DUNIA HAINA USAWA
Wanausalama waliokuwa ndani ya chumba kile walionekana kukasirika mno, walimwangalia Godwin, kwa jinsi alivyokuwa akizungumza nao alionekana kabisa kwamba alikuwa kiburi na kamwe asingeweza kuifungua simu ile na kuwaacha kufanya kile walichotaka kufanya.
Walikasirika, walijiona kuwa na uwezo wa kufanya kitu chochote kile walichotaka kukifanya lakini wakaonekana kuogopa. Mpaka mtu kuwajibu jeuri ilionyesha kabisa kwamba inawezekana alikuwa mtoto wa kiongozi mkubwa au alikuwa mwanasheria ambaye angeweza kuwashtaki na kutaka malipo makubwa.
Wakaangaliana, wakachukuana na kuelekea nje huku wakiwa na simu ile. Huko wakajadili kwa dakika kadhaa, walichokubaliana ni kwamba waendelee kuweka msimamo wao mpaka awakubalie kuifungua simu ile kwani tayari walikuwa na wasiwasi na kijana huyo.
Wakarudi ndani ya chumba kile, kwa jinsi walivyomuacha ndivyo alivyokuwa japokuwa tabasamu lile liliongezeka usoni mwake kuwaonyesha kwamba hawakuwa na ubavu wa kumlazimisha kufungua simu yake na hata kama wangetaka kumpiga, ilikuwa ni lazima kuwafungulia mashtaka.
“Jiandae twende polisi,” alisema mwanausalama mmoja.
“Kwa kosa gani?”
“Kukataa kutufungulia simu yako!”
“Kwani hilo kosa? Mnataka kuingilia uhuru wangu! Mimi ndiye natakiwa kuwashtaki, tena ikibidi mnilipe na pesa si chini ya milioni mia tatu kwa kosa la kunipotezea muda kiboya,” alisema Godwin maneno ambayo yaliwatisha wanausalama wale lakini wakajifanya kutokujali, hawakutaka Godwin ajue kama walianza kuogopa.
Wakaendelea na msimamo wao wa kutaka kufunguliwa simu ile lakini wakati wakiendelea kukaza, wakasikia mlango unafunguliwa na mwanaume mmoja kuingia, alikuwa mwenzao.
“Tumempata!” alisema mwanaume huyo.
“Amepatikana! Ahsante Mungu!” alisema mwanausalama na hivyo kumrudishia Godwin simu yake.
Wakamruhusu kuondoka huku wakimuomba msamaha kwa usumbufu uliojitokeza mahali hapo. Akaondoka huku nao wakielekea kule walipoambiwa kwamba mtu huyo alikuwepo.
Wanausalama wakaelekea huko, wakaingia ndani ya chumba kimoja, macho yao yakatua kwa kijana mmoja aliyekuwa chumbani humo ambaye muda wote alikuwa akilia tu. Alizungukwa, kila mmoja alitaka kujua kile kilichokuwa kikiendelea.
Walimlazimisha kufungua akaunti yake ya Instagram, alipoifungua wakaona akiwa na akaunti mbili, moja ilikuwa yake lakini nyingine ilikuwa ni ya Mabadiliko ya Kweli. Wakaamini kwamba kijana huyo ndiye alikuwa mmiliki wa akaunti hiyo, wakachukua hati yake ya kusafiria ambayo ilisomeka kwamba alitokea nchini Australia.
“Wewe ndiye mmiliki wa akaunti ya Mabadiliko ya Kweli?” aliuliza mwanausalama mmoja.
“Hiyo si akaunti ambayo nyie mnasema namiliki. Hiyo ina wafuasi elfu kumi na tatu, hiyo mnayoitaka ina wafuasi milioni ishirini na mbili. Si akaunti hiyo, niliweka ili nipate wafuasi wengi tu mkuu,” alijibu kijana huyo huku akitetemeka.
Hawakutaka kumuelewa, kila mmoja alijua fika kwamba kijana aliyekuwa akihitajika ndiye alikuwa huyo aliyekuwa ndani ya chumba kile. Walibaki humo huku wakimuhoji maswali mengi, kwa jinsi alivyokuwa akiongea na kujibu maswali yake ilionyesha kabisa hakuwa yeye bali alikuwa mtu mwingine.
Walikaa naye kwa nusu saa nzima, wakapigiwa simu na mkuu wao na kuambiwa kwamba kulikuwa na ujumbe mzito wao katika akaunti ile hivyo waingie na kuangalia. Wakaingia, walipoifungua akaunti ile, wakakutana na picha ya chumba kile walichomuweka Godwin huku chini kukiwa na maneno yaliyosomeka ‘Nimeingia Tanzania salama kabisa. Waliniita ndani ya chumba chao kwa ajili ya kupekua simu yangu. Nilikataa kutoa namba za siri, nikawaogopesha kuwashtaki. Wameniachia, niwaambie tu kwamba nipo salama, kazi inaanza upya.’ Ilisema posti ile.
“Ni yule kijana!” alisema usalama mmoja.
Hawakutaka kubaki ndani ya chumba kile, haraka sana wakatoka na kuelekea katika chumba walichokuwa wakimuhojia Godwin, walipofika huko, hakuwepo, aliondoka huku hata ile simu yake aliyokuwa nayo ikiwa haipo ndani ya chumba kile.
Wakachanganyikiwa. Haraka sana wakatoka na kuelekea nje ya jengo la uwanja ule, wakaanza kuangalia huku na kule, Godwin hakuonekana. Hilo liliwaumiza sana, hawakuamini kama walishindwa kumgundua mtuhumiwa ambaye walikuwa naye.
Walichokifanya ni kwenda katika chumba cha kuhifadhi picha zilizokuwa zikipigwa katika uwanja ule na kuhitaji kuangalia picha za Godwin wakati alipokuwa ameingia. Hilo halikuwa tatizo, kijana wa uwanjani hapo akafungua kompyuta na kuanza kuzitafuta picha hizo.
Halikuwa tatizo sana na hakutumia muda mrefu kuzipata kwani zilipigwa saa moja lililopita. Wakaanza kuziangalia, walijiona jinsi walivyokuwa wakielekea ndani ya chumba kile. Ilionekana kama Godwin alijua kwamba mahali pale kulikuwa na kamera kwani kila alipokuwa akipigwa picha, alificha uso wake mpaka walipoingia ndani ya chumba kile.
“Alijua kwamba kamera zilikuwa zikimchukua,” alisema jamaa mmoja.
Walikuwa na uhakika kwamba yule waliyekuwa wamemuhoji mpaka kukataa kufungua simu yake ndiye alikuwa mtu waliyekuwa wakimuhitaji sana. Walichokifanya ni kwenda katika orodha ya majina ya abiria walioingia kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Fly Emirate ambapo walipopewa majina, wakaambiwa kwamba mtu huyo alikuwa akiitwa Godwin Melkizedek Mapoto.
Kumfahamu alikuwa nani tu iliwapa uhakika kwamba kumpata halikuwa jambo gumu tena. Jina lake halikuwa gumu, walichokifanya ni kuanza kufuatilia ili hata kama watakwenda kumpa taarifa Rais Bokasa basi wajue ni mtu gani alikuwa akisababisha yote hayo.
Walimfahamu baba yake, walihisi kwamba alikuwa mtoto wake hivyo kuanza kufuatilia kwa makini. Ni kweli, alikuwa ndiye yule yule, mtoto wa mwanasiasa mkubwa nchini Tanzania, Bwana Melkizedeki Mapoto ambaye alikufa katika ajali ya gari nchini Marekani alipokwenda kulitumikia taifa kama balozi nchini humo.
“Hebu endeleeni kufuatilia mniambie zaidi, baada ya hapo nini kiliendelea,” alisema mkurugenzi wa usalama wa taifa ambaye alichaguliwa kwa haraka sana, aliitwa Maliki Idrisa.
“Baada ya hapo, familia yake iliendelea kuishi Tanzania, mkewe alipokonywa nyumba katika mazingira ya kutatanisha. Baadaye akafa kwa kugongwa kwa gari, wakabaki wawili, baadaye dada wa huyu aliyeitwa Irene akafariki dunia,” alisema jamaa aliyepewa kazi hiyo.
“Mmh! Nahisi kuna kitu! Hebu naombeni hiyo ripoti nikampe rais,” alisema Maliki na hivyo kuichukua ripoti hiyo.
Hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, ilikuwa ni lazima kumpelekea Rais Bokasa ili ajue kile kilichokuwa kikiendelea. Akampigia simu binafsi na kuomba kuonana naye kwani tayari kwa asilimia kadhaa alifanikiwa kupatikana kwa jina la mtu aliyekuwa akimtafuta usiku na mchana.
Hilo halikuwa tatizo, Rais Bokasa akamwambia kwamba aelekee ikulu ambapo huko akaonana naye na kumpa ripoti ile huku akimwambia kwamba mtoto wa marehemu Mapoto ndiye aliyekuwa akihusika katika kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
“Haiwezekani!” alisema Rais Bokasa huku akihamaki.
“Kwa nini?”
“Kijana huyo alikufa miaka mingi iliyopita. Alikufa baharini!” alisema rais huku akisimama na ripoti yake mkononi.
Alikumbuka kila kitu, yeye ndiye aliyekuwa akiimaliza familia hiyo kwa kuamini kwamba ingetokea siku ambayo wangejua kwamba baba yao, Mzee Mapoto aliuawa hivyo kuifanya nafasi yake ikulu kuwa ngumu.
Alijilinda kwa nguvu zote, alijitahidi kuiangamiza familia hiyo kwa kusudi la kulinda cheo chake ikulu na alikumbuka kabisa kwamba mara ya mwisho mtu aliyetakiwa kuuawa alikuwa Godwin ambaye aliagiza kutupwa baharini akiwa ndani ya boksi, sasa ilikuwaje mpaka mtu huyo awe hai?
“Huyu mtu alikufa! Nakumbuka kwamba niliyemtuma kumuangamiza alikuwa Kihampa! Hakuifanya kazi au?” alijiuliza huku akiiangalia ripoti ile.
Alihitaji kujua ukweli juu ya kilichokuwa kimeendelea, Kihampa alikuwa akijua ukweli kwani yeye ndiye aliyemtuma kwenda kumteka Godwin na kumuua, alikumbuka vilivyo kwamba hata siku hiyo kijana huyo alimpa taarifa kwamba alifanikisha suala hilo.
“Ninamtaka Emmanuel Kihampa!” alisema Rais Bokasa huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Yule mchungaji?”
“Ndiyo! Ninataka mniletee hapa,” alisema rais huyo.
Hayo yalikuwa maagizo ambayo yalitakiwa kufanyika haraka sana. Kihampa alibadilika, tangu siku ya mwisho alipotakiwa kumuua Godwin aliamua kuyabadilisha maisha yake na ndiyo maana hata ndani ya boksi aliweka maboya ili asizame na aweze kuokoka kutoka katika mikono ya rais huyo.
Hilo halikuwa tatizo, haraka sana vijana wakaondoka mpaka nyumbani alipokuwa akiishi, wakamchukua na kumpeleka ikulu. Siku hiyo Bokasa alionekana tofauti, alikuwa na hasira sana, alipomuona Mchungaji Kihampa, kitu pekee alichotaka kujua, je, ni kweli alimuua Godwin siku ile au hakumuua?
“Nilimtupa baharini nikiwa nimemuwekea maboya,” alisema mchungaji huyo.
“Kwa nini ulifanya hivyo?”
“Kwa sababu Yesu Kristo aliyabadilisha maisha yangu! Sikutaka kuua tena,” alijibu Kihampa huku akionekana kutokuogopa hata kidogo.
Rais Bokasa akaingiwa na hasira mno, majibu yale kwake yalionekana kama dharau kubwa. Alimwangalia mchungaji huyo, alikuwa Kihampa yuleyule wa zamani lakini maisha yake yalikuwa yamebadilishwa. Hakujua ni kitu gani alitakiwa kumfanya, kama ni kumuua au kumuachia aondoke zake.
Wakati akijifikiria hayo ni kitu gani alitakiwa kufanya, akasikia mlio wa meseji ukiwa umelia kwenye simu yake. Haraka sana akaichukua na kuanza kuangalia, alitaka kujua ni nani aliyekuwa amemtumia meseji hiyo. Alipoifungua tu akakutana na ujumbe huo uliotoka katika Hospitali ya St. Lucas nchini Marekani uliosomeka
‘Thank you for helping epileptic kids and funding them with 100 million dollars. May the Almighty bless you!’ (asante kwa kuwasaidia watoto wanaougua kifafa kwa kutoa kiasi cha dola milioni mia moja. Mungu akubariki)
“Mungu wangu! Kuna mtu kahamisha pesa zangu zote katika akaunti yangu nchini Uswisi!” alisema Rais Bokasa huku akionekana kuchanganyikiwa. Akahisi presha ikianza kupanda, akakishika kifua chake, akaanguka chini kama mzigo.
***
Godwin hakutaka kuendelea kubaki ndani ya chumba hicho, akaondoka na kuungana na msichana Manka ambapo wakaanza kuelekea nje ya jengo la uwanja huo. Msichana yule alibaki na mawazo mengi, alikuwa akimuuliza maswali ambayo hakupata majibu papo hapo.
Hakujua sababu ya wanaume wale kuchukua muda mrefu kuzungumza na Godwin ndani ya chumba kile zaidi ya watu wengine. Alipomuuliza Godwin, hakumpa jibu zuri zaidi ya kumwambia kwamba walitakiwa kuondoka mahali hapo
Wakaifuata taksi moja na kuingia. Haraka sana dereva aliyekuwa nje ya gari hilo naye akaingia, akawaangalia watu wake, Godwin hakuonekana kuwa katika hali ya kawaida, alionekana kama mtu fulani aliyekuwa na mambo mengi kichwani.
“Niwapeleke wapi?” aliuliza mwanaume huyo.
“Chuichui Hotel,” alisema Godwin, dereva akawasha gari na kuanza kuondoka mahali hapo.
Njia nzima hakukuwa na mtu aliyezungumza lolote, Godwin alikuwa bize na simu yake, huo ndiyo ulikuwa wakati wa kuwaambia wafuasi wake kila kitu kilichokuwa kimetokea uwanja wa ndege ndani ya kile chumba.
Watu wengi walimsifu kwa ujasiri wake, hakuonekana kuogopa, si kama Watanzania wengine ambao mioyo yao ilijawa na hofu kubwa hata pale walipokuwa wakifanyia kitu ambacho sheria haikuruhusu kufanyiwa.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika katika Hoteli hiyo, haraka sana Godwin akateremka na kuanza kuelekea ndani ya hoteli huku akionekana kumsahau Manka na hata kumlipa dereva.
“Bro...broo..!” dereva akaita huku akiteremka na kumfuata, akamwambia amlipe, hilo halikuwa tatizo, akamuomba msamaha kwa kujisahau kisha kumlipa kiasi cha pesa alichokuwa akikihitaji.
“Naondoka!” alisema Manka huku akimwangalia Godwin.
“Haina shida! Safari njema!” alisema Godwin huku akianza kupiga hatua kuondoka.
“Hukunipa namba ya simu!”
“Usijali Manka! Utanikuta hapahapa. Ukijisikia kunitembelea, unakaribishwa,” alisema Godwin na kuondoka.
Kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, hakuamini kama alifanikiwa kutoka salama katika mikono ya watu hao. Alijipongeza kwa kuonyesha msimamo wake, hakutaka kabisa kuona akikamatwa na wakati bado kulikuwa na kazi kubwa mbele yake ya kuikomboa Tanzania kutoka katika mikono ya watu waliokuwa wakiyaangalia matumbo yao kwa kuwaibia pesa wananchi ambao kila siku walikuwa wakikatwa kodi.
Akaingia chumbani. Alikuwa amefanya kazi kubwa, mbele yake kulikuwa na kazi moja tu aliyotaka kuifanya, nayo ilikuwa ni kumuibia pesa zote Rais Bokasa, pesa ambazo alizificha katika akaunti yake ya Uswisi.
Alijua kulikuwa na kazi kubwa lakini alitakiwa kuifanya pasipo kuogopa kitu chochote kile. Alijua kwamba kulikuwa na viongozi wengi waliokuwa wamejilimbikizia pesa nyingi katika akaunti zao ndani ya benki zilizokuwa nchini humo, alitaka kupambana kwa nguvu zote na hatimaye kuzichukua pesa hizo na kuzipeleka katika taasisi mbalimbali za kusaidia watoto na wagonjwa.
Haikuwa kazi nyepesi kuingia katika data base ya benki za huko, alijua kwamba zilikuwa zikilindwa, watu waliosomea IT ambao walikuwa na uwezo mkubwa ndiyo waliokuwa wakiziendesha benki hizo tena wakati mwingine kubadili ‘codes’ kila wakati.
Hakutakiwa kuogopa, mbele yake hakuamini kama kulikuwa na kitu kigumu. Ugumu wa jambo ulikuwa pale mpaka alipokuwa akifanya na kushindwa ndipo angesema kwamba kitu hicho kilikuwa kigumu, ila kabla ya kujaribu kwa kufanya, hakuamini kama kulikuwa na jambo gumu.
Akaanza kazi, akafungua laptop yake, alichokuwa akikihitaji ni kuingia kwenye ‘data base’ za benki ya Geneva ambayo ilisadikiwa kuwa na akaunti nyingi za pesa kutoka kwa viongozi mbalimbali wa Afrika.
Haikuwa kazi ndogo, yeye mwenyewe alijua kabisa kwamba kulikuwa na kazi kubwa ya kuingia katika data base ya akaunti hiyo, alipofanikiwa kuiona, kuingia na ‘kudownload’ mafaili ilikuwa kazi nyingine.
Alijaribu kila njia, kila faili alilotaka ‘kudownload’ lilionekana kuwa gumu, hakutaka kukata tamaa, alitulia kwenye kompyuta yake, kichwa chake kilikuwa kikifikiria mambo mengi. Alianza kazi hiyo majira ya saa mbili asubuhi lakini mpaka inafika saa kumi na mbili jioni hakuwa amefanikiwa.
Hakutaka kula wala kufanya kitu chochote kile, alikuwa akipambana kwa nguvu zote kuhakikisha kila kitu kinakuwa kama alivyotaka kiwe. Alipoona kwamba ameshindwa kabisa hapo ndipo alipoamua kutumia virusi vyake kwenda katika data base hiyo na kuharibu kila kitu.
Virusi vilevile vya mateshi ambavyo alivitumia kuyaficha mafaili ya chuo ndivyo alivyovitumia kuzivuruga data za benki hiyo. Kila kitu kikafichwa, hakukuwa na mtu aliyeweza kuingia katika ‘data base’ za benki hizo kwa kipindi hicho mpaka yeye mwenyewe atakapoamua kuruhusu mtu mwingine kuingia.
Japokuwa mwili wake ulikuwa umechoka lakini baada ya kufanikiwa kuwaingiza virusi hao na kuvuruga kila kitu, mwili wake ukapata nguvu na kuendelea kufanya kila alilokuwa akilifanya kuhakikisha kwamba anafanikiwa kuchukua pesa hizo.
Kitu cha kwanza akaanza kulitafuta jina la Bokasa katika orodha ya majina ya wateja waliokuwa katika benki hiyo. Alishindwa kuliona jina hilo zaidi ya kuliona jina la Catherine Bokasa ambalo moja kwa moja akajua kwamba hilo ni jina la binti yake, rais huyo alifungua akaunti kwa jina la binti huyo ili asiweze kugundulika mambo yatakapoharibika.
“Anajifanya mjanja! Ngoja nimuonyeshee!” alisema Godwin, akajiweka vizuri, akaisogeza laptop yake karibu naye.
Akaangalia taarifa zote za kibenki, alishangaa, rais huyo alikuwa akiingiza kiasi kikubwa cha pesa katika akaunti hiyo kila mwezi, alionekana kuwa bilionea mkubwa, hivyo ili kumchanganya na kumfanya kuwa na presha ilikuwa ni lazima kuzihamisha pesa hizo na kuzipeleka katika Hospitali ya St. Lucas iliyokuwa New York.
Akachukua namba za akaunti ya hospitali hiyo kutoka katika tovuti yao na kisha kuhamisha kiasi chote cha pesa, zaidi ya dola milioni 100 kutoka katika akaunti ya Rais Bokasa.
“It’s done,” (kazi imekamilika) alisema huku akiachia tabasamu pana. Hakutaka kuishia hapo, akaanza kutafuta na majina ya viongozi wengine wa serikali wa Tanzania ambao walikuwa na akaunti katika benki hiyo, alitaka kuhamisha pesa zao kwenda katika miradi na taasisi mbalimbali za kijamii
Je, nini kitaendelea?