Unapoona PM anataja sababu za umasikini ambazo ndiyo maeneo ya kuchochea maendeleo kama ongezeko la idadi ya watu..........huku Uchina idadi ya watu imekuwa kichocheo cha maendeleo..........na PM hayuko tayari kuzungumzia au hata kukiri ufisadi uliokithiri serikalini ndicho chanzo cha umasikini basi ujue hilo taifa ambalo viongozi wake wanakwepa ukweli na kujitumbukiza kwenye uongo kamwe halitaweza kuendelea..................
Waziri Mkuu aelezea ongezeko la umasikini
Wednesday, 30 March 2011
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema kasi kubwa ya ongezeko la idadi ya watu, kiwango kikubwa cha ukuaji wa miji na kiwango kidogo cha ukuaji wa sekta ya kilimo ni miongoni mwa sababu zinazochangia kutopungua kwa umasikini nchini.
Aliyasema hayo jana wakati akifungua Mkutano wa 16 wa Mwaka wa Taasisi ya Utafiti kuhusu Kuondoa Umaskini (REPOA) katika hoteli ya White Sands, jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo wa siku mbili ambao ulianza jana, mada yake kuu ni: "Tija, Ajira na Usalama wa Maisha ya Kiuchumi na Kijamii".
Waziri Mkuu alisema umefika wakati wa kujiuliza utafiti unaofanyika nchini umefanya nini kuleta mabadiliko na kwamba matokeo ya utafiti huo unatumikaje kupunguza umasikini wa Mtanzania na nini kifanyike ili kuondoa hali hiyo.
"Jambo ambalo ni changamoto kwetu ni hoja ya kwamba, pamoja na jitihada hizo, taasisi za utafiti hazijaleta matumaini makubwa, hususan upande wa uchumi… miongoni mwa sababu zinazochangia kutopungua kwa umasikini wa wananchi wengi ni pamoja na kasi kubwa ya ongezeko la idadi ya watu ambalo haliendani na kiwango cha ukuaji wa uchumi," alisema.
"Kwa sasa kiwango cha ukuaji wa uchumi ni wastani wa asilimia sita, wakati kiwango cha ongezeko la idadi ya watu kinakadiriwa kufikia asilimia tatu. Kwa mfano, mwaka 2009 Pato la Taifa lilikuwa sh. trilioni 28.2, wakati idadi ya watu ilikadiriwa kuwa milioni 40.7 na hivyo kufanya pato la wastani wa kila mwananchi kuwa sh. 693,185, ikilinganishwa na sh. 628,259 mwaka 2008. Hili ni ongezeka kidogo la asilimia 10.3."
"Kwa kiwango hiki tunapaswa kujiuliza utafiti wetu unatusaidiaje katika kuongeza kwa haraka ukuaji wa Pato la Taifa na hivyo kuongeza pato la Mtanzania mmoja mmoja? Vilevile, tujiulize utafiti wetu unatueleza tutumie sera zipi zinazofaa na ambazo ni 'effective' kuwa na idadi ya watu inayoendana na ukuaji wa Pato la Taifa. Sera za idadi ya watu zilizopo je ni 'effective' au tubadili mwelekeo?"
Alisema taarifa zinaonyesha umasikini pia unasababishwa na kiwango kidogo cha ukuaji wa sekta ya kilimo, takriban asilimia 4.5 kwa mwaka licha ya kuwa kinaajiri asilimia kubwa ya Watanzania.
"Kiwango hiki ni juu kidogo ya kiwango cha ukuaji wa idadi ya watu cha asilimia tatu. Kwa kuangalia kiwango cha ukuaji huo ni dhahiri kwamba tija katika kilimo bado ni ndogo. Kwa misingi hiyo, tunajiuliza utafiti wetu unasaidiaje katika kuongeza ukuaji wa mchango wa kilimo katika Pato la Taifa?" alihoji.
Alisema ukuaji wa miji una changamoto nyingi, ikiwamo shughuli chache za uzalishaji wa viwanda, ikilinganishwa na miaka ya nyuma na ambazo kama zingekuwa nyingi zingewezesha kutoa ajira kwa wakazi wengi walioko mijini.
Kwa mujibu wa makadirio ya idadi ya watu yaliyotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2002, Tanzania inakadiriwa kuwa na watu wapatao 43,187,823 mwaka 2010, ambao kati yao watu 31,809,808 sawa na asilimia 73.7 wanaishi vijijini na watu 11,378,015 sawa na asilimia 26.3 wanaishi mijini.
"Kuongezeka kwa watu mijini ambako kunasababishwa na wengi wao kuhama kutoka vijijini, kunaathiri shughuli za uzalishaji za kilimo katika maeneo ya vijijini na hivyo kupunguza kipato na hatimaye kuongeza umasikini kwa wananchi wa vijijini," alisema.
Hali hiyo, Waziri Mkuu alisema inasababisha wananchi wengi, hususan vijana katika miji kujiingiza katika shughuli zisizo rasmi na kuishi katika makazi duni yanayoashiria umasikini.
"Hili nalo ni tatizo ambalo taasisi zetu za utafiti zinatakiwa ziliangalie kama zinasaidiaje nchi katika kuondokana na hali hiyo. Tuangalie taasisi hizi zinachangiaje katika kuongeza ajira na kuwafanya watu, hususan vijana kuendelea kubaki vijijini na kuacha kukimbilia mijini," aliongeza.
Mapema, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya REPOA, Profesa. Esther Mwaikambo alisema wao kama watafiti wanatambua mchango wa Waziri Mkuu katika kuthamini masuala ya utafiti na umuhimu wa watafiti.
Naye Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Dk. Ad Koekkek alisema tija, ajira na usalama wa maisha kiuchumi na kijamii vina mchango mkubwa katika maisha ya Mtanzania pamoja na usalama wake binafsi, lakini ni lazima viendane na matumizi ya teknolojia.
Alisema maendeleo ya kiteknolojia yaweza kubuniwa, yanaweza kufundishwa vyuoni au kuagizwa kutoka nje ya nchi au mawili kati ya hivyo, lakini kikubwa ni kuona yanamsaidiaje mwananchi kuboresha maisha yake.
"Miaka ya hivi karibuni, serikali imeongeza kwa kiwango kikubwa bajeti ya kilimo… lakini je tumefanya utafiti kuona kama ongezeko hilo limesaidia kuongeza uzalishaji mazao ya mkulima? Je, tumechunguza kuona kama wakulima wana uhuru wa kuchagua teknolojia zinazowafaa? Je, tumefanya utafiti kuona kama serikali inatumia njia sahihi katika kutekeleza mpango huu?" alihoji.