Dunia haina usawa

Dunia haina usawa

Oooops! Godwin take care, huko kwenye mahojiano jifanye mwehu wala hujui kinachoendelea duniani.

DUNIA HAINA USAWA

Vijana wa IT nchini Uswisi walikuwa wakihangaika kuzichukua pesa ambazo zilihamishwa kwenye akaunti moja nchini Marekani katika Benki ya American. Waliweza kuzizuia pesa hizo nyingi zisiweze kutoka lakini kitu cha ajabu kabisa hawakuwa wakiweza kuzichukua na kuzirudisha katika akaunti zilipotolewa.
Walitumia wataalamu wengi lakini kitu kilichokuwa kikiwatatiza kilikuwa ni virusi vilivyokuwa vimeingizwa katika data base yao ambavyo vilizuia pesa kurudishwa katika akaunti ile iliyokuwepo.
Mkurugenzi wa benki hiyo, Bwana Peterson hakulala kwa siku mbili mfululizo, kichwa chake kilichanganyikiwa na hakujua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea. Vijana wa IT aliokuwa amewaita kwa ajili ya kufanya kazi hiyo walionyesha kila dalili za kushindwa kwani walichukua muda mrefu mno na hakukuwa na kitu chochote kile kilichofanyika.
Kwa siku tatu mfululizo watu walikuwa wakihangaika, wakaitwa wataalamu mbalimbali kutoka sehemu tofauti lakini hakukuwa na mtu aliyeweza kuzirudisha pesa hizo zilizokuwa zimetumwa katika akaunti ile ya Hospitali ya St. Lucas.
“Hebu tuwasiliane na mteja kwanza ili tumuombe radhi kwani tunaweza kuchukua muda mrefu kidogo,” alisema Bwana Peterson.
Ilikuwa ni lazima kuwasiliana na Rais Bokasa kumuomba radhi kwa kile kilichokuwa kikiendelea. Mawasiliano kwa njia ya simu yakafanyika na kilichowashtua zaidi ni kwamba mtu huyo alikuwa hoi hospitalini baada ya kuzimia alipopewa taarifa kwamba kiasi hicho kilikuwa kimechukuliwa katika akaunti yake.
Wakati wakiongea na mtu wa pili ndipo mkurugenzi huyo akaambiwa kila kitu kilichokuwa kimetokea. Aliambiwa kuhusu akaunti ya Mabadiliko ya Kweli, akaambiwa kwamba mtu aliyekuwa na akaunti hiyo ndiye ambaye alikuwa ameziiba pesa hizo na kuziweka katika akaunti hiyo, serikali ya Tanzania ilikuwa ikipambana kumtafuta lakini ubaya zaidi ni kwamba walikutana na mtu aliyekuwa akijua sana kutumia kompyuta.
“Kwa hiyo huyo mtu yupo huko?” aliuliza Bwana Peterson.
“Ndiyo! Ila hatufahamu yupo wapi!”
“Na akaunti hiyo anaitumia?”
“Ndiyo!”
“Hebu subiri!”
Alichokifanya Peterson ni kuwasiliana na rais wa nchi hiyo na kumwambia kile kilichokuwa kimetokea. Kwanza akamuhadithia kuanzia mwanzo mpaka pale ambapo vijana waliitwa kwa ajili ya kurudisha pesa hizo, alipomaliza akamwambia kuhusu ile akaunti na mtu aliyefanya mambo hayo yote alikuwa nchini Tanzania.
“Haiwezekani!”
“Ndiyo hivyo!”
“Kwa hiyo ni Mwafrika?”
“Ndiyo mkuu!”
“Hebu subiri!”
Yaliyokuwa yakifanyika yalikuwa ni mawasiliano kwa njia ya simu. Ilikuwa ni lazima waunganishe nguvu zao kwa ajili ya kumpata mtu huyo ambaye alikuwa akiwasumbua muda wote. Rais hakutaka kukubali kwamba mtu aliyekuwa akiyafanya mambo hayo alikuwa Mwafrika.
Hakuamini kama Waafrika walikuwa na akili kubwa kama Wazungu, kwake, watu hao walionekana kama maboksi fulani ambayo yalikuwa yakifanya kile walichoambiwa wafanye lakini si wao kuwaongoza Wazungu.
Akawasiliana na Mkurugenzi wa usalama wa taifa nchini humo, The Federal Intelligence Service (FIS), Bwana Henrik Kom ambaye akamwambia kila kitu kuhusu mchakato mzima ulivyokuwa na kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima maofisa wawili wa FIS watumwe kuelekea nchini Tanzania kwa ajili ya kumtafuta mtu huyo ambaye aliisumbua Benki ya Geneva kwa kile alichokuwa amekifanya.
“Hilo si tatizo! Wamesema ni Mwafrika?”
“Ndiyo!”
“Mmh! Inawezekana vipi?”
“Ndiyo tunataka muendele mkajue ukweli huko,” alisema rais.
Hilo ndilo walilolifanya, ndani ya siku mbili, vijana wawili, wataalamu kwa masuala ya upelelezi wakatumwa kwenda nchini Tanzania huku wengine wakibaki hapo kwa ajili ya kuifuatilia akaunti hiyo ya Mabadiliko ya Kweli iliyokuwa katika Mtandao wa Kijamii wa Instagram.
****
Hakukuwa na mtu aliyejua kwamba yule kijana masikini aliyekuwa amehamia mtaani Tandale ndiye aliyekuwa akihusika katika kuuendesha mtandao huo. Hapo Tandale alipokuwa akiishi alikuwa mtu wa watu, alitaka kuyaficha maisha yake, kusiwe na mtu yeyote kumfahamu au hata kuhisi kwamba alikuwa yeye.
Alichokifanya ni kuanza kwenda katika vilabu vya pombe haramu na kuanza kushinda huko. Kazi yake ilikuwa ni kupiga stori, hakuwa mnywaji ila kila alipokuwa akirudi nyumbani kwake alijifanya kuwa mlevi mkubwa.
Watu walimshangaa, hawakuwahi kumuona mgeni ambaye alifahamiana na watu wengi kwa haraka kama ilivyokuwa Godwin, kila mtu aliyekuwa akiongea naye alijua kabisa kwamba alikuwa akizungumza na mlevi ambaye kila siku asubuhi, mchana mpaka jioni kazi yake ilikuwa ni kushinda klabuni tu.
Akajulikana zaidi kama mlevi, hawakujua kama mtu huyo ndiye aliyewanyima usingizi viongozi mbalimbali, kila siku usiku ilikuwa ni lazima kuangalia kwenye akaunti yake kuona ni jinsi gani watu walikuwa wakitaka aendelee kuwaumbua viongozi wa serikalini kwa maovu waliyokuwa wakiyafanya.
Alijua mambo mengi, watu waliokuwa wakimfuata inbox na kumtumia meseji walimwambia mambo mengi kuhusu viongozi wa serikali ilivyokuwa ikiwatumia wachungaji, maaskofu kwa ajili ya kuwaibia wananchi pesa.
Hakutaka kuliingilia suala hilo kwa pupa, kitendo cha kuwazungumzia wachungaji ilikuwa ni kama kuizungumzia dini fulani au kundi kubwa la watu fulani. Alitaka kufanya uchunguzi wake, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kutafuta namba za wachungaji na maaskofu hao, wala hakupata tabu, akazipata na kisha kuzidukua ili aweze kunasa mazungumzo yao, na cha zaidi alichokifanya ni kudukua barua pepe zao.
***
Kwenye barua pepe hizo ndipo Godwin alipopata kila kitu alichokuwa akikihitaji, aliuona uovu mkubwa uliokuwa ukifanyika kwa wachungaji hao. Hakutaka kuvumilia, watu wengi walikuwa wakiangamia pasipo kujua kwamba watumishi hao wa Mungu walikuwa wakitumika kwa ajili ya kuwachukulia pesa zao.
Alitaka kuweka kila kitu wazi, alitaka Tanzania na dunia nzima ifahamu kile kilichokuwa kikiendelea hivyo kuwaambia Watanzania kwamba alikuwa akitaka kuzitoa taarifa hizo, tena zikiambatana na ushahidi mkubwa mpaka watu ambao walikuwa wakitumika kwa ajili ya kuhakikisha kwamba baadhi ya viongozi serikalini walikuwa wakitumika kwa ajili ya kuwaibia wananchi.
“Nitaanza na Mchungaji Peter Kibatari,” alianza kuandika Godwin na baadaye kuweka picha ya mchungaji huyo na kuandika mambo mengi kuhusu huduma yake, jinsi alivyokuwa akitumika na viongozi wa serikali.
Kila mtu aliyekuwa na simu yake mkononi, alikuwa akisoma kila kitu kilichokuwa kimeandikwa. Kila mmoja alimfahamu mchungaji huyo, alikuwa ni mtu mwenye nguvu nchini Tanzania, alipokuwa akihubiri kitu chochote kile kila mtu alikuwa makini kumsikiliza.
Wakati mwingine, watu walikuwa wakitoka nyumbani kwao na kwenda kusikiliza mahubiri kanisani kwake. Alijua kucheza na akili za watu, alikuwa na usanii mkubwa ambao hakukuwa na mchungaji mwingine aliyekuwa nao.
Aliwachanganya watu, alipendwa, alikuwa mtu aliyezungumziwa, kitu cha kushangaza kabisa, kila kiongozi serikalini alikuwa akimzungumzia kwa mazuri, kila kitu kilichokuwa kikizungumziwa juu ya mchungaji huyo, kilizungumziwa kwa uzuri tu.
Watu hawakujua kilichokuwa kikiendelea, hawakujua siri iliyokuwa nyuma ya pazia. Televisheni ya Taifa ndiyo ilikuwa ikimtangaza kila siku kwamba alikuwa mchungaji mwenye nguvu ambaye alitakiwa kusikilizwa na kila mtu.
Maneno mengi ya kisiasa, kuingilia burudani na kuzungumzia kuhusu viongozi wengine wa siasa kuliwafanya hata Waislamu wengine nao kwenda kanisani kwake kusikiliza mahubiri, si kwamba walitaka kuingia katika dini nyingine bali walichokitaka ni kwenda kusikiliza siku hiyo mchungaji huyo alikuwa na umbeya gani.
Hakukuwa na mtu aliyejua kwamba mchungaji huyo alikuwa akitumika. Serikali ilimtumia, watu zaidi ya elfu tano walikwenda kanisani kwake kila Jumapili, mapato ya sadaka yaliyokuwa yakipatikana yaligawanywa kwa viongozi mbalimbali ambao wao ndiyo waliokuwa wakihusika kumletea washirika wengi.
Viongozi hao wakawa wakinunua magari ya kifahari na kuyaingiza nchini kupitia kanisa la mchungaji huyo, biashara zote haramu kama madawa ya kulevya yalikuwa yakiingizwa nchini kupitia kivuli cha kanisa hilo, mizigo haikuwa ikikaguliwa, ilipita na kila mtu alipokuwa akiuliza, aliambiwa ni msaada kutoka nchini Marekani kwa ajili ya kanisa la Praise And Worship la Mchungaji Kibatari.
“Whaaaat?” (nini?) aliuliza jamaa mmoja, hakuwa akiamini alichokuwa akikiona, yeye mwenyewe alikuwa mshirika mzuri wa kanisa hilo.
“Kumbe Kibatari naye ni mtumishi wa serikali, na si mtumishi wa Mungu kama tunavyojua! Mungu wangu! Ni nini tena hii?” aliuliza mwanamke mmoja.
Kanisa la Praise And Worship likawa limechafuka, kila mshirika wa kanisa hilo akajitokeza na kuweka maoni yake hadharani. Mchungaji Kibatari ambaye alizoea kupigiwa promo kila siku akajitokeza na kuanza kujitetea lakini kujitetea kwake hakukuwa na nafasi hata kidogo kwa kuwa kila siku ushahidi ulikuwa ukiwekwa katika akaunti ile kwamba alikuwa akitumika.
“Kumbe hata Lucy si mke wake!” alisema jamaa mwingine, wote walijiuliza, kila siku mchungaji huyo alimtambulisha mwanamke aitwaye kwa jina la Lucy kama mkewe, kumbe hakuwa mkewe bali ni mwanamke aliyepewa kwa ajili ya kuwa naye kwa lengo la kuangalia mapato ya kanisa kila yalipokuwa yakiingia.
“Jamani! Kweli Lucy si mkewe?” aliuliza mtu mwingine.
Ili kuwaaminisha kwamba kila kitu kilikuwa ni ukweli, Godwin akaweka picha za mwanamke huyo akiingia katika nyumba nyingine nyakati za usiku kuonyesha kwamba alikuwa akienda kulala, kama kweli alikuwa mke wa Mchungaji Kibatari, kwa nini usiku alikuwa akieka kulala nyumba nyingine?
Kulikuwa na walinzi wanne wa nyumbani kwa Kibatari ambao walikufa katika vifo vya kutatanisha! Hakukuwa na mtu aliyejua kwamba walinzi hao waliuawa kwa kuwa walitaka kutoa siri kwamba Lucy hakuwa mke wa Mchungaji Kibatari? Yaani kila kitu alichokuwa akikiandika Godwin, watu walishangaa mpaka wengine kufikia hatua ya kutotaka kwenda kanisani tena.
“Siwezi kwenda kanisani. Nilidhani nahubiriwa na mchungaji kumbe nahubiriwa na mhuni! Sirudi tena kanisani pale,” alisema mwanamke mmoja huku akionekana kukasirika hasa.
Siri hazikuwa hizo tu, Godwin aliendelea kuzitoa nyingi kuhusu mchungaji huyo, jinsi alivyokuwa akiwatumikia viongozi wa serikali na kuonekana kwamba alikuwa na nguvu kubwa, watu waliokuwa wakianguka mapepo kanisa, walitengenezwa kwa malipo makubwa.
Kwa kuwa kila alipokuwa akifanya mambo mengi makubwa alizungumziwa katika mitandao ya kijamii, hata alipogundulika kwamba alikuwa msanii pia aliandikwa sana katika mitandao hiyohiyo.
Jumapili ya kwanza tangu kashfa kubwa ilipoanza kuzungumziwa kwenye mitandao, hakutaka kwenda kanisani, alijifanya kuumia na hivyo kuomba udhuru kwamba alitaka kusafiri kuelekea nchini Israel kwa ajili ya kumuomba Mungu wake kwani kama kudhiakiwa, alidhiakiwa sana na ulikuwa muda wa Mungu wake wa Mbinguni kumsafisha.
Ilikuwa ni aibu, alipokuwa uwanja wa ndege kwa ajili ya kuondoka kuelekea nchini humo, watu walikuwa wakimwangalia, walimshangaa, hakuonekana kuwa kama mtumishi wa Mungu tena bali alionekana kuwa kama kituko cha mwaka, mtu ambaye alipambana usiku na mchana kuhakikisha anaingiza pesa kwa kutumia migongo ya viongozi wa serikali na kanisa ambalo kila siku alikuwa akiling’ang’ania.
“Nimechafuka sana,” alikuwa akizungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani, Godfrey Kamau ambaye naye alikuwa akimtumia mchungaji huyo kuingiza magari bandarini kwa kutumia kivuli cha kanisa lake.
“Pole sana. Nimeona jinsi yule mtu anavyokuchafua, huu ni wakati ambao hutakiwi kuteteleka,” alisema Kamau.
“Nitapambana na huyu mtu!”
“Utapambana naye? Utaanzia wapi? Hajulikani, halafu inaonekana ni mtu mwenye nguvu sana, kama utaweza kumuomba Mungu na kukuonyeshea mtu huyo, jua tutakuwa nyuma yako,” alisema Kamau wakati alipokuwa akizungumza na Mchungaji Kibatari kwenye simu pasipo kujua kama mazungumzo yao yalikuwa yakidukuliwa na Godwin na kuyarusha moja kwa moja katika akaunti yake kwenye Mtandao wa Instagram.
“Nitamjua tu!” alisema Kibatari na kukata simu.
Kila kitu ambacho walikizungumza kwenye simu, dakika arobaini zilikuwa nyingi sana kuyaona mazungumzo yao kwenye akaunti ile. Kila mmoja alishangaa, wakagundua kwamba simu zao zilikuwa zimedukuliwa na hivyo kuwasiliana na Kampuni ya Simu ya Alcatel na kuwaambia kile kilichokuwa kimetokea.
Watu wa kampuni hiyo ya simu hawakujua kilichokuwa kikiendelea, hawakujua kama kulikuwa na mtu aliyekuwa akidukua mawasiliano ya wateja wao. Wakawasiliana na wataalamu kutoka Afrika kusini ambayo nao wakaingia kwenye system kuona kama kulikuwa na mtu alikuwa na uwezo wa kudukua mawasiliano ya wateja wao, hawakubahatika kuona lolote lile.
“Ila Mchungaji Kibatari anasema kwamba mawasiliano yake na mheshimiwa waziri yalidukuliwa. Hebu ingia kwenye akaunti ya Mabadiliko ya Kweli,” alisema mkurugenzi wa kampuni hiyo.
Akaingia na kuangalia, posti alizokutana nazo huko zilihusu mawasiliano baina ya watu hao wawili. Walichanganyikiwa, hawakujua ni kwa namna gani mtu huyo alikuwa ameingia kwenye mitambo yao na kudukua mawasiliano hayo.
Wakati mitandao ya simu ikisumbuka kuziba udukuaji wa mawasiliano ya wateja wao, usalama wa taifa walikuwa mitaani wakimtafuta Godwin. Hawakumfahamu mtu huyo, walikuwa na kazi kubwa mno mbele yao. Kila walipokuwa, waliwaambia watu wawasaidie kumtafuta mtu aliyekuwa akitumia akaunti ya Mabadiliko ya Kweli ambayo kwao ilionekana kama kuibua vuguvugu la vurugu nchini Tanzania.
“Hakikisheni kwamba mnafanya kila liwezekanalo huyo Godwin anapatikana. Sawa?” alisema mkurugenzi wa usalama wa taifa.
“Sawa.”
Wakati wao wakiendelea kumtafuta Godwin, mwanaume huyo aliendelea kujichimbia, hakutaka kugundulika kwamba yeye ndiye alikuwa mtumiaji wa akaunti hiyo.
Alikuwa mtu wa kushinda Tandale huku kila kitu alichokuwa akikifanya akikifanya chumbani kwake. Baada ya kukaa kwa wiki mbili ndipo alipoamua kuwa mpiga debe katika Kituo cha Daladala cha Makumbusho.
Hakukuwa na mtu aliyemfahamu, alikuwa mgeni kituoni hapo, alionekana kuwa kijana mwenye njaa kali, aliyechoka ambaye mwili wake huku mwili wake ukiwa dhaifu.
Alikuwa mchangamfu, aliyeongea sana, kila siku alipokuwa kituoni hapo alivalia kipensi kichafu, nywele timtim, chini alivaa kandambili zilizokuwa zimechoka huku wakati mwingine vipensi vya jinsi alivyokuwa akivivaa akivifunga kamba badala ya mkanda.
Ilikuwa ni vigumu kujua kwamba huyo ndiye alikuwa kijana aliyewanyima usingizi viongozi wa nchi na viongozi wa dini. Alitafutwa pasipo kujulikana alikuwa vipi. Akaanza kuzoeleka katika kituo hicho, hakuona kama kulikuwa na tatizo lake kujitambulisha kwamba alikuwa akiitwa Godwin, kwa jinsi alivyokuwa, ilikuwa vigumu sana hata kugundua kama mwanaume huyo alikuwa amesoma.
Hayo ndiyo yakawa maisha yake kila siku. Aliendelea kuwatesa viongozi, alionekana kuwa shujaa mkubwa, Watanzania wengi wakataka kumfahamu kwamba alikuwa nani, walitaka kumpongeza, hawakujua kama mtu huyo kila siku walipishana naye katika kituo hicho na hata wakati mwingine kumtukana kila alipowaletea utani wasichana.
Alipokuwa akiendelea kupiga debe katika kituo hicho ndipo alipokutana na msichana aliyeitwa Winfrida, msichana mrembo aliyekuwa akiwatetemesha wanaume wengi chuoni alipokuwa akisoma.
Hakujua lolote kuhusu msichana huyo, hakujua kama alikuwa akimpenda mpaka siku ambayo msichana huyo alimwambia ukweli. Kwanza akacheka sana, ilikuwaje msichana mrembo kama huyo ampende mwanaume kama yeye, mchafu, asiyekuwa na pesa, wakati mwingine akahisi kwamba inawezekana Winfrida alikuwa ofisa wa usalama wa taifa, akakubaliana naye kishingo upande na hivyo kuanza uhusiano wa kimapenzi, ila alikuwa na tahadhari kubwa mno kwani hakutakiwa kumwamini kila mtu.
***
Madaktari katika Hospitali ya Ganga nchini India walikuwa wakibadilishana ndani ya chumba alichokuwa amelazwa Rais Bokasa. Walikuwa wakihangaika kuhakikisha afya ya rais huyo inarudi na kuwa katika hali ya kawaida. Alikuwa kimya, tangu alipofikishwa hospitalini hapo hakuwa akizungumza kitu chochote kile, aliyafumba macho yake na kitu pekee ambacho kiliwaambia kwamba alikuwa hai ni mapigo ya moyo yaliyokuwa yakidunda kwa chini mno.
Mke wake, Bi Consolatha alikata tamaa, hakuona kama mume wake angeweza kufumbua macho yake tena kwani tangu alipokuwa ameanguka na kupoteza fahamu, mpaka siku hiyo alikuwa hivyohivyo, yaani kitandani pale alikuwa kama alivyokuwa ameingia.
Siku ziliendelea kukatika, madaktari walikuwa wakiifuatilia afya yake kwa ukaribu sana. Pale alipokuwa ameanguka, aliumia vibaya kichwani mwake, akatoka damu ambayo iliganda kwa kiasi kidogo katika ubongo wake na hivyo kuwa na hatari ya kupata ugonjwa mmoja kati ya magonjwa matatu.
“Inawezekana atapata kifafa, atapooza mwili wake au kusahau milele kila kitu kilichokuwa kimetokea maishani mwake,” alisema daktari huku akimwangalia Bi Consolatha pamoja na maofisa wa usalama waliokuwa wameongozana naye huko India.
“Jamani mume wangu!” alisema Bi Consolatha huku akilia.
“Tunajitahidi sana, tuna uhakika kwamba hatokufa lakini anaweza kupata tatizo moja kati ya hayo niliyowaambia,” alisema daktari.
“Daktari! Nini kinaendelea?” aliuliza Rais Bokasa mara baada ya kufumbua macho.
Kilichomfahamisha kwamba hapo palikuwa ni hospitali ni mavazi waliyokuwa wamevalia madaktari hao pamoja na kitanda alichokuwa amekilalia. Aliangalia kwa juu aliiona dripu ikiwa inaning’nia.
Hakujua kitu gani kilitokea mpaka kuwa mahali hapo lakini baada ya sekunde kadhaa, akaanza kukumbuka kila kitu kilichokuwa kimetokea. Aliikumbuka meseji aliyokuwa ametumiwa kwamba kiasi cha dola milioni mia moja kilichukuliwa kutoka kwenye akaunti yake iliyokuwa nchini Uswisi, moyo wake ulimuuma mno na hapohapo kitandani alipokuwa akaanza kulia.
Alirudiwa na fahamu lakini mwili wake ukawa na tatizo kubwa la kupooza. Alijaribu kuunyanyua mkono na mguu wake wa kulia lakini vilishindwa kuinuka, alihisi kama kulikuwa na mtu alikuwa amevikandamiza, alishangaa, alijaribu mara kwa mara lakini akashindwa kufanya hivyo.
“Nimepooza! Daktari nimepooza,” alisema Rais Bokasa huku akianza kulia kitandani pale alipokuwa.
Huo ndiyo ulikuwa ukweli wenyewe, kwenye matatizo aliyosema daktari, tatizo la kupooza lilikuwa mojawapo, alishindwa kufanya kitu chochote kile kwa upande wa kulia. Moyo wake ulimuuma, hali hiyo ilimaanisha kwamba kwa miaka yote mpaka kifo chake maisha yake yangekuwa juu ya kiti cha walemavu.
Alilia sana, hata alipomuona mke wake, hakuacha kulia, moyo wake uliumia sana, wakati mwingine alibaki akimuomba Mungu kitandani pale kwa kumtaka kubadilisha kila kitu kwamba maisha yake halisi yaliyokuwa yakiendelea basi yawe ndoto moja ya kusisimua ambapo baada ya muda fulani ashtuke kutoka usingizini.
“Mungu! Fanya kitu, nifanyie muujiza, wewe ni mponyaji, naomba uniponye Mungu wangu,” alisema Rais Bokasa pale kitandani. Kwa kipindi cha shida kama hicho ndicho kilikuwa kipindi cha kumkumbuka Mungu wake.
****
Godwin alihisi kwamba msichana aliyeanza kuzoeana naye alikuwa ni miongoni mwa maofisa wa Usalama wa Taifa. Hakutaka kuzungumza naye sana, kila alipokuwa akimfuata, msichana huyo alikuwa akimbugudhi kwa kumwambia maneno mengi ambayo hakutaka kujali kabisa.
Kila siku Winfrida alikuwa akifika hapo Makumbusho na kutaka kuzungumza naye, haikuwa kazi nyepesi kumzoea Godwin kwani alimuona kila mtu mbele yake akiwa adui mkubwa ambaye alikuwa akimtafuta kwa udi na uvumba.
Alihitaji muda mwingi kumzoea msichana huyo aliyekuwa akisomea mambo ya biashara katika chuo kimoja jijini Dar es Salaam. Marafiki zake waliokuwa katika kituo hicho cha Makumbusho walimuona kuwa mmoja wa watu waliokuwa na bahati kubwa, hawakuamini kama kungekuwa na msichana mrembo kama alivyokuwa Winfrida kutokea kumpenda Godwin ambaye kwa kumwangalia tu, muonekano wake ulionyesha kwamba alikuwa mhuni asiyekuwa na mbele wala nyuma.
“Ninataka kuzungumza na wewe,” alisema Winfrida huku akimwangalia Godwin aliyekuwa kimya akimwangalia.
“Kuhusu nini?”
“Ninahitaji muda wa kukaa na wewe sehemu. Ninahitaji kuzungumza sana na wewe,” alisema msichana huyo huku akimwangalia Godwin aliyekuwa akionekana kushangaa sana.
“Sina muda.”
“Nakuomba.”
“Kweli sina muda. Unaweza kuniacha nikatafute pesa kwanza?” aliuliza Godwin huku akisimama.
Hakuwahi kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na msichana yeyote yule zaidi ya mwanamke mtu mzima Bi Rachel ambaye mpaka kipindi hicho hakujua mwanamke yule alikuwa akiendeleaje, kama alikuwa hai au alikufa pale hospitalini alipokuwa amemuacha.
Wakati Godwin akiondoka, moyo wa Winfrida ulikuwa ukimuuma sana, hakuamini kama mwanaume huyo alikuwa akiondoka pasipo kumsikiliza alichotaka kumwambia wakati huo, akaondoka mpaka kulipokuwa na magari ya kwenda Gongo la Mboto na kuanza kuita abiria.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake ya kila siku, Winfrida hakukoma, kila siku ilikuwa ni lazima kufika mahali hapo na kutaka kuzungumza na Godwin. Mwanaume huyo alikasirika, alimchoka Winfrida kwani kila alipokuwa akija, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kutaka kutumia muda mrefu kuwa naye tu.
“Unanikera!” alisema Godwin, hakutaka kumficha msichana huyo.
“Najua! Nisamehe tu ila ninakupenda sana,” alisema Winfrida huku akimwangalia Godwin.
“Unanipenda mimi?”
“Ndiyo!”
“Hivi nilivyo?”
“Mapenzi hayachagui Godwin. Naomba unipende!” alisema Winfrida.
“Siwezi!”
“Nakuomba Godwin. Nakuomba unipende,” alisema msichana huyo, tayari machozi yakaanza kumtoka.
“Nimesema haiwezekani!”
Huo ulikuwa msimamo wake, hakutaka kuwa karibu na msichana huyo hata kidogo. Kila aliporudi nyumbani kwake, alijifungia ndani huku akiwa na rundo la magazeti na kuanza kuyasoma huku akisikiliza mawasiliano ya siri ya namba za simu alizokuwa amezidukua ambazo alikuwa akizirekodi kusikiliza kila kitu kilichokuwa kikiendelea wakati yeye alipokuwa kazini kwake.
“Vijana bado wanaendelea kumtafuta. Halafu nimepata taarifa kwamba vijana wa FIS (The Federal Intelligence Service) walikuwa wameingia nchini Tanzania tayari kwa kuanza kazi yao,” alisikika mkurugenzi wa Usalama wa taifa akimwambia waziri mkuu.
“Safi sana! Sasa hili jambo lisitoke, hutakiwi kumwambia mtu yeyote,” alisikika waziri mkuu.
“Haina shida mkuu!”
Godwin alijua kwamba watu hao walifika nchini Tanzania kumtafuta yeye, si kwa sababu alikuwa akitumia akaunti hiyo bali ni kwa sababu alizihamisha pesa hizo kwenda kwenye akaunti moja nchini Marekani.
Hakutaka kuchelewa, muda huohuo akaingia Instagram na kuwaambia wafuasi wake kwamba kulikuwa na wapelelezi kutoka nchini Uswisi ambao walifika Tanzania kwa ajili ya kumtafuta lakini kamwe wasingeweza kumpata hata kidogo.
Kila mtu alishangaa, mambo hayo yalitakiwa kufanyika kisiri lakini tayari mhusika aliyekuwa akitafutwa tayari alifahamu kila kitu. Watu wengine walishangaa lakini viongozi wengi wakajua kwamba mtu huyo alikuwa amedukua mawasiliano ya waziri mkuu na mkurugenzi wa usalama wa taifa, kumzuia Godwin kupata taarifa lilikuwa jambo gumu sana.
Hakutaka kuishia hapo, ilikuwa ni lazima aendelee kuwaumbua wachungaji wengine, hakuacha, aliwataja wachungaji wengine waliokuwa wakihusika katika kushirikiana na baadhi ya viongozi wakiwemo mawaziri kuwaibia Watanzania pesa zao huku wakati mwingine mtafaruku mkubwa ukitokea baina ya mchungaji na mchungaji mara baada ya kuona wakizidiana katika wingi wa washirika.
****
Kwa kilichokuwa kimetokea, jinsi Godwin alivyokuwa amewachoma wachungaji wengi, washirika wakaanza kupungua makanisani na wengine kuacha kabisa kuelekea huko. Ilikuwa ni sifa mbaya kwa kanisa kwa ujumla, kila mtu alishangaa kwamba ilikuwaje wachungaji waliokuwa wakiwaamini kila siku, kuwatolea mafungu ya kumi na zaka kufanya mambo ya kijinga kama hayo.
Ilikuwa ni vita kubwa, wachungaji wengine wakaamua kuondoka Tanzania na kukimbilia nchi nyingine kujificha, hakukuwa na mchungaji aliyetamani kubaki nchini Tanzania, kila mtu aliondoka kuyaokoa maisha yao kwani tayari kulikuwa na baadhi ya wananchi walikuwa wamepaniki mpaka kufikia hatua ya kutaka kuwamaliza wachungaji hao.
Wakati kila kitu kikionekana kwenda shaghalabaghala hapo ndipo mkurugenzi wa usalama wa taifa akaja na wazo moja kwamba watu wote waliokuwa na jina linaloitwa na Godwin walitakiwa kutekwa kinyemela na kupelekwa sehemu fulani ambapo huko walitakiwa kufanyiwa mahojiano.
Waliamini kwamba kwamba sababu Godwin alikuwa akijiamini kwamba asingeweza kukamatwa ilikuwa ni lazima kutumia jina lake kama kawaida kwa kuwa tu kulikuwa na watu wengi waliokuwa na jina hilo.
Msako huo ukaanza kufanyika kimyakimya. Vijana wengi waliokuwa na jina hilo kwenye mitandao ya kijamii wakaanza kutekwa na kushirikiwa ambapo huko walipolekwa kulikuwa na maswali mengi waliyokuwa wakihojiwa na wakati mwingine wakipigwa ili kusema wao walikuwa wakina nani na kwa nini walikuwa wakiisumbua serikali hiyo.
Rundo la vijana wenye jina hilo walikuwa wakitekwa. Hakukuwa na mtu aliyekuwa akijua sababu ya vijana hao kupotea ghafla kwani kila kilichokuwa kikiendelea kilifanyika kimyakimya mno. Vyuoni, mitaani na sehemu zingine zote watu waliokuwa na jina la Godwin ilikuwa ni lazima kupotea mazingira ya kutatanisha.
“Kwa Dar es Salaam tuna Godwin mia saba mpaka sasa hivi,” alisema jamaa wa usalama wa taifa.
“Ni wote?”
“Hapana ndiyo tunaendelea kuwatafuta wengine.”
“Basi sawa.”
Godwin hakujua kilichokuwa kikiendelea. Siku moja akiwa katika kituo cha Daladala cha Makumbusho akiendelea na mambo yake akashangaa wanaume wawili waliokuwa na miwani ya jua wakija pale alipokuwa amekaa, hata kabla hajauliza swali lolote lile, mwanaume mmoja akamshika mkono na kumvuta pembeni.
“Jamani kuna nini?” aliuliza Godwin kwa sauti ya kisela tena huku akiwa na kipensi chake na sikioni akiwa na sigara.
“Twende huku!”
“Wapi masela! Mbona mnanishika kibabe washikaji?” aliuliza Godwin huku akiwashangaa watu hao, tayari alihisi kwamba walikuwa usalama wa taifa.
Wakati akiwa anauliza maswali zaidi, akashangaa kuona gari moja aina ya Noah ikija kule alipokuwa, mlango ukafunguliwa, akasukumiwa ndani ya gari na kuondoka mahali hapo huku kila mmoja akishangaa kwamba ilikuwaje mshikaji wao wa nguvu akamatwe kibabe namna ile.
***
Thomas First na Bruno Mendez wakaingia nchini Tanzania kama wapelelezi waliotumwa kutoka nchini Uswis na kwenda Tanzania kwa ajili ya kumtafuta mtu aliyekuwa amehamisha pesa kutoka katika akaunti ya Rais Bokasa na kwenda kwenye akaunti ya hospitali ya St. Lucas nchini Marekani.
Hakukuwa na mtu aliyejua chochote kuhusu watu hao, walionekana kuwa wa kawaida ambapo vibali vyao vyote vilionyesha kwamba waliingia nchini Tanzania kwa ajili ya kutembelea mbuga mbalimbali za wanyama.
Hapo uwanja wa ndege wakachukua teksi ambayo iliwapeleka moja kwa moja mpaka katika Hoteli ya Jumanji iliyokuwa Posta Mpya na kutulia hapo. Vichwa vyao vilikuwa vikifikiria kazi kubwa iliyokuwa mbele yao, hawakujua pa kuanzia lakini waliamini kwamba kama wangekutana na maofisa wa usalama wa taifa basi ingekuwa kazi nyepesi mno kujua ni kit gani walitakiwa kufanya.
Wakakaa katika vyumba tofauti ila kwa kuwa walikuwa na mengi ya kuzungumza, wakatumia chumba kimoja na kuanza kujadili ni kitu gani walitakiwa kufanya. Hawakujua Kiswahili ila kwa kuwa akaunti ya Mabadiliko ya Kweli ilikuwa hewani na ilikuwa ikifanya kazi kama kawaida, wakataka kuitumia kumpata mtu wao.
Ilionyesha kwamba mtumiaji huyo alikuwa nchini Uingereza, walijua kwamba taarifa hizo hazikuwa sahihi hivyo walichokuwa wakikitaka ni kujua kwanza namba iliyokuwa ikitumika ilikuwa eneo gani kwa kipindi hicho.
“Kwenye hii akaunti ameweka namba yake ambayo inatumiwa na kila mtu anayetaka kumtumia taarifa, nadhani tukianza na hii tunaweza kufanikiwa,” alisema Bruno.
Katika akaunti yake ya Mabadiliko ya Kweli, Godwin aliweka namba ya simu ambayo ilitumika kwa watu waliokuwa mbali naye kumtumia taarifa za ukweli juu ya kitu kilichokuwa kikiendelea wakati wowote ule, kwa kupitia namba hiyo ya Kimarekani, alitumiwa picha na taarifa zingine ambazo hakuwa akizifahamu.
Alichokifanya Bruno ni kupiga picha na kisha kuituma katika namba hiyo, alipohakikisha kwamba picha imetumwa, akapiga simu mpaka Uswisi ambapo akaomba wawasiliane na watu wa mtandao wa WhatsApp na kuwaambia kuhusu namba ile na picha iliyokuwa imetumwa.
Hilo halikuwa tatizo, mawasiliano yakafanyika. Mara ya kwanza WhatsApp walipoambiwa walikataa kwani hawakutaka kabisa kutoa taarifa za mteja wao yeyote yule, waliwaambia hivyo kwa kuwa hata siku chache zilizopita kampuni ya Apple ilikutana na suala hilohilo la kutoa taarifa za mteja wao katika suala zima la kigaidi lakini wakakataa kufanya hivyo.
Waliwabembeleza mno, tena wakati mwingine kumtumia rais wao na kuwaambia ni kwa jinsi gani walikuwa wakimuhitaji mtu huyo ambaye alionekana kuwa hatari kupita kawaida kwa kufanya muhamala wa kifedha pasipo kibali cha mwenye akaunti.
Baada ya kuambiwa hivyo, WhatsApp wakakubaliana nao na kuwafanyia kile walichotaka kukipata. Wakapewa taarifa kwamba mtumiaji wa namba hiyo hakuwa nchini Marekani kama ilivyokuwa ikionyesha bali alikuwa barani Afrika, nchini Tanzania katika Jiji la Dar es Salaam.
“Dar es Salaam kubwa sana. Tutampataje sasa?” aliuliza Thomas.
“Subirini akifungua picha tutajua yupo wapi. Ila taarifa za mwisho zinaonyesha kwamba yupo ndani ya Jiji la Dar es Salaam.
“Sawa. Tunasubiri!”
“Haina shida.”

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumamosi hapahapa.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom