Jackal
JF-Expert Member
- Apr 10, 2012
- 10,258
- 14,102
DUNIA HAINA USAWA
Rosemary aliishi kwa kujificha, kila alipokuwa akitoka nje ya kibanda chake alikuwa akijifunga kilemba na uso wake, asilimia kubwa ulikuwa umefunikwa kwa kitambaa kikubwa.
Hakutaka kujulikana, hakutaka kuona akigundulika na watu wengine kwani ingekuwa aibu kubwa kwa taifa, aibu kubwa kwa viongozi wa Chama cha Tanzania National Party ambao mpaka wakati alipoanza kupata matatizo hakukuwa na mtu aliyejali, kila mmoja alimpuuzia kana kwamba hakukuwa na mtu aliyeyaona matatizo aliyokuwa akipitia.
Aliamua kuishi maisha yake na familia yake, hakutaka kumbughudhi mtu yeyote yule. Japokuwa alikuwa akiumia moyoni mwake lakini hakuwa na jinsi, hakutaka kuona watoto wake wakiyaona maumivu makubwa yaliyokuwa moyoni mwake, alitaka watoto wake waamini kwamba katika kila hatua waliyokuwa wakipitia, hakuumia kama alivyotakiwa kuumia.
Wakati Godwin na Irene wakiwa barabarani kuombaomba pesa, yeye alikuwa akibaki nyumbani, aliandaa chakula cha mchana ambapo walirudi kula na baadaye kurudi tena barabarani kama kawaida yao.
Siku ya Jumamosi, katika tarehe 1 mwezi wa 5, siku ambayo wafanyakazi huadhimisha siku yao ndiyo siku ambayo mauaji ya mwanamke huyo yalitakiwa kufanyika kama ilivyopangwa.
Alikuwa ndani ya kibanda chake akiandaa chakula kama kawaida. Ilipofika majira ya saa nne asubuhi, huku akiwa amejipumzisha katika maboksi yaliyokuwepo ndani ya kibanda hicho ambayo waliyafanya kama kitanda, ghafla gari moja, Land Cruiser nyeusi ikasikika ikija kwa kasi kule alipokuwa.
Hakuogopa, ilikuwa ni kawaida kwa kuwa kibanda chake hakikuwa mbali sana na barabara ya vumbi ambapo magari machache yalikuwa yakipita mara mojamoja. Ghafla, akiwa ndani ya kibanda hicho huku hajui hili wala lile, gari hilo likakigonga kibanda kile, akaanguka, matairi ya gari hilo yakapita tumboni mwake.
Watu wote waliolishuhidia tukio hilo wakashika vichwa, hawakuamini kile walichokiona, hata kabla hawajashika namba za gari lile vizuri, likaondoka mahali hapo kwa kasi kubwa.
“Mungu wangu! Kuna mtu mule?” aliuliza jamaa mmoja, hata kabla jibu halijatolewa, sauti ya mwanamke ikaanza kusikika kwa shida.
Sauti hiyo ndiyo iliwashtua watu kusogea kule kilipokuwa kibanda kile, kila mtu alishika kichwa kwa majonzi, hawakuamini kile walichokuwa wakikiona. Rosemary alikuwa chini, alishika tumbo lake huku akilia kwa maumivu makali.
Kabla ya kumsogelea, watu wale wakaanza kumwangalia, aliumia vibaya, ubavuni mwake kulibonyea kuonyesha kwamba mbavu zake zilikuwa zimevunjika na damu kuvilia kwa ndani pasipo kuonekana kwa nje.
“Jamani tumpelekeni hospitali,” alisema mwanaume mmoja.
Huo ndiyo uamuzi walioufanya, hawakutaka kumuacha, wakambeba na kumpeleka katika barabara ya lami ambapo hapo wakapata msaada wa gari moja na kuanza kumpeka katika Hospitali ya Palestina iliyokuwa Sinza.
Ndani ya gari kila mtu alimuonea huruma Rosemary, pale alipokuwa alikuwa akilia kwa maumivu makali, hakutoka damu hali iliyoonekana kuwa mbaya zaidi kwani ilionyesha kwamba damu ilivilia kwa ndani na hivyo kusababisha hatari kubwa kwa maisha yake.
Kila mmoja alikuwa akilizungumzia gari lililomgonga mwanamke huyo, hakukuwa na mtu ambaye aliziona vizuri namba za gari lakini kijana mmoja aliwaambia wenzake kwamba gari ambalo lilimgonga mwanamke huyo lilikuwa na namba za serikali.
“Unasemaje?” aliuliza jamaa mwingine kwa mshtuko.
“Lile gari lina namba za serikali!”
“Namba za serikali?”
“Ndiyo!”
“Una uhakika?”
“Ndiyo kwa sababu niliziona herufi zake,” alisema kijana huyo.
Kila mmoja aliongea lake, hawakuamini kama dereva wa serikali angeweza kufanya unyama kama huo kwani hata kama alimgonga kwa bahati mbaya basi ilikuwa ni lazima ateremke na kumsaidia na si kukimbia kama alivyofanya.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika katika hospitali hiyo ambapo moja kwa moja machela ikasogezwa na mwanamke huyo kupakizwa kisha kuanza kusukumwa kuelekea ndani.
Kila mtu alishangaa, walimuona Rosemary akilia lakini hawakujua tatizo lilikuwa nini. Hakutoka damu hivyo kila mtu aliyekuwa akimwangalia aliona kuwa mwanamke huyo alikuwa na tatizo la kawaida, kuumwa na tumbo au maumivu mengine.
“Kuna nini?” aliuliza daktari mmoja, mwanaume aliyekuwa na ndevu nyingi nyeupe huku akiwa na mashine ya kusikilizia mapigo ya moyo.
“Amegongwa na gari!”
“Amegongwa na gari?” aliuliza daktari huyo huku akionekana kushangaa.
“Ndiyo!”
“Mleteni huku.”
Manesi wawili wakaisukuma machela ile mpaka katika chumba cha upasuaji ambapo huko madaktari walitakiwa kuangalia tatizo kubwa alilokuwa nalo mwanamke huyo.
Baada ya kusikia kwamba mwanamke huyo aligongwa na gari, walishangaa, hakukuwa na mtu aliyekuwa na uhakika wa mwanamke huyo kupona kwani kitendo cha kugongwa na damu kuvilia ndani kwa ndani kilikuwa kitu kibaya mno kutokea kwa mtu yeyote yule.
“Sidhani kama atapona,” alisema dokta huyo kimoyomoyo, pamoja na ubingwa wake katika mambo ya matibabu lakini yeye mwenyewe hakuwa na uhakika kama mwanamke huyo angeweza kupona.
***
Godwin na Irene walikuwa barabarani kama kawaida, waliendelea kuomba huku wakitembea huku na kule. Kila gari ambalo lilisimama katika foleni walilifuata na kuanza kuomba kwa kugonga kioo, wengine walioguswa na maisha yao waliwasaidia lakini wengine hata kufungua vioo hawakufanya hivyo.
Waliendelea kama kawaida, hawakutaka kuacha, ili mama yao nyumbani apike ilikuwa ni lazima kuomba pesa mitaani na kumpelekea. Walizunguka mpaka ilipofika majira ya saa kumi na moja jioni ndipo wakaanza kurudi katika kibanda walichokuwa wakiishi.
Walichokikuta, hawakuamini macho yao, kibanda kile ambacho ndicho walichokuwa wakikitumia kama nyumba yao kilikuwa kimevunjwa, hakukuwa na mtu aliyejua kilichotokea, wakahisi kulikuwa na jambo la hatari lilikuwa limetokea.
Wakaanza kukimbia kuelekea kule huku wakimuita mama yao. Walipofika, wakaanza kulia, mama yao hakuwepo, wakajaribu kutoa mbao kwa kuhisi kwamba inawezekana alikuwa amefunikwa na mbao hizo pamoja na mabati lakini hawakuambulia kitu.
Hawakujua ni kitu gani kilitokea. Walibaki wakilia, majirani zao waliokuwa pembeni kabisa na mahali pale ndipo wakawafuata na kuwaambia kile kilichokuwa kimetokea.
“Wamemuua mama!” alisema Godwin huku akionekana kushtuka.
Hawakutaka kubaki mahali hapo, wakaambiwa mahali mama yao alipokuwa, wakaanza kukimbia kuelekea huko. Kila mmoja alikuwa akilia kwa maumivu makali, hawakuamini kile kilichokuwa kimetokea.
Hawakuwa radhi kuona mama yao akifariki, walimpenda, alikuwa kila kitu katika maisha yao, kitendo cha kumuua mama yao kilimaanisha kwamba wangebaki yatima maisha yao yote.
Njiani, watu walikuwa wakiwashangaa, walikuwa watoto wa mitaani, wengine walihisi kwamba walikuwa wezi na kuangalia kama kulikuwa na watu waliokuwa wakiwakimbiza.
Walichukua dakika thelathini mpaka kufika katika hospitali hiyo ambapo wakamsimamisha nesi mmoja na kumwambia kuhusu mama yao aliyepelekwa mahali hapo saa kadhaa zilizopita.
“Yule aliyeletwa mchana wa leo?” aliuliza nesi.
“Ndiyo!” alijibu Godwin, muda wote Irene aliyekuwa pembeni yake alikuwa akilia tu.
“Twendeni!”
Wakaanza kumfuata nesi yule, wakaongozana naye mpaka katika ofisi ya daktari na kuugonga mlango ambapo wakakaribishwa. Kitendo cha kumuona daktari huyo tu, Godwin akashindwa kuvumilia, naye akaanza kulia mfululizo kama ilivyokuwa kwa ndugu yake.
“Kuna nini tena?” aliuliza daktari huku akishangaa.
“Hawa ni watoto wa yule mama!” alijibu nesi.
“Mama yupi?”
“Yule aliyeku…” alijibu nesi lakini hata kabla ya kumalizia jibu lake akanyamaza na harakaharaka kutoka ndani ya chumba hicho.
“Mama amekufa? Mama yetu amekufa?” aliuliza Godwin huku akiisogelea meza ya daktari ambaye alibaki kimya, hakujua ni kitu gani angewaambia watoto hao, hakujua kama alitaka kuwaambia ukweli juu ya kilichotokea au kuwadanganya.
“Mama yetu amekufa?” aliuliza Godwin, tayari alianza kulishika koti la daktari huyo. Maumivu makali aliyokuwa nayo moyoni mwake, hayakuweza kusimulika.
***
Hawakuambiwa kuhusu mama yao lakini muonekano aliokuwa nao daktari ulionyesha kabisa kwamba mama yao alikuwa amefariki dunia. Waliumia, walilia mno humo ndani, Godwin hakutaka kuliachia koti la daktari, alilishikilia huku akiendelea kumsisitiza amwambie ukweli kuhusu mama yao kwamba alikuwa amekufa au la.
Daktari alinyamaza, alimlaumu nesi kwa kuongea sentensi ambayo haikumalizika, ambayo kwa mtu yeyote yule angegundua kwamba mwanamke huyo alikuwa amekufa.
Huo ndiyo ulikuwa ukweli, Rosemary, mwanamke shupavu alikuwa amefariki dunia. Alivunjika mbavu, mapafu yake yalipasuka hali iliyopelekea kifo chake.
Manesi na madaktari waliumia kwani walijitahidi sana kuyaokoa maisha ya mwanamke huyo lakini ilishindikana kabisa. Hawakumjua ndugu yeyote yule, hawakujua kama mwanamke huyo alikuwa wa mitaani tu, hakujua kama yule aliyekuwa akimtibu alikuwa Rosemary, mke wa Mapoto, mwanaume aliyekuwa na kiu kubwa ya kuibadilisha Tanzania.
“Nyamazeni! Huu si mwisho wa maisha yenu. Kama Mungu alivyokuwa akiwalinda, ataendelea kuwalinda,” alisema daktari huku akiwaangalia watoto hao waliokuwa wakiendelea kulia.
“We want her back! Lord! Why? Why us?” (Tunamtaka arudi! Bwana! Kwa nini? Kwa nini sisi?) aliuliza Godwin huku akilia.
Daktari alishtuka, hakuamini kama watoto hao walikuwa wakijua kuzungumza Kiingereza, walionekana kuwa watoto wa mitaani kama wengine, hakuamini kama watoto hao walikuwa wamepitia maisha ya kifahari kwani muonekano wake ulifanana na watoto wengine.
Alibaki akiwashangaa, alitamani kuwauliza ni kwa namna gani waliifahamu lugha hiyo lakini alishindwa kabisa kutokana na hali waliyokuwa nayo mahali hapo.
Akawachukua na kuwapeleka nje, akawaweka kwenye benchi na kuwataka wapumzike mahali hapo. Hawakunyamaza, bado waliendelea kulia kwa uchungu mkubwa, mioyo yao iliumia na hawakujua wangeweza kuishi vipi pasipo mama yao ambaye alikuwa kila kitu katika maisha yao.
Watu waliokuwa mahali hapo walikuwa wakiwaangalia, hawakuwafahamu, walionekana kutoka katika familia ya kimasikini, muonekano wao uliwafanya kuona kwamba walikuwa watoto wa mitaani tu.
“Kuna nini? Wamepatwa na nini tena?” aliuliza jamaa mmoja huku akiwaangalia.
“Mmh! Sijui! Labda wamefiwa!”
“Haiwezekani! Nahisi kuna kitu kingine zaidi,” alisema jamaa huyo.
Walilia, walihuzunika sana lakini machozi na huzuni zao zilishindwa kubadilisha kitu chochote kile, walishindwa kuubadilisha ukweli, mama yao hakurudi, alikuwa amefariki dunia na hivyo kuiomba hospitali hiyo kusimamia mazishi kwani hawakuwa na kitu chochote kile.
Baada ya siku mbili, Rosemary akazikwa katika makaburi ya Sinza na hivyo Godwin na Irene kuanza maisha mapya, maisha bila mama. Maisha hayakuwa kama walivyozoea, yalibadilika, muda mwingi walitawaliwa na majonzi mazito, walilia kila siku.
“Mama aliuawa!” alisema Godwin huku akimwangalia Irene.
“Unasemaje?”
“She was murdered,” (aliuawa!)
“How do you know?” (umeajuaje?) aliuliza Irene huku akimshangaa kaka yake ambaye hakujibu kitu, akanyamaza huku akionekana kuwa na hasira kali moyoni mwake.
***
Kila kitu kilichokuwa kimepangwa kilifanyika kama kilivyotakiwa kufanywa. Mwanaume mwenye mwili mkubwa ambaye alitumwa kwa kazi ya kumuua Rosemary akarudi ofisini na kupeleka taarifa kwamba kila kitu kilikuwa kimefanyika kwa mafanikio makubwa ya asilimia mia moja.
Taarifa hiyo ilimfurahisha kila mmoja, wakapongezana kwamba hatimaye walikuwa wakienda kukamilisha lengo lao walilokuwa wamejiwekea. Hakukuwa na mtu aliyekuwa na huruma, hakukuwa na mtu aliyehuzunika juu ya kifo cha Rosemary, kila mmoja alionekana kuwa na furaha na kubwa zaidi wakaweka pombe kwenye glasi zao na kuanza kunywa.
“Na watoto wake?” aliuliza mwanaume mmoja.
“Nao wafe. Kwa kifupi ni kwamba familia nzima ipotee katika uso wa dunia,” alisema jamaa mwingine.
“Kwa hiyo nitume watu wakawaue?”
“Hapana! Subiri kwanza waishi maisha yenye majonzi, mioyo yao iume kila siku, baada ya hapo, tutawaua,” alisema mwanaume huyo maneno ambayo yaliungwa mkono na kila mmoja mahali hapo.
****
Mwezi mmoja ulikuwa umepita, maisha yao yaliendelea kuwa ya mitaani. Hawakuwa wamehama pale walipokuwa, kibanda kile ambacho kilikuwa kimebomolewa ndicho hichohicho wakakisimamisha na kuendelea na maisha yao kama kawaida.
Baada ya siku kadhaa, Godwin akakutana na kijana mmoja, masikini kama alivyokuwa na kumpa kazi ambayo kama angeifanya, hakika wangeingiza kiasi kikubwa cha fedha.
“Una uhakika tutapata pesa?” aliuliza Godwin huku akimwangalia mwanaume huyo.
“Ndiyo! Watu wengi wanajenga, tena majumba makubwa. Tukafanye hivyo huko,” alisema jamaa huyo.
Hicho ndicho walichokipanga kufanya. Godwin akamwambia Irene kwamba alipata kazi ya ujenzi, kuwa mmoja wa wasaidizi wa mafundi waliokuwa wakijenga nyumba mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Irene alifurahi lakini moyo wake ulikuwa mzito kukubaliana na Godwin, alikuwa na hofu kubwa moyoni mwake na alihisi kama kulikuwa na jambo baya lililokuwa likienda kutokea.
Hakutaka kumficha Godwin, alimwambia ukweli jinsi alivyokuwa akijisikia moyoni mwake. Alijua fika kwamba angemtia hofu kaka yake lakini hakuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima amwambie jinsi alivyokuwa akijisikia.
Godwin alipoambiwa, kwanza akacheka, akamwambia Irene kwamba hakutakiwa kuwa na hofu yoyote ile kwani kila kitu kingekuwa salama kama inavyotakiwa kuwa.
“Una uhakika?”
“Niamini Irene! Hakuna baya lolote lile,” alisema Godwin.
Baada ya siku tatu, kijana yule aliyeongea naye, Albert Mazongozongo akafika katika kibanda hicho na kumchukua kwenda katika moja ya ghorofa kubwa lililokuwa likijengwa Masaki jijini dar es Salaam.
Kabla ya kuanza kazi hiyo, aliyaona maisha yake yakibadilika, aliamini kwamba kama angefanya kazi hizo za ujenzi basi maisha yake na Irene yangebadilika milele.
Kazi ikaanza, huko akakutana na mafundi wengi, wakaanza kulijenga jengo hilo huku wakilipwa kiasi cha shilingi elfu saba kwa siku. Ilikuwa ni kazi kubwa na ngumu lakini alihakikisha anapambana nao kila siku.
Alipokuwa akirudi, alikuwa akichoka sana, alifikia kulala mpaka siku nyingine aliporudi tena. Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake kila siku. Kutokana na ucheshi wake, akajikuta akipata marafiki wengi, akapendwa na hata wakati mwingine kupewa michongo mingine ya kazi nyingine nyingi.
“Utakuwa unapeleka hizi nondo kwenda kule juu. Kuwa makini na ngazi,” alisema jamaa mmoja, fundi mkuu, alikuwa akimwambia Godwin.
“Haina tatizo!”
“Chukua kofia ngumu uvae!”
“Mkuu! Kofia ngumu na hili joto! Kichwa kitawaka, wala usijali,” alisema Godwin.
“Basi sawa.”
Siku hiyo kazi yake kubwa ilikuwa ni kupandisha vifusi kwenda ghorofa ya saba. Ilikuwa kazi kubwa na ngumu kwani nondo zenyewe zilikuwa nzito mno. Alizipandisha kwa mahesabu makubwa, kazi hiyo ilichukua saa mbili, akamaliza na kwenda kupumzika chini.
Sehemu aliyokaa haikuwa sehemu salama, kwa juu kulikuwa na vifusi vya kokoto na mchanga vilivyokuwa vimewekwa katika chombo kimoja kwa kilichokuwa kikivutwa na kamba ngumu kupelekwa juu.
Wakati kila mmoja akiwa hana habari, huku Godwin akiwa chini amepumzika, ghafla kamba ngumu iliyokuwa imeshikilia chombo kilichobeba vifusi vile ikakatika na vifusi hivyo kuanza kuanguka chini.
Walioliona tukio hilo wakaanza kupiga kelele, vifusi hivyo vilianza kuangukia kule alipolala Godwin. Wakati akishtuka kutokana na kelele za mafundi wengine, hata kabla hajachukua uamuzi wowote mahali hapo, vifusi zaidi ya kumi na tano vikamuangukia pale alipokuwa na kumfunika.
“Mungu wangu!” alisema jamaa mmoja huku wakishuka kwa kasi kuelekea kule alipokuwa Godwin ambaye alifunikwa na vifusi zaidi ya kumi na tano.
“Toa vifusi….toa vifusi,” alisema fundi mmoja akiwaambia wenzake, kila mtu alichanganyikiwa na walichokijua ni kwamba Godwin alikuwa amekufa mahali pale kwani vifusi vilivyokuwa vimemwangukia vilikuwa vyenye mchanga na kokoto nyingi.
***
Kila mmoja alichanganyikiwa, hawakujua kama Godwin aliyekuwa chini ya kifusi alikuwa hai au alikufa. Waliogopa, vifusi vile vya mchanga na kokoto vilikuwa vizito mno na hata walipokuwa wakivitoa, walipata wakati mgumu mno.
Walisaidiana, walivitoa vyote juu yake na kisha kumfikia yeye. Alikuwa kimya, damu zilikuwa zikimtoka kichwani, alitulia, kwa kumwangalia harakaharaka alionekana kama mfu mahali pale.
“Mungu wangu!” alisema jamaa mmoja huku akishika kichwa kwa mshtuko.
Wakamtoa mahali pale, kwa haraka sana wakamkimbizia kwenye gari na kuanza kuelekea naye hospitalini. Kila mmoja alikuwa na hofu juu ya hali aliyokuwa nayo Godwin, mapigo yakeya moyo yalikuwa yakidunda kwa mbali sana kiasi kwamba kila mmoja akahisi kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wake.
Rafiki yake, Albert alikuwa kimya, aliogopa, hakuona kama kulikuwa na dalili za Godwin kupona. Kichwani mwake akaanza kumfikiria Irene, hakujua ni kwa kiasi gani angeumia kama angemwambia kwamba kaka yake mpendwa, alikuwa katika hali mbaya na muda huo walikuwa njiani kuelekea hospitalini.
Hawakuchukua muda mwingi wakafika katika Hospitali ya Mwananyamala ambapo gari lilipoingia, kwa haraka sana machela ikaletwa, akapakizwa juu na kuanza kusukumwa kuelekea ndani.
Kila mtu aliyekuwa akimwangalia Godwin, alishika kichwa, hakukuwa na aliyeamini kama kijana huyo angepona kwani kwa muonekano aliokuwa nao, damu zilizokuwa zikiendelea kumtoka, kila mmoja aliamini kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wake.
“Nini jamani? Ajali?” aliuliza nesi mmoja huku akimshangaa Godwin kana kwamba hakuwahi kupokea mgonjwa aliyekuwa kwenye hali mbaya kama aliyokuwa nayo Godwin.
“Yeah! Ameangukiwa na vifusi saiti! Tunaomba mumsaidie jamani, jembe letu hili!” alijibu jamaa mmoja.
Mtihani mkubwa ukabaki kwa Albert, bado kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, mtu aliyekuwa akimfikiria alikuwa Irene ambaye hakujua angezipokeaje taarifa za kaka yake kupata ajali mbaya ya kuangukiwa na vifusi saiti.
Hakutaka kuondoka hospitalini hapo, alitaka kujua ni kitu gani ambacho kingeendelea. Alibaki kwenye mabenchi pamoja na wenzake, kwa zaidi ya saa moja walikuwa hapo mpaka hao wenzake walipoamua kuondoka na yeye kubaki.
Hakutaka kumuacha Godwin mahali hapo, alikuwa rafiki yake mkubwa, alimzoea na kwa kipindi hicho alikuwa akiishi naye kama ndugu yake wa damu. Pale kwenye benchi, alikuwa akimuomba Mungu, hakutaka kuona Godwin akifa, hakutaka kuona Mungu akiichukua roho yake.
Baada ya saa mbili, Godwin akapelekwa katika wodi ya wagonjwa wengine na kulazwa humo. Japokuwa kulikuwa na wagonjwa wengi lakini hawakuacha kumwangalia Godwin aliyekuwa kwenye hali mbaya kuliko hata wagonjwa wengine waliokuwa katika wodi hiyo.
Muda wa kuona wagonjwa ulipofika, Albert akaelekea katika wodi ile na kusimama pembeni ya kitanda alicholazwa Godwin, alikuwa akimwangalia, moyo wake ulikuwa kwenye majonzi tele, hakuamini kama rafiki yake huyo alikuwa kwenye hali hiyo, alimwangalia kwa masikitiko makubwa, akashindwa kuyazuia machozi yake ambayo yalianza kumtiririka.
Moyo wake ulimuuma mno, alimchukulia Godwin kama ndugu yake ambaye alimpa nafasi kubwa katika maisha yake, kitu kilichomuhuzunisha ni ajali mbaya aliyokuwa ameipata, aliumia kwa kuwa yeye ndiye aliyemtafutia kazi hiyo ambayo ilionekana kuyabadilisha maisha yake na kumlaza kitandani.
Hakukaa sana hospitalini hapo, muda ulipokwisha, akaondoka kurudi nyumbani. Bado alikuwa akijifikiria namna ya kumfikishia Irene ujumbe kwamba kaka yake alikuwa hoi hospitalini, hakujua binti huyo angezipokeaje taarifa hizo.
Wakati mwingine alisita kwenda huko lakini wakati mwingine aliona kwamba kulikuwa na umuhimu mkubwa wa kwenda nyumbani hapo kwani iwe isiwe ilikuwa ni lazima ajue kuhusu kile kilichoendelea kwa kaka yake.
Hakuwa na jinsi, akaondoka na kuelekea huko. Hakuchukua muda mrefu akafika katika kibanda hicho, akapiga hodi na kuingia ndani. Hakuonekana kuwa na furaha, alitamani kutoa tabasamu kumdanganya Irene lakini ilishindikana kabisa, uso wake ukavaa sura ya kile kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake.
“Kuna nini? Godwin yupo wapi?”aliuliza Irene huku akimwangalia Albert aliyeonekana kuwa na huzuni tele machoni mwake.
Albert hakujibu kitu, akabaki kimya akimwangalia msichana huyo, hakujua ni kitu gani alitakiwa kumwambia, hakujua ni kwa jinsi gani msichana huyo angeumia moyoni mwake.
Irene akahisi kulikuwa na jambo baya lililokuwa limetokea kwani kama kusingekuwa na jambo baya, Albert angemjibu swali lake au angekuja kibandani hapo akiwa na kaka yake. Akamlazimisha mno kumwambia, hata kama alikuwa amekufa, amwambie kwani hata kama angemficha ilikuwa ni lazima aujue ukweli.
Albert hakuwa na jinsi, akaanza kumuhadithia Irene kilichokuwa kimetokea. Moyoni mwake aliumia lakini hakuwa na jinsi. Irene alikuwa kimya akimsikiliza Albert, alionekana kuwa katika hali ya kawaida lakini wakati ambao Albert alimaliza kumuhadithia, hapohapo akaanza kulia kwa sauti kubwa.
Aliumia moyoni mwake, hakuamini kilichokuwa kimetokea, moyo wake ulichoma kupita kawaida, kitendo cha kuambiwa kwamba kaka yake alikuwa kwenye hali mbaya ilimuuma mno.
Wazazi wao walikufa, walibaki wawili tu lakini jambo la kuumiza kabisa, kaka yake alikuwa njiani kufa kitu ambacho kingemfanya kubaki peke yake. Aliumia, hakutaka kuona hilo likitokea maishani mwake.
Alitaka kumuona kaka yake, hata kama alikuwa kwenye hali mbaya, hata kama alikuwa amekufa, alitaka kuiona maiti yake. Alikuwa akipika, akaacha kupika na kutoka ndani ya kibanda hicho.
Alijua mahali Hospitali ya Mwananyamala ilipokuwa hivyo kuanza kukimbia kuelekea huko. Moyo wake ulihuzunika, njiani alionekana kuwa kama kichaa, kila mtu alimwangalia, khanga yake aliyoivaa ilianza kumvuka na kubaki na sketi lakini hakujali, kubaki mtupu kwake halikuwa jambo baya, kitu cha muhimu alichokuwa akikihitaji wakati huo ni kujua hali ya kaka yake tu.
Wakati akikimbia kuelekea hospitalini, naye Albert alikuwa nyuma yake akimkimbiza huku akimtaka asimame na wazungumze kwanza. Si kwamba Irene hakusikia, alisikia lakini hakuwa radhi kusimama.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika hospitalini hapo. Kama kulia, Irene alikuwa amelia vya kutosha, aliumia pasipo kawaida. Akaingia ndani ya eneo la hospitalini hapo, haukuwa muda wa kuona wagonjwa hivyo akazuiliwa.
“Irene! Ungenisubiri kwanza,” alisema Albert huku akihema kwa nguvu.
“Nimeumia. Ninataka kumuona kaka yangu, ninataka kumuona Godwin,” alisema Irene huku akilia, akamsogelea Albert, akamkumbatia na kuendelea kulia kifuani mwake.
Kila mtu aliyemuona Irene alimuonea huruma, alikuwa akilia sana kana kwamba alikuwa amefiwa na kaka yake. Wakaondoka karibu na sehemu ya kuingilia ndani ya jengo la hospitali na kuelekea sehemu ya kupumzikia watu wanaofika mahali hapo kwa ajli ya kuwaona wagonjwa wao.
Irene hakuwa na raha, alikuwa na huzuni kubwa moyoni mwake. Muda mwingi alikuwa akilia kwa uchungu, kilichomuumiza kichwa na kumchoma moyo ni kwamba walibaki wawili tu na kaka yake huyo ndiye alikuwa kila kitu.
Alimuomba Mungu, alimkumbusha kwamba Godwin ndiye alikuwa kaka yake pekee, hakuwa na ndugu yeyote yule, kumchukua kutoka mikononi mwake ilikuwa ni sawa na kuchukua kila kitu alichokuwa nacho mikononi mwake.
“Mungu! Sina mwingine, Godwin ndiye kaka yangu, mama yangu na baba yangu. Kumchukua kutoka mikononi mwangu ni sawa na kuchukua kila kitu kutoka kwangu! Nakuomba usimchukue kaka yangu, nakuomba uniachie kaka yangu! Mungu! Bado tuna safari ndefu pamoja, naomba tuimalize lakini si kumchukua kaka yangu huyu,” alisema Irene huku akilia kama mtoto pale alipokuwa amekaa.
Walikaa hapo kwa dakika kadhaa. Muda wa kuona wagonjwa ulipofika, wakaondoka na kuelekea ndani ya wodi ile. Irene akapiga hatua mpaka katika kitanda alicholazwa Godwin. Alimwangalia, alionekana kuwa mfu, ni mashine ya oksijeni ndiyo ilimfanya kugundua kwamba kaka yake huyo alikuwa hai.
“Godwin kaka yangu! Nakuomba usiniache peke yangu, naomba ubaki nami, naomba ufumbue macho yako na kuniangalia. Naomba usiondoke, Mungu alitupokonya wazazi wetu, nakuomba usiondoke, sitotaka kumuona Mungu akinipokonya wewe kutoka maishani mwangu. Godwin, naomba usife, naomba ufumbue macho na kuniangalia tena,” alisema Irene huku akiwa pembeni ya kitanda cha Godwin, alikuwa akibubujikwa na machozi tu mashavuni mwake.
***
Godwin alikuwa kimya kitandani pale, hakujua kitu chochote kilichokuwa kikiendelea. Dripu ilikuwa ikining’inia pembeni ya kitanda chake huku huku mashine ya oksijeni ikiwa mdomoni mwake huku ikimsaidia kupumua pale kitandani alipokuwa.
Irene hakuondoka, alibaki pembeni ya kitanda kile huku akilia. Moyo wake uliendelea kuchoma mno, maumivu aliyoyasikia kipindi hicho hayakuelezeka, aliongea peke yake pembeni ya kitanda kile akimtaka Godwin ayafumbue macho yake lakini hilo halikuweza kutokea.
Moyo wake ukakata tamaa, kwa mbali aliisikia sauti ikimwambia kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wa ndugu yake huyo, kama wazazi wao wote walifariki, huo ndiyo ulikuwa muda wa kaka yake, naye alitakiwa kufariki kama hao wengine.
Albert alisimama pembeni, alikuwa akimwangalia rafiki yake jinsi alivyokuwa akiteseka kitandani pale. Alihuzunika mno na muda wote alikuwa akimuomba Mungu afanye muujiza, rafiki yake huyo afumbue macho na kuangalia tena lakini jambo hilo halikutokea.
Madaktari walikuwa wakiingia ndani ya wodi hiyo kuwaangalia wagonjwa lakini kila aliyeingia ilikuwa ni lazima kusogea katika kitanda alicholala Godwin na kumjulia hali.
Waliguswa na hali yake, mioyo yao ilitokea kumpenda tofauti na wagonjwa wengine na kwa kuwa Irene alikataa kuondoka hospitalini hapo, iliwabidi madaktari wampe chakula cha wagonjwa kwani muonekano aliokuwa nao uliwaonyesha ni kwa jinsi gani msichana huyo alikuwa masikini.
“Kula kwanza…” alisema Dk. Mende, mmoja wa madaktari maarufu hospitalini hapo.
“Hapana! Siwezi kula!” alijibu Irene.
“Kwa nini?”
“Sina hamu ya kula.”
“Jaribu kujilazimisha. Utakaaje bila kula hata kidogo?” aliuliza daktari huyo.
“Siwezi kula na wakati kaka yangu hana hata uwezo wa kufumbua mdomo. Siwezi kula,” alisema Irene huku akimwangalia daktari huyo.
Hakuwa radhi kula, hakuona kama kulikuwa na umuhimu wa kufanya hivyo na wakati kaka yake alikuwa hoi kitandani na hakujua ni muda gani angeweza kufumbua tena macho yake.
Muda ulizidi kwenda mbele, wakati mwingine alitakiwa kutoka ndani ya wodi hiyo, aliondoka na kwenda nje ambapo akakimbilia chini ya mti kulipokuwa na viti vingi na kutulia hapo pamoja na wenzake waliokuja kuwaona ndugu zao.
Irene hakutaka kurudi nyumbani, alikuwa akishinda hospitalini hapohapo. Hakutaka kumuacha kaka yake akiendelea kuteseka, alitaka kumuona kuanzia hatua moja mpaka nyingine.
Mara nyingi Dk. Mende alikuwa akimuita na kuzungumza naye. Alitaka kufahamu zaidi kilichokuwa kimetokea maishani mwao kwani tangu Godwin apelekwe hospitalini hapo, mbali na mafundi wa ujenzi, hakukuwa na watu wengine waliofika mahali hapo kumjulia hali.
Alimdadisi Irene lakini msichana huyo hakumwambia kitu chochote kile. Hakutaka ajue walipotoka, hakutaka ajue historia ya maisha yao, kuhusu wazazi wake kwani alihisi kwamba endapo angejua basi angeweza kuwasiliana na waandishi wa habari na kuwaambia kuhusu wao.
“Sisi ni watoto wa mitaani tu,” alijibu Irene huku akimwangalia Dk. Mende.
“Sawa. Najua ni watoto wa mitaani! Ila ilikuwaje mpaka mkawa hapo?” aliuliza daktari huyo.
“Wazazi wetu walifariki. Baada ya hapo ndipo tukaanza kuishi maisha ya mitaani bila ndugu,” alijibu Irene.
Kila swali alilouliza daktari huyo, jibu alilokuwa akipewa halikuwa la ukweli. Irene alificha mengi kuhusu maisha yao ya nyuma, alimficha mengi tu kuhusu wazazi wake. Dk. Mende hakujali, aliuamini uongo alioambiwa hivyo kumruhusu msichana huyo kwenda kumuona kaka yake.
Kila alipoingia ndani ya wodi hiyo Irene alikuwa akilia tu hata kabla hajamfikia kaka yake. Moyo wake ulichoma mno na alipokifikia kitanda, kitu cha kwanza kilikuwa ni kupiga magoti na kuanza kumuomba Mungu huku machozi yakimtoka.
“Mungu! Naomba usimchukue kaka yangu. Tazama ninavyoumia moyoni, nimekosa furaha kwa kipindi chote hiki. Uliwachukua wazazi wetu kutoka mikononi mwetu, bado hujaridhika, unataka kumchukua Godwin kutoka mikononi mwangu. Nitaishi vipi Mungu! Ni nani atanifuta mchozi? Nitakimbilia wapi? Mungu! Ni mapema mno, naomba unipokonye kila kitu kutoka mikononi mwangu lakini si kunipokonya Godwin!” alisema Irene huku akilia.
Hali ya Godwin haikubadilika, aliendelea kuwa vilevile, kila siku ilikuwa ni afadhali ya jana. Kila mtu aliogopa, madaktari walikata tamaa kwani tayari wiki moja ilipita na hakukuwa na mategemeo yoyote yale, jinsi alivyokuwa amefikishwa hospitalini hapo ndivyo alivyokuwa siku hiyo.
Siku ziliendelea kukatika huku Irene akiendelea kubaki hapohapo hospitalini. Hakujua kibanda chao kiliendeleaje, hakujua kama kilikuwa palepale au kilitolewa, kwa wakati huo kitu alichokuwa akikijali kilikuwa ni hali ya kaka yake tu.
***
“Kuna taarifa mpya mkuu!” alisikika mwanaume mmoja kwenye simu.
“Taarifa gani?”
“Kuhusu wale watoto!”
“Imekuwaje?”
“Ni kwamba yule wa kiume amepata ajali. Aliangukiwa na kifusi alipokuwa akifanya kazi ya ujenzi!” alisema mwanaume huyo.
“Unasemaje?”
“Ndiyo hivyo mkuu! Kwa sasa amelazwa hospitalini. Taarifa zinasema zaidi kwamba hali yake mbaya, alivyoingia ndivyo alivyo mpaka sasa hivi,” alisema mwanaume huyo.
“Ni habari mpya kwangu! Ni lazima lifanyike jambo fulani!”
“Ndiyo nakusikiliza mkuu!” alisema kijana aliyekuwa amepiga simu.
“Hii ndiyo nafasi! Mnachotakiwa kufanya ni kimoja tu. Muueni hapohapo kitandani kwa kuwa sababu ipo wazi kwamba ni mgonjwa. Jipangeni na hakikisheni mauaji yanafanyika kidigitali,” alisema mwanaume huyo.
“Sawa mkuu! Na msichana?”
“Huyo zamu yake itafika!”
“Haina shida.”
Yalikuwa ni mazungumzo ya simu baina ya pande mbili. Kilichokuwa kikitakiwa kufanyika kwa haraka sana kilikuwa ni kumuua Godwin kitandani alipokuwa. Alikuwa hoi, hakujitambua na wao waliona kwamba kama wangemuua kitandani hapohapo ingekuwa rahisi sana kuwaaminisha watu wengine kwamba mtu huyo alikufa baada ya kupata ajali hiyo na hakuweza kupata nafuu.
Hawakutaka kukurupuka kufanya kazi hiyo, walitaka kumuua kwa staili ambayo hata madaktari wasingeweza kufahamu. Vijana watatu wakajipanga kwa ajili ya kufanya kazi hiyo. Kwa kuwa Godwin alilazwa katika wodi iliyokuwa na wagonjwa wengi, hivyo walitakiwa kujifanya watu wa dini ambao walikuwa na lengo la kutembelea hospitalini humo na kujifanya kuwaombea wagonjwa Mungu aweze kuwalinda na kuwaponya.
Ulikuwa mpango kabambe na hata wakubwa walipopewa mpango huo, wakaridhika nao na hivyo kuwaongezea kwamba katika vijana hao watatu, mmoja alitakiwa kutolewa na kuingizwa msichana ambaye ndiye angekuwa na nguvu kubwa ya kuwashawishi madaktari kwamba kweli wao walikuwa watu wa msaada.
“Ni wazo zuri!”
Msichana aliyetakiwa kuifanya kazi hiyo aliitwa Magdalena Urassa, msichana mwembamba, mrefu aliyekuwa na mwanya uliomfanya kuvutia kila alipokuwa akitabasamu au kucheka.
Kabla ya kwenda huko walitaka kuona wakiwa na muonekano wa kikanisa ili iwe rahisi kwao kufanya kile walichotaka kukifanya. Haikuwa hivyo tu bali walitaka kuhakikisha wanatumia kiasi cha fedha kwa ajili ya matunda na maji kwa ajili ya wagonjwa hospitalini hapo.
Mipango yote hiyo, gharama zote hizo zilikuwa ni kwa ajili ya kumuua mgonjwa mmoja ambaye alikuwa akiteseka kitandani akipumulia mashine ya gesi.
Hawakujali gharama, kitu pekee walichokijali ambacho walitaka kukiona kikitokea ni kumuua Godwin kitandani pale ili baadaye wamalizane na Irene kisha kufunga daftari lao la mauaji kwa familia hiyo.
“Tunakwenda Alhamisi, tutarudi Ijumaa na Jumamosi, wakati wametuzoea, Jumapili tunafanya kazi yetu,” alisema Majura, mmoja wa vijana waliokuwa wametumwa.
“Haina shida. Kitu cha kwanza tuandae mavazi. Nitakuwa padri wa Kanisa Katoliki,” alisema mwanaume mwingine aliyeitwa Yusufu, alizungumza kwa utani huku akicheka.
“Na mimi nitakuwa sista. Nitaitwa Sista Theopista. Mkiona jina mnalisahau sana, mtaniita Sista T, nitawaelewa,” alisema Magdalena na wote kuanza kucheka. Mipango ikaanza kusukwa.
Je, nini kitaendelea?
Watoto hao watauawa?
Tukutane Ijumaa hapahapa.