Dunia haina usawa

Dunia haina usawa

DUNIA HAINA USAWA

Kila mtu chuoni Waseda alikuwa na hamu ya kumuona Godwin, hawakuamini kama mtu mweusi angekuwa na uwezo wa kuyarudisha mafaili na wakati watu wengi weupe walishindwa kufanya hivyo.
Mkuu wa chuo, Tamashi hakutulia, alitaka kumuona Godwin kwa mara nyingine na kumuomba msamaha kwa yote ambayo aliyasema dhidi yake, kwa dharau aliyomuonyeshea kwamba hakuwa na uwezo wa kufanya jambo lolote lile kwa kuwa tu kulikuwa na wataalamu wengi ambao walishindwa.
Godwin hakuonekana, kila mmoja alijua kwamba kijana huyo aliondoka chuoni hapo, kitu kilichowatia hofu walimu wote chuoni hapo ni kwamba inawezekana kijana huyo akahama chuo kwa kile kilichokuwa kimetokea kwa kipindi kirefu na wakati alikuwa na uwezo mkubwa.
Kupitia Godwin, waliamini kwamba chuo kingetangazwa sana kwamba kulikuwa na mwanafunzi aliyekuwa balaa, mwanafunzi aliyefanya kazi ambayo hata watalaamu kutoka serikalini walishindwa kuifanya.
Taarifa za kile alichokifanya zikaanza kusambazwa kila kona, watu walishangazwa mara baada ya kuzina picha za mwanaume mweusi katika mitandao ya kijamii. Hakukuwa na aliyeamini kwamba mwanaume huyo ndiye aliyefanya jambo hilo lilimuacha mdomo wazi kila mmoja.
Kwa kila kila mmoja alitamani sana kumuona Godwin, wengi wakaanza kutafuta namba yake ya simu kwa ajili ya kuwasiliana naye. Hilo halikuwa tatizo, Takoshima aliwapatia namba kwa lengo la kuwasiliana naye.
Walipiga na kupiga lakini simu haikuwa ikipokelewa, si kwamba Godwin hakuziona namba hizo zilizokuwa zikiingia katika simu yake, aliziona lakini hakutaka kabisa kupokea kwani alijua kabla kwamba angepigiwa sana simu baada ya kufanya jambo kubwa ambalo kila mtu alishindwa kulifanya.
“Mbona simu hapokei?” aliuliza mwanafunzi mmoja, alikuwa amempigia simu zaidi ya mara kumi na tano na zote Godwin hakuwa amepokeea.
“Hata mimi mwenyewe najiuliza. Nimempigia sana simu lakini naona kimya,” alisema mwanaume mwingine.
Godwin alitulia chumbani kwake, moyo wake ulikuwa na furaha kubwa, kwa kila alichokuwa amekifanya kwake kilionekana kuwa ushujaa mkubwa. Alibaki akiwa amejilalia chumbani kwake, kichwa chake kilikuwa na mambo mengi, kwanza kabisa alikuwa na kiu ya kutaka kumfahamu mtu aliyekuwa ameiangamiza familia yake.
Maisha aliyopitia yalimuumiza kupita kawaida, alikuwa na hasira, alijua kulikuwa na kitu kilichokuwa kimetokea, alitaka kujua ukweli juu ya sababu zilizowafanya watu hao kuiangamiza familia yake na sababu ambayo iliwafanya kutaka kumuua mpaka yeye mwenyewe.
“Ila kama walitaka kuniua, kwa nini waliniwekea boya kwenye boksi?” hilo lilikuwa swali jingine kabisa lililokuja kichwani mwake, alibaki akijiuliza sana juu ya kile kilichokuwa kimetokea, kwa nini watu waliotaka kumuua ndani ya boksi walimuwekea boya? Je, hawakutaka kumuona akifa au lile boya liliwekwa na mtu mwingine? Kila alichojiuliza, alikosa jibu.
Wakati akifikiria mambo mengi ndipo akaona simu nyingi zikianza kuingia, akazichukua na kugundua kwamba zilikuwa namba ngeni, alijua kilichokuwa kimetokea, alijua ni kwa jinsi gani watu walitaka kufahamu kila kitu kilichotokea kwamba ilikuwaje mpaka kuweza kuyarudisha mafaili na wakati watu wengine walishindwa.
Hakutaka kujiuliza maswali mengi, akalala na alipoamka, kitu cha kwanza kabisa Mzee Yokosoko akaingia chumbani kwake huku akiwa na simu mkononi, hata kabla hajazungumza lolote lile, akampa ile simu na kumtaka kuangalia kilichokuwa kimeandikwa.
Godwin akaichukua na kuangalia, kulikuwa na taarifa kuhusu kile alichokuwa amekifanya. Kila mmoja alishangaa, hawakuamini kama kungekuwa na mtu aliyekuwa na uwezo wa kufanya kile kilichofanywa.
“Wewe ndiye umefanya hivi?” aliuliza mzee huyo huku akimwangalia Godwin kwa macho yaliyojaa mshangao.
“Oopss! Yaani kila mtu anakizungumzia kitu kidogo kama hiki,” alisema Godwin huku yeye mwenyewe akishangaa, hakuamini kama kila sehemu alizungumziwa yeye tu.
“Ni jambo kubwa sana. Nimepigiwa simu na marafiki zangu wanaofanya kazi katika kampuni kubwakubwa, wanataka kufanya kazi na wewe,” alisema Mzee Yokosoko.
“Wanataka kufanya kazi na mimi?”
“Ndiyo! Achana na hao, nimesikia pia taarifa za chinichini kwamba hata Microsoft na Apple wote wanataka kufanya kazi na wewe. Godwin! Wewe ni mtu wa aina gani?” alisema Mzee Yokosoko na kumalizia kwa swali.
Moyo wake ulifarijika, alikaa na Godwin kwa kipindi kirefu na kuamua kumsomesha, alishangaa kuona kumbe mtu aliyekuwa naye alikuwa na uwezo mkubwa namna hiyo.
Alikuwa akidharaulika na majirani wengi walimlaumu kwa kuamua kuishi na mtu mweusi lakini kwa kile ambacho Godwin alikifanya, kila mtu alimsifia huku wengine wakitamani hata kumfuata na kupiga naye picha.
“Nitahitaji kusoma zaidi,” alisema Godwin huku akimwangalia mwanaume huyo.
“Hutaki kufanya kazi?”
“Si kwa sasa!”
“Unajua kwamba Microsoft na Apple wanakuhitaji! Hutaki pia? Kila mtu anatamani sana kufanya kazi katika kampuni kubwa kama hizo, kwa nini hutaki?” aliuliza Mzee Yokosoko huku akionekana kutokuamini kama Godwin hakuwa na mpango wa kufanya kazi katika kampuni hizo zaidi ya kusoma.
“Hapana! Bado kuna mambo mengi nitahitaji kufanya. Kama kweli unahitaji pesa, hutakiwi kuwa na haraka ya kuzipata. Subira inahitajika ili upate zaidi,” alisema Godwin huku akimwangalia mzee huyo.
Walizungumza mambo mengi, aliendelea kumwambia kwamba hakuwa na lengo la kufanya kazi kwa kipindi hicho. Mzee Yokosoko hakutaka kuumlazimisha, akakubaliana naye na hivyo kumruhusu kuendelea na maandalizi yake ya kwenda chuoni.
****
Tanzania ilibadilika, kila mtu aliyekuwa akikaa nchini humo alikuwa akilalamika kutokana na ugumu wa maisha uliokuwa umetawala kila kona. Masikini walikuwa wakilia, pesa haikuonekana na hata ile kidogo iliyokuwa mitaani ilishikiliwa na watu wenye nguvu.
Uchumi ulishuka, idadi kubwa ya watu waliokuwa wamepigika kipindi cha nyuma, maisha yao yalizidi kuwa mabaya zaidi. Kila mtu alilia, hakukuwa na maisha mazuri tena, kila kona ni malalamiko tu ndiyo yalikuwa yakitawala.
Chama pinzani cha Tanzania National Party kilikuwa katika kazi nzito ya kuhakikisha inawaambia wananchi juu ya kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Udhaifu uliokuwa ukionekana katika uongozi huo, waliutumia huohuo kuhakikisha kwamba wanashinda katika uchaguzi ujao ambao ulitakiwa kufanyika baada ya miaka mitatu.
Watanzania walichoka, waliamini kwamba uchaguzi ndicho kitu pekee ambacho kingewafanya kuleta mabadiliko lakini hawakuwa na matumaini ya kutosha kwa kuwa tu kwenye kila uchaguzi, chama tawala kilishinda zaidi na zaidi.
Watu walitaka kuongea na Rais Bokasa, hawakujua ni kwa namna gani walitakiwa kufanya ili kumpata. Walipanga namna ya kumfikia rais huyo kwa kutumia maandamano lakini kitu cha ajabu kila walipokuwa wakiandamana, walipigwa vibaya na polisi waliokuwa wakihakikisha maandamano yanayofanyika ni yale yaliyokuwa na vibali tu.
“Kwani kelele zote zinatoka wapi?” aliuliza Bokasa huku akimwangalia Waziri wa Ulinzi, Bwana Edward Ngoshima.
“Eti maisha yamekuwa magumu. Umekaza sana,” alisema Ngoshima huku uso wake ukiwa na tabasamu.
“Kwa hiyo wanataka nilegeze?”
“Sijajua! Ila kwa mtazamo tu wanataka ulegeze, eti kuna watu wanakufa njaa,” alisema waziri huyo.
“Hahaha!”
“Ila tulichokigundua ni kwamba wapinzani ndiyo wanatumia watu hao, hakuna shida yoyote ile mitaani. Mambo yote yapo supa,” alisema waziri huku uso wake ukitawaliwa na tabasamu pana.
Watanzania walilalamika, walipiga kelele kila siku lakini hakukuwa na mabadiliko yoyote yale. Viongozi waliendelea kula bata huku wakiwasahau watu waliokuwa chini yao. Baada ya kuhangaika sana bila kupata msaada wowote ule ndipo Watanzania wakaanzisha mapambano mapya kupitia mitandao ya kijamii.
Akaunti mbalimbali zikaanzishwa, hizo zote zilikuwa ni za kuisema serikali kwamba kilichokuwa kikiendelea Tanzania hakikuwa kitu kizuri kwani watu walihitaji maisha bora ambayo yalihubiriwa kila siku kwenye majukwaa lakini mwisho wa siku kile walichokuwa wakikipata hawakuwa wakikitarajia.
Huko kwenye mitandao, watu wakaweka dukuduku zao, kurasa nyingi za kuipinga serikali zikaanzishwa lakini baada ya kuweka posti kumi, akaunti hizo zilisimama huku habari za nyuma ya pazia zikisema kwamba wamiliki wa akaunti hizo walikuwa wakiuawa baada ya kutafutwa.
“Mmh! Kwa hiyo hata mimi nikianzisha akaunti yangu ya kuipinga serikali nitauawa?” aliuliza jamaa mmoja.
“Ndiyo! Tena watakusaka kwa nguvu zote,” alisema jamaa mwingine, wakati watu wakijadili ni nani alitakiwa kuanzisha akaunti ya kuizungumzia vibaya serikali ndipo kukaibuka akaunti moja, akaunti iliyoitwa Mabadiliko ya Kweli ambayo kazi yake kubwa ilikuwa ni kuikosoa serikali na kuweka hadharani skendo nzitonzito za viongozi wa nchi hiyo.
***
Watanzania waliishi kwa hofu, kila mmoja aliogopa, maisha yao waliyaona yakiwa hatarini kwa kuhisi kwamba kwa lolote ambalo walitakiwa kulifanya au kuzungumza kinyume na sheria ilikuwa ni lazima watu wakamatwe na wengine kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
Watu hawakuwa na amani na matumizi ya mitandao, wengine waliweka posti zao zilizoirekebisha serikali lakini kwa kuwa ilikuwa na mkono mrefu, wengi wakajikuta wakikamatwa na kupelekwa sehemu ambayo hawakuwa wakiifahamu na kupewa onyo kali kwamba hawakutakiwa kuandika kitu chochote kile.
Kitendo cha akaunti ya Mabadiliko ya Kweli kuibuka ikawachanganya viongozi wengi wa serikali. Akaunti hiyo ilikuwa ikizungumzia maovu mengi waliyokuwa wakiyafanya viongozi huku ikiwa na picha iliyokuwa na ramani ya Tanzania iliyokuwa ikilia machozi ya damu.
Viongozi walichanganyikiwa, wengi wakahisi kwamba kulikuwa na kiongozi mmoja aliyekuwa akiwasaliti kwani wakati mwingine walikuwa wakizungumza mambo ya siri katika simu lakini siku iliyofuata kila kitu kiliwekwa wazi.
Picha zilisambazwa, mawaziri walionekana wakiingia katika hoteli za kifahari na michepuko yao, wakati mwingine video ziliwekwa kuonyesha kwamba mawaziri hao walikuwa katika vyumba vya hoteli na kufanya ufuska na wanawake mbalimbali kitu kilichowaletea aibu kubwa.
Mara kwa mara viongozi walikuwa wakikutana na kuweka vikao, kwa kile kilichokuwa kikiendelea kiliwaumiza vichwa vyao, walitaka kumfahamu mtu aliyekuwa katika mtandao huo ambaye alipata data kwa kiwango kikubwa na kuziweka wazi kwa Watanzania wote ambao walishabikia kutumika kwa mitandao.
Katika kila vikao walivyokuwa wakikaa kwa ajili ya kumzungumzia mtu aliyekuwa akitumia akaunti hiyo, walishindwa kumfahamu, mbele yao waliona giza, viongozi walizidi kuchafuliwa kila siku.
“Jamani! Hii ishu ni siriazi sana, ni lazima tumfahamu mtu anayefanya haya yote. Siri zetu anazipata wapi? Kama si sisi tunaompa, ni nani anampa?” aliuliza waziri mkuu huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Ni kweli mkuu! Hili suala linachanganya sana. Juzi nilikuwa nimeongea na rais kuhusu tatizo langu na kile kimada changu cha Sinza kinachonisumbua. Nimezungumza na rais kwa siri, tena kwenye simu usiku. Saa moja baada ya kukata simu, mazunguzmo yote yamewekwa kwenye ile akaunti. Nani alikwenda kusema? Rais? Hapana! Mimi mwenyewe? Hapana! Sasa nani alikwenda kumwambia?” aliuliza Makamu wa Rais, Bwana Issa Jumanne.
“Hapa kuna kitu! Hebu zungumzeni na vijana wetu wa IT na muwaambie kwamba hii akaunti inatakiwa kufungwa haraka sana,” alisema Rais Bokasa huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Sawa mkuu!”
“Ina wafuasi wangapi mpaka sasa?”
“Laki nane!”
“Ifungeni haraka sana!”
“Saa mkuu!”
Hilo ndilo lililotakiwa kufanyika kwa haraka mno. Mawasiliano yakafanyika, vijana wa IT wakaitwa kwa ajili ya kuifanya kazi hiyo. Kwao, kila kitu kilionekana kuwa chepesi sana hivyo wakaingiza programu zao kwa ajili ya ‘kuihack’ akaunti hiyo na kuifunga.
Matokeo yake yalikuwa ni tofauti na jinsi walivyofikiria kabla, walijua kuwa kuifunga kilikuwa kitendo cha haraka sana kama walivyofanya kwa akaunti za watu wengine. Kwa akaunti hii, walichanganyikiwa, walifanya kila liwezekanalo kwa ajili ya kuifunga lakini hawakuweza.
Hawakuishia kuifanya kazi hiyo wao tu bali waliwashirikisha watu wengine kwa ajili ya kuifunga akaunti hiyo lakini ikawa ngumu kufungika. Viongozi wa chama tawala wakachanganyikiwa, hawakutaka kudili na watu wa vyama pinzani, kwao, walichokuwa wakidili nacho usiku na mchana kilikuwa ni akaunti hiyo ambayo kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele ndivyo siri zao zilivyozidi kuvuja.
“Vijana wanaendeleaje?” alisikika Rais Bokasa.
“Kiongozi! Tumewaambia, wanahangaika nayo!”
“Wiki mbili bado tu?”
“Wanasema ni kazi ngumu mno, tuwape siku zaidi,” alisema waziri mkuu.
“Sawa. Waambie wajitahidi sana!”
Wakati wao wakihangaika kuifunga akaunti hiyo, Watanzania walizidi kuifuata katika Mtandao wa Instagram na ‘kuifollo’ kitu kilichoifanya kuwa na wafuasi wengi kila siku.
Huko ndipo Watanzania walipokuwa wakipata taarifa zote mbaya za viongozi, ndipo ambapo walipokuwa wakijua kiongozi yupi alikuwa akitoka kimapenzi na kiongozi yupi.
Watu wakasahau maisha machungu ya viongozi waliokuwa wakiwanyonya, macho na masikio yao yalikuwa katika akaunti hiyo iliyokuwa ikisema siri zao nyingi kiasi cha kuwachanganya wote.
Watu wa IT baada ya kuona kwamba wameshindwa kuifunga akaunti hiyo wakaanza kupambana kuhakikisha wanajua mahali ilipokuwa ikifunguliwa.
Hilo likaonekana kuwa tatizo pia kwani taarifa walizokuwa wakizipata zilikuwa zikiwachanganya wote. Wakati wakianza kufuatilia, waliona kabisa kwamba mtumiaji kwa kipindi hicho alikuwa Mbagala Zakhem, wakati wakifutailia huko, wakaona kwamba mtumiaji alihama na alikuwa Mikocheni B. Wakageuza gari harakaharaka na kuanza kuelekea huko, wakati wakiwa njiani, ikaonyesha kwamba mtumiaji huyohuyo alihama na kuhamia Kibaha, walichanganyikiwa.
Wakati wakijiuliza nini kilikuwa kikiendelea, ikaonyesha kwamba mtumiaji huyo alikuwa amehama na kuhamia nchini Sweden, tena katika siku hiyohiyo na baadaye kuonyesha kwamba alikuwa nchini Argentina.
Kwa mabadiliko hayo machache wakagundua kwamba walikuwa wakidili na mtu aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kuchezea mitandao. Walichanganyikiwa, hata kuwapa ripoti viongozi wao kwamba walishindwa waliogopa kufanya hivyo.
“Huyu jamaa yupo wapi hasa?” aliuliza kijana mmoja wa IT.
“Inachanganya sana. Eti hapa inaniambia kwamba mtumiaji yupo Ufaransa. Jamani! Huyu mtu ni nani?” aliuliza jamaa mwingine huku kwa kumwangalia tu alionyesha ni jinsi gani alikuwa amechanganyikiwa.
“Umeingia kwenye Mabadiliko ya Kweli leo?’ aliuliza jamaa mmoja.
“Hapana! Si unajua nipo job. Kuna nini?” aliuliza jamaa aliyepewa taarifa.
“Kumbe Spika wa Bunge, Bwana Ramadhani Nyakunyaku alikuwa akimtongoza mke wa Waziri wa Jinsia, Wazee na Watoto, Bi Zubeda,” alisema jamaa huyo.
“Acha uongo bwana!”
“Ndiyo hivyo! Ingia huko uone.”
Hiyo ilikuwa habari kubwa ya siku hiyo ambayo watoto wa mjini walisema kwamba ulikuwa ubuyu wa moto kabisa. Kila Mtanzania hakuamini alichokuwa akikiona, meseji za kimapenzi za watu hao wawili zilikuwa zimewekwa hadaharani, kila mtu aliona kilichokuwa kimetokea, wengi walishangaa kwamba ilikuwaje wawili hao watongozaje kiasi cha spika wa bunge kusema kwamba alikuwa tayari kupoteza kila kitu ila si kulipoteza penzi la mwanamama huyo?
Ilikuwa ni aibu kubwa. Kila mmoja alitoa maoni yake katika mitandao ya kijamii. Wengi walishtushwa na baada ya serikali kuona kiongozi huyo akiingia doa, wengi wakajitokeza na kusema kwamba habari hizo hazikuwa za kweli.
Wakati viongozi mbalimbali wakitetea kwamba zilikuwa ni habari za uongo, hapo ndipo ukaandikwa ujumbe katika akaunti ya Mabadiliko ya Kweli ikisema kwamba kwa kiongozi yeyote aliyekuwa akiona kwamba posti zote kuhusu meseji zile zilikuwa zimetengenezwa aibuke na kusema mbele ya watu ili waanze kudili na mtu huyo kuonyesha hadharani maovu yake ya nyuma ya pazia.
“Mkuu tulisikia kwamba wewe ndiye ulisema kwamba posti zile si za kweli,” alisema mwandishi mmoja wa Gazeti la Uwazi, alikuwa akimhoji waziri mkuu.
“Mimi? Walaaaa! Sijawahi kusema maneno hayo! Kwanza lini? Nilihojiwa?” aliuliza waziri mkuu kwani alijua kwamba kama angesema kuwa yeye ndiye aliyesema hivyo basi kesho tu habari zake zingekuwa katika akaunti ya mtandao huo.
“Kwa hiyo nani alisema?”
“Wala sijui! Naomba msinipakazie! Kwanza hiyo habari si ya kuandika. Mmenisikia? Yaishie hapahapa,” alisema waziri mkuu na kumalizia kwa mkwara mzito.
Hakukuwa na kiongozi aliyejitokeza hadharani kuonyesha kwamba posti zilizokuwa zimewekwa kuhusiana na meseji zile hazikuwa za kweli kwani kila mmoja aliogopa kusema lolote lile kutokana na mkwara uliokuwa umewekwa kwamba kwa yeyote ambaye angejitokeza ilikuwa ni lazima siri zake za nyuma ya pazia ziwekwe wazi.
Wakati watu wakijadili kuhusu mjadaa wa spika wa bunge kumtongoza mke wa waziri ndipo ujumbe mwingine wa neno moja ukaonekana kwenye akaunti ile, ujumbe mfupi uliosomeka ‘Boooom’ kumaanisha kwamba kulikuwa na bomu lililokuwa limelipuka ambalo watu walitakiwa kusubiri ili kujua ni bomu gani hilo ambalo lingewavua nguo viongozi wengi.
“Jamani tumekwisha!” alisema mkurugenzi wa idara ya mawasiliano, kwa kile kilichokuwa kikiendelea, hakuna mtu aliyekuwa salama.
“Kuna nini?”
“Kuna bomu linalipuliwa huko mitandaoni! Jamani huyu mtu atatuua kwa presha,” alisema mkurugenzi huyo.
“Lini?”
“Kesho! Sijui linahusu nini! Mungu naomba lisinihusu mimi wala kituo changu cha kazi manake nitajinyonga,” alisema mkurugenzi huyo.
Huo ndiyo ubuyu uliokuwa umesambazwa kila kona. Kila mtu alitaka kujua hilo bomu kubwa lililokuwa limeandaliwa, kila mmoja alitaka kufahamu ni bomu gani ambalo lingewavua nguo viongozi wengi.
Kila mmoja alichanganyikiwa, hakukuwa na waziri aliyekuwa na raha, kila mmoja alikuwa na hofu ya kuona kwamba alikuwa ndani ya bomu hilo kubwa. Waziri mkuu hakuwa na furaha, mawaziri wengine mpaka Rais Bokasa wote hawakuwa na furaha, walitamani kuifungia akaunti hiyo lakini kila walichokuwa wamejaribu kufanya, hawakufanikiwa.
“Hakika hili bomu halitomuacha mtu salama,” alisema jamaa mmoja kwenye mtandao wa Facebook huku akitanguliza na ‘emoj’ nyingi za kucheka. Kila mtu akasubiri kuona ni bomu gani hilo lingewekwa katika akaunti hiyo iliyokuwa imefikisha wafuasi milioni moja na nusu.
***
Kila mtu alikuwa akisikilizia akaunti ya Mabadiliko ya Kweli kwenye Mtandao wa Kijamii wa Instagram kuona ni kitu gani kingeandikwa ambacho kingetafsiriwa kama bomu nchini Tanzania.
Watu wakapeana taarifa, kila mmoja alikuwa makini kwenye akaunti hiyo, waandishi wa habari za mitandaoni nao wakajiweka mkao wa kula, walitaka kuona kile ambacho kingeandikwa na kuwekwa katika akaunti hiyo.
Ilipofika majira ya saa saba mchana, watu wakaona kile kilichokuwa kikisubiria, kulikuwa na orodha ya majina ya viongozi waliokuwa wakitoka kimapenzi na wasichana mbalimbali wakiwemo wale wa Bongo Muvi.
Kila mmoja alikuwa na hamu ya kusoma, waliambiwa kwamba kwa kila kiongozi aliyekuwa akitoka kimapenzi na mwanamke wa nje, meseji zao za kimapenzi zingewekwa katika mtandao huo na mtu wa kwanza kabisa ambaye meseji zake zilitakiwa kuweka hadharani katika mtandao huo alikuwa Waziri Mkuu, Godfrey Francis.
Waziri huyo alikuwa akitoka kimapenzi na mwanadada aliyekuwa akitamba kwenye muziki kipindi hicho, Lady Maggy aliyekuwa akiimba RnB. Meseji zao za kimapenzi zikawekwa hadharani, zilionyesha jinsi waziri huyo alivyokuwa akimtongoza Lady Maggy mpaka walipoonana hotelini na kulala pamoja.
Hawakumaliza hapo, waliendelea kwenye uhusiano huku wakati mwingine wakisafiri kwenda Marekani kula raha. Kila uovu wa waziri huyo uliwekwa wazi na kilichowakasirisha watu wengi ni kuona kwamba alimpa mimba msichana huyo na kumwambia autoe.
“Kumbe ile kukemea kwake utoaji wa mimba hata yeye alishindwa kujikemea! Mtu mzima, una mke na watoto lakini bado tu unaendekeza wanawake wa nje, watakusaidia nini?” aliuliza jamaa mmoja, kwa kumwangalia tu alionekana kuwa na hasira mno.
Ilikuwa ni aibu kubwa kwa waziri mkuu, hakuamini alichokuwa akikiona, alijifungia chumbani kwake huku akilia. Mbele yake, hakujua angefanya nini, hata kujitetea alishindwa kwani kwa jinsi posti hiyo ilivyoandikwa katika akaunti ile, ilikuwa na ushahidi wote na hata baadhi ya mambo aliyokuwa akiyafanya, yaliwekwa kuonyesha kwamba hakusingiziwa.
“Siwezi kuishi tena! Hii ni aibu! Nitauficha wapi uso wangu,” alisema waziri mkuu huku akionekana kuchanganyikiwa.
Alishindwa kuvumilia, alikuwa na mke, watoto, ndugu na kubwa zaidi kulikuwa na Watanzania, wangemuonaje? Wangemzungumziaje kwa ule uchafu aliokuwa ameufanya?
Aliendelea kukaa chumbani kwake, hakutaka kutoka, alijifungia na hata mke wake alipogonga kwa ajili ya kuzungumza naye, hakuufungua mlango. Moyo wake ukashindwa kabisa kuvumilia, akafungua droo iliyokuwa kwenye kabati lake, akachukua bastola na kurudi kitandani ambapo akajiwekea kichwani mwake.
“Ni bora nife! Nitauficha wapi uso wangu mimi!” alisema waziri mkuu, hakutaka kuchelewa hapohapo mlio wa bastola ukasikia chumbani kwake.
“Paaaaa…” akaamua kujiua.
****
Kila mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Waseda akamkubali Godwin, alikuwa mwanafunzi mwenye uwezo mkubwa ambaye aliwafanya watu wote kugundua kwamba si watu weupe tu waliokuwa na akili kubwa bali hata watu weusi nao walikuwa balaa.
Hilo lilimpa furaha, akafarijika kwani alibadilisha kila kitu, dharau za Wazungu na Wajapan zikapotea na hivyo kuwafanya hata watu weusi kujisikia fahari kila walipokuwa wakipita mitaani.
Huo ulikuwa mwaka wake wa kwanza. Ulipoingia mwaka wa pili, uwezo wake ukaongezeka maradufu, kila mwanafunzi akatamani kufundishwa na Godwin kiasi kwamba kila alipokuwa watu walimzunguka, kila mmoja alitaka kuona ni kitu gani mwanaume huyo alikuwa akikifanya katika kompyuta yake.
Kila alipokuwa, kompyuta ilikuwa pembeni yake, makampuni mengi yalimfuata yakitaka kumuajiri lakini hakutaka kuangalia pesa, aliamini kwamba zingekuja kama tu angesoma sana na kuijua kompyuta vilivyo.
Wasichana nao hawakuwa nyuma, wale waliokuwa wakimtenga na kumuona si lolote, wakaanza kujigonga kwake, wakachukua namba yake ya simu na kuanza kumsumbua.
Kichwa cha Godwin kilikuwa kwenye masomo yake tu, hakufikiria mapenzi, alijiona kuwa na safari ndefu mbele yake na hivyo ilikuwa ni lazima kupambana kwa nguvu zote.
Alipoingia mwaka wa tatu ndipo akapata wazo kwamba ilikuwa ni lazima apambane kwa ajili ya nchi yake. Kila alipofuatilia katika mitandao ya kijamii alikutana na komenti nyingi za watu wakiilalamikia serikali iliyokuwa chini ya Rais Bokasa kwamba iliwanyonya Watanzania na waliifanya nchi kuwa kwenye kipindi kigumu.
Aliyafahamu maumivu hayo, hakutaka kuona yakiendelea na ndipo hapo alipoamua kufanya jambo kwa ajili ya Tanzania yake, kama viongozi ndiyo waliokuwa wakilalamikiwa kufanya uchafu wote basi ilikuwa ni lazima kupambana nao kupitia mitandao ya kijamii.
“Nitaanzisha akaunti! Nitaiita Mabadiliko ya Kweli, nitakuwa na kazi ya kutoa siri za viongozi. Ila nitapata vipi baadhi ya vitu? Ngoja nitengeneze urafiki na baadhi ya watu katika mitandao ya kijamii,” aliwaza.
Hicho ndicho alichokifanya, ilikuwa ni lazima kupata namba za simu za viongozi mbalimbali, hakujua angezipata vipi lakini baada ya kupata marafiki kadhaa katika Mtandao wa Kijamii wa Facebook ndipo hapo alipoomba namba za viongozi mbalimbali na kupewa.
Mtu ambaye alikuwa rafiki yake wa karibu katika Mtandao wa Facebook alikuwa Ally Abdul, mmoja wa waandishi wa magazeti ya Siasa nchini Tanzania. Mwanzo alimwambia kwamba yeye mwenyewe alikuwa mwandishi wa kujitegemea ambaye alikuwa akifanya kazi nchini Japan hivyo alikuwa na uhitaji wa kuwa na namba za viongozi wengi kitu ambacho hakikuwa na tatizo lolote lile.
Akapewa namba za viongozi mbalimbali, akazichukua na kuanza kuziingiza katika system yake na ‘kuzihack’, akawa na uwezo wa kuangalia simu zilizokuwa zikitoka na kuingia, alikuwa na uwezo wa kusikia sauti za mawasiliano na kuyarekodi, alikuwa na uwezo wa kusoma meseji zote pasipo wenyewe kufahamu lolote lile.
Hilo lilimsaidia na ndilo lililomfanya kupata mawasiliano ya viongozi hao na kuweka katika akaunti yake ya Mabadiliko ya Kweli iliyokuwa katika Mtandao wa Instagram.
Kwa uwezo wake wa kuwa na digrii ya kwanza katika masuala ya kompyuta, hakukuwa na mtu aliyembabaisha, aliifunga akaunti yake vilivyo, hakukuwa na mtu aliyeweza kuingia kwenye akaunti yake kimagendo na ilikuwa ikibadilisha maeneo kila baada ya dakika kumi kwa ajili ya kuwachanganya watu wengi ambao wangejitolea kuifuatilia.
Kwa kupitia namba hizo ndipo akagundua kwamba kulikuwa na viongozi wengi waliokuwa wakitoka kimapezi na wanamuziki, kulikuwa na matukio mengi ya aibu ambayo aliamini kwamba kama angeyaweka katika akaunti yake, Tanzania ingetikisika, akaamua kuanza na Waziri Mkuu, Bwana Godfrey Francis.
****
Kila mmoja alisikitika baada ya kusikia kifo cha waziri mkuu, hakukuwa na mtu aliyeamini kwamba waziri huyo angechukua uamuzi mkubwa kiasi hicho cha kuitoa roho yake.
Waliokuwa wakitumia mitandao ya kijamii, waliandika maoni yao, wachache walikuwa wakimlaumu mtu aliyekuwa akitumia akaunti ya Mabadiliko ya Kweli lakini wengi walipongeza kwa kile kilichokuwa kimetokea.
Kifo chake kiliwatisha viongozi wengi, wakaogopa kwa kuona kwamba huo ndiyo ulikuwa mwanzo na baada ya yeye kungekuwa na wengine wengi ambao meseji zao zingewekwa hadharani kwa mambo yote waliyoyafanya gizani.
“Sisi tunataka wengine. Watu waovu ni lazima wawekwe wazi kabisa, haiwezekani watu wafanye ujinga kama huu halafu tukae kimya tu,” alisema jamaa mmoja aliyekuwa akikisapoti chama pinzani cha Tanzania National Party.
Hakukuwa na kiongozi aliyekuwa na amani kipindi hiicho, kila mmoja aliogopa kwa kuona kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wao kwani mambo ambayo yalifanyika gizani yalikuwa makubwa mno.
Wakati watu wakihuzunika kwa msiba uliotokea, wakapata taarifa nyingine kwamba hata Spika wa Bunge, Mheshimiwa Ramadhani Nyakunyaku naye alijiua usiku uliopita baada ya meseji zake za kimapenzi akimtongoza mke wa waziri kuwekwa siku mbili zilizopita.
Akaunti ya Mabadiliko ya Kweli ikawa gumzo kila kona, ikazidi kuwa maarufu na kuwafanya hata wale watu ambao hawakujua kilichokuwa kikiendelea huko kutamani kusoma kila siku kilichokuwa kikiendikwa.
Rais Bokasa alichanganyikiwa, aliona kabisa kwamba mwisho wa kila kitu mtu aliyekuwa akitumia akaunti hiyo angeweka mambo yake, hivyo akataka kujilinda kwa kuwaita watu waliokuwa wataalamu wa kompyuta kutoka Afrika Kusini kwa ajili ya kufanya kazi ya kuifuta akaunti hiyo.
Ndani ya siku mbili, wataalamu hao wakafika nchini Tanzania na kupewa rasmi kazi hiyo kwa malipo makubwa. Bila tatizo lolote lile, vijana hao wakaanza kufanya kazi ya kuhangaika kuifuta akaunti hiyo.
“Hii si kazi ngumu! Kitu kama hiki kilitokea nchini kwetu. Kulikuwa na kichaa mmoja alianzisha akaunti kama hii, kutwa nzima alikuwa akimzungumza Nelson Mandela, hakuchukua muda mrefu, ndani ya wiki tu, tukaifuta,” alisema jamaa mmoja, alikuwa akijigamba mbele ya Rais Bokasa.
“Safi sana. Ndiyo maana nimewaita. Ngoja niwaache mfanye kazi yenu,” alisema Rais Bokasa na kutoka ndani ya chumba hicho huku akiwaacha vijana hao wawili wakiwa wanajiandaa kufanya kazi ya kuifuta akaunti ya Mabadiliko ya Kweli katika Mtandao wa Kijamii wa Instagram.
***
Ilionekana kuwa kazi nyepesi mno kabla ya kuifanya lakini baada ya kuianza ndipo wakagundua kwamba haikuwa kazi nyepesi hata mara moja. Vijana wa IT waliotoka Afrika Kusini wakaanza kuhangaika kuifuta akaunti hiyo, ilikuwa kazi kubwa mno, walitumia kila aina ya programu, ujuzi wao wote katika kufuta akaunti hiyo lakini ilishindikana kabisa.
Walihangaika kwa saa kumi na mbili, vijasho vilikuwa vikiwatoka, hawakujua namna ambavyo mtu huyo alikuwa ameifunga akaunti yake, walijaribu kila aina ya mbinu na wakati mwingine kuwasiliana na watalaamu wenzako wa Kiholanzi waliokuwa Uholanzi lakini hawakufanikiwa.
Kwao, tangu waanze kufanya kazi ya kufanya lolote katika kompyuta, iwe kwenye programming au network hawakuwahi kukutana na kitu kigumu kama hicho. Pamoja na kuwa na masters zao lakini hawakufanikiwa kabisa kuifuta akaunti hiyo.
Rais Bokasa aliwaamini vijana hao kwamba wangeweza kufanikiwa kuifunga akaunti hiyo ambayo kila siku ilizidi kuongeza watu waliokuwa wakiifuata kwa ajili ya kupata habari chafu za viongozi wa nchi hiyo.
Alitulia ikulu huku akiwa ameweka miguu juu, alifurahia, alikenua kila wakati huku muda mwingi akiiangalia simu yake kwani alijua kwamba angepigiwa na vijana hao ambao wangempa taarifa kwamba akaunti ile ilifungwa na asingeweza kuiona tena.
Alisubiri simu hiyo kwa saa nyingi, hakuona dalili za kupigwa, akaingiwa na hofu kitu kilichomfanya kuichukua na kuwapigia vijana ambao aliwaacha kusimamia kazi hiyo ambao walimwambia kwamba bado hawakuwa wamefanikiwa.
“Kwa saa kumi na mbili?” aliuliza huku akiwa haamini alichokuwa akikisikia.
“Bado mkuu!”
“Unavyoona kuna dalili za kufanikiwa?”
“Sidhani! Wote naona wanatokwa na jasho jembamba, nahisi hii kazi imekuwa ngumu sana kwao,” alisikika kijana huyo kwenye simu.
Rais Bokasa akakata simu, uso wake ukabadilika, ndita zikaanza kuonekana, moyo wake ulimuuma mno, kwa kipindi hicho hakukuwa na kitu kilichomuuma kama kuona akaunti hiyo ikiendelea kuwa hewani.
Hakuona kama maisha yake yangekuwa na usalama, kulikuwa na mambo mengi machafu aliyokuwa ameyafanya nyuma ya pazia na aliamini kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima mmiliki wa mtandao huo ayapate mambo hayo na kuyarusha hewani kama ilivyokuwa kwa waziri mkuu.
Wakati akiwa chumbani kwake huku akiwa hajui ni kitu gani alitakiwa kufanya, ghafla akashtushwa na mlio wa simu, alichohisi ni kwamba alikuwa akipigiwa na kijana yule kuambiwa kwamba kazi ilifanikiwa, alipoichukua na kuangalia kwenye kioo, macho yake yakatua katika jina Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Selemani Kimwinyi
“Niambie kuna nini” alisema Rais Bokasa huku akiwa ameiweka simu hiyo sikioni kwake.
“Kazi imeanza upya mtandaoni! Kuna tuhuma nyingine nzito, ni nzito zaidi ya zile za waziri mkuu,” alisikika Kimwinyi kwenye simu.
Kabla ya kuzungumza lolote juu ya tuhuma hizo zilizokuwa mtandaoni, Rais Bokasa akanyamaza kwa muda, akahisi mwili wake ukianza kutoka na kijasho chembama, mwili ukakosa nguvu na hapohapo kukaa kochini.
Alijua fika kwamba mtu aliyekuwa ameandikwa kwenye mtandao ule alikuwa yeye na kilichomfanya kuhisi hivyo ni kwa sababu tu alipigiwa simu na mkurugenzi huyo wa usalama wa taifa kwani kama tuhuma hizo zisingemhusu yeye, asingepigiwa simu hiyo kupewa taarifa.
“Subiri kwanza!” alisema rais huyo huku akishusha pumzi zake.
Akakata simu, hakutaka kuendelea kuiacha simu hiyo hewani, alitaka kuona ni kitu gani kilichokuwa kimeandikwa katika akaunti hiyo. Hakutaka kuchelewa, hapohapo, huku akitetemeka akafungua akaunti yake ya siri iliyokuwa kwenye Mtandao wa Kijamii wa Instagram na moja kwa moja kwenda kwenye akaunti hiyo.
Alipoifungua tu, moyo wake ukapiga paaa! Kulikuwa na picha kubwa ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Michael Lazaro ambapo kwa chini kulikuwa na maneno mengi yaliyoeleza kuwa alikuwa mtu aliyejihusisha na mapenzi ya jinsia moja huku pia kukiwa na idadi ya watu ambao amewahi kutembea nao.
“Ni waziri anayelala na wanaume wenzake! Ni mtu mbaya, amelala na viongozi wengi, ila wa kwanza kabisa ambaye nitamtaja ni mtu mliyempa dhamana, Rais Bokasa, ushahidi upo, nawatumia mazungumzo yao katika posti inayofuata. Kama akijitokeza kubisha, nitawawekea na picha zao wakiwa chumbani, yaani wawili tu,” ilisema posti iliyowekwa katika akaunti hiyo.
Bila kutarajia, machozi yakaanza kumtoka rais huyo, hakuamini alichokuwa akikiona, alishindwa kujua afanye nini kwani kila alipoisoma posti hiyo zaidi na zaidi, aliwaona Watanzania wakiwa mbele yake, walimcheka huku wakimdhihaki kwa kile alichokuwa amekifanya.
Wachangiaji kwenye posti hiyo walijitokeza kwa wingi. Waliiamini akaunti hiyo, kila kitu kilichokuwa kikiandikwa kilikuwa na ushahidi wa kutosha, na wengi waliokuwa wakichangia walionyeshwa kuguswa na kile kilichokuwa kikiendelea, yaani rais wa nchi afanye mambo ya kishoga kama hayo, kila mtu alishtushwa kwa posti hiyo.
“Jamani! Dunia inakwenda wapi huku? Kumbe tunaongozwa na rais mpumbavu kama huyu! Yaani nchi inapinga vitendo vya kishoga kila siku kumbe yeye ndiye namba moja kwa kufanya ushenzi huo. Hakika dhambi hii haitomuacha salama,” aliandika jamaa mmoja, kwa jinsi komenti hiyo ilivyoandikwa, alionekana kukasirika mno.
Hilo ndilo likawa gumzo nchi nzima, kila mmoja aliyeiona posti hiyo alimwambia mwenzake, mitandaoni hakukukalika, kila mmoja alionekana kuguswa kwa kile kilichokuwa kimetokea.
Wengi waliumia, hawakuamini kama watu wastaarabu kama wao waliongozwa na mtu mpumbavu kama Rais Bokasa. Kila mmoja alitaka kusikia ikulu ingesema nini juu ya tuhuma hizo kwani mbali na kuweka posti hiyo kungekuwa na ushahidi wa meseji walizokuwa wakiwasiliana
“Jamani mwenzenu napenda abishe ili tuzione hizo picha,” alisema jamaa mmoja.
Viongozi wa Chama Pinzani, Tanzania National Party wakatumia mwanya huohuo kuweka mikutano isiyo rasmi na kuzungumza na wananchi juu ya kile kilichokuwa kikiendelea ambacho kilionekana kuichafua nchi.
Wakati hayo yote yakiendelea, akaunti ya Mabadiliko ya Kweli iliendelea kupata wafuasi wengi, zaidi ya watu laki mbili walikuwa wakiongezeka kwa siku na ndiyo ikawa akaunti ya kwanza kufikisha watu milioni kumi nchini Tanzania.
Vichwa vya watu wengi vilijiuliza juu ya mtu aliyekuwa nyuma ya akaunti hiyo, wengi walihisi kwamba mtu huyo alikuwa mmoja wa viongozi serikali na alikuwa akifanya kazi zake kwa siri sana na ndiyo maana alijua mambo mengi ya siri yaliyokuwa yakiendelea nchini humo.
Hakukuwa na haja ya kumwamini mtu, kila mmoja alijua lazima mhusika wa akaunti hiyo alikuwa ndani ya chama au mtu wa karibu wa viongozi fulani lakini kitu kikubwa kilichokuwa kikiwatatiza watu, ilikuwaje mtu huyo kupata mawasiliano ya simu na wakati mwingine aliweka mpaka sauti za watu waliokuwa wakitongozana.
“Jamani! Hili ni janga la taifa! Rais ajitokeze basi akane tuhuma hizo! Au hataki watu tuone picha?” aliuliza jamaa mmoja aliyekuwa na wenzake, wote wakaanza kucheka.
Siku hiyohiyo baada ya saa moja picha za mawasiliano ya Waziri Lazaro na rais yakawekwa katika akaunti ile, kila mmoja alishangaa, kwa jinsi mawasiliano yale yalivyokuwa, kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba kweli mawasiliano hayo yalikuwa ya watu hao.
Rais Bokasa alikuwa akimshukuru waziri huyo kwa kumwambia kwamba alikuwa mtu muhimu hata zaidi ya mke wake, alikuwa na muonekano mzuri hata zaidi ya mwanamuziki wa Kimarekani, Beyonce. Alimpa sifa kemkem, alimsikifia kana kwamba alikuwa akimsifia mwanamke mrembo aliyewahi kukutana naye mahali fulani.
****
Kikao kizito cha watu sita akiwemo Rais Bokasa kilikuwa kimewekwa ndani ya chumba kimoja kilichokuwa ikulu. Kila mmoja aliyekuwa ndani ya chumba hicho alionekana kutokuwa sawa, wote walionekana kuwa na hofu nzito, nyuso zao zilikuwa na huzuni kubwa kana kwamba walikuwa wamepokea taarifa ya msiba mzito.
Wote waliitwa na rais Bokasa kwa ajili ya kujadili ni kitu gani walitakiwa kufanya ili kuhakikisha wanammaliza mtu aliyekuwa na akaunti hiyo. Hawakumfahamu lakini waliona kabisa kwamba kama wangetumia uwezo wao wa kuzaliwa basi wangeweza kumgundua na kumuua mara moja.
Katika kikao hicho, kulikuwa na majina hamsini ya watu kwenye karatasi, walitakiwa kuyasoma majina yote hayo, yalikuwa ni ya watu mbalimbali, wengine walikuwa wanachama wenzao na wengine walikuwa vijana machachari wa chama pinzani ambao walikuwa wakishadadia kila kitu kilichokuwa kikiandikwa katika mitandao ya kijamii.
Wote walitakiwa kuchagua majina ya watu ishirini ambao walihisi kabisa walikuwa wakihusika, watu ambao walitakiwa kuuawa mara moja, kwa kufanya hivyo ingewapa urahisi kumbahatisha kumpata mtu ambaye alikuwa akihusika katika akaunti hiyo.
“Majina hamsini yapo mbele yenu, yachukueni, najua mnawajua wote hao. Akili yangu inaniambia mmojawapo ndiye mhusika wa akaunti hii. Chagua watu ishirini unaowahisi, wale watakaochaguliwa kwa wingi mpaka mwisho ni lazima tuwaue ili tuone kama akaunti ile itaendelea kuandika upuuzi,” alisema Rais Bokasa kwa sauti ndogo kana kwamba hakutaka watu wa vyumba vingine wasikie.
***
Kilikuwa kikao kizito, kila mmoja alikuwa akiyaangalia majina hayo yaliyokuwa yameandikwa katika karatasi zile. Waliona majina ya watu wengi waliokuwa wakituhumiwa kwamba ndiyo watu waliokuwa na mtandao huo.
Hawakumjua mmiliki wa akaunti ile ila kilichokuwa kikifanyika kilikuwa ni kumbashiri mtu ambaye alikuwa nyuma ya kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Ilikuwa ni kazi nzito kumbashiri mtu ambaye alikuwa akihusika katika akaunti ile.
Kila wakati, wote walikuwa wakishusha pumzi nzito, lilikuwa suala gumu lakini baada ya saa moja, wote waliwabashiri watu wao, wale waliokuwa wamechaguliwa kwenye kila karatasi walitakiwa kuuawa haraka iwezekanavyo.
“Kimwinyi simamia kila kitu,” alisema Rais Bokasa huku akimwangalia mkurugenzi wa usalama wa taifa.
Baada ya kumaliza kikao hicho, wakaruhusiwa kuondoka. Kila mtu ndani ya gari alikuwa na mawazo yake, walijua kwamba kile walichokuwa wamekifanya hakikuwa sahihi kwa kuwa walijua kabisa walikuwa wakienda kuwaua watu wasiokuwa na hatia lakini kwa kuwa mkuu wao ndiye aliyeamua hivyo, hawakuwa na jinsi, utekelezaji ulitakiwa kufanyika haraka iwezekanavyo.
Wakati mipango ikiwa imesukwa kabisa kwamba mauaji hayo yalitakiwa kufanyika haraka iwezekanavyo, wote wakashtuka baada ya kuona kila kitu kilichokuwa kimejadiliwa ndani ya chumba kile kidogo kuwekwa wazi katika akaunti ya Mabadiliko ya Kweli.
Hakukuwa na mtu aliyejua jinsi mawasiliano yale yalivyomfikia mtu huyo kwani walifanya kila kitu kwa siri, hakukuwa na mtu aliyekuwa akifahamu chochote kile zaidi ya wao waliokuwa humo lakini kitu cha ajabu kabisa, ndani ya saa ishirini na nne, kila kitu kilikuwa wazi.
Kila Mtanzania alishangaa, hawakuamini kuona rais wao akiwa ameandaa kikao kile kwa ajili ya kuwaua watu ambao walihisi kwamba walikuwa nyuma ya kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
Ulikuwa mpango uliozidi kumchafua Rais Bokasa kwani mbali na kutaja tu kuhusu kikao hicho, akaunti ile ilizungumza kila kitu kilichojadiliwa ndani ya kikao hicho mpaka namna ambavyo rais alivyomuachia mkurugenzi wa usalama wa taifa kuhakikisha kwamba watu wote ambao majina yao yalikuwa yamechaguliwa kutakiwa kuuawa haraka sana.
“Kuna mtu anatuuza! Tena mtu huyo alikuwa mulemule ndani, yaani ni mtu ambaye alikuwepo kwenye kile kikao,” alisema Rais Bokasa huku akionekana kuchanganyikiwa.
Hakutaka kupoteza muda, akampigia simu Kimwinyi na kumwambia kwamba alikuwa na kitu cha kujadili naye. Hilo halikuwa tatizo, haraka sana Kimwinyi akakutana na rais huyo ikulu na kuanza kujadili.
Uamuzi wa rais ulikuwa mmoja tu kuhakikisha kwamba watu wote waliokuwa kwenye kile kikao wauawe mara moja pasipo kuangalia nani ni nani na alikuwa na nguvu gani nchini kwani alihisi kwamba mmojawapo kati ya wale watu ndiyo aliyekuwa akihusika kwa kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
“Haiwezekani tuongee kwa siri halafu baada ya saa ishirini na nne kila kitu kiwe wazi, kuna mtu mule alitusaliti, kuna mtu anatusnichi mule,” alisema rais huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Haina shida mkuu! Nitafanya kila kitu utakachoniagiza,” alisema Kimwinyi.
“Ua watu wale wanne tuliokuwa nao kwenye kile chumba,” alisema rais.
“Sawa mkuu!”
Walichokubaliana ndicho kilichofanyika, Kimwinyi akaondoka na kuwaandaa vijana wake kwa kuwapa majina ya watu ambao walitakiwa kufa haraka iwezekanavyo.
Hilo halikuwa tatizo, mtu wa kwanza kabisa kuuawa alikuwa katibu wa Chama Tawala cha Labour party, Mzee Filipo Zabedayo.
Ili kuonekana kwamba hakuhusika kwa kitu chochote kile, Rais Bokasa akaondoka nchini na kwenda Uswisi huku nyuma akiacha mauaji yakifanyika.
Saa kadhaa tu baada ya kuachana na Kimwinyi taarifa zikamfikia hukohuko alipokuwa kwamba Katibu wa Chama, Mzee Filipo alipata ajali mbaya alipokuwa akielekea Dodoma kukutana na mwenyekiti wa kamati ya bunge kuzungumzia kile kilichokuwa kimetokea mpaka spika wa bunge hilo kujiua.
Ilikuwa ajali iliyotengenezwa kwa ustadi mkubwa. Gari lake lilipinduka kwa kile kinachodhaniwa dereva kuendesha kwa mwendo wa kasi huku barabara ikiwa imelowa. Hakukuwa na mtu aliyetoka salama ndani ya gari hilo kwani lilikwenda kugonga mti mkubwa uliokuwa kichakani ambapo miili ya dereva wa Mzee Filipo na yeye mwenyewe kutolewa nje kwa kuwa hawakufunga mkanda.
“Mimi niliiona hii ajali! Ilikuwa mbaya sana! Gari liliseleleka, likaja huku nilipokuwa, likagonga huu mti! Miili yote ikatolewa ndani ya gari! Lawama zote ziende kwa dereva,” alisema jamaa mmoja, kwa kumwangalia ilikuwa rahisi kudhani alikuwa mwanakijiji lakini ukweli ni kwamba alikuwa mmoja wa vijana waliokuwa wametumwa kufanya kazi hiyo.
Ulikuwa ni msiba mzito uliokikumba Chama cha Labour Party, kila mtu alisikitika kwa kile kilichokuwa kimetokea kwani hakukuwa na mtu aliyekuwa akiaminika kwa kufanya kazi kwa kujitolea kama alivyokuwa Mzee Filipo.
Msiba huo ukawa gumzo Tanzania, kila mtu alizungumza lake, wengi walitaka kujua kile kilichokuwa kimetokea kwamba ilikuwa ni ajali kama ajali au kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea.
Kila mmoja macho yake yalikuwa kwenye akaunti ya Mabadiliko ya Kweli, waliamini kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima mtumiaji wa akaunti hiyo aandike kitu chochote kuhusu ajali hiyo ambayo tayari kulikuwa na minong’ono iliyosikika kwamba kulikuwa na mtu aliyehusika katika ajali hiyo.
“Kazi nzuri sana Kimwinyi!”
“Nashukuru mkuu! Kwa jinsi tulivyomuua, hakuna mtu atakayejua!” alisema Kimwinyi.
“Ilikuwaje?”
“Tulimuweka mtu wetu ndani ya gari hilohilo kwa kisingizio cha kuelekea Dodoma kikazi kwa chama. Huyo ndiye aliyefanya kazi ya kuwaua wote wawili ndani ya gari hilo hata kabla halijafika Dodoma, akashikilia usukani, akaenda kuligonga gari hilo kwenye mti, miili tukaitoa kuonyesha ilitoka garini,” alisema Kimwinyi.
“Kazi nzuri sana! Bado wengine,” alisema rais Bokasa.
“Haina shida! Niachie mimi!”
Kila mmoja alikuwa akijipongea kwa kazi nzuri aliyokuwa ameifanya, wale wote waliohusika katika mchakato mzima wa kufanya mauaji hayo wakakutana baa na kuanza kunywa pombe kama ishara mojawapo ya kujipongeza kwa kazi hiyo.
Wakati wakiendelea kunywa tena huku wakicheka ndipo Kimwinyi alipopokea ujumbe kutoka kwa mtu ambaye hakumfahamu, tena namba ngeni iliyomwambia kwamba alijua kila kitu kilichokuwa kimetokea, hivyo asubiri kulipuliwa katika akaunti yake ya Mabadiliko ya Kweli.
“Wewe nani?” aliandika ujumbe Kimwinyi huku akitetemeka.
“Mtetezi wa wanyonge. Mwenye akaunti ya Mabadiliko ya Kweli,” ulisema ujumbe aliotumiwa.
Pombe hazikupanda tena, alichanganyikiwa, hakuamini kile alichokuwa ametumiwa, haraka sana akasimama kutoka katika kiti chake pale baa na kwenda ndani ya gari lake, akauegemea usukani wa gari lake, alikuwa na hofu kubwa kwamba hatimaye naye jina lake lingeenda kuandikwa katika akaunti hiyo kama msuka mipango wa ajali ile iliyokuwa imetokea.
Hapohapo akaingia kwenye akaunti yake ya Instagram, alijua kwamba mtu huyo atakuwa ameandika kuhusu ajali hiyo, alichokikuta humo ni picha ya ajali huku kwa chini kukiwa na maswali matano tata ambayo Watanzania walitakiwa kujiuliza juu ya ajali hiyo. Maswali hayo matano yalikuwa haya:
“Wanasema kwamba gari liliseleleka kwa kuwa barabara ilikuwa imelowa. Kwa siku ya ajali hiyo, hakukuwa na mvua kubwa iliyokuwa imenyesha, yalikuwa ni manyunyu tu, je, iweje ripoti iseme kwamba gari liliseleleka kwa kuwa kulikuwa na maji mengi?”
“Swali la pili ambalo Mtanzania unatakiwa kujiuliza ni kuhusu yule mtu pekee aliyetoa taarifa. Anasema kwamba yeye ni mwanakijiji wa pale lakini kamuulize mwanakijiji yeyote kama anamfahamu, kijiji kizima hakimfahamu, na si kijiji hicho tu bali hata vijiji vya jirani, je, kama kweli mtoa taarifa anasema yeye ni mkazi wa kijiji hicho, kwa nini wanakijiji wote hawamfahamu?”
“Swali la tatu. Gari linapokuwa katika mwendo wa kasi na kugonga sehemu basi ni lazima miili iwe na majeraha makubwa na damu nyingi. Angalia kioo ambacho wanasema miili ilitolewa, kwa jinsi ilivyovunjika, kweli ni rahisi kwa mtu kutoka humo bila hata kuchanika? Inawezekana mmoja asichanike, lakini je, ni rahisi kwa wote kutokuchanika hata damu kutoka?”
“Swali la nne. Wanasema kwamba walitolewa nje kwa kuwa hawakufunga mikanda. Kuna picha nyingi zinaonyesha Mzee Filipo alipokuwa safarini, hata awe anatoka Magomeni kwenda Kinondoni ilikuwa ni lazima kufunga mkanda, zipo picha zaidi ya ishirini zinazothibisha hilo. Sasa iweje leo mzee huyo asafiri kutoka Dar mpaka Dodoma, gari liwe kwenye mwendo wa kasi na asifunge mkanda?”
“Swali la tano. Baada ya ajali kutokea, kitu cha ajabu kabisa wakatokea watu waliodhaniwa kutoa msaada, waliichukua miili harakaharaka kabla watu hawajajaa na kuondoka nayo na kusema kwamba wote walikuwa wamekufa. Je, watu hao walikuwa wakina nani? Na kwa nini wawaondoe haraka sana na wakati tayari walikufa? Kwa nini napo gari liliondolewa haraka sana eneo la tukio? Ukijiuliza maswali hayo yote, utagundua kwamba ajali ilikuwa imepangwa na watu hao walikuwa wameuawa kabla ya tukio hilo.
“Tafuteni mbinu nyingine, hizo zenu zimepitwa na wakati. Kesho nitakwenda kuwaambia Watanzania kila kitu kilichotokea kabla ya hawa watu kuuawa, mpango ulikuwa ni kumuua Mzee Filipo tu. Nitaeleza jinsi kikao cha watu wawili kilichopangwa, badala ya hawa kufa, kuna watu watatu nao wanatakiwa kuuawa haraka iwezekanavyo, sababu yake nitaiweka kesho pia,” ilisema posti hiyo ndefu.
Baada ya kumaliza kuisoma posti hiyo ndefu, Kimwinyi akabaki akitetemeka, mwili ukafa ganzi, akahisi muda wowote ule presha ingepanda na kufariki ndani ya gari hilo.

Je, nini kitaendelea?

Safi sana...

Cc: mahondaw
 
Duuh.!! Malipo ni hapa hapa kwa duniani. Godwin Mungu azidi kukulinda.!! Nam fan an sha Bokasa na Jamba Pasipo Mashuzi.!!
 
Daaah! Hizi episode za leo ndefuuu halaf hazina episode namba

Jackal uwe una ziweka kwa episode kama anavo fanya Shunie basi
Mm napenda sana story zikiwa kwwa urefu huu napataje uvivu sema hakuna namna tu acha nisome hivyo hivyo
 
Mkuu nazitupia kama zinavyowekea,halafu nikiweka namba zinatofautiana na Shunie.Ila ziko kwenye mfulululizo bila kurukwa kipengele chochote.Tujaribu kuvumiliana mkuu.Kama ndefu basi nikiweka moja niwe nasubiri kama Siku ndio niweke nyingine ili wadau waweze kusoma,waonaje hilo?
Au uweke mbili kwa siku jacka nimekuachia uendelee mpaka mwisho
 
Sasa hii inahitaji nikae kwenye laptop niwe nafanya hiyo kazi.Au labda niwe namrushia Shunie Inbox,halafu yeye anafanya huo mchakato,Shunie sijui uko wapi tuchangie mawazo hapa!
Hapana endelea tu uweke mbili kwa siku
 
Oyoooo. Wakati Wa revenge sasa.huzuni zilizidi.na bado.asante kwa uhondo
 
Aah jamani 2 tena.mimi sichoķ kusoma.kama ipo mpaka mwisho sio mbaya kuimalizia yote. Kama bado mwache aweke tu mpaka ukomo Wa hadithi yenyewe.angalau ni time ya revenge. Huzuni huzuni tupa kule
Nyie mnatumia pc ndio mana ni ndefu sana aweke tu mbili
 
SEHEMU YA 107

“Hapahapa panatosha,” alisema Rosemary huku akiliweka chini begi lake la nguo.
“Mama! Tunafanya nini hapa?” aliuliza Godwin.

“This is our new home,” (hapa ni nyumbani kwetu kupya!)
“A new home?” (nyumbani kupya?)
“Ndiyo!”

Hiyo ndiyo ilikuwa nyumba yao mpya, hawakubishana na mama yao, alikuwa mwanamke shupavu ambaye alikuwa tayari kupambana kwa ajili ya watoto wake hao.

Kwa kuwa giza lilikwishaanza kuingia, Rosemary akatandika kanga chini kwa lengo la kulala. Hakukuwa na mtu aliyelala, kila mmoja alikuwa akiyafikiria maisha yake, jinsi walipotoka mpaka kuwa mahali hapo.


Yalikuwa ni maisha yaliwaumiza, yaliyowasikitisha ambapo kwa Godwin kila siku alijiapiza kwamba ni lazima alipe kisasi, hata kama ingechukua miaka mingapi.

Walikesha, ilipofika asubuhi, wakatoa vyombo vyao vya kupikia. Kila mtu aliyekuwa akipita mahali hapo aliwashangaa, watu wengine, matajiri waliokuwa wakielekea kazini walisimamisha magari yao na kuanza kuiangalia familia hiyo.

Hilo liliwashangaza kila mmoja. Huo ulikuwa mtaa wa matajiri, kila jumba lililojengwa lilikuwa la kifahari, hawakujua watu hao walitoka wapi na kwa nini waliamua kuhamia hapo na wakati kulikuwa na sehemu nyingi za watu masikini ambapo wangeweza kwenda.


Hakukuwa na mtu aliyejua kwamba hiyo ilikuwa familia ya Mapoto. Kila walipokuwa wakimwangalia Rosemary, alijitahidi sana kuuficha uso wake, hakutaka mtu yeyote agundue kama wameanza maisha mapya.

Hakukuwa na shule tena, Irene na Godwin walitakiwa kusahau kila kitu kuhusu kusoma na kilichokuwa kimefuata ni kuendelea kuishi maisha ya mtaani huku wakitakiwa kutoka nyumbani na kwenda mitaani kuomba kwa ajili ya pesa za kumsaidia mama yao.


“Irene! Tumekuwa ombaomba mitaani! Kweli?” aliuliza Godwin, alikuwa amechanganyikiwa kupita kawaida.

“Godwin! Kila kitu kinatokea kwa sababu, hujui ni sababu gani imemfanya Mungu kuamua kutupa maisha haya, cha msingi ni kumshukuru kwa kila jambo,” alisema Irene.
Duh....maisha haya ila malipo huwa ni hapa hapa duniani, nitamsaidia Godwin kulipa kisasi
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom