yake, mwanaume aliyeuteka moyo wake na kuuburuza vilivyo.
Siku moja alipofika hapo, akaambiwa kwamba Godwin hakuwa mahali hapo, alitekwa na watu wasiojulikana na kuondoka naye. Moyo wake ulichoma, alihisi kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa kumuona mpenzi wake akiwa hai kwani wengi waliokuwa wakitekwa na gari aina ya Noah walikuwa wakiuawa na wakati mwingine kurudishwa wakiwa walemavu.
Akabaki akimuomba Mungu amlinde Godwin huko alipokuwa. Hakuacha kwenda Makumbusho, mara kwa mara alikuwa akienda huko kwa ajili ya kusikilizia kama mpenzi wake alikuwa amerudi au la.
Siku zilikatika mpaka siku ambayo alikwenda huko na kuambiwa kwamba mwanaume huyo alikuwa ameruhusiwa siku hiyo lakini kwa bahati mbaya alikuwa ameondoka na kurudi nyumbani kwake alipokuwa akiishi huko Tandale.
“Naomba mnielekeze,” alisema Winfrida.
“Haina shida!”
Akaanza kuelekezwa alipokuwa akiishi mwanaume huyo, hakutaka kupoteza muda hapo kituoni, akaondoka zake na kuelekea Tandale ambapo aliamini kwamba angemkuta mpenzi wake huko.
Hakuchukua muda mrefu akafika Tandale, akaanza kuulizia mpaka pale alipokutana na mtu aliyekuwa akimfahamu mwanaume huyo na kuanza kumpeleka huko alipokuwa akiishi.
Alipofika katika nyumba hiyo, moyo wake ulimuuma mno, hakuamini kama mwanaume aliyekuwa akimpenda alikuwa akiishi katika nyumba chakavu kama hiyo. Akaingia ndani, akakaribishwa na mwanamke aliyekaa ukumbini akikuna nazi.
“Karibu dada,” alimkaribisha mwanamke huyo.
Akamuulizia Godwin, akaambiwa kwamba alikuwa chumbani kwake, akaonyeshewa mlango na kwenda kugonga, sekunde ishirini nyingi, mlango ukafunguliwa na mwanaume huyo.
Moyo wa Winfrida ukamlipuka, hakuamini kama angeweza kumuona mpenzi wake, akamsogelea na kisha kumkumbatia kwa furaha ambayo ilimzidi na kuanza kumtoa machozi.
“Nimekukumbuka mpenzi,” alisema Winfrida huku akilia kwa furaha.
“Nimekukumbuka pia. Karibu,” alisema Godwin na kuingia naye ndani.
****
Walichokuwa wakikisubiri Thomas First na Bruno Mendez ni kuona picha ile ikipakuliwa na kuonekana mahali alipokuwa mpakuaji huyo. Baada ya kupiga siku kadhaa, wakaona picha ile ikiwa imepakuliwa ambapo moja kwa moja WhatsApp wakawapa eneo la mahali picha hiyo ilipopakuliwa.
“Tandale!” alisema Bruno.
“How can we get there?” (tutafikaje?)
“We have Google Map, let’s roll,” (tuna Google Map, twende) alisema Thomas na kuanza kuondoka kwenda huko.
Kutumia programu hiyo ya Google Map iliwarahisishia kupafahamu mahali walipokuwa wakielekea. Walichukua teksi na kuelekea huko ambapo hawakuchukua muda mrefu wakafika na kuendelea kuifuata simu yao ambayo ilionyesha mahali Godwin alipokuwa.
“We are hundred metre from red dot,” (tupo umbali wa mita mia moja kutoka kwenye kidoti chekundu) alisema Thomas huku wakiiangalia simu yao iliyoweza kuidukua simu ya Godwin, kidoti chekundu ndicho kilichokuwa kikionyesha mahali simu ya Godwin ilipokuwa.
Walitembea kwa mwendo wa haraka, kitendo cha kuwasiliana na WhatsApp na kuwaambia kwamba mwanaume huyo alikuwa Tandale na tena kuwapa ramani ya kumpata kwa kutumia simu yake iliwapa unafuu kupita kawaida.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika nje ya nyumba moja na kusimama kwa nje, kidoti kilisema kwamba mtumiaji wa simu hiyo alikuwa ndani ya nyumba hiyo. Wakatoa bastola zao, hata watu waliokuwa hapo nje hawakutaka kuzungumza nao, wakaingia ndani, kitu walichokuwa wakikitaka ni kumkamata Godwin ambaye walihisi kwamba alikuwa ndani ya nyumba hiyo.
Wakatembea mpaka kulipokuwa na chumba ambacho kilionyesha kwamba ndani ya nyumba hiyo ndipo kulipokuwa na mtu huyo, walipotega sikio, wakasikia mwanaume na mwanamke wakizungumza ndani ya chumba hicho, hawakuwa na wasiwasi, hapohapo kwa teke moja tu, wakavunja mlango na kuingia ndani huku bastola zikiwa mikononi mwao.
“You are under arrest,” (upo chini ya ulinzi) alisema Thomas huku akiwa ameshika bastola yake, mwanaume huyo aliyeshika simu akaanza kutetemeka kwa hofu, akatamani kukimbia, akashindwa, alitamani hata kujificha chini ya kitanda, napo akashindwa, msichana aliyekuwa pembeni yake ambaye alikuwa mpenzi wake, akabaki akilia tu.
***
Mkurugenzi wa usalama wa Taifa Tanzania, Bwana Idrisa alikuwa na taarifa za kuwepo kwa maofisa wa Usalama wa Taifa wa nchini Uswisi nchini Tanzania lakini kitu cha ajabu kabisa mpaka kipindi hicho hakuwa amepewa taarifa juu ya mahali walipokuwa watu hao.
Akawasiliana na vijana wake kwa lengo la kutaka kujua mahali walipofikia maofisa hao, hilo halikuwa tatizo, wakamwambia mahali walipofikia na hivyo kuwatuma kwenda huko kwani alitaka kuzungumza nao hata kabla hawajaanza kazi ya kumtafuta Godwin.
Vijana wake wakaelekea huko lakini hawakuweza kuruhusiwa kwani watu hao walikataa kuonana nao na hivyo kuambiwa kurudi kesho. Hilo halikuwa tatizo, wakampa taarifa Idrisa ambaye akakubaliana nao na hivyo siku iliyofuata kurudi tena.
“Waliondoka,” alisema dada wa mapokezi.
“Kwenda wapi?”
“Walinionyeshea ramani, wakasema Tandale, ila sijajua Tandale sehemu gani,” alisema daa huyo, aliambiwa mahali walipokuwa wakielekea Thomas na mwenzake kwa kumuonyeshea ramani hata kabla ya kuchukua teksi.
Hawakutaka kubaki mahali hapo, wakahisi kwamba kulikuwa na kitu mahali huko hivyo nao kuanza kwenda Tandale. Hawakuchukua muda mrefu wakafika, hawakujua wanaume hao walipokuwa wameelekea, walitaka kuuliza lakini hawakujua wangeuliza kwa jinsi gani ili waweze kuwapata.
Wakati wakiangalia huku na kule, wakaliona kundi la vijana, wakaona hiyo ndiyo ilikuwa nafasi yao ya kuwauliza kwani kwa jinsi walivyokuwa wengi, iliwezekana kuwauliza kuhusu Wazungu na wakapata kitu cha kuwaambia. Walipowakaribia, vijana hao nao walikuwa bize kuzunungumzia habari ambayo ikawafanya kusogea zaidi.
“Aisee! Wale Wazungu kama Arnold na Rambo. Kwanza wapo seriazi sana, halafu ile miwani, cheki zile bastola walizokuwa nazo, kitu cha Hollywood kabisa,” alisema jamaa mmoja, alikuwa akiwaambia wenzake.
“Kweli kabisa. Mhuni alivyotulia, anabaki analialia tu. Sasa sijui kwa nini wamekwenda kumkamata msela, au anauza madawa ya kulevya?” aliuliza mwingine.
Mpaka kufikia hapo maofisa wa usalama wa taifa wakaona kabisa kwamba hakukuwa na kazi kwao kuwatafuta wanaume hao, walichokifanya ni kuendelea kusikiliza kwani mwisho wa siku wangesema mahali walipokuwa.
“Sasa wanampeleka Marekani au?” aliuliza jamaa mmoja.
“Sijajua. Wameanza na hapo kituoni, sasa sijui nini kitaendelea. Ila ishu ilikuwa kama muvi la kibabe vile,” alisema jamaa mwingine.
Hawakutaka kuuliza, wakajua kwamba Wazungu hao walikuwa wameelekea katika Kituo cha Polisi cha Tandale na hivyo kuanza kwenda huko. Gari liliendeshwa kwa mwendo wa kasi, lilipita Tandale Sokoni kama lilikuwa kwenye mashindano ya magari kiasi kwamba kila mtu alikuwa akishangaa.
Ni ndani ya dakika mbili tu tayari walikuwa wamefika kituoni hapo, wakateremka na kuanza kwenda ndani ambapo wakawakuta Thomas na Bruno wakiwa kituoni hapo, wakawasalimia na kujitambulisha, hawakuishia hapo, wakataka kuonana na mkuu wa kituo na kuzungumza naye.
“Imekuwaje?” aliuliza jamaa mmoja, huyu aliitwa Issa.
“Hawa Wazungu wamemleta mtuhumiwa hapa,” alijibu mkuu wa kituo.
“Mtuhumiwa wa nini?”
“Si unajua ile ishu ya Godwin wa mtandaoni?”
“Ndiyo!”
“Ndiyo wamemleta. Wameniambia kwamba walikuwa wakifuatilia simu yake kwa kutumia GPS na hatimaye waliweza kubaini kwamba alikuwa Tandale na ndiyo maana wamekuja naye hapa,” alijibu mkuu wa kituo.
“Godwin?”
“Ndiyo! Wamefanikiwa kumpata!”
“Hebu tumuone!”
****
Kwa jinsi walivyoonekana, Thomas na Bruno walikuwa na hasira kali, walimwangalia mwanaume waliyekuwa wamemvamia chumbani kwake na kumchukua mzobemzobe na kutopka naye ndani huku wakimwacha mwanamke yule akilia ndani ya chumba kile.
Watu kutoka sehemu nyingine wakashangaa, hawakujua kitu kilichokuwa kikiendelea, hawakujua wale Wazungu walikuwa wakina nani na kwa nini walikuwa wakimkamata mwanaume huyo aliyejulikana Tandale kwa ukorofi na ulevi kupindukia.
Kwa jinsi Wazungu wale walivyoonekana, hawakuwa watu wa mchezomchezo hata kidogo, mikononi mwao walikuwa na bastola huku wakiwa wamevaa miwani hali iliyoonyesha hawakutaka kusogelewa hata kidogo.
Walimchukua mtu wao, wakamuingiza ndani ya teksi na kumwambia dereva kwamba walitakiwa kupelekwa kituo cha polisi.
“Braza! Waambie mimi sijafanya jambo lolote lile. Braza, waambie braza watakuwa wananionea tu,” alisema mwanaume huyo huku akilia, hakupigwa, ila kwa jinsi alivyokuwa ameshikwa wakati akipelekwa ndani ya gari, alishikwa kwa staili iliyomuumiza nyonga.
Dereva hakujibu kitu, alinyamaza tu mpaka walipofika kituoni ambapo wakamshusha kwa staili ileile iliyompa maumivu makali na kumpeleka kituoni ambapo walitoa maelezo yote kuhusu mwanaume huyo huku wakisema kwamba ilikuwa ni lazima kusafirishwa na kupelekwa nchini Uswisi haraka iwezekanavyo.
“Okey! Let’s loc him up,” (sawa! Acha tumfunge kwanza) alisema mkuu wa kituo.
Walichokifanya ni kuwasiliana na mkuu wao nchini Uswisi na kumwambia kwamba walifanikiwa kumpata Godwin aliyekuwa amejifungia uswahili Tandale kitu kilichomfurahisha kila mmoja na kuona kwamba kazi kubwa waliyokuwa nayo ilikuwa imefanikiwa kwa asilimia mia moja.
Mpaka Issa na wenzake wanafika kituoni hapo, tayari zilikuwa zimepita dakika ishirini, wakaambiwa kila kitu na kuhitaji kumuona Godwin na hivyo kuruhusiwa, walipomuona, hawakuamini kama kijana huyo angeweza kuisumbua serikali kiasi hicho, na hawakuamini kama kwa jinsi alivyokuwa alikuwa na uwezo hata wa kuwasha kompyuta.
“Yaani wewe ndiye umetusumbua sana mpaka rais wetu kupooza, hakika kiama chako kimefika,” alisema Issa huku akionekana kuwa na hasira mno.
“Braza sijafanya kitu. Braza...braza watasha wananionea, sijafanya kitu,” alisema mwanaume huyo huku akilia kama mtoto.
Hakukuwa na mtu aliyejali kitu chochote kile, walichokijua ni kwamba huyo ndiye mtu waliyekuwa wakimuhitaji, haraka sana mawasiliano yakafanyika, rais Bokasa akaambiwa kwamba Godwin alikuwa amepatikana.
Kwa jinsi alivyokuwa na hamu ya kumuona, hakutaka hata kubaki ikulu, akaagiza kwamba kijana huyo abakizwe hapohapo na yeye kwenda huko kituoni, alikuwa na hasira naye mno, alikuwa na uwezo wa kumnyonga hata siku hiyo ila kwa kuuwa Wazungu wale walikuwa na kazi naye, akaamua kumwangalia kwa hasira sana huku akiwa haamini kama kijana huyo ndiye aliyewasumbua namna hiyo.
“Ninahitaji pesa zangu! Ninahitaji pesa zangu, kwa jinsi ulivyozichukua kwenye akaunti yangu, zirudishe mulemule,” alisema rais mara baada ya kufika katika kituo hicho.
Thomas na Bruno hawakutaka kuzungumza jambo lolote lile, walichokuwa wakikihitaji ni kumchukua kijana huyo na kuondoka naye kuelekea nchinii Uswisi kwa ajili ya kufunguliwa kesi na kuzirudisha pesa zile katika akaunti aliyokuwa amezichukua.
Siku iliyofuata, kijana huyo akapandishwa ndani ya ndege. Siku hiyo ilikuwa ni hatari, kila kona stori zilikuwa zimetapakaa kwamba Godwin alikuwa amekamatwa, kwenye mitandao ya kijamii, stori zilikuwa ni Godwin ambapo taarifa hizo ziliendelea kusoma kwamba mtu huyo alikuwa njiani kuelekea nchini Uswisi.
Kila mmoja alisikitika, Godwin alikuwa shujaa wao, wengine walilalamika mpaka kulia, kwa jinsi mwanaume huyo alivyoonekana, alionekana kuwa shujaa mkubwa ambaye alitakiwa kupewa heshima kwani alikuwa na uchungu mpaka kuanza kuikosoa serikali pale ilipokuwa ikikosea.
“Kwa hiyo Mabadiliko ya Kweli ndiyo basi tena?” aliuliza jamaa mmoja.
“Ndiyo! Wazungu wamekuja kumkamata na kuondoka naye. Wale jamaa noma sana, sijui walimpataje!” alisema jamaa mmoja huku akionekana kushangaa.
Ndege ilichukua saa kumi na sita ndipo ikafika nchini Uswisi ambapo maofisa wa usalama wa taifa nchini humo, FIS walikuwa wakiwasubiria mahali hapo. Mtu huyo alipoteremshwa, akapakizwa ndani ya gari na kuanza kupelekwa sehemu kwa ajili ya mahojiano maalum.
“A man from Tanzania who stole more than $100m in Geneva Bank is under arrest,” (Mtu kutoka nchini Tanzania aliyeiibia Benki ya Geneva dola milioni mia moja amekamatwa) yalikuwa ni maneno makubwa yaliyosomeka katika televisheni wakati Kituo cha Redio cha CNN kilipokuwa kikiitangaza habari hiyo kwa mbwembwe nyingi.
****
“Guys...guys...come and look at this...” Jamani hebu njooni muone hii kitu) alisikika mwanaume mmoja aliyekalia mbele ya kompyuta yake, alikuwa akiwaita wenzake waliokuwa kwenye kompyuta nyingine.
“What is it?” (kuna nini?)
“Another $80m transferred from one account in Geneva Bank to American bank. Ooh my God! It is transferred in the same account,” (Pesa nyingine, dola milioni themanini kutoka kwenye akaunti moja ya Benki ya Geneva imehamishwa kwenda kwenye Benki ya Marekani. Ooh Mungu wangu! Imepelekwa kwenye akaunti ileile) alisema jamaa huyo wa kitengo cha IT katika Benki ya Geneva.
Kila mtu alichanganyikiwa, hawakuamini kilichokuwa kimetokea, haraka sana wakaangalia mmiliki wa akaunti hiyo, alikuwa mteja aliyeitwa Cosmas Buberwa, Mtanzania aliyekuwa na nyadhifa ya Uwaziri wa Nishati na Madini.
Wakampigia simu mkurugenzi wa benki hiyo, Bwana Peterson na kumwambia kilichotokea ambapo hata yeye mwenyewe alichanganyikiwa kwani kwa jinsi alivyokuwa ameambiwa, jinsi tukio lilivyokuwa, hata virusi vilivyokuwa vimecheza na data base ilionyesha kwamba alikuwa mtu yuleyule.
“How is it possible? He is under arrest already,” (inawezekanaje? Tayari amekwishakamatwa)
Alichokifanya ni kuwasiliana na mkurugenzi wa usalama wa taifa hapo Uswisi, Bwana Henrik Kom na kumwambia kilichokuwa kimetokea katika benki yao kwamba kulikuwa na pesa zingine zilizokuwa zimehamishwa kinyemela kwenda kwenye akaunti ileile nchini Marekani na inaonekana mhusika wa mwanzo ndiye yuleyule.
“It is impossibe, we have him here,” (haiwezekani! Tunaye hapa) alisema Bwana Kom huku akionekana kuchanganyikiwa.
***
Moyo wa Godwin ulikuwa kwenye maswali mengi, hakujua ni mtu gani alikuwa amemuelekeza msichana Winfrida nyumbani hapo. Hakutaka ukaribu naye kwani alihisi kwamba hakuwa mtu mzuri hata kidogo, alihisi kwamba angeweza kufanya jambo lolote lile baya kwa ajili ya kumkamatisha kwa polisi ambao kila siku walihangaika kila kona kumtafuta.
Alichokifanya, kitu cha kwanza ni kulog off akaunti zake za Mabadiliko ya Kweli kwenye Mtandao wa Instagram na Facebook kisha kuendelea na stori kwa kisingizio kwamba hata kama kungetokea kitu gani huko lingekuwa jambo gumu kwa msichana huyo kujua kwamba aliyekuwa akizungumza naye ndiye yule aliyekuwa mtu hatari katika kucheza na kompyuta.
Alibaki na msichana huyo chumbani kwake, walikuwa wakiangaliana tu na wakati mwingine walikuwa wakizungumza mambo mengi tangu siku ya kwanza kukutana na mpaka siku hiyo. Kila mtu alionekana kuwa na furaha lakini wakati mwingine Godwin alionekana kuwa na hofu kubwa.
Hakujua sababu, baada ya dakika kadhaa akamwambia Winfrida amsubiri kwa kuwa alitaka kwenda kumnunulia kinywaji, akamwambia kinywaji alichokuwa akikihitaji na mwanaume huyo kutoka kuelekea dukani huku akiwa na simu yake.
Akaondoka na kuelekea dukani. Wakati huo ilikuwa ni saa 1:15 usiku, alipofika katika kichochoro kimoja, macho yake yakatua kwa kijana aliyesimama mbele yake huku akiwa ameshika panga. Kijana huyo alikuwa akihitaji kitu kimoja, kuachiwa kila kitu alichokuwa nacho Godwin na kisha kuondoka zake.
Alibaki akitetemeka, matukio ya kihuni yaliyokuwa yakitokea Tandale yalimfanya kuogopa zaidi. Alitaka kukimbia lakini akashindwa kufanya hivyo kwani kijana yule alikuwa amemfikia na alichokifanya, hapohapo akampekua mifukoni, akamkuta na pesa kiasi cha shilingi elfu kumi na simu.
Wakati akiwa ametulia, mwanaume mwingine akatokea nyuma yake, naye alikuwa na panga, wakamuweka mtu kati, hakutakiwa kufanya lolote lile.
“Mtoto wa mama unatembea na elfu kumi tu! Nyie wengine ndiyo mnatufanya tuwaue, mwanaume mzima unatembeaje na elfu kumi?” alihoji kijana huyo huku akimchukulia simu yake.
“Nisamehe bro.”
“Siku nyingine nikikukuta na elfu kumi nakucharanga mapanga,” alisema kijana huyo, akachukua simu na kuondoka nayo.
Hiyo ikawa salama yake, hakutaka kujuta kupokonywa vitu bali alichokuwa akikihitaji ni maisha yake tu. Walipoondoka, hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo bali walichokifanya ni kuondoka zako.
Vijana hao ndiyo waliotafuta mtu wa kumuuzia simu hiyo, asubuhi sana tayari walikuwa wamempata mteja na kumuuzia simu hiyo, mteja wa hapohapo Tandale na ndiye ambaye huyohuyo alikamatwa kwa kuwa simu hiyo ilionyesha signo kwamba ilikuwa ikitumika mahali fulani, na bila kujua wakamkamata kijana aliyeuziwa simu hiyo kwa kudhani kwamba alikuwa Godwin waliyekuwa wakimtafuta.
****
Waziri wa Nishati na Madini, Bwana Buberwa alichanganyikiwa, hakuamini kilichokuwa kimetokea, alitumiwa ujumbe mfupi kwa njia ya simu akishukuriwa kwa kuchangia kiasi cha dola milioni themanini, zaidi ya bilioni mia moja sitini kutoka katika Hospitali ya St. Lucas iliyokuwa nchini Marekani.
Baada ya kuupokea ujumbe huo, akatulia katika sofa lake sebuleni, mkono wake akaupeleka kwenye sehemu ya moyo na kuanza kupumua juujuu, presha ilikuwa ikipanda, kiasi ambacho kilichukuliwa katika akaunti yake nchini Uswisi kilikuwa kikubwa mno na hakujua ni kwa jinsi gani angeweza kuishi bila pesa hizo.
“Mume wangu kuna nini?” aliuliza mkewe huku akimsogelea, alishangaa kumuona mumewe akiwa kimya, kijasho kikimtoka huku akiwa kwenye hali ambayo haikuwa kumkuta kabla.
Uzuri ni kwamba mkewe alikuwa daktari hivyo alivyoona hali hiyo akajua kwamba mumewe alikuwa na presha iliyopanda ghafla na hivyo kuanza kumpatia huduma.
Alijua kabisa kwamba kilichokuwa kimetokea kilisababishwa na simu ile, alitaka kujua ni kitu gani kilichokuwa kimetumwa katika simu ya mumewe, akaichukua na kuanza kuangalia kuona kulikuwa na kitu gani.
Akaiona meseji ile, akaanza kuisoma, yeye mwenye mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kwa nguvu, hakuamini alichokuwa akikiona, ilikuwaje kupoteza kiasi kikubwa cha pesa tena kwenda kwenye akaunti nyingine ambayo hawakuifahamu? Ni nani alikuwa amehamisha pesa hizo? Wakati akijiuliza maswali hayo ndipo kumbukumbu zikamjia kwamba hata Rais Bokasa naye aliwahi kufanyia hivyohivyo, pesa zake zilikuwa zimechukuliwa na mpaka siku hiyo hakuwa amezipata.
“Mume wangu...mume wangu...” aliita mwanamke huyo lakini alikuwa amechelewa, presha ya mume wake ilipanda kwa kasi kubwa mwilini mwake, moyo wake ukashindwa kuhimili mshtuko mkubwa aliokuwa ameupata, hapohapo kitandani alipokuwepo, akatulia tuli, pumzi ikakata na kufariki dunia huku mkewe akishuhudia.
***
Ulikuwa ni msiba mkubwa, hakukuwa na mtu aliyeamini kama waziri huyo alikuwa amekufa. Watu wengi walikuwa wakijiuliza sababu ya kifo chake lakini hakukuwa na mtu aliyejua kitu chochote kile.
Mkewe alilia, sababu kubwa ya mume wake kufariki ilikuwa siri, hakutaka kuzungumza kitu chochote kile kuhusu ujumbe mfupi wa maneno uliokuwa umetumwa katika simu ya mume wake, alitaka iwe siri lakini akashindwa kuitunza siri hiyo, siku hiyohiyo, tena huku akiwa analia ndipo akataja kilichokuwa kimetokea.
Kila mtu alishangaa, wengi wakajiuliza kuhusu pesa hizo. Buberwa alionekana kuwa mtu mwema, aliyependa maendeleo ya Watanzania, alijificha kwa mwamvuli wa utumishi wa Mungu, kila mtu alimwamini kwamba alikuwa mtu aliyependa sana dini na asingeweza kufanya jambo baya kama kuficha pesa katika akaunti moja huko nchini Uswisi.
Hata kabla ya watu hawajamaliza msiba tayari tetesi juu ya kilichomuua Bwana Buberwa kilianza kusikika kwamba alikufa alipopokea ujumbe wa simu uliooonyesha kwamba pesa zake, zaidi ya bilioni mia moja na sitini zilikuwa zimehamishwa kutoka katika akaunti yake huko Uswisi na kupelekwa katika akaunti nyingine nchini Marekani.
“Eeh!” alishangaa jamaa mmoja.
“Kuna nini?”
“Hujasikia kilichomuua mgonjwa?” aliuliza jamaa huyo, alishangaa mno.
“Kitu gani?”
“Kumbe alipata presha baada ya kuona pesa zake zilizokuwa Uswisi zimehamishwa na kupelekwa katika akaunti nyingine! Kama alivyofanyiwa Rais Bokasa!” alisema jamaa huyo.
Hakukuwa na siri tena, kila kitu kilichokuwa kimetokea kilijulikana huku watu wengine katika habari hiyohiyo wakiongeza chumvi kwamba pesa hizo alitaka kununua jumba la kifahari nchini Uswisi.
Wengi hawakuamini kama kweli waziri huyo angeweza kufanya jambo kama hilo. Alionekana kuwa mtu mwema kumbe upande wa pili alikuwa mtu aliyekuwa akipiga madili mengi na pesa kuzikimbizia katika akaunti yake hiyo.
Kwa kuwa pesa hizo zilipotolewa zilipelekwa katika akaunti ileile iliyopelekewa pesa za Rais Bokasa, watu wakajua kwamba mhusika alikuwa yuleyule wa Akaunti ya Mabadiliko ya Kweli kwenye Mtandao wa Kijamii wa Instagram.
Hilo likaibua gumzo katika mitandao ya kijamii, kila mtu alikuwa akielezea lake, wengi walimpongeza Godwin bila kumfahamu kwamba alikuwa akifanya kazi kubwa ambayo hakukuwa na mtu mwingine ambaye angeweza kuifanya kama alivyokuwa akiifanya.
Rais Bokasa na usalama wa taifa walichanganyikiwa, hawakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, ilikuwaje Waswisi waseme kwamba walimkamata Godwin na kuondoka naye kuelekea nchini Uswisi huku nyuma pesa hizo zikaibiwa katika mazingira yaleyale?
Rais hakutaka kukubaliana nao, akaanza kuamini kwamba mtu aliyekuwa amekamatwa hakuwa Godwin yule waliyekuwa wakimfahamu bali alikuwa mtu mwingine kabisa. Siku hiyohiyo kikao cha dharura kikafanyika akiwepo Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Bwana Idrisa, rais alichanganyikiwa kupita kawaida, mbele yake aliona giza kubwa, kitendo cha waziri huyo kuchukuliwa kiasi cha fedha katika akaunti yake ilimaanisha kwamba viongozi wote waliokuwa na akaunti katika Benki ya Geneva pesa zao zingechukuliwa na kupelekwa katika akaunti nyingine.
“Nimewaita hapa niseme kitu kimoja,” alisema rais huku akimwangalia kila mtu aliyekuwa mahali hapo.
“Ndiyo mkuu!”
“Huyu Godwin bado hajapatikana, na inawezekana kabisa wale Waswisi watakuwa wammpata Godwin mwingine,” alisema rais bokasa maneno ambayo kila mtu yalimfanya kushangaa mahali hapo.
Hakukuwa na mtu aliyehisi kwamba Wazungu wangeweza kukosea, walikuwa watu makini katika kazi zao, walikuwa wakimfuatilia Godwin kwa kipindi kirefu na hatimaye kumpata kule Tandale alipokuwa akiishia.
Mazingira ya kukamatwa kwake yalionyeshwa kwamba alikuwa mwenyewe kwani hata simu aliyokuwa akiitumia ilionyesha kwamba ni yeye, sasa ilikuwaje rais aseme kwamba yule aliyekuwa amekamatwa si Godwin na wakati Wazungu walithibisha hilo?
“Mkuu!” aliita Bwana Idrisa.
“Nimesema hivi kwa sababu moja. Au tufanye kwamba yule aliyekamatwa ndiye Godwin, sasa inakuwaje achukue tena pesa kutoka katika akaunti ya Bwana Buberwa?” aliuliza rais kitu kilichomfanya kila mtu kubaki kimya na kuanza kuangaliana kwani kwa kile alichokizungumza rais kilionekana kuwaingia akilini mwao.
“Sasa mkuu kama yule si Godwin! Godwin yupo wapi? Wamechukua simu, hivi kweli tutaweza kumpata? Tutampata kwa njia gani?” aliuliza waziri mkuu huku akimwangalia kila mtu aliyekuwa mahali hapo.
“Jenerali unasemaje hapo?” aliuliza Rais Bokasa.
“Ni habari ambayo inachanganya sana, sijui huyu mtu yupo wapi kwa kweli,” alisema Jenerali
Kikao cha dharura kilikuwa kizito, Godwin alivichangany vichwa vyao kiasi kwamba wakati mwingine walikuwa kimya wakijifikiria ni kitu gani walitakiwa kufanya lakini hawakuwa na majibu yoyote yale.
Muda ulizidi kwenda, wakati kikao kikiendelea, tayari taarifa ikaandikwa kwenye akaunti ile ya Mabadiliko ya Kweli kwamba kulikuwa na kikao kizito kilichokuwa kikiendelea ikulu.
“Guys! This man is back in business,” (Jamani! Huyu jamaa amerudi kazini) alisema waziri mkuu mara baada ya kuangalia kwenye akaunti yake Instagram.
Kila mtu akaingia kwa lengo la kuangalia kilichokuwa kikiendelea. Kila mmoja alishangaa, ilikuwaje mwanaume huyo ajue kwamba kulikuwa na kikao cha siri kilichokuwa kimeitishwa ikulu na wakati hakukuwa na mtu mwingine aliyejua hilo?
“Idrisa, simu yangu walirekebisha ili isidukuliwe, si ndiyo?” aliuliza Rais Bokasa.
“Ndiyo mkuu!”
“Sasa huyu mtu amejuaje?”
“Hata mimi sifahamu!” alijibu Idrisa huku akionekana kuchanganyikiwa.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumatano
 
Haaaahaaaaaaaa nasomaga sana dada angu story nyingi kila cku tena ila sometimes nabanwa kabla sikuwa na account Jf ko nikawa natumia opera ambayo uruhusiwi KUKOMENT
Sawa mkuu karibu sana
 
Sio j3 mkuu Shunie kutupia ni J5,umesoma vibaya .Hili movie kama vile laenda ukingoni.Shigongo mwenyewe anatupia kimachale.J5 saa 6.01 goma liko hapa!
Wapi huko anatupia
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom