Coco Beach kuwa eneo la uwekezaji, kivutio na utunzaji wa mazingira

Muuza Kangala

JF-Expert Member
Jul 21, 2021
1,126
4,168
#HABARI MANISPAA ya Kinondoni imesema imejipanga kuhakikisha eneo la ‘Coco Beach’ linakuwa la uwekezaji, kivutio na utunzaji wa mazingira.

=======

Ofisa Elimu Manispaa hiyo, Theresia Kyara, alieleza mikakati hiyo jana mkoani Dar es Salaam, wakati wa upandaji wa miti uliofanywa na kampuni binafsi ya mipango miji na wauzaji wa viwanja Property Ltd kwa lengo la kuboresha mazingira hayo.

"Manispaa tumejipanga ipasavyo kufanya mabadiliko eneo la ufukwe wa Coco Beach na tayari wawekezaji wamejitokeza kuanza biashara, mtu ambaye hajafika Coco muda mrefu aje aone kulivyokuwa na kunavyopendeza," alisema.

Alisisitiza kuwa, mbali na miti inayopandwa na kampuni ya Property eneo lote la fukwe na utengenezaji wa bustani nzuri za maua, ujenzi wa vibanda vinavyovutia, watu watapumzika na familia zao au faragha.

Alisema lengo ni kuhakikisha kunakuwa na uboreshaji wa mazingira, kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan alivyoelekeza akitaka kuona Coco Beach inakuwa kivutio na kuondokana na mazingira machafu yasiyopendeza katika maeneo hayo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Property, Haleem Zahran, alitoa wito kwa wadau wa ardhi, zikiwamo kampuni binafsi na serikali kuhakikisha wanaweka viwango maalumu vya uuzaji ardhi ili kupata eneo la kupanda miti na kusimamia mipango miji.

Alisema, mpango wa kupanda miti Coco ni mwendelezo wa kampuni hiyo kuunga mkono jitihada za Rais Samia katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi na utunzaji wa mazingira.

"Kwetu ukinunua kiwanja kinakuwa kimepimwa, kina hati na kipo katika mipango miji na lazima kuna eneo limetengwa kwa ajili ya huduma za kijamii na katika kila eneo la ujenzi kuna mita zimetolewa za kupanda miti," alisema.

Chanzo: Nipashe
 
Back
Top Bottom