Kauli ya Dkt. Nchimbi ina uzito hasa ukiangalia mahali aliposema, kwenye Mkutano Mkuu wa Watetezi wa Haki za Binadamu, si jukwaa la chama.
Lakini baada ya kauli hiyo, baadhi ya watu wameanza kuuliza maswali mazito.
Wanauliza:
01. Kama Rais anaitaka, kwa nini tuipambanie? "Yaani kuna vita baridi, wapo wanaoitaka na wasioitaka."
02. Tunapambana na nani ili tuipate? "Yaani adui ajulikane wazi, tusipigane vita ya gizani."
03. Kama Rais anaitaka, kwa nini asiseme yeye mwenyewe? "Yaani Rais aufikishe ujumbe huo kwa kauli yake mwenyewe, kwani kauli ya Rais ina uzito wa kutekelezwa moja kwa moja."
Maswali haya yanauma kisiasa, na yana mvuto wa kisiasa pia. Lakini ukweli ni kwamba yote yanabeba dhana moja iliyofichika, dhana kwamba tunasubiri ruhusa kutoka juu, na kwamba mtu fulani lazima aturuhusu kwanza ndipo tupate Katiba. Hapo ndipo mtego ulipo.
Katika msingi wa kikatiba, mamlaka ya kutunga Katiba ni ya wananchi wenyewe, siyo ya viongozi. Katiba haitoki kwa kupewa, inatoka kwa wananchi kuiunda. Kwa mantiki hiyo, swali sahihi si "adui ni nani," bali "sisi wananchi tumeshafanya nini kutumia mamlaka tuliyonayo." Ukiendelea kuwahoji viongozi nia zao, unabaki umesimama, unasubiri. Ukianza kushughulikia maudhui yenyewe, umeanza kutembea.
Ndiyo maana nasema hakuna haja ya kuendelea kuzunguka kwenye maswali hayo kama jibu tayari lipo mezani. Ipo rasimu kamili ya
pendekezo la Katiba, ibara kwa ibara, inayojaribu kujibu tatizo la usimamizi wa madaraka kwa kuongeza muhimili wa nne, Baraza la Usimamizi wa Taifa, sambamba na Bunge, Mahakama na Serikali. Siyo kazi rasmi ya serikali, ni pendekezo la kujadiliwa na kupingwa.
Badala ya kuuliza nani anatuzuia, twende tukaone Katiba inaweza kuonekanaje kwa vitendo:
www.katibampya.com. Isome, uihoji, uikosoe. Hapo ndipo mapambano ya kweli yalipo, kwenye maudhui, si kwenye maswali.
Angalizo: hoja hizi ni kwa lengo la kuelimisha, kuzua tafakari huru na kuibua mjadala wa muelekeo wa pamoja kama Taifa, si vinginevyo.