DUNIA HAINA USAWA
Kihampa alikuwa njiani akiwahi kuelekea Fire alipowaambia vijana wake wammpeleke Godwin waliyekuwa wamemteka. Aliendesha gari kwa mwendo wa kasi kuwahi huko kwani hakukuwa na kitu alichokuwa na hamu nacho kama kumuua Godwin.
Alipofika njiani maeneo ya Jangwani, akakumbana na foleni kubwa, mbele kabisa, Fire kulikuwa na ajali iliyotokea ambayo iliziba njia. Alikasirika, mara kwa mara alikuwa akipiga usukani huku akiwa na hasira mno.
Hakutaka kuendelea kubaki, alichokifanya ni kuingia katika upande mwingine wa barabara na kuingia kule kulipokuwa na Uwanja wa Jangwani. Alikuwa akiendesha taratibu kwani napo huko kulikuwa na watu wengi waliokuwa katika mkutano wa injili.
“Huku napo kuna nini?” aliuliza Kihampa kwa hasira.
Mbele yake kulikuwa na gari moja lililokuwa limekwama kwenye shimo, alijitahidi kupiga honi lakini haikuweza kusaidia, hakukuwa na sehemu nyingine ya kupita zaidi ya hapo ambapo gari lilipokuwa limekwamba.
Kwa hasira akateremka na kwenda kule lilipokuwa, yeye mwenyewe alishangaa, kwa nini shimo lilikuwa dogo lakini gari hilo lilikwama. Alijaribu kuwaambia watu hao jinsi ambavyo walitakiwa kuliondoa gari hilo lakini haikuwezekana, kwa hasira, huku akionekana kuvimba akarudi ndani ya gari lake, akaingia, akashusha kioo na kutulia.
Sauti ya mchungaji aliyekuwa akihubiri katika mkutano uliokuwa uwanjani hapo ilikuwa ikisikika, maneno yote yalisikika vema masikioni mwake.
“Mungu anataka kuzungumza na moyo wako, haijalishi wewe ni mtu wa aina gani, haijalishi umeua watu wangapi, haijalishi umelala na wanaume wangapi au wanawake wangapi, jioni ya leo Mungu anataka kuzungumza na wewe. Inawezekana kabisa ukawa na mpango wa kwenda kuua leo, inawezekana una mpango wa kwenda kuzini leo, Mungu wa Mbinguni anakuona, Mungu anataka utubu dhambi zako, Mungu anataka umsogelee kule alipo,” alisikika mchungaji aliyekuwa akihubiri.
Hakuishia hapo, alizidi kuzungumza maneno mengi, maneno yote hayo yalikuwa yakisikika masikioni mwa Kihampa. Hakuamini alichokisikia, ni kama mchungaji huyo aliambiwa kuhusu maisha yake, akauona moyo wake ukianza kupoa, akaona moyo wake ukianza kuumia.
Alishindwa kuyazuia machozi machoni mwake, yakaanza kumtoka na kutiririka mashavuni mwake. Maneno yote hayo yalimuumiza, akajikuta akilia, mauaji aliyokuwa ameyafanya maishani mwake yakaanza kuwa huku nzito moyoni mwake.
Akaanza kusikia sauti za watu wakimlilia, sauti nyingi zilimlaumu kwa kuamua kuwamaliza kabisa. Aliogopa, ndani ya gari alikuwa kama amechanganyikiwa, hakutaka kubaki humo, ni kama alikuwa na mauzauza, akatoka na kuanza kuelekea kule kulipokuwa mkutano ule.
Alitembea, alikuwa akilia kama mtoto, moyo wake ulichoma mno na kitu alichokitaka wakati huo ni kutubu dhambi zake, aanze maisha mapya na Mungu kwani kwa maisha aliyokuwa ameishi kwa kipindi chote yalikuwa machafu mno.
Mchungaji akamkaribisha, mbali na yeye, pia kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakitaka kutubu dhambi zao, wakafanyiwa sala ya toba na kuwa watu wapya, mioyo yao ikaumbwa, wakamrudia Mungu na kuachana na maisha waliyokuwa wakiishi.
“Nifanye nini?” alijiuliza.
Alikuwa na kazi aliyopewa, hakutaka kubaki hapo, akaondoka kwa ajili ya kuifanya kazi hiyo. Moyo wake ulikuwa mzito kufanya mauaji tena, alitubu dhambi zake na hakuwa tayari kuona akifanya dhambi nyingine kwa kumuua mtu.
Hakuchukua muda mwingi akafika alipokuwa akienda, vijana wake wakamwambia kwamba tayari Godwin alikuwa ndani ya jumba hilo katika chumba alichokuwa amehifadhiwa. Alichokifanya ni kumfuata na kumchoma sindano ya usingizi.
Hakutaka kumuua Godwin, alitaka aendelee kuishi. Kama kuua, aliua sana na muda huo ulikuwa ni wa kuishi na Mungu wake na si kuua tena kama ilivyokuwa.
Akachukua boksi, kabla ya kumuingiza humo Godwin, akaelekea stoo ambapo akachukua maboya na kuyaingiza ndani ya boksi lile. Hakutaka kuona Godwin akifa, alitaka kumuokoa na muda wote alikuwa akimuomba Mungu kwamba kwa kile alichokuwa akikifanya basi amlinde na asimuache akifa katika bahari waliyopanga kwenda kumtupa.
Kwa kuwa aliwatoa vijana wake ndani ya chumba kile, akamchukua Godwin na kamuingiza ndani ya boksi lile lililokuwa na maboya, akalifunga na kisha kuwaita vijana wale ambao wakalichukua na kulipeleka ndani ya gari tayari kwa kwenda kulitupa baharini.
Muda wote alikuwa akilia kwa uchungu, moyo wake haukuamini kama yeye ndiye aliyekuwa akifanya yale yote. Baada ya boti kufika baharini, wakalitupa humo na haraka sana kuwaambia waondoke kwani hakutaka wagundue kwamba boksi halikuzama zaidi ya kuelea juu ya maji tu.
****
Godwin alikuwa ndani ya boksi, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea. Usingizi ulimchota baada ya kuchomwa sindano ile ndani ya jumba lile. Boksi lilikuwa likipelekwa huku na kule, halikuwa likielekea nchi kavu bali lilizidi kusonga mbele kabisa kuelekea mbali kabisa na nchi kavu.
Mawimbi yalilipiga lakini halikuzama, liliendelea kuelewa juu ya maji mpaka baada ya saa moja ndipo akaamka kutoka katika usingizi mzito. Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuangalia huku na kule, hakuelewa mahali alipokuwa, alichokiona ni kwamba alikuwa ndani ya chumba kimoja kidogo mno ambacho kisingemfanya kuweza kusimama.
Mbali na kuwa humo, akawa anasikia sauti za mawimbi yakipiga, akahisi kwamba alikuwa katikati ya maji. Akaogopa, alipogusagusa pembeni na chini akakuta vitu ambavyo kwa haraka sana akili yake ikamwambia kwamba yalikuwa ni maboya.
Hakutaka kujiuliza sana, akahisi kwamba alikuwa ametupwa baharini lakini kitu kilichokuwa kikimsumbua kichwa chake zaidi ni juu ya kuwekewa maboya hayo, kama kweli watu waliomtupa walitaka kuona akifa, kwa nini walimuwekea maboya?
Hakutaka kupoteza muda, haraka sana akayachukua maboya hayo na kuyavaa kisha kulichana boksi hilo gumu na kubaki akielea juu ya bahari. Hakujua mahali alipokuwa, akaangalia huku na kule, hakukuwa na dalili za nchi kavu, ilikuwa ni usiku lakini hakuona hata mwanga wa taa za nyumba zozote zile.
Hakutaka kupiga mbizi, akakubaliana na hali iliyokuwepo na kuanza kupelekwa huku na kule. Usiku mzima alikuwa juu ya maji, hakuona msaada wowote ule na mbaya zaidi hakuona dalili za kisiwa chochote kile.
Aliendelea kuelea juu ya maji na kitu ambacho kilimtesa sana kwa usiku huo kilikuwa ni baridi kali lililokuwa likipiga. Hakujua ni kwa jinsi gani angeweza kupona kutokana na baridi kali lililokuwa likimpiga baharini hapo.
“Mungu naomba uniokoe! Naomba usiichukue roho yangu,” alisema Godwin huku akielea juu ya bahari.
Siku hiyo akashinda tena baharini. Hakukuwa na msaada wowote uliofika mahali hapo, alikata tamaa kwani kwa jinsi muda ulivyokuwa ukizidi kwenda mbele ndivyo ambavyo njaa ilivyokuwa ikimuuma mpaka kuhisi kwamba kitu ambacho kingemuua hapo baharini kilikuwa ni njaa tu.
Muda ulizidi kwenda mbele, aliendelea kuelea juu ya maji. Hakuyafumba macho yake, aliendelea kuangalia huku na kule ili kuona kama kungekuwa na msaada wowote ule.
Mchana ukaingia, muda ukazidi kwenda mbele, tumbo likaanza kumuuma, hakujua ni kwa jinsi gani angepata msaada. Mpaka inafika jioni, bado hakupata msaada wowote ule, aliendelea kuelea juu ya maji.
Ilipofika usiku wa saa moja, bahari ikachafuka, akaanza kupiga kelele kuomba msaada, mawimbi makubwa yakaanza kumpiga, yakampeleka huku na kule, hapo ndipo akaona kwamba mwisho wa maisha yake ulikuwa umewadia kwani mawimbi yaliyokuwa yakimpiga yalikuwa makubwa na yenye nguvu ambayo yalimfanya muda mwingine kukosa nguvu kabisa.
Akajilaza juu ya maji, hakuwa na la kufanya zaidi ya kusubiri kifo tu baharini hapo kwani kwa jinsi njaa ilivyokuwa ikimuuma, wakati mwingine akaona kabisa giza likianza kuwa kubwa machoni mwake.
***
Godwin alikata tamaa baharini pale kwani kila alipokuwa akiangalia hakuona msaada wowote ule. Bahari ilichafuka usiku huyo, alipelekwa huku na kule, alipiga kelele kuomba msaada, alilia sana lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyejitokeza kumsaidia na mbaya zaidi kila alipokuwa akiangalia, hakuona meli wala kisiwa chochote kile.
Ukafika muda akakata tamaa, asingeweza kuendelea kuwa baharini pale na wakati hakuwa na kitu chochote kile. Njaa ilimkamata na mwisho wa siku kuendelea kuelea juu ya maji kama kipindi cha nyuma.
Ilipofika majira ya saa nane usiku, huku akiwa amekata tamaa kabisa akashtuliwa na mwanga mkali wa tochi uliokuwa ukimmulika, alishtuka, huo ukaonekana kuwa msaada mkubwa kwake. Akajitahidi kujitingisha mahali pale lakini akashindwa kabisa, akajikuta akiuangalia mwanga wa tochi ile lakini hakufanya lolote lile.
Akasikia watu wakitumbukia ndani ya maji na kuanza kumfuata kule walipokuwa, yote hayo yaliyokuwa yakiendelea aliyasikia vizuri lakini alishindwa hata kujitingisha pale alipokuwa.
Baada ya sekunde chache, watu wawili wakamfikia na kumchukua kisha kumuweka katika boya jingine lililofungwa na kamba kubwa kutoka ndani ya meli na kuanza kuvutwa kuelekea kule.
Mwili wake ulichoka, kila mtu aliyemwangalia alibaki akishangaa, hawakujua ni kitu gani kilikuwa kimetokea mpaka kuwa baharini pale. Mara ya kwanza walidhani kwamba meli aliyokuwa amepanda ilikuwa imezama lakini walipoliangalia eneo lile halikuwa na dalili za meli yoyote kuzama.
Walitaka kujua ukweli na waliona kabisa Godwin angewaambia kila kitu kilichokuwa kimetokea. Walipofika karibu na meli, akabebwa na kupakizwa ndani.
Kila mtu alikuwa akimshangaa, wakampa huduma ya kwanza na kumpa muda wa kupumzika. Watu hao hawakuwa Waswahili, walikuwa ni Wajapan ambao walikuwa baharini wakiendelea na shughuli zao za uvuvi na kwa bahati nzuri wakamuona mtu akielea juu ya maji na ndipo wakaamua kumsaidia.
Alikuwa kijana mdogo, mwenye sura nzuri, wakatokea kumpenda, wakamsaidia kwa kumpa chakula na mavazi. Mpaka siku iliyofuata ndipo Godwin akaweza kurudi katika hali yake ya kawaida. Kitu cha kwanza kabisa akabaki akishangaa, watu hao walikuwa wakina nani na walikuwa wakielekea wapi.
Kumbukumbu zake zilimwambia kwamba mara ya mwisho walikuwa baharini, sasa ilikuwaje muda huo awe ndani ya meli kubwa huku akiwa amezungukwa na Wajapan?
“Who are you?” (nyie ni wakina nani?) aliuliza Godwin huku akiwaangalia watu hao kwa macho yaliyojaa hofu.
“We are good people! We are here to help you?” (sisi ni watu wema! Tupo hapa kukusaidia) alisema mwanaume mmoja aliyekuwa na uso wa kutabasamu kila wakati.
Wanaume wale wakajitambulisha kwamba walikuwa wavuvi waliokuwa wakivua samaki hapo baharini, hawakutaka kumficha kitu chochote kile, walimwambia kila kitu lakini cha zaidi ni kwamba walikuwa watu wazuri ambao walimuokoa kutoka baharini.
Watu hao hawakuishia hapo, wakamuuliza kuhusu yeye, ilikuwaje mpaka kuwa baharini katika kipindi kama hicho. Kama kulikuwa na meli ilikuwa imezama, mbona eneo lile halikuonekana kuwa na dalili za meli yoyote ile kuzama?
“Nilikuwa na wenzangu ndani ya meli moja kubwa,” alianza kudanganya Godwin huku watu wote wakiwa kimya kumsikiliza.
“Mlikuwa mnakwenda wapi?”
“Nchini Italia. Tulitaka twende huko kusoma kwani maisha yalikuwa magumu sana huko tulipotoka,” alindelea kudanganya, na kwa jinsi alivyokuwa akionekana, ilikuwa vigumu sana kugundua kwamba kila kitu alichokuwa akikisimulia kilikuwa ni uongo.
“Wewe ni mtu wa wapi? Nigeria, Afrika Kusini au?” aliuliza mwanaume mmoja.
“Tanzania!”
“Kwa Nyerere?”
“Ndiyo!”
Alivyojibu hivyo, mwanaume huyo aliyeuliza swali hilo akawavuta wenzake pembeni na kuanza kuzungumza nao. Aliwaambia jinsi alivyokuwa akiifahamu Tanzania, ilikuwa nzuri iliyokuwa na watu waliokuwa na upendo mkubwa na kubwa zaidi ni kwamba iliwahi kuwa chini ya kiongozi mmoja aliyeheshimika duniani, Julius Nyerere.
“Kwa hiyo ni mtu mwema?”
“sijawahi kumuona Mtanzania mwenye roho mbaya. Nimeishi huko kwa miaka kumi. Ni watu wema sana. Nahisi hata huyu kijana atakuwa mwema,” alisema mwanaume huyo.
Walimwamini, walitaka kumrudisha lakini kwa sababu mwenzao aliwaambia kwamba inawezekana alikuwa mtu mwema, tena alikuwa akienda nchi nyingine kwa ajili ya kusoma na kutafuta maisha, wakapanga kumsaidia kwa kila kitu.
Hu ndiyo ukawa mwanzo wa maisha yake mapya, alilia sana lakini mwisho wa siku Mungu akaonekana katika maisha yake na kuwatuma watu kwa ajili ya kumsaidia. Hakutaka kurudi tena nchini Tanzania, alikuwa akitafutwa sana hivyo kilichofanyika ni kuanza safari ya kwenda nchini Japan tayari kwa kuanza maisha mapya.
Hakutaka kuwa na huzuni tena, alionekana kuwa na furaha, alizungumza na wavuvi wachache waliokuwa wakifahamu Kiingereza, moyo wake ulifurahia kwani kwa jinsi alivyokuwa akicheka na kufurahia, alihisi kabisa kwamba aliipata familia bora ambayo ilikuwa tayari kufanya jambo lolote lile kwa ajili yake.
Hawakutaka kurudi nchini Japan, wakaendelea na shughuli zao za uvuvi, kila siku Godwin alikuwa akifundishwa mambo mengi kuhusu uvuvi, alijisikia vizuri kwani kila mtu aliyekuwa ndani ya meli hiyo akawa kama rafiki yake.
Shughuli hiyo ilichukua wiki nzima ndipo ikakamilika na hivyo kuanza safari ya kurudi nchini Japan. Kutoka katika Bahari ya Hindi mpaka Pasifiki kulikuwa na umbali mkubwa, hawakwenda moja kwa moja nchini humo bali walichokifanya kilikuwa ni kupitia katika baadhi ya nchi kama Indonesia, Thailand na ndipo wakaingia nchini Japan.
Huo ndiyo ukawa mwisho wa safari yao, wote wakateremka na kuanza kuondoka kuelekea majumbani kwao huku wale ambao walihusika katika soko la biashara wa samaki hao wakiwachukua na kuanza kutafuta soko ambalo lilikuwepo muda wote huo.
Kwa Godwin, akachukuliwa na yule mzee aliyezungumzia sana kuhusu Tanzania, akamchukua na kuelekea nyumbani kwake huku akimuahidi kufuatilia vibali vyote ambavyo vingemfanya kusoma nchini Japan kabla ya kuamua ni kitu gani atafanya baada ya elimu hiyo.
“Utaishi vizuri sana! Nitafuatilia kila kitu,” alisema mzee huyo aliyejitambulisha kwa jina la Tokoyo Yokosoko ambaye alikuwa akiishi pembeni kidogo mwa Jiji la Tokyo.
“Haina shida! Nitashukuru sana!”
Hicho ndicho alichokifanya Mzee Yokosoko. Akamtambulisha Godwin nyumbani kwake. Akaiambia familia yake kila kitu kilichokuwa kimetokea baharini, kila mmoja alishtuka, waliifahamu bahari, hakikuwa kitu cha kawaida mtu kupona mara baada ya meli kuzama au kutoswa baharini lakini kwa Godwin, kuokolewa kwake ulikuwa kama muujiza.
Siku iliyofuata, mzee huyo akaanza kufuatilia vibali vya Godwin kumruhusu kukaa nchini humo. Ilikuwa kazi ndogo kwani sheria zao hazikuwashika sana wageni kutoka nchi nyingine, ndani ya siku tano tu, tayari Godwin alipata vibali hivyo na hivyo kuruhusiwa kukaa nchini humo kwa miaka mitano, muda wake ungekwisha, angeamua kama ni kuongeza au kurudi nchini mwake.
“Nashukuru sana!” alisema Godwin.
“Haina shida. Unataka kusomea nini?” aliuliza Mzee Yokosoko.
“Information Technology.”
“I.T?”
“Ndiyo!”
“Sawa. Nitaanza kufuatilia katika Chuo cha Waseda, ni chuo kizuri sana hapa Tokyo naamini kabisa kwamba kama utakwenda kuanza hapo, hakika utafanikiwa sana kwani wataalamu wote wa masuala ya kompyuta wamesoma katika chuo hicho, naamini hata nawe utafanikiwa sana tu,” alisema mzee huyo na siku iliyofuata akaanza kufuatilia.
Alitaka Godwin asome kwa pesa zake, hakutaka kuona akishindwa kwa kitu chochote kile kwani kila alipomwangalia kijana huyo, moyo wake ulimwambia kwamba afanye lolote lile lakini kijana huyo apate elimu bora kwa manufaa ya maisha yake.
***
Godwin alijiandaa kusoma katika Chuo cha Waseda kilichokuwa hapo Tokyo nchini Japan, hakuwa akijiamini, kwa kuwa alikuwa akitafutwa sana nchini Tanzania, akahisi kwamba mpaka nchini Japan watu hao wangeweza kuwatafuta tena.
Hakutaka kujiachia, hata alipokuwa akipita katika mitaa mbalimbali alionekana kuwa na hofu kubwa. Hakujiamini, hata siku ya kwanza kuingia chuoni hapo kila mtu alikuwa akimshangaa.
Waseda kilikuwa miongoni mwa vyuo vilivyokuwa na Wajapan wengi kuliko watu wa mataifa mengine. Japokuwa kulikuwa na wanafunzi zaidi ya elfu arobaini lakini kitu cha ajabu kabisa chuoni hapo hakukuwa na mwanafunzi mweusi, wengi walikuwa Wajapan, Wachina na Wazungu.
Ubaguzi ulitawala chuoni hapo, kila mwanafunzi mweusi alipotaka kujiunga na chuo hicho, alikataliwa kwa visingizio vingi lakini kwa kuwa Godwin aliombewa nafasi na Mzee Yokosoko ambaye aliheshimika sana hapo Tokyo, akajikuta akiingia na kuanza kusoma katika chuo hicho.
Hakukuwa na mtu aliyekuwa akimpenda, chuoni hapo, watu wengi walikuwa wakimtenga, hawakuamini kama Afrika kungekuwa na mtu aliyekuwa na akili, wengi walihisi kwamba Afrika ilijaza watu wa porini na hata sehemu walipokuwa wakiishi ilikuwa ni rahisi kukutana na simba.
Godwin alikuwa kimya, alijua kwamba kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakimbagua kwa sababu ya ngozi aliyokuwa nayo. Hakutaka kujali, kichwa chake kilifikiria zaidi masomo, alitaka kufanya kila liwezekanalo kwa ajili ya kuwa mtaalamu katika masuala ya kompyuta.
Hakutaka kucheza, hakutaka kuonyesha dharau katika masomo yake kitu kilichomfanya kuanza kusoma sana. Hakutaka kuishia darasani, alikesha akisoma, aliona kwamba kama angefanikiwa kufanya vizuri katika masomoo yake basi hata watu waliokuwa hapo chuoni wangemheshimu na kuacha kumbagua.
Hakupata muda mzuri wa kulala, muda mwingi alikuwa akijisomea, aliingia katika Tovuti ya Google na kutafuta mbinu mbalimbali kuhusu kompyuta. Hakutaka kushindwa kitu chochote kile, alisoma sana, kwa miezi miwili ya kwanza akafanikiwa kujua mambo mengi kuhusu kompyuta.
Akajifunza kutengeneza tovuti, akajifunza kutengeneza virusi kwa kutumia Java na C++. Alitaka kuwa mtu hatari kwa hiyo kukesha kwake ilikuwa ni kujifunza mambo mbalimbali, alitaka kuwa mkali kiasi kwamba kila mtu aogope.
Ingawa alikuwa akibaguliwa sana lakini akajikuta akianza kutengeneza urafiki na kijana mmoja wa Kijapan aliyeitwa Hilahima Takoshima. Huyu alikuwa kijana mrefu, msafi ambaye muda mwingi alikuwa akivaa miwani.
Alikuwa mcahngamfu, alipenda kuzungumza na watu wote chuoni hapo, alipomfuata Godwin na kuzungumza naye, akagundua kwamba kijana huyo alikuwa tofauti na watu wengine. Alijua kuongea, alionekana kama mtu aliyekuwa na vitu fulani kichwani mwake, Takoshima alishangaa, akahisi kabisa kwamba kama angeendelea kuwa kwenye urafiki na Godwin basi kungekuwa na vitu vingi ambavyo angejifunza kutoka kwake.
Huo ndiyo ukawa mwanzo wa urafiki wao. Wanafunzi wengi walimshangaa Takoshima kwamba aliwezaje kuwa na urafiki na mtu kama Godwin ambaye alikuwa mweusi, mwanaume ambaye kila siku watu walimuita Kegareta, neno la Kijapani lililomaanisha mchafu.
“それはいかに簡単ですか?” (imekuwaje kirahisi namna hii?) aliuliza jamaa mmoja huku akimwangalia Takoshima.
“何,” (nini?)
“なぜあなたは彼と話をしていますか?,” (kwa nini unazungumza naye?)
“彼は明るいので ,” (kwa sababu ana akili sana) alijibu.
Hilo ndilo lilikuwa jibu lake kila siku, hakuacha kuwaambia wenzake kwamba kila alipokuwa akizungumza na Godwin alimuona mtu wa tofauti kabisa, kijana huyo alionekana kuwa na akili sana kiasi kwamba kwa mtu yeyote ambaye angezungumza naye asingeacha kufanya hivyo.
Wengi walicheka, hawakuamini kama kungekuwa na mtu mweusi ambaye alikuwa na akili. Walizoea kuambiwa kwamba Waafrika wengi walikuwa wakiishi msituni hivyo hata kuoga hawakuwa wakioga na ndiyo maana miili yao ilikuwa michafu mno.
Pamoja na kuonyeshewa dharau zote chuoni hapo lakini Godwin hakutaka kujali, alichokuwa akikiangalia ni maisha yake ya mbele, angeishi vipi mpaka kufanikiwa kuwa vile alivyotaka kuwa kwa kipindi kirefu.
“Naomba namba ya siri,” alisema Godwin, alikuwa akimwambia Takoshima.
“Ipi?”
“Ya intaneti ya hapa chuoni.”
Takoshima akampa Godwin neno la siri ili aweze kuitumia intaneti ya chuoni hapo. Hakuwa na matumizi nayo bali alitaka kuifunga, hakutaka kuona chuoni hapo watu wakiendelea kuitumia intaneti hiyo, kwa sababu walikuwa wakimbagua, alitaka kuwaonyeshea kwamba alikuwa kiboko.
Hata kabla ya kufanya hivyo, alihitaji kusoma zaidi. Alipenda sana kompyuta na bahati nzuri nayo ikampenda, akafahamu vitu vingi sana na baada ya miezi minne, akaamua kuifunga intaneti ya chuoni hapo.
Hakuwa na pupa, alijua kwamba kama angeifunga kikawaida watu wangegundua hivyo kitu cha kwanza kilikuwa ni kutengeneza virusi vyake ambavyo alitaka viende vikashambulie mafaili kwenye server na kuyaficha kabisa.
Hilo halikuwa tatizo, ilikuwa kazi kubwa lakini alitakiwa kuifanya kwa nguvu zote. Hakuona kama kungekuwa na mtu ambaye angembabaisha katika masuala ya kompyuta kwa wakati huo, alisoma sana, na kwa kuwa alikuwa genius, hakupata ugumu wowote wa kulielewa somo hilo.
Siku hiyo alikesha kwenye kompyuta yake chumbani kwake, hakutaka kula, alikuwa bize kuangalia ni kwa namna gani angeweza kuficha mafaili yote ya chuo hicho yaliyokuwa kwenye server. Alihangaika kwa siku ya kwanza, hakufanikiwa, siku ya pili ikaingia lakini bado hakuweza kufanikiwa.
Hakutaka kumshirikisha mtu, alikuwa akifanya kazi kwa juhudi zote kwani aliamini kwamba angefanikiwa kwa kile alichokuwa akikifanya. Hakuonekana chuoni, wanafunzi walikuwa wakiuliziana mahali alipokuwa lakini hakukuwa na aliyejua.
Wengi wakahisi kwamba alihama chuo kama wengine mara baada ya kubaguliwa lakini kila walipozungumza na Takoshima aliwaambia kwamba Godwin alikuwepo na angerudi chuoni hapo siku si nyingi.
“Kwani amekwenda wapi? Afrika?” aliuliza mwanafunzi mmoja.
“Hapana! Yupo hapahapa Tokyo!”
“Mbona haji chuo?”
“Sijajua! Ila aliniambia kwamba yupo na kuna siku angekuja,” alisema Takoshima.
Alibaguliwa chuoni lakini kitu cha ajabu kabisa alikumbukwa mno kipindi hicho. Kila siku ilikuwa kazi ya Wajapan kuuliza mahali alipokuwa kwani haikuwa kawaida kwa mwanafunzi kukaa nyumbani kwa kipindi chote hicho.
Baada ya wiki moja na nusu kupita ndipo akarudi chuoni hapo, alikuwa na kompyuta yake ya mapajani, uso wake ulikuwa kwenye tabasamu kubwa. Siku zote hizo alikuwa na kazi kubwa ya kujaribu kuficha mafaili yaliyokuwa kwenye server ya chuo, aliifanya kazi hiyo kwa kujitoa sana, alitaka kumuonyesha kila mtu kwamba alikuwa mtu hatari sana katika masuala ya kompyuta.
Hakuzungumza na mtuu yeyote yule, alikuwa kimya mpaka alipokwenda darasani na kutulia ambapo baada ya muda rafiki yake, Takoshima akaingia na kuanza kuzungumza naye.
“Vipi?” aliuliza Godwin.
“Poa! Umesikia kilichotokea?” aliuliza Takoshima huku akimwangalia Godwin.
“Kitu gani?”
“Si unajua kwamba tulitakiwa tuwe na mitihani wiki ijayo?” aliuliza Takoshima.
“Ndiyo!”
“Nimesikia hakuna! Mafaili yote yaliyokuwepo kwenye server yameliwa na virusi,” alisema Takoshima pasipo kugundua kwamba kila kitu kilichotokea kilifanywa na Godwin.
“Mafaili yameliwa?”
“Ndiyo! Walimu wamechanganyikiwa, wamejaribu kuyarudisha, wameshindwa kabisa hivyo wamewapigia simu Mashatikana, kampuni moja ya watu wa kompyuta waje kufanya kila liwezekanalo mafaili yaruri,” alisema Takoshima maneno yaliyomfanya Godwin kutabasamu.
Kila mwanafunzi aliyesikia kwamba mafaili ya chuo yameliwa na virusi alishangaa, hawakutegemea kusikia kitu kama hicho, waliamini kwamba kwa sababu server hizo zilikuwa zimehifadhi data nyingi za chuo basi hata ulinzi wake ungekuwa mkubwa.
Hawakujua nini kilitokea bali walichosubiri ni kuona Kampuni ya Mashatikana ikifika chuoni hapo na kutatua tatizo lililokuwa limetokea.
Walimu wote walichanganyikiwa, mkuu wa chuo alitoka kijasho chembamba, hakujua ni kitu gani kilitokea, alijaribu kuwaita baadhi ya wanafunzi watatue tatizo lakini hawakufanikiwa, na mbaya zaidi hawakujua kama mtu aliyefanya hivyo alikuwa yule kijana wa Kiafrika waliyekuwa wakimuita mchafu kila kona chuoni hapo.
Siwezi kuficha mafaili halafu mtu akayaona, watayatafuta na hawatoyaona mpaka pale nitakapowasaidia,” alijisemea Godwin huku akitoa tabasamu pana.
Watu wa kampuni ya Mashatikana walipofika, moja kwa moja wakaelekea katika ofisi ya mkuu wa chuo ambapo akawachukua na kuwapeleka katika chumba kilichokuwa na server nyingi. Walipofika huko, wakachukua kompyuta zao, wakziwasha, wakaunganisha nyaya na kuanza kufanya kazi hiyo ya kuyarudisha mafaili hayo huku mkuu wa chuo na watu wengine wakiwa pembeni wakisubiri kuona kitu gani kingetokea.
***
Mkuu wa chuo alichanganyikiwa, hakujua zaidi kitu kilichokuwa kimetokea lakini alikuwa na uhakika kwamba watu waliokuja kutoka katika Kampuni ya Matashatikana kwa ajili ya kurudisha mafaili hayo wangefanikiwa kwa kiasi kikubwa zaidi.
Akawaangalia watu hao waliokuwa ndani ya chumba kile kilichokuwa na server, walikuwa bize na kompyuta zao, waliangalia kila kitu, walijua kwamba wao ndiyo waliokuwa wakitegemewa kurudisha mafaili yaliyokuwa yamefichwa. Kitu cha kwanza kabisa walichokigundua ni virusi ambavyo vilivyokuwa vimeficha mafaili hayo.
Virusi hivyo viliitwa Takeshi, vilikuwa virusi vyenye nguvu ambavyo havikuwahi kuonekana kabla. Wataalamu wale walibaki wakiangalia kompyuta zao, walikuwa na ant-virus lakini ilishindwa kabisa kuvishambulia virusi hivyo.
Hawakujua ni kitu gani walitakiwa kufanya. Wakaingia online na kuchukua ant-virus nyingine lakini zote hizo zilishindwa kuvishambulia virusi vile vilivyokuwa vimeshikilia mafaili ya chuo hicho.
Walifanya kazi hiyo kwa saa kumi na moja, kila mmoja alichoka, walihangaika kwa saa nyingi hizo lakini hawakufanikiwa kile walichokuwa wakikihitaji na mwisho wa siku kumwambia mkuu wa chuo, Bwana Tamashi kwamba hawakuwa na jinsi, chuo kilitakiwa kuingia gharama kwa ajili ya kuwaita watu wengine, hasa Wamarekani ambao waliaminika kwa ajili ya kupambana na virusi wagumu kama hao.
“Imeshindikana vipi?” aliuliza mkuu wa chuo, alichanganyikiwa, alichohisi ni kwamba kazi ilikuwa nyepesi lakini mwisho wa siku wakagundua kwamba kazi hiyo ilikuwa ngumu zaidi ya walivyokuwa wakifikiria kabla.
“Ni kazi ngumu!”
“Ugumu wake upo wapi?”
“Kuna virusi vipya. Kuna mtu alivitengeneza na kuvituma katika server yenu iliyohifadhi mafaili,” alisema mtaalamu mmoja kutoka katika Kampuni ya Mashatikana.
“Mtu gani?”
“Hata sisi wenyewe hatujui! Cha msingi hebu jaribuni kuwaita wataalamu wengie kwani kama tukiendelea kuwaondoa, hawa virusi wataingia kwenye kompyuta zetu, na wanaonekana ni hatari sana,” alisema jamaa huyo.
Wakaondoka pasipo kufanikiwa kile kilichowapeleka chuoni hapo. Tamashi alichanganyikiwa, ilikuwa ni lazima afanye juu chini ili mafaili yaliyokuwa yamefichwa yapatikane kwani ndiyo yalihifadhi kila kitu kilichokuwa kimetokea chuoni hapo na mitihani yote chuoni hapo ilihifadhiwa humo.
Akawasiliana na kampuni ya Microsoft ya nchini Marekani, akawaelezea tatizo alilokuwa nalo na watu hao kuahidi kwamba wangefika nchini Japana baada ya siku moja tu hivyo walitakiwa kusubiri. Hilo halikuwa tatizo, aliamini kwamba Microsoft wangeweza kulitatua tatizo hilo kwani ilikuwa moja ya kampuni iliyokuwa ikitengeneza programu nyingi zikiwemo ant-virus iitwayo Microsoft Security Essential.
Baada ya siku moja wataalamu hao wakafika chuoni hapo na kuambiwa kila kitu kilichokuwa kimetokea. Hilo halikuwa tatizo, wakaomba kupelekwa katika chumba kilichohifadhi server za chuo hicho na walipofika huko wakafanya kama walivyofanya watalaamu wa Mashatikana.
Kazi yao kubwa ilikuwa ni kucheza na kompyuta zao, waliviona virusi vya Takeshi vilivyokuwa vimeshikilia mafaili hayo. Walichokifanya ni kuingiza ant-virus zao kwa ajili ya kupambana na virusi hivyo lakini kitu kilichowashangaza zaidi ni kwamba hawakuweza kufanikiwa.
“Tunamuhitaji mtu aliyetengeneza virusi hivi,” alisema Brown, mmoja wa wanaume waliotoka katika Kampuni ya Microsoft.
“Wa nini?”
“Tuzungumze naye. Hii ni biashara kubwa sana, kama tukionana naye natumaini tunaweza kufanya jambo fulani,” alisema Brown huku akionekana kuwa na uhitaji wa kuonana na mtu huyo.
Hakukuwa na mtu aliyejua kama aliyetengeneza virusi hivyo alikuwa Godwin. Mwenyewe alitulia, alikuwa akifuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Hakumwambia mtu yeyote yule, kila kilichotokea kilikuwa siri kubwa.
Aliwaona watu walivyokuwa wakihangaika. Kila mwalimu shuleni hapo alichanganyikiwa kwani mitihani yao waliyokuwa wameitunga haikuwa ikionekana. Shule haikufanya usajili tena kwa sababu fomu zote zilikuwa humo na wanafunzi walitakiwa kuingia kwenye mtandao wa chuo kwa ajili ya kujaza fomu hizo.
Taarifa za kufichwa kwa mafaili ya chuo hicho zikaanza kusambaa jijini Tokyo, wataalamu wengi wa kompyuta walipopata taarifa hizo wakafurahi na kuona kwamba hiyo ndiyo ilikuwa nafasi yao ya kwenda kuvuna pesa.
Wengi wakajitolea na kwenda huko lakini bahati mbaya kwao ni kwamba kila walipokuwa wakifika kwa ajili ya kufanya utundu wao na kuyarudisha mafaili walishindwa na hivyo kurudi walipotoka.
Ndani ya wiki nzima chuo kilikuwa kikihangaika kurudisha mafaili hayo. Haikuwa kazi nyepesi hata kidogo, walijitahidi usiku na mchana lakini hakukuwa na mtu aliyekuwa na uwezo wa kupambana na virusi hao.
“Mkuu! Kuna mtu muhimu inatakiwa tuwasiliane naye,” alisema jamaa wa kitengo cha IT kutoka chuoni hapo.
“Yupi?”
“Kuna mzee anaitwa Thierry kutoka nchini Ufaransa, ni mtu hatari sana ambaye kama kweli akifika chuoni hapa, nina uhakika atafanikiwa kwani ana ujuzi wa hali ya juu sana,” alisema jamaa huyo.
“Hakuna shida.”
Hawakuwa na jinsi, walikuwa wakiingia gharama lakini mwisho wa siku walitaka kufanikiwa kwa kile walichokuwa wakikihitaji. Mawasiliano yakafanyika, wakampata Thierry ambaye kitu cha kwanza kabisa ni kutaka kukatiwa tiketi yake, hilo halikuwa tatizo, akakatiwa na kuelekea huko.
Godwin aliposikia mwanaume huyo alikuwa njiani akija chuoni hapo alishtuka, alimfahamu, aliujua uwezo wake, alikuwa mtu hatari sana katika kupambana na watu waliokuwa wakijifanya kuwa hatari katika kompyuta.
Thierry alikuwa mwanaume aliyekuwa amewakamatisha wezi wengi wa mitandao hasa wale waliokuwa wakifanya uhalifu katika mashine za ATM nchini Ufaransa na wakati mwingine mpaka Marekani. Wengi walimchukia kwa kuwa alizika madili ya watu wengi, na wengi walimtafuta wamuue lakini walimkosa.
Hakutaka kuajiliwa, kazi yake kubwa ilikuwa ni kuitwa kufanya kazi huku na kule, kwa lugha nyepesi ya mtaani tungemuita mchezaji wa ndondo. Alipokuwa akiitwa sehemu kwa ajili ya kufanya kazi yake alifanya kwa moyo mmoja, tena kwa nguvu kubwa na kufanikiwa kwa asilimia mia moja.
“Kwa huyu jamaa tutafanikiwa,” alisema Takoshima, alikuwa akimwambia Godwin pasipo kujua maneno hayo yalimuumiza mwanaume huyo kiasi gani.
“Ataweza?”
“Ni mtu hatari sana. Subiri afike, hutoamini,” alisema Takoshima huku uso wake ukiwa na tabasamu pana.
Siku iliyofuata Thierry akaingia ndani ya chuo hicho. Kila mtu aliyemuona akawa na matumaini kwamba mwanaume huyo angefanikiwa kwani kwa jinsi alivyokuwa akiifahamu kompyuta, alivyokuwa akicheza na data, waliamini kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wa matatizo.
Akapelekwa katika chumba kilichokuwa na server, alipofika huko, akaanza kuangalia huku na kule, alionekana kama mtu aliyekuwa na mbwembwe nyingi. Akawaambia watu wote watulie kwani ndani ya dakika chache tu mafaili yangeweza kuonekana.
Akachukua kompyuta yake ndogo, akachukua nyaya kutoka katika server na kuunganisha katika kompyuta yake na kuanza kuangalia huku na kule. Muda wote alikuwa akitabasamu, aliona kazi iliyokuwa mbele yake kuwa nyepesi sana na wakati mwingine alikuwa akishangaa kwamba kwa nini watu walishindwa kazi hiyo na wakati ilikuwa nyepesi sana?
“Ni kazi nyepesi mno. Naombeni soda kwanza ninywe,” alisema huku akiwa ameachia tabasamu, tena akakunja na nne kabisa.
Haraka sana soda ikaletwa na kuanza kunywa taratibu, alikuwa makini kwa kila alichokifanya, aliviona virusi vilivyoshikilia mafaili hayo, vilikuwa virusi hatari ambavyo wakati mwingine mwenyewe aliviogopa.
Aliingia kwa mbwembwe, muda wote tabasamu pana usoni lakini kadiri muda ulivyokuwa ukizidi kwenda mbele akaanza kubadilika, tabasamu likaanza kupotea taratibu, uso wake ukabadilika, na kilichomshangaza kila mmoja humo ndani ni kwamba mzee huyo akaanza kutokwa na kijasho chembamba hali iliyoonyesha kwamba hata yeye pia, pamoja na utaalamu wakee mkubwa, alianza kuchemka kuyarudisha mafaili hayo.
“Mmh! Huyu aliyetengeneza virusi hivi alitengeneza kwa C++ au java? Mbona naona kama ni virusi ambavyo havijawahi kutengenezwa katika ulimwengu huu?” alijiuliza huku akiikodolea macho kompyuta yake, wakati mwingine alihisi joto kali ingawa ndani ya chumba hicho kiyoyozi kilikuwa kikipiga kwa nguvu kabisa.
***
“Is it done?” (imekamilika?) aliuliza mkuu wa Chuo, Bwana Tamashi huku akimwangalia Thierry aliyeonekana kuweweseka.
“Who did this?” (nani alifanya hivi?)
“We don’t know yet! Is there any possibility of working again?” (bado hatujajua! Kuna uwezekano wa kufanya kazi tena?) aliuliza Tamashi.
“Just give me some minutes,” (nipe dakika kadhaa)
Kulikuwa na dalili zote za Thierry kushindwa kuyarudisha mafaili yale, alihangaika kwa nguvu zote lakini hakuwa amefanikiwa, hakutaka kuwaweka wazi, alikuwa akijulikana kwa kuwakomesha wezi wa mitandao, alijua ‘programing na network’ lakini kuyarudisha mafaili yaliyokuwa yamefichwa na virusi vile ilikuwa kazi ngumu kupita kawaida.
Alichoka mwili, alichoka kiakili, alihitaji kupumzika na hata soda ambayo aliiagiza kwa mbwembwe hakuwa ameimaliza, akatulia huku mtu mzima akitokwa na kijasho chembamba.
Mkuu wa chuo, Tamashi akaona kabisa kwamba kazi ilishindikana, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya, hakujua kama kungekuwa na mtu ambaye angeweza kuyarudisha mafaili yale. Kama Thierry, mwanaume aliyejulikana kwa utaalamu wake wa kompyuta duniani alishindwa kuyarudisha, ni nani angeweza kufanya kazi hiyo?
Tamashi aliona dalili za chuo hicho kupata hasara, hakutaka kuona hilo likitokea, serikali ya Japan haikutaka kukubali, kwa kuwa chuo hicho kilikuwa sehemu ya vyuo vya serikali, wakawaita wataalamu kufanya kazi lakini kila aliyefika alivishangaa virusi hivyo, hawakuamini kama kulikuwa na virusi vya kuficha mafaili kwa uwezo mkubwa kama huo.
Wakati kila kitu kikiendelea, Godwin alikuwa ametulia, alitaka kuona mwisho wa yote ungekuwa nini. Alisumbuka kutengeneza virusi hivyo, alishinda usiku kucha kwa siku kadhaa, hakuona kabisa kama kungekuwa na watu ambao wangeweza kuyafichua mafaili yaliyokuwa yamefichwa kwa ufundi mkubwa.
Siku zikaendelea kukatika, wataalamu wote wakashindwa na mwisho wa siku chuo kutangaza kwamba walishindwa, na kama kungekuwa na mtu wa kuyarudisha mafaili hayo, angelipwa kiasi cha dola laki moja (zaidi ya milioni mia mbili) kama pongezi kwake.
“Mimi nataka nikayarudishe! Watanikubalia?” aliuliza Godwin huku akimwangalia rafiki yake, Takoshika.
“Wewe?”
“Ndiyo! Au watanikatalia?”
“Mmh! Utaweza?”
“Unanionaje? Nitaifanya kazi hiyo Jumatatu,” alisema na kuondoka.
Takoshima hakutaka kufuatilia sana, alijua kwamba Godwin asingeweza kuyarudisha mafaili hayo, hivyo akapuuzia japokuwa aliwaambia marafiki zake wengine kama utani kwamba Godwin alitaka kujarabu kuyarudisha mafaili hayo.
Kila mtu aliyesikia akacheka, walimdharau, waliona ni kitu kigumu kwa mtu kama yeye kuyarudisha mafaili hayo. Kama Wazungu, Wajapan na Wachina walishindwa kuyarudisha, ilikuwaje kwa mtu mweusi kama yeye.
Kwa chuoni hapo ilikuwa ni kama kichekesho, kila mtu aliyesikia kwamba Godwin naye alikuwa miongoni mwa watu waliotaka kujaribu walicheka kupita kawaida, hawakuona kama kijana huyo angeweza kubadilisha matokeo.
Japokuwa kulikuwa na watu wengi waliotaka kujaribu lakini gumzo alikuwa Godwin na hata alipokuwa akienda chuo kila mmoja alikuwa akimjadili kwamba angewezaje kuyarudisha mafaili na wakati kulikuwa na watu wengi, tena wataalamu waliokuwa wameshindwa kufanya hivyo.
Hakutaka kujali, alijua fika kwamba kazi ilikuwa nyepesi sana. Siku ambayo alitakiwa kufanya hivyo ilipofika, akaelekea katika ofisi ya mkuu wa chuo na kuanza kuzungumza naye. Alimwambia wazi kwamba alitaka kufanya kazi hiyo na kuwashangaza watu wote ambao walihisi kwamba hawezi kufanya lolote lile.
“Hapana! Unaweza kuharibu hata server zenyewe,” alisema Tamashi, yeye mwenye hakumwamini kabisa Godwin kama angeweza kufanikiwa kwa kile alichokuwa akitaka kukifanya.
“Unaniamini au huniamini?” aliuliza Godwin huku akimwangalia Tamashi.
“Unajua ni watu wangapi wameshindwa?”
“Ni wengi sana. Ninataka nimdhihirishie kila mtu kwamba ninaweza,” alisema Godwin.
“Kwamba unawashinda mpaka wataalamu wa serikali?”
“Unawahusudu sana? Ni kazi ndogo mno. Andaa pesa yangu,” aliseema Godwin huku akimwangalia mkuu wa chuo usoni.
Moyo wake ulimwambia wazi kwamba Godwin hakuweza kuifanya kazi ile, ilikuwa vigumu kwa mtu kama yeye kuifanya na wakati kulikuwa na watu wengi waliokuwa wameshindwa. Hilo hakujali, aliendelea kumwambia mkuu huyo kwamba kama angepewa nafasi basi ilikuwa ni lazima kuifanya kazi hiyo kwa mafanikio makubwa.
Kwa kuwa kulikuwa na wengi waliojaribu na kushindwa, mkuu wa chuo hakuwa na jinsi, akampa nafasi Godwin kujaribu kufanya kile alichotaka kufanya.
“I wanna show them how to do it,” (nataka niwaonyeshe namna ya kulifanya jambo hili) alijisemea wakati akiingia ndani ya chumba kilichokuwa na server.
Wanafunzi wote walikuwa wakisikilizia nje, kila mmoja aliamini kwamba Godwin asingeweza kuyatoa mafaili yale yaliyokuwa yamefichwa. Kwa kuwa alitaka kuwaonyeshea kwamba alikuwa na uwezo wa kuifanya kazi ile, alipoingia tu, akavuta kiti, akatulia na kukunja nne.
“Mbona ni kazi nyepesi sana!” alisema Godwin huku akiwaangalia vijana wa IT waliokuwa humo ndani.
“Wenzako walisema hivyohivyo!”
“Hebu muiteni mkuu wa chuo!”
“Wewe wa nini? Si ufanye tu hiyo kazi!”
Hakutaka kufanya kazi hiyo pasipo mkuu huyo kuwepo ndani ya chumba hicho. Alikumbuka jinsi alivyomdharau na kumuona hajui kufanya chochote kwa kuwa tu alikuwa mtu mweusi. Siku hiyo ilikuwa ni siku maalumu ya kuwaonyeshea watu wote chuoni hapo kwamba kwamba watu weusi hawakuwa watu wa mchezo mchezo.
Mkuu huyo alipopewa taarifa kwamba alihitajika, akaanza kuelekea huko, hakupenda kwenda kwa kuwa tangu aanze kuzungumza na Godwin hakuwahi kumwamini, hakuona kama kijana huyo alikuwa na uwezo wowote ule.
Alipoingia ndani ya chumba kile, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuuliza kama kazi ilifanyika kwani alikuwa na mambo mengi ofisini kwake. Godwin akamwambia kwamba alitakiwa kutulia kwani kulikuwa na kazi ambayo alitaka kuifanya huku mkuu huyo akiwa ndani ya chumba hicho.
“Kwa hiyo haiwezi kufanyika bila mimi kuwepo?” aliuliza Tamashi.
“Yeah! Ngoja nikuonyeshee mbele yako kwamba siku nyingine hutakiwa kuwadharau watu weusi,” alisema Godwin na kuanza kuifanya kazi hiyo.
Haikuwa kazi ngumu kwake, yeye ndiye aliyetengeneza virusi hivyo na alijua jinsi ya kupambana navyo. Kila mmoja alikuwa kimya akimwangalia, hakuonekana kuwa na wasi, alikuwa akiifanya kazi hiyo huku wakati mwingine akiimba Wimbo wa Where is the Love wa Black Eyed Peas.
Hakuchukua muda mrefu, alitumia dakika kumi tu, akasimama na kuwaambia kwamba kazi waliyokuwa wamempa alikuwa ameifanikisha kwa mafanikio makubwa. Mkuu wa chuo, Tamashi hakuamini, akaiwasha kompyuta moja ndani ya chumba kile kwa lengo la kuangalia kama mafaili yalikuwa yamerudi kweli, alipofungua tu mtandao wa chuo, macho yake yakatua kwa mafaili yote yaliyokuwa yamefichwa.
“Haiwezekani! Mafaili yamerudi!” alisema huku akishtuka, tabasamu pana likaonekana usoni mwake, hapohapo akageuza macho yake kumwangalia Godwin, kijana huyo hakuwepo ndani ya chumba hicho.
Wanafunzi walimuona Godwin akitoka ndani ya chumba kile, alionekana kama mtu aliyekuwa na haraka, alikuwa akitembea kwa mwendo wa kasi, kwa jinsi alivyoonekana, kila mmoja akahisi kwamba alikuwa amechemka kama wengine walivyokuwa wamechemka.
Wengi wakaanza kucheka na kumpuuzia, walimuona mjinga fulani ambaye alitaka kufanya jambo chuoni hapo kwa lengo la kutafuta kiki ili azungumziwe kwa mazuri na si kwa mabaya kama ngozi yake ilivyokuwa ikijionyesha.
Wakati Godwin akiwa amefika mbali kabisa, mlango ukafunguliwa na mkuu wa chuo kutoka. Alionekana kuwa mtu mwenye furaha, alikuwa akiangalia huku na kule kama alikuwa akimtafuta mtu au kitu fulani. Akamuona Godwin akiwa mbali kabisa akitokomea, akamuita kwa sauti kubwa, watu wote wakashtuka na kumwangalia mkuu huyo.
Hawakujua kitu gani kilitokea lakini kijana mwingine kutoka katika chumba kile alipoufungua mlango na kupayuka kwamba mafaili yalikuwa yamerudi, kila mmoja akashangaa.
“Mafaili yamerudi! Mafaili yamerudi!” alisema kijana huyo huku akipiga kelele zilizowafanya watu kujiuliza, je, ni Godwin ndiye aliyeyarudisha mafaili hayo au kulikuwa na mtu mwingine.
Japokuwa mkuu wa chuo alikuwa akiita kwa sauti na Godwin kumsikia vilivyo hakutaka kusimama, hakuangalia nyuma, macho yake yalikuwa mbele, alipiga hatua ndefu tena za harakaharaka kusonga mbele na kupotea kabisa.
Gumzo kubwa chuoni hapo lilikuwa ni Godwin tu, kila mtu akaanza kumzungumzia kwa kumsifia na wengi walishangaa, iliwezekanaje mtu mweusi aweze kufanya jambo ambalo watu weupe walihangaika nalo kwa siku nyingi tu.
Kila mmoja akahisi kwamba Godwin alikuwa na kitu cha pekee kichwani mwake, walitaka kujua mengi zaidi, walitamani kuujua uwezo wake ulikuwa ni wa namna gani.
“Is this Ben Carson Jr?” (huyu ni Ben Carson mdogo?) aliuliza Mjapani mmoja huku akishangaa, kwa kile alichokifanya chuoni hapo, kila mtu alistaajabu.
Je, nini kitaendelea?
Ubize umekuwa mkubwa.