Dunia haina usawa

Dunia haina usawa

SEHEMU YA 72

“Wewe ni kama mimi. Huu ni msumari wa moto moyoni mwangu na sidhani kama utaweza kupoa. Kweli mapoto amekufa! Kweli nimeamini Mungu anataka Watanzania tuendelee kuteseka milele na milele, sijui tumemkosea nini sisi,” alisema mwanamke mmoja, kama alivyokuwa mwanaume yule wa kwanza, hata naye alikuwa na maumivu makali moyoni mwake.

Nyumbani kwake kulikuwa na idadi kubwa ya watu, vilio vilitawala kila kona, kila aliyekuwa mahali hapo sura yake ilionyesha majonzi makubwa, hakukuwa na aliyeamini kama huo ndiyo ulikuwa mwisho wa mwanaume huyo aliyedhamiria kuibadilisha Tanzania.

Watoto wake, Godwin na Irene walilia mno, mioyo yao iliwauma kupita kawaida, walionekana kuwa na huzuni mno. Japokuwa ndugu zao wengine walikuwa wakiwabembeleza na kuwataka kunyamaza lakini hawakunyamaza, waliendelea kulia zaidi.

Kila mtu aliyekuwa nyumbani hapo alikuwa akizungumza lake, wengine walisema kwamba inawezekana marehemu aliuawa lakini watu wengine walibisha hilo kutokana na mazingira ya kifo jinsi yalivyokuwa.

“Kuna gari lilifika na kuligonga gari lake, unadhani kuna mtu atakuwa amemuua?” aliuliza jamaa mmoja.
“Huwezi kujua lakini!”
“Hakuna kitu kama hicho! Halafu nchi kama Marekani, utapanga vipi mipango ya kumuua mtu kwa ajali halafu nchi isijue? Ni ajali, tukubali kwamba ni ajali na tugange mambo yajayo,” alisema mwanaume mwingine huku akiwaangalia watu wachache waliokuwa wamemzunguka.

Hicho kilikuwa kipindi kigumu mno, kilikuwa kipindi cha masikitiko kwa kila mtu aliyetamani mabadiliko nchini Tanzania. Msiba huo ulihudhuriwa na watu wengi, viongozi mbalimbali kutoka katika nchi nyingi walifika Tanzania kwa ajili ya kumzika balozi huyo ambaye alikuwa mtu aliyedhamiria kuibadilisha Tanzania.
 
SEHEMU YA 73

Rais Bokasa alikuwa kwenye majonzi makubwa, hakuamini kile kilichotokea. Kwake, Mapoto alikuwa mtu wa nguvu, mwenye kufanya kazi kwa kujitolea japokuwa alikuwa mtu aliyesimama katika chama tofauti na chama alichokuwa.
Msibaki hapo alishindwa kuyazuia machozi yake, aliumia moyoni na hata macho yake yalikuwa mekundu mno kuonyesha kwamba kabla ya kufika msibani hapo alikuwa amelia vya kutosha.

Kila mtu aliyemwangalia, alimuonea huruma, ilikuwa vigumu kumuona rais huyo akilia, kila mmoja aliamini kwamba alikuwa na roho mbaya, ambaye kila siku alitamani lolote baya litokee kwa Balozi Mapoto, lakini siku hiyo, kila mmoja hakuamini alichokuwa akikiona.
“Mpaka rais imemuuma! Huu msiba umegusa watu wengi sana,” alisema jamaa mmoja huku akimwangalia Rais Bokasa ambaye alishindwa kabisa kuyaficha majonzi yake.

Baada ya siku mbili, mwili wa Balozi Mapoto ukazikwa katika Kijiji cha Matombo mkoani Morogoro. Ilikuwa ni siku ya masikitiko mno, Rosemary alishindwa kuvumilia, akalifuata kaburi la mumewe na kuanza kugalagalaga juu yake, moyo wake ulimuuma kupita kawaida na kila mtu aliyemwangalia mwanamke huyo, moyo wake ulimuonea huruma.

“Mume wangu! Kwa nini unaniacha? Nitabaki na nani? Nani atakuwa mfariji wangu? Kwa nini umeondoka mume wangu? Kwa nini Mungu amekuchukua mapema hivi? Nitaishi na nani mimi?” aliuliza Rosemary huku akilia kama mtoto juu ya kaburi la mume wake.

Je, nini kiliendelea?
 
SEHEMU YA 74

Ulikuwa ni msiba mzito uliotokea nchini Tanzania, kila mtu alihuzunika, furaha ikatoweka mioyoni mwa Watanzania wengi. Mtu ambaye walimwamini kwamba angeweza kuyabadilisha maisha yao, aliondoka, Mungu alimchukua hata kabla hajapata nafasi hiyo.

Vijana wengi wakakata tamaa, walitamani kuona Tanzania ikiingia katika mabadiliko ya kweli, hawakukipenda Chama cha Labour Party, hawakumpenda Rais Bokasa kwa sababu hakujua kitu chochote kile kuhusu uongozi, aliongoza ilimradi tu kitu kilichowafanya watu wengi kuumia.

Ilikuwa imebaki miezi kadhaa kabla ya kuingia katika uchaguzi mkuu. Kuanzia kipindi hicho maisha yakawa magumu zaidi, serikali ikabana fedha kwa ajili ya kuitumia katika kipindi cha uchaguzi. Wananchi wakakosa pesa, mitaani hakukuwa na pesa tena hali iliyofanya hata matendo ya kikatili, wizi kuongezeka.

“Hakuna hela!” alisema kijana mmoja.
“Ndiyo! Rais amezibana eti kwa sababu ya uchaguzi wa mwaka kesho! Hii siyo haki kabisa,” alisema jamaa mwingine.
“Nyamaza! Ukisikiwa tu, msala. Hutakiwi kumwamini mtu yeyote yule, jikaze kisabuni kwani usalama wamemwagwa kila kona,” alisema jamaa mwingine na kumfanya jamaa aliyeanzisha mazungumzo hayo kunyamaza.

Hakukuwa na unafuu, Watanzania wenyewe waliichukia nchi yao, wengine wakadiriki hata kukimbia na kwenda nje ya nchi, matajiri hawakutaka kukaa nchini humo, walichokifanya wao na familia zao kuondoka na kuelekea Dubai, Oman, Marekani na sehemu nyingine kuendelea na maisha yao.

Kila kitu kikawa shaghalabaghala, ugumu wa maisha ukatawala kila kona, masikini walilia, kwa kile kiasi kidogo walichokuwa nacho ikawa kama wamenyang’anywa, ili upate pesa ilikuwa ni lazima ufanye kazi kwa nguvu, pesa iliyokuwa ikipatikana kwa urahisi, haikupatikana tena.

Maisha ya Rosemary na watoto wake yalibadilika, hakukuwa na furaha tena, kila siku kwao ilikuwa ni majonzi mazito. Kifo cha mapoto kilibadilisha maisha yao yote, kwa watoto wake, Godwin na Irene, nyumbani hawakuwa na furaha tena, hawakuwa kama zamani kwani baba yao ambaye ndiye alikuwa furaha kubwa mioyoni mwao hakuwa nao tena, baba yao ambaye kila siku aliwauliza kuhusu ndoto zao aliondoka maishani mwao.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom