Dk. Bilal ana ajenda gani?
Omar Maftah, Mkunazini, Zanzibar
Tanzania ni nchi yenye bahati nzuri ambayo inawapa wananchi wake fursa kubwa ya kuzungumza na kujadili mambo yanayowahusu wao au jamii katika vyombo vya habari na hata hadharani. Hivi karibuni tumekuwa tukishuhudia baadhi ya watu, wakiwamo wanasiasa, wanavyuo, wanaharakati, wanahabari na kadhalika wakizungumzia tuhuma za ufisadi dhidi ya viongozi fulani.
Hilo jambo si baya ila ieleweke kuwa mazungumzo kama hayo lazima yawe na muelekeo fulani, ama kurekebisha au kuzuia uhalifu. Si vyema hata kidogo kuyageuza mazungumzo haya au mada hii kuwa ni baraza la kujinadi kisiasa.
Inavyoonekana hivi sasa ni kwamba baadhi ya wachangiaji wa mada hiyo wamepoteza muelekeo na wamo katika kujitafutia umaarufu wa kisiasa.
Kwa bahati mbaya, kiongozi mmoja ambaye aliwahi kuwa na cheo kikubwa katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar amejiingiza katika sakata hilo. Huyo si mwingine ila ni Waziri Kiongozi Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Mohammed Gharib Bilal. Ni haki yake ya kidemokrasia, Dk. Bilal, kuzungumzia jambo liliopo midomoni mwa watu lakini azingatie ukweli wakati anapotoa maelezo yake. Inaonekana katika mazungumzo na mwandishi wa habari, Dk. Bilal alikuwa na dhamira hasa ya kutafuta baraza la kuzungumzia.
Kutokana na mazungumzo yaliyochapishwa katika gazeti moja la kila siku la Dar es Salaam, Dk. Bilal amechukua fursa ya mazungumzo ya muda ya tuhuma za kile kinachodaiwa, bila ushahidi, kuwa kuna ufisadi miongoni mwa viongozi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano na kugeuza kuwa baraza la kusengenya uongozi wa siasa Zanzibar. Kwa mujibu wa madai yake CCM Zanzibar imedororana kwamba hivi sasa hakuna mwamko. Dk. Bilal alitoa madai kama haya katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.
Inafaa ifahamike kuwa Chama cha Mapinduzi kiko hai, imara na chenye kukubalika kwa wananchi walio wengi, kimeweza kushinda kwa kishindo kikubwa katika chaguzi zote kuu pamoja na ule uliofanyika baada ya madai yasiyo na msingi ya Dk. Bilal, wa mwaka 2005.
Mfano mzuri umeonekana katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo ambao ulishuhudiwa na Waangalizi mbali mbali wa Uchaguzi wa Kimataifa. Waangalizi hao walikubali na kuridhika na mwenendo wa uchaguzi huo ambao uliendeshwa kwa amani, utulivu na ulikuwa huru na haki. Mafanikio hayo kwa upande wa CCM Zanzibar, yalitokana na uongozi mzuri wa chama uliopo wenye kusimamia Sera na Ilani ya CCM kwa umahiri mkubwa. Iweje leo kiongozi wa CCM, mjumbe wa Kamati Kuu, akurupuke na kutamka kwamba chama kimedorora? Ni vyema akaeleza wazi kama ana ajenda ya siri.
Ieleweke kuwa Chama cha Mapinduzi katika kuimarisha umadhubuti wake kimeteua viongozi wakuu kadhaa kuwa ni walezi wa Chama katika mikoa. Miongoni mwa walezi hao ni yeye Dk. Bilal ambaye aliteuliwa kuwa Mlezi wa Chama wa Mkoa wa Mjini Magharibi na pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama. Jukumu la viongozi hawa ni kushughulika na kushirikiana na wenzao kuhakikisha uimara wa chama wakati wote. Katika mfumo wa demokrasia, chama hakiongozwi na mtu mmoja bali huwa na uongozi wa pamoja (collective responsibilities).
Pia, sehemu moja ya chama haiwezi kujiendesha kama ndio chama peke yake. Sisi wana CCM Zanzibar, tumeshuhudia ushirikiano na ushiriki wa uongozi wa juu wa Chama Zanzibar, chini ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Mheshimiwa Amani Abeid Karume, ukishiriki katika shughuli zote za chama katika ngazi mbalimbali.
Kwa mujibu wa madai hayo ya Dk. Bilal inaonekana yeye hakuwa mshiriki katika shughuli hizo za chama au hakuwa akitekeleza dhamana zake za uongozi alizokabidhiwa, kwani ingekuwa rahisi kwake kubaini uhai na uimara wa CCM kama angekuwa mtekelezaji mzuri wa majukumu yake ya Mlezi wa CCM katika Mkoa wa Mjini Magharibi. Hiyo ni hasara kubwa kwa mtu kama yeye.
Uimara na uhai wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar unakwenda sambamba na uendeshaji imara wa Serikali ya Mapinduzi. Serikali hiyo katika kipindi hiki tokea mwaka 2000 imekuwa na mafanikio yanayoonekana na yanayotolewa sifa na nchi za nje pamoja na mashirika ya kimataifa. Hawezi mtu ye yote, seuze kiongozi wa CCM, kudai kuwa chama ambacho kinaendesha serikali hii, kimedorora ila mtu huyo anaishi nje ya mazingira ya Zanzibar na hataki kukubali ukweli uliopo.
Tumeshuhudia na kusikia mara kadhaa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakitangaza ukweli kwamba nchi yetu imo katika mapambano dhidi ya umasikini. Wakati huo huo, sisi sote ni mashahidi wa jitihada na hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi, katika kutatua matatizo yaliyopo na kuhakikisha kuna maendeleo ya jamii na uchumi yanayowanufaisha watu. Maendeleo yaliyofikiwa katika elimu kwa kufikia malengo ya Milenia kabla ya 2015, afya na miundombinu zikiwamo umeme vijijini na barabara ni ushahidi wa kutosha wa kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Mapinduzi inayoongozwa na CCM.
Aidha, mipango kama ya Mpango Mkuu wa Maji Zanzibar Mjini ni mojawapo tu ya mipango mingi iliyo katika utekelezaji. Sisi wananchi tunaamini kuwa kufikia mwaka 2010 mafanikio makubwa zaidi yatakuwa yamepatikana.
Kama raia mwema, ningelipenda kumshauri Dk. Bilal awe kiongozi anayeshirikiana na wenzake na pia awe mkweli katika kutetea uhai na uimara wa chama chake ambao upo dhahiri kwa watu wote. Katika kuendesha kampeni, ni vyema atumie sifa bora zilizomo ndani ya Chama badala ya kujaribu kuchafua uongozi imara uliopo ambao yeye ni miongoni mwake akiwa mlezi wa chama, au ameshindwa katika jukumu hilo? Pia, Dk. Bilal ameonekana kupitiwa kutolitumia gazeti la Uhuru la chama ambalo yeye ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya gazeti hilo badala ya kutumia vyombo vingine.
Kuhusu sakata la tuhuma za ufisadi, Dk. Bilal bila ya shaka anaelewa msimamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, kuwa Serikali inachunguza yote yaliyosemwa na kwamba sheria ichukue mkondo wake baada ya uchunguzi kukamilika na iwapo makosa yatabainika. Si vyema kwa watu kujifanya wachunguzi, askari, waendeshaji mashitaka na mahakimu.
Kama kada wa chama, Dk. Bilal awe wa mwanzo kutii maagizo ya Mwenyekiti wa chama chake.
Source: HabariLeo