SEHEMU YA 62
Rais Bokasa alikuwa kimya katika kiti chake, akili yake haikuwa sawa hata kidogo, hatua alizopitia katika uongozi wake zilimnyima raha, muda mwingi alionekana kuwa na mawazo tele.
Aliona kulikuwa na mambo mengi ya kufanya mbele yake, hakujua ni mahali gani alitakiwa kuanzia na kuishia. Wakati mwingine aliwaona watu wakiwa wamemzunguka, wakimzomea kwa kila kitu alichokuwa akikifanya.
Serikali ikaanza kukosa fedha, kodi zilizokuwa zikikusanywa kwa kiasi kikubwa zikapungua, akashikwa na hofu na wafanyabiashara kwa kuhisi kwamba walikuwa wakimzunguka, hawakuwa wakilipa kodi kama ilivyotakiwa kuwa.
Aliandaa mikutano na wafanyabishara mbalimbali na kuwaambia umuhimu wa kulipa kodi lakini hawakutaka kuelewa kwani kama wao wangeendelea kulipa kodi kama ilivyotakiwa basi kusingekuwa na shida yoyote ile.
Nchi ikaanza kuyumba kiuchumi, pesa ikakosekana mitaani, kila mtu aliyekuwa akiulizwa kuhusu pesa, alisema kwamba hakuwa nayo. Aliwalalamikia wafanyabiashara wengi, bado hofu yake ilikuwa ni kuhusu ulipaji wa kodi, aliamini kuwa wafanyabishara walikuwa wakikwepa ulipaji wa kodi hiyo.
Mahospitalini, watu walikosa dawa, vyuoni, idadi ya wanavyuo waliokuwa wakipelekwa ilipunguzwa na mikopo ikafungwa. Nchi ilikuwa kwenye hali ya hatari lakini alifanya hivyo kwa kuwa tu alitaka serikali ibaki na fedha, abane matumizi yaliyokuwa makubwa kwa ajili ya nchi yake.
Baada ya kufikiria sana, akagundua kwamba hata mabalozi waliokuwa katika nchi za nje ambao walikuwa wakiwasomesha watoto wao huko kwa kutumia pesa za serikali, walitakiwa kuwarudisha nchini na kusoma katika shule za hapahapa Tanzania.
Hakutaka kupokea ushauri juu ya jambo hilo, akawaita waandishi wa habari ikulu na kuwaambia kile kitu ambacho alikifikiria kwamba watoto wa mabalozi ambao walikuwa wakisoma nje ya nchi walitakiwa kurudishwa nchini Tanzania kwa kuwa tu nchi haikuwa na pesa ya kutosha.
“Warudi Tanzania?” aliuliza Mapoto, alikuwa akipewa taarifa na mkewe.
“Ndivyo alivyosema.”
“Daah! Kweli?”
“Ndiyo!