Chongolo: Watanzania wako tayari uwekezaji wenye tija na mabadiliko bandarini

Ngaliwe

Senior Member
Dec 30, 2015
161
364
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Daniel Chongolo amesema Watanzania kwa ujumla wao wameonesha utayari na uhitaji mkubwa wa kuona uwekezaji na uendeshaji utakaoleta maboresho, ufanisi na kuongeza mapato katika Bandari ya Dar Es Salaam, hivyo ameielekeza Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kuharakisha utekelezaji wa hatua mbalimbali zilizobakia za uwekezaji bandarini hapo, ili wananchi waanze kuona matokeo.

Ndugu Chongolo amesema kuwa CCM inatambua kuwa wapo Watanzania wenye nia njema na mapenzi mema kwa nchi yao, ambao wametoa maoni ya aina mbalimbali yanayolenga kuboresha mkataba wa uwekezaji katika Bandari ya Dar Es Salaam, ambapo amesema maelekezo ya Chama kwa Serikali ni kuhakikisha mawazo ya wananchi hao yanachukuliwa na kufanyiwa kazi ili yasaidie kupatikana kwa tija na matokeo makubwa zaidi yanayotarajiwa kwa ajili ya maendeleo ya watu na ustawi wa Tanzania.

Ndugu Chongolo ameyasema hayo wakati akihutubia mkutano mkubwa uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Jumapili Julai 30, 2023, wakati akihitimisha ziara yake iliyotumika kuwapatia elimu wananchi kuhusu makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai, yanayolenga kuweka msingi wa uwekezaji katika Bandari ya Dar Es Salaam ili kuboresha utendaji na ufanisi wa kazi bandarini hapo.

“Msimamo wa Chama Cha Mapinduzi kuhusu uwekezaji wa bandari ni kuitaka serikali kuhakikisha kasi ya utekelezaji wake iende kwa haraka iongezwe ili tuanze kupata manufaa na matokeo kwa haraka. Tunasema hivyo kwa sababu msingi wake ni Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020/25 tuliyoinadi na kupitishwa na wananchi katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 na kwetu kwenye suala la utekelezaji wa ilani mtu yeyote akitaka kutukwamisha ni lazima tusimame kuwa kitu kimoja tushikamane tuhakikishe haturuhusu fitina, hila, maneno ya uchokozi ili tusifanikishe hilo na kwenye hili wana CCM wameonesha kwa dhati kabisa kulikubali na kuwa kitu kimoja, niwashukuru sana.

“Wananchi na wanaCCM wameonesha utayari mkubwa sana, wameonesha uhitaji mkubwa wa kuona mabadiliko na tija tunayoizungumzia kwenye uwekezaji wa bandari ikitokea kwa haraka, niwapongeze sana kwenye maeneo yote tuliyopita. Chama Cha Mapinduzi tunasema hili ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020/25 kwa sababu kwenye ibara ya 22 na 59 tumeahidi na tulieleza kwa kina mpango wa suala hilo. Msimamo wa Chama Cha Mapinduzi kuhusu uwekezaji wa bandari ni kuitaka Serikali kuhakikisha kasi ya utekelezaji wake iende kwa haraka iongezwe ili tuanze kupata manufaa na matokeo kwa haraka,” amesema Ndugu Chongolo na kuongeza;

"Chama Cha Mapinduzi kinaisisitizia serikali kuweka msukumo katika hatua zinazoendelea ili kama kuna jambo au maoni ya kuongeza tija kwenye kuboresha mkataba yachukuliwe yawekwe ili kutupeleka kwa spidi kule tunapotaka. Sasa kuna watu wametoa maoni ya aina mbalimbali kuna watu wamesema uwekezaji huu ni muhimu sana lakini kwenye ule mkataba kuwe na mambo kidogo yanayoendana na kile wanachokipendekeza, hayo ndiyo mawazo ya msingj yenye tija.

“Na sisi CCM tunaiagiza serikali pia kuhakikisha inatekeleza hilo na kufanya mapitio kuangalia mazingira na kuona umuhimu wa kuyaruhusu mawazo yenye tija kuingia na kuchangia uboreshaji wa mkataba huu ili utufikishe kule ambapo tutapata tija na matokeo makubwa zaidi. Tunasema hivyo kwa sababu mkataba sio Msahafu wala Biblia, hatuwezi kushikilia tukasema aah hauna dosari…hapana, umeandikwa na wanadamu, macho na elimu vinatofautiana na elimu inatofautisha watu kuona mambo kwa namna tofauti,” amesema Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Chongolo.

Katika ziara hiyo ya kuwaelimisha Watanzania kuhusu uwekezaji unaolenga kuboresha utendaji na ufanisi wa Bandari ya Dar Es Salaam, aliyoihitimisha Mwanza, baada ya kufanya mikutano mikubwa iliyohudhuriwa na maelfu ya wananchi kwa kuanzia Mbeya, Mtwara, Tanga, Arusha, Singida, Kigoma, Dar es Salaam na hatimae Mwanza, Ndugu Chongolo aliambatana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa – Oganaizesheni, Ndugu Haji Issa Usi Gavu, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Ndugu Stephen Wasira, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, Mhe. Jerry Silaa (Mbunge wa Ukonga) na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Wakili Albert Msando.

Mbali ya kuielekeza Serikali kuzingatia na kufanyia kazi maoni chanya na yenye tija yanayotolewa kuboresha uwekezaji, Katibu Mkuu Ndugu Chongolo pia ligusia uwepo kwa kundi dogo la wanasiasa na wanaharakati wanaopita na kutumia majukwaa mbalimbali kufanya upotoshaji na kufanya uchonganishi, wakilenga kupinga suala hilo muhimu lenye maslahi makubwa kwa taifa lisifanyike na baada ya hoja zao zote kujibiwa, sasa kundi hilo limeanza kutumia lugha za matusi dhidi ya viongozi wakuu wa nchi, waliopo madarakani, waliostaafu na wale waliotangulia mbele ya haki.

"Kuna kundi la pili ambalo lenyewe linapinga tuu…mwanzo lilianza kwa kukosoa mkataba. Baada ya kuona kwenye mkataba wanakosa eneo la msingi la kusimamia sasa wamebadilika wanaenda wanasema hakuna uwekezaji huu kufanyika, eti hauna tija. Maana yake ni nini…maana yake CCM tusitekeleze ilani yetu kwa kiwango cha juu chenye tija ili wakija wawe na kazi rahisi ya kuichonganisha CCM na wananchi wasitupatie ridhaa kwa mara nyingine. Sasa nani yupo tayari kuchonganishwa? Hatupo tayari. Tuliahidi na tutatekeleza kwa hiyo serikali lazima itekeleze kwa kishindo.

"Sasa hawa jamaa wamegundua msimamo wetu umenyooka na hatuyumbi wameamua sasa kuanza matusi na wanatukana kweli, hadi mara nyingine unajiuliza huko duniani kuna chuo kinachotoa shahada ya matusi? Kwa sababu ukiangalia namna wanavyopanga na kuyasema vizuri hayo matusi unajiuliza hawa wenzetu hii professional (taaluma ya kutukana) wameisomea wapi,” amesema Ndugu Chongolo, na kurudia tena wito wake alioutoa mara kadhaa, hasa katika mikutano ya Tanga, Arusha, Singida na Dar Es Salaam, kuwataka wanaCCM kuonesha ukomavu wa Chama chao, kwa kutojibu matusi, bali wasimame imara kutekeleza dhamana ya kuongoza nchi;

"Ndugu zangu niwaombe sana CCM ni kubwa mno na ina historia kubwa na heshima kubwa barani Afrika na dunia nzima kwa ujumla tusihangaike kuingia kujibizana nao sisi tuna kazi kubwa ya kujenga nchi yetu, kuratibu maendeleo ya Watanzania na kutatua changamoto za wanachi, tukianza kuhangaika na matusi wanayotoa tutaondoka kwenye reli na baadae mambo yetu hayatakaa vizuri ni lazima tusimame imara, tunyooshe mguu tuhakikishe tunafikia tija ile tuliyoaihidi kwenye ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/25. Matusi kwetu tuachane nayo, tuyadharau na ndugu zangu kila mmoja huchagua kile ambacho anakiweza, sisi tumeamua kufanya kazi kwa bidii, wao wameamua kututukana tuwaache, walichagua huko kwa sababu ndio kazi wanayoiweza na sisi watuache tuendelee kujenga nchi sababu ndio kazi tunayoiweza, CCM OYEE.

“Hawa jamaa wa upinzani wametukana sana watu juzi wakiwa huko Bukoba na walianza kutukana viongozi wetu wastaafu marais wetu, wamemtukana sana Hayati Benjamini Mkapa, wamemtukana sana mzee wetu Jakaya Kikwete, wakamtukana sana Hayati John Magufuli na wakamtukana sana Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wote nyinyi ni mashahidi na mmewasikia matusi makubwa, matusi ya ajabu yasiyo na staha na sisi pia tuliwasikia"

"Majibu yetu kwao kama Chama Cha Mapinduzi ni…tunawashukuru sana kwa matusi yao hatuna muda wa kuwajibu hiyo ndiyo heshima waliyojijengea na hiyo ndio hadhi yao kukosa heshima na kuishiwa sera. Sisi kazi yetu ni maendeleo na matusi yetu ni kuisimamia serikali kuhakikisha inatekeleza ipasavyo ilani yetu ya uchaguzi ya mwaka 2020/25,” amesema Katibu Mkuu Chongolo.

Aidha, Ndugu Chongolo aliwaambia maelfu ya wananchi hao kuwa kuwepo kwa kundi la watu wanaopinga kila jambo kubwa, lenye malengo mazuri ya kuimarisha misingi ya kujenga mazingira ya fursa za maendeleo ya watu na ustawi wa Tanzania, haijaanza kwa mradi wa uwekezaji wa Bandari ya Dar Es Salaam, akitolea mifano ya jinsi baadhi ya wanaharakati na wanasiasa wa vyama vya upinzani kwa kushirikiana na watu kutoka nje ya Tanzania walivyowahi kupinga miradi mingine ya uwekezaji mkubwa wenye manufaa ya nchi, ikiwemo ujenzi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere na Reli ya Kisasa (SGR) na Bomba la Mafuta la Uganda – Tanzania.

“Labda mnadhani kwamba upingaji wa maendeleo umeanzia hapa kwenye suala la uwekezaji wa bandari leo…niwapitishe kidogo miaka ya nyuma serikali iliwahi kufanya maamuzi ya kujenga mradi wa kuzalisha umeme katika mto Malagalasi. Baada ya uamuzi huo wakaja jamaa wanaitwa Jumuiya ya Kimataifa na wataalamu wa huko duniani wakisema wao ni wataalamu wa viumbe hai na viumbe adimu wakatuambia tukitekeleza mradi pale mto malagalasi kuna samaki wadogo kwa dagaa yaani wale dagaa mnaowajua sasa samaki hao ni wadogo kuliko hata dagaa.

“Lakini samaki hao hawafai hata kwa mboga wala chochote lakini wakasema tukiweka huo mradi samaki hao watapotea, tukawasikiliza tukasema labda jambo la ukweli lakini mpaka leo hii mniambie hapa mmewahi kusikia kuna pesa imekuja kusaidia nchi yetu ili tuwalinde wale samaki? Yaani samaki wasiofaa kwa mboga wale chochote walikuwa bora kuliko Watanzania kupata umeme. Kuanzia hapo tuliweka nukta kwamba wakija na jambo lolote watusikilize sisi na sio kusikiliza ya kwao zaidi.

“Changamoto ya umeme ilikuwa kubwa tukaenda kujenga Bwawa la Kihansi kule Morogoro. Tulipoanza wakaja wakasema mpango wenu utapoteza vyura adimu duniani. Yaani vyura wenyewe lazima uwaangalie kwa darubini ndiyo unaweza kuwaona halafu eti tuache kujenga bwawa lituzalishie umeme tutunze vyura. Tukawaambia akili za kuambiwa tunachanganya na zetu hivyo hilo tumeligundua na tukasimamia msimamo wetu na kujenga Bwawa la Kihansi. Leo hii umeme tunaoutumia sehemu yake unachangiwa na Bwawa la Kihansi. Tuliwaambia toeni vyura wahifadhiwe pembeni gharama ya kuhifadhi vyura haiwezi kuwa kubwa kuliko Watanzania kukosa umeme wa uhakika"

"Tulipokuja kwenye bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Mkoani Tanga wakaibuka na kubeba mabango wanasema mradi utahatarisha mazingira. Tulisimama na leo mradi unaendelea na wana Kanda ya Ziwa hii ni sehemu ya wanufaika wa mradi huo…CCM OYEE.

“Tulienda kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere kule Mto Rufiji…nyinyi ni mashahidi uamuzi wa kujenga bwawa ulifanywa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere miaka ya 70, muda mwingi tumekuwa tukitafuta namna ya kutekeleza ule mradi, mwaka 2016/17 uamuzi ukafanyika mpango wa ujenzi ukaanza na tukaweka mazingira yote sawa lakini jamaa hawakukaa kimya wakaja kusema Hifadhi ya Selous ni maalum, tukijenga bwawa itaharibika na mazingira yataharibika na tutaiondosha kwenye vivutio vya dunia, Serikali ya CCM tukalikataa hilo na kufanya uamuzi wa kujenga na tukabadilisha jina la hifadhi kuita Mwalimu Nyerere ili vivutio vitokane na jina jipya na kujengwa na yaliyopo katika jina jipya. Leo hii tunasubiria zaidi ya megawati 2000 za umeme hayo ndio mambo ya watu wanaofikiria kwa ajili ya wananchi, walitaka tukose umeme tuendelee kuwa kwenye mgao.

"Hata wakati tumeanza ujenzi wa reli ya umeme (SGR) bado walikuwa na lengo la kutukwamisha kuanzia mchakato ulivyokuwa umeanza. Zabuni ilipotangazwa, walijitokeza wengi sana, lakini wakajitoa wote ili tu kutukwamisha. Lakini leo hii SGR imekuwa hadithi inayoenda kutimia kwa vitendo nchini. Utaweza kusafiri kutoka Dar Es Salaam hadi Kigoma kwa masaa kadhaa na hii ndio kazi kubwa inayotokana na misimamo ya CCM kwa Serikali kutekeleza Ilani ya CCM ya uchaguzi, wenye hila tusihangaike kupoteza muda nao.”

Katibu Mkuu Chongolo amesema lengo la watu wanaopinga hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Tanzania katika kuimarisha misingi ya maendeleo ya watu wake na ustawi wa taifa, hasa ni kutotaka CCM itekeleze ilani yake kikamilifu, hali ambayo itawakosesha wanasiasa wa upinzani na wanaharakati wachache agenda wakati wa uchaguzi, pia ni kutaka kuikwamisha nchi ili iendelee kuwa tegemezi kwenye mifumo ya kinyonyaji na ukandamizaji ya kidunia, jambo ambalo alihitimisha kwa kusema “Kwenye hilo wana bahati mbaya tulishavuka, tupo mbali sana.”
 
Back
Top Bottom