Dunia haina usawa

Dunia haina usawa

SEHEMU YA 64

Aliipokea simu hiyo na kuanza kuongea na mtu huyo ambaye alimwambia kwa kifupi kwamba kulikuwa na taarifa mbaya kutoka nchini humo.
“A bad news?” (taarifa mbaya?) aliuliza huku akionekana kushtuka.

“Yes mom!” (ndiyo mama)
“What is it?” (habari gani?) aliuliza huku kijasho kikianza kumtoka na mwili kumtetemeka.
“Please calm down,” (tulia tafadhali)
“Just tell me about it….please tell me,” (niambie tu kuhusu hiyo habari….niambie tafadhali) alisema Rosemary kwa sauti iliyojaa hofu kubwa.

*** Wananchi wengi walijeruhiwa vibaya kwa sababu tu waliamua kuandamana kwa kuitaka mahakama kumuachia huru mwandishi mashuhuri Matamshi ambaye alikuwa ameshikiliwa kwa tuhuma za kuingiza madawa ya kulevya nchini Tanzania.

Baada ya kupigwa sana na polisi, huo ndiyo ulikuwa mwisho wa maandamano hayo, Kwa siku hiyo, kesi hiyo ilisikilizwa na mwandishi huyo kurudishwa rumande na hivyo kutakiwa kurudi mahakamani hapo baada ya wiki mbili.

Hiyo ilikuwa kesi nzito iliyotingisha sana katika vyombo mbalimbali vya habari, kwenye kila kona, watu walikuwa wakiizungumzia kesi hiyo, magazeti hayakutoka bila kuandika kuhusu tuhuma hizo nzito, waandishi wa habari wakaungana na hata kwenye televisheni, habari kubwa ilikuwa ni ya mwandishi Matamshi huku kila mmoja akiituhumu serikali kwa kushindwa kumsikiliza mtu huyo alipokuwa akiwaambia ukweli kwamba hakusafirisha madawa ya kulevya.
 
SEHEMU YA 65

“Basi apimwe kwa mkemia mkuu wa serikali kuona kama anatumia madawa hayo,” alishauri waziri mkuu.
Serikali ilikuwa na presha kubwa, kwa jinsi wananchi walivyoonekana kuchachamaa walijua kabisa kwamba suala hilo lilionekana kuwa dogo lakini kwa upande wa pili lilikuwa kubwa mno.

Walitaka kumuachia mwanaume huyo huru lakini hawakutaka kumuachia hivihivi bali kilichofanyika ni kumpima na mkemia mkuu kujiridhisha kwamba Matamshi hakuwa akitumia madawa ya kulevya.

“Kwa hiyo?”
“Kesi iahirishwe, kwanza akae rumande hata miezi sita halafu ndiyo aachwe huru,” alisema rais alipokuwa akizungumza na waziri mkuu.

“Sawa.”
Hilo ndilo lililofanyika, Matamshi aliendelea kusota rumande na kila alipokuwa akipelekwa mahakamani, kesi yake iliahirishwa na kutakiwa kusikilizwa tena siku nyingine.

Alihangaika, waandishi waliendelea kumtetea mwandishi mwenzao kwa kutumia kalamu zao na baada ya miezi sita, mwandishi huyo akashinda kesi kwa kuonekana kwamba kweli si yeye aliyekuwa akiingiza madawa ya kulevya.

“Umeshinda kesi, ukijaribu kuishitaki serikali, utapotea katika mazingira ya kutatanisha,” alisikika mwanaume kwenye simu, alikuwa akimwambia Matamshi.
“Sawa. Sitofanya hivyo!” alisema Matamshi huku akionekana kuogopa, kwa jinsi serikali ilivyokuwa na mkono mrefu, alijua tu kwamba kama asingefanya kile walichokitaka, kweli wangempoteza.

Je, nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 66

Baada ya familia yake kurudi nchini Marekani, Mapoto hakuonekana kuwa na furaha hata kidogo, upweke ukamuingia kwani aliizoea familia yake na alitamani kuwa nayo miaka yote.

Alikuwa akiwasiliana nao kama kawaida, aliwapenda na kwake walikuwa kila kitu. Aliendelea kumsisitiza mke wake kwamba watoto wao walitakiwa kupata elimu bora kwa ajili ya maisha yao ya baadaye na ndiyo maana baada ya kufika nchini Tanzania, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuwapeleka katika shule ya watu wenye fedha na kuwataka wasome hapo.

“Najua elimu ndiyo kitu pekee ambacho kitakuja kuwasaidia hapo baadaye,” alisema Mapoto wakati akiongea na mkewe kwenye simu.
“Nitahakikisha wanapata elimu bora,” alisema Rosemary.
Maisha yaliendelea kama kawaida, kila siku alikuwa na jukumu la kuamka asubuhi na mapema na kuelekea ofisini mwake na kufanya kazi zake kama kawaida.

Siku ya Jumatatu ya tarehe 07/10/2002, kama kawaida yake Mapoto akaamka asubuhi na mapema kwa ajili ya kwenda kazini. Siku hiyo alitaka kuwasiliana na mwenyekiti wa Chama cha Tanzania National Party, Edward na kumwambia mpango wake wa kurudi nchini Tanzania mwezi wa kumi na mbili kwa ajili ya kufanya kampeni za uchaguzi mkuu wa Tanzania uliotakiwa kufanyika mwezi Juni mwaka 2003.

Alipokuwa ndani ya gari, akampigia simu na kumwambia kwa kifupi juu ya kitu ambacho walitakiwa kuzungumza kwa kirefu kwani asingeweza kuendelea kubaki nchini Marekani na wakati alikuwa na nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi nchini Tanzania na kuwa rais wa nchi hiyo.
“Sawa. Ukifika ofisini niambie. Huku kwetu ni jioni sasa nafikiri nitapata muda mzuri wa kuongea nawe,” alisema Edward.

“Haina shida.”
Baada ya kuzungumza kwa kifupi, akaendelea na safari, hakuchukua muda mwingi akafika ofisini ambapo kitu cha kwanza kabisa kukifanya kilikuwa ni kuinua simu yake ya mezani na kumpigia Edward.

Siku hiyo walizungumza mambo mengi, walipanga vitu mbalimbali juu ya kuiteka tena Tanzania, kuwaambia wananchi kwamba huo ndiyo ulikuwa muda sahihi wa ukombozi.
 
SEHEMU YA 67

Bado Watanzania walihitaji mabadiliko, kila mtu alijiandikisha kwa ajili ya kupiga kura kwani kitendo cha kuwa na kadi ya kupiga kura ilimaanisha kwamba ungepiga kura na kumchagua kiongozi uliyekuwa ukimtaka, na wengi waliaidi kumwangusha Bokasa na kumchagua kiongozi wa chama pinzani.

“Mwaka ujao tunashinda, cha msingi ni kuziba mianya yote ya wizi wa kura na kuwataarifu watu juu ya upigaji kura ili tusije kuchezewa mchezo kama mwaka ule,” alisema Edward.

Alifanya kazi zake kama kawaida, ilipofika mchana, muda wa kurudi nyumbani akaingia ndani ya gari lake na kuanza kurudi nyumbani. Wakati gari likiwa linaingia katika barabara kubwa ya Lansdowne, ghafla wakakutana uso kwa uso na gari moja kubwa ambalo lililigonga gari lao, na kwa sababu lilikuwa kwenye mwendokasi, gari la balozi Mapoto likaharibiwa vibaya kiasi kwamba ilikuwa ni vigumu kuamini kama ndani ya gari hilo kungekuwa na mtu ambaye angetoka salama.

“Mungu wangu!” alisema mwanaume mmoja aliyekuwa kwenye gari jingine.
Kila mtu alishtuka, ajali iliyokuwa imetokea ilikuwa mbaya mno, gari la balozi Mapoto liliharibika vibaya na watu waliposogea kuangalia, kulitapakaa damu na hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa akitingishika kuonyesha kwamba alikuwa hai.

Ulikuwa ni uzembe mkubwa mno kwani gari la balozi Mapoto lilikuwa katika njia yake lakini gari kubwa ambalo liliwagonga halikuwa kwenye njia yake, lilihama kutoka kati magari yanayoelekea upande wa Mashariki na kuhamia katika upande wa magari yanayokwenda upande wa Magharibi.

Ilikuwa ni ajali mbaya mno, kila mmoja aliyeiona, aliogopa, alitetemeka kwani katika histori ya ajali za barabarani hasa katika Jiji la New York, hakukuwa na ajali mbaya ya magari kugongana ambayo iliwahi kutokea kama ilivyokuwa ajali hiyo.
 
SEHEMU YA 68

Hakukuwa na sababu ya kuyasubiri magari ya wagonjwa yafike mahali hapo, watu waliokuwa na magari binafsi wakajitolea kuibeba miili ile iliyokuwa ndani ya gari lile na kuipeleka katika Hospitali ya St. Monica Medical Centre ambayo haikuwa mbali kutoka mahali ilipotokea ajali hiyo.

“Vipi?” aliuliza nesi mara baada ya kuipokea miili hiyo.
“Ajali!”
“Ya ndege?” aliuliza huku akionekana kushangaa kwani kwa jinsi miili ile ilivyokuwa, ilikuwa vigumu kuamini kama ilikuwa ni ajali ya gari.

“Hapana! Gari!”
“Gari?”
“Ndiyo!”
Watu waliokuwa hospitalini hapo hawakuamini kile walichokuwa wakikiona, waliogopa, picha iliyokuwa ikionekana ilimtisha kila mmoja. Ni kweli kwamba waliwahi kuona ajali mbaya zilizokuwa zikitokea lakini kwa miili ile waliyokuwa wakiiona, walijua kabisa kwamba hiyo ilikuwa ajali mbaya ambayo hawakuwahi kuiona jijini hapo.

Miili ile ikachukuliwa, haikupelekwa katika chumba cha upasuaji, moja kwa moja ikapelekwa mochwari kwani hakukuwa hata na mtu mmoja aliyeonekana kuwa mzima.
Ilikuwa ni vigumu kuzitambua maiti zile ila kilichowafanya watu kugundua kwamba alikuwa ni balozi wa Tanzania, Mapoto ni namba za gari alizokuwa akizitumia.

“Kumbe ni balozi!”
“Huyu aliyekufa?”
“Ndiyo!”
Polisi walikuwa na taarifa hiyo, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuwasiliana na serikali ya Tanzania na kuwaambia kile kilichokuwa kimetokea lakini pia ilikuwa ni lazima kuitaarifu familia yake na hivyo kuchukua simu ya balozi MApoto na kumpigia mkewe kwa ajili ya kumpa taarifa.

“Mumeo amefariki!” ilisikika sauti ya upande wa pili.
“Mume wangu amefariki?”
“Ndiyo!”
Miguu ya Rosemary ikakosa nguvu, hapohapo akakaa chini na kuanza kulia kama mtoto.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom