Dunia haina usawa

Dunia haina usawa

SEHEMU YA 69

Rosemary alilia kwa uchungu, moyo wake ulimuuma mno, hakuamini kile alichoambiwa kwenye simu kwamba mume wake mpendwa, Mapoto alikuwa amefariki dunia.

Hakuishia kulia tu, baada ya muda akapoteza fahamu na mtu wa kwanza kabisa kumsaidia alikuwa mfanyakazi wa ndani ambaye akawaita majirani zake na walipofika, wakambeba na kuondoka naye kuelekea katika Hospitali ya Upendo wa Mungu iliyokuwa Masaki jijini Dar es Salaam.

Godwin na Irene walikuwa na hofu, hawakujua ni kitu gani kilitokea kwa mama yao, waliogopa, wakati mwingine nao walikuwa wakilia kwa kuamini kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wa mama yao mpendwa.

Hospitalini hapo, mfanyakazi wa ndani hakutaka kuwaambia kilichokuwa kimetokea, alihisi kwamba mwanamke huyo alikuwa amefariki na kama angewaambia watoto hao ilikuwa ni lazima kulia sana kitu ambacho hakutaka kabisa kukiona kwani moyo wake uliwaonea huruma.

Rosemary aliwekewa dripu, aliendelea kulala hospitali na baada ya saa moja, akayafumbua macho yake na kuanza kuangalia huku na kule. Hakuelewa alikuwa wapi, ilikuwaje mpaka dripu kuning’inia juu yake lakini baada ya kukumbuka kilichokuwa kimetokea, akaanza kulia tena, kumbukumbu juu ya mume wake zikamrudia kitu kilichomfanya kuwa kwenye huzuni kubwa.

“Mume wangu amekufa…” alisema huku akimwangalia nesi ambaye alionekana kushtuka.
“Mumeo amekufa?”
“Ndiyo! Nilipigiwa simu na kuambiwa hivyo. Mungu! Kwa nini umemchukua mume wangu?’ aliuliza Rosemary na kuanza kulia tena.

Kitendo cha nesi yule kuambiwa hivyo, akatoka ndani ya chumba kile na kuelekea katika ofisi ya daktari na kumwambia hali aliyokuwa nayo mgonjwa. Nesi huyo hakuishia hapo, akachukua simu yake na kuwaambia marafiki zake kwamba Balozi Mapoto alikuwa amefariki dunia nchini Marekani.

“Amefariki! Wewe nani kakwambia huyo ubuyu?” aliuliza rafiki yake kwenye simu.
“Mkewe.”
“Umeonana naye?”
“Amekuja hapa hospitali akiwa amepoteza fahamu, na yeye ndiye aliyesema kwamba mumewe amefariki,” alisema nesi huyo.
“Jamaniiii! Huyo ndiye niliyetaka kumpa kura yangu mwaka kesho,” alisema rafiki yake huyo.
 
SEHEMU YA 70

Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kusambazwa kwa taarifa hiyo, kupitia marafiki zake aliokuwa amewapigia, nao wakawapigia marafiki zao na hatimaye taarifa hiyo kuwafikia waandishi wa habari.

Waandishi hawakutaka kuchelewa, walitaka kujua ukweli juu ya kile kilichotokea hivyo kwenda katika hospitali hiyo na kuhitaji kuonana na Rosemary. Hilo lilionekana kuwa jambo gumu, daktari mkuu wa hospitali hiyo hakuruhusu jambo hilo kwani mgonjwa wake alihitaji muda wa kupumzika.
“Ila sisi tunataka kujua ukweli. Yaani aseme ndiyo tu, halafu kujaza gazeti tuachie sisi,” alisema mwandishi wa habari kutoka katika Gazeti la Kumekucha.

“Hapana!”
“Dokta! Yaani kuzungumza naye kidogo tu! Tunakuomba dokta, Watanzania wangependa kusikia kuhusu hili,” alisema mwandishi huyo lakini daktari hakutaka kukubaliana naye, alimwambia kwamba yeye na wenzake walitakiwa kusubiri mpaka Rosemary atakapopumzika vya kutosha.

Hawakuwa na jinsi, walitakiwa kusubiri mahali hapo. Hawakuondoka kwani Mapoto alikuwa mtu mwenye nguvu nchini Tanzania, aliheshimika na kila mmoja aliamini kwamba mwaka unaofuata mwanaume huyo angekuwa rais wa Tanzania kwani kila mmoja aliiandaa kura kwa ajili yake.

Walisubiri kwa saa mbili ndipo wakaruhusiwa kuzungumza na mwanamke huyo. Aliwaambia ukweli kwamba alipigiwa simu kutoka nchini Marekani na kuambiwa kwamba kweli mumewe alikuwa amefariki dunia.

“Kwa hiyo huna uhakika?” aliuliza mwandishi wa habari.
“Sijajua! Sijui chochote kile.”
“Basi subiri! Utajua ukweli!”
Walichokifanya baadhi ya waandishi ni kupiga simu nchini Marekani na kuwaambia marafiki zao kwamba walitakiwa kufuatilia kile kilichokuwa kimetokea.

Hilo halikuwa tatizo, marafiki hao wakafuatilia mpaka katika hospitali ambayo waliamini kwamba inawezekana mwili wa Balozi Mapoto ungekuwa umefikishwa huko, walipofika, wakapewa taarifa juu ya mwili uliokuwa umeletwa kwamba ulikuwa ni wa balozi wa Tanzania nchini humo.

“Kweli amekufa!” alisema mwanaume aliyetumwa.
“Mwili upo hospitali gani?”
“St. Monica Medical Centre.”
 
SEHEMU YA 71

Hiyo ilitosha kabisa kuandika habari hiyo iliyosisimua. Kesho, magazeti yakawa na taarifa ya kifo cha Balozi Mapoto. Watu hawakuamini, kitu cha kwanza kabisa walichohisi ni kwamba serikali ilihusika katika kifo chake lakini baada ya kuambiwa kilichotokea, jinsi kifo kilivyokuwa, wakagundua kwamba ilikuwa ni ajali tu, kitu ambacho hakukuwa na mtu wa kupewa lawama.

“Ni ajali! Ila nasikia ilikuwa mbaya sana,” alisema mwanaume mmoja.
“Wacha weee….”
Katika kipindi hicho cha mwaka 2002, mitandao ya kijamii iliyokuwepo kama Yahoo na Bearshare haikuwa na nguvu hivyo ilikuwa ni vigumu kupata taarifa kutoka katika mitandao ya kijamii, kila mmoja alitegemea magazeti na televisheni.

Tanzania ikanyamaza, ikaomboleza, kifo cha Balozi Mapoto kilimsisimua kila mmoja. Vilio vilitawala kila kona, hakukuwa na mtu aliyekuwa na furaha kwani mtu ambaye alikuwa amekufa alikuwa mtu wa watu, tumaini jipya kwa Watanzania, mtu ambaye alikuwa mabadiliko sahihi kwa Watanzania wote.

Rosemary hakutaka kubaki nchini Tanzania, akapanga kuondoka na kuelekea nchini Marekani, alitaka kwenda kuuona mwili wa mume wake hospitalini lakini hata kabla hajafanya hivyo, akapigiwa simu na rais na kuanza kuzungumza naye.

Kwanza akampa pole kwa kile kilichotokea, akamfariji katika kipindi kigumu alichokuwa akipitia lakini pia alimwambia kwamba serikali yake ingefanya kila liwezekanalo kuupeleka mwili wa Balozi Mapoto nchini Tanzania.
Hilo ndilo lililofanyika, siku mbili baadaye, mwili wa mwanaume huyo ukaingia nchini Tanzania.

Uwanja wa ndege watu walijaza kupita kawaida, wengi hawakuamini kama kweli mwanaume huyo alikufa nchini Marekani, walitaka kujionea wenyewe, walitaka kuona kama kweli aliyekufa alikuwa Balozi Mapoto waliyekuwa wakimpenda au mtu mwingine.

“Inauma sana, ni bora angekufa ndugu yangu yeyote yule kuliko Mapoto,” alisema mwanaume mmoja, alionekana kuguswa sana na msiba wa Mapoto.
 
Daah!!
Sijui kama mkono wa bokasa haujahusika na hii ajali.
Jamaa asingekubali kuona nchi inaendeshwa na upinzani.

Shunie asante
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom