SEHEMU YA 63
Mapoto alipokea taarifa hiyo kutoka kwa mke wake, alishtuka, hakutegemea kupta taarifa kama hiyo. Aliwapenda watoto wake, alitaka wapate elimu bora ambayo ingewafanya kuwa watu fulani huko baadaye, walikaa nchini Marekani kwa miaka minne na muda huo ulikuwa ni wa kurudi nchini Tanzania.
Hakupenda lakini hakuwa na jinsi, akamwambia mke wake kwamba Godwin na Irene wangerudi nyumbani nchini Tanzania haraka iwezekanavyo na hivyo ndivyo ilivyofanyika, wakarudishwa.
Huko, kwa kuwa bado familia ilikuwa na pesa, wakapelekwa katika shule ya watoto wa matajiri kwa ajili ya kusoma darasa la saba na kuendelea. Uwezo wao haukushuka, bado waliendelea kuongoza darasani kitu ambacho kila mwalimu alikuwa akiwashangaa.
Wazazi wao waliwekeza katika elimu yao, waliamini kwamba ili watoto wawe na maisha mazuri ilikuwa ni lazima wasome katika shule nzuri na kufanya vizuri na ndiyo maana walifanya kila liwezekanalo kuhakikisha watoto wao wanapata elimu bora.
“Do you still want to be a pastor?” (bado unataka kuwa mchungaji?) aliuliza Rosemary huku akimwangalia Godwin.
“Yes! I will preach the world of God around the globe,” (Ndiyo! Nitalihubiri neno la Mungu dunia nzima) alijibu Godwin.
Hakuwa na ndoto nyingine maishani mwake zaidi ya kuwa mchungaji. Alimpenda Mungu, alitaka kumtumikia katika maisha yake yote hapa duniani.
Kila siku alikuwa mtu wa kusali tu, alipenda kujifungia chumbani kwake na kusali kama kawaida. Shuleni alipokuwa akisoma, kwenye begi lake ilikuwa ni lazima kuwa na Biblia, pale alipokuwa akipata nafasi alikuwa akisoma kitu kilichowafanya wanafunzi wengine wa darasa la saba kumuita kwa jina la mchungaji.
Rosemary alifarijika, moyo wake ulikuwa na furaha tele, alimpenda sana mtoto wake, Godwin. Kitendo cha kushika sana dini kilimfanya kuwa na mapenzi makubwa kwake.
Siku ziliendelea kukatika. Baada ya watoto wake kumalizia mtihani wa darasa la saba, siku moja akiwa sebuleni amekaa na watoto wake wakiangalia televisheni, akapigiwa simu na mtu ambaye hakumfahamu aliyekuwa nchini Marekani.