Mkuu amani iwe nawe.
Naomba niandike machache labda utanielewa kidogo. Nami nilikuwa kama wewe katika kumchukia Edward Lowassa kwamba ni Fisadi, na nilimchukia kwa sababu "kusikia kwamba ni Fisadi" wakati sikuwa na ushahidi wowote.
Katika suala la Richmond kama utaangalia kiundani na kusikia kile Edward Lowassa alichosema utaona wazi kwamba ilikuwa ni mpango maalumu wa kumchafua na kumuondoa Edward Lowassa katika kiti cha Uwaziri mkuu. Kilichompoza Lowassa mpaka kusukiwa mpango huo mchafu ni ukali, umakini wa kufuatilia mambo na usimamizi wa yale anayoyaamini. Alipokuwa waziri mkuu tuliona wazi kwamba mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya walikuwa wanawajibika kisawasawa tokana na ukali wa Lowassa. Walikuwa hawaondoki vituo vyao vya kazi bila ruhusa maalumu toka ofisi ya waziri mkuu.
Muheshimiwa pale magogoni akaona wazi kwamba anafunikwa na Lowassa kwani viongozi wengi walikuwa wanachukua maelekezo na maagizo toka kwa Lowassa, ndipo zengwe lilipikwa la kumuondoa Lowassa madarakani.
Jiulize kwa makini sana, kama kweli Lowassa alifanya uchafu ule na kama ushahidi upo kwanini asipelekwe mahakamani?
Chadema walimuingiza Lowassa kwenye list of shame sababu kama zako wewe leo unayemchukia Lowassa kwa sababu za kusikia na kuambiwa. Juzi Lowassa karudia live kwenye TV kwamba alitaka kuvunja mkataba wa Richmond baada ya kujua kwamba ulikuwa fake, lakini bosi wake hakutaka kumsikiliza. Ulitaka Lowassa afanye nini zaidi?. Unaamini kabisa suala kama la Richmond mkuu wa nchi hakulijua toka mwanzo?. Unakumbuka tume ya Mwakyembe ilisema wazi kabisa kwamba inaficha baadhi ya mambo ili kuinusuru serikali, unafikiri walimaanisha nini?. Tume hiyohiyo ya Mwakyembe ilipewa mamlaka makubwa sana ya kumuhoji mtu yeyote bila kuogopa cheo alichonacho. Tume iliweza kuwahoji wahusika karibu wote na iliweza kusafiri mpaka USA kuwahoji wahusika, kwanini ilishindwa kumuhoji Edward Lowassa aliyekuwa na ofisi zikitazamana na ofisi ya tume hiyo?
Ni kweli kabisa Dr Slaa amejitolea sana katika kuifikisha Chadema hapa ilipo leo. Amejitolea kwa kila hali na mali, na kuna muda aliweka rehani mpaka maisha yake, lakini kuiacha Chadema leo juhudi zake zote alizofanya kuijenga na kuifikisha chadema hapa ilipo zitakuwa hazina maana tena. Slaa kama padri nilitegemea sana kwamba angefurahi kuona watu kama Lowassa wanajiunga na Chadema huku wakieleza (kutubu) ukweli machafu yaliyomo ndani ya CCM na yale tuliyokuwa tunasikia wametenda.
Mimi, wewe, wale na yule bila ubishi tumeichoka CCM. Sasa ni wakati wa kuunganisha nguvu kuitoa CCM madarakani. Ujio wa Lowassa na wenzake ndani ya Chadema naona iwe ni baraka kwetu wala isiwe laana. Kama umepitia mafunzo ya kijeshi utakumbuka kwamba tulifundishwa mateka anaweza kukusaidia kushinda vita, anajua siri nyingi za adui zako hivyo ukimtumia vyema utashinda vita. Nasi tunataka kuishinda CCM na kuitoa madarakani, huyu mateka itabidi afuate matakwa yetu, aishi kama sisi ili awe salama. Lowassa na wenzake wamejiunga Chadema na si Chadema wamejiunga na Lowassa, hivyo Lowassa na wenzake itabidi waishi na kufuata matakwa na malengo ya Chadema.