Zitto,
Kwa nini Chadema isifanye msukumo wa kutaka kuundwa kwa Katiba Mpya ya Tanzania ili kukidhi mahitaji ya Tanzania na kwa mazingira yetu na si kukimbilia kuiga ya Afrika Kusini au Canada?
Je hili suala la majimbo ni njia moja ya kukwepa kutangazia umma kuwa Chadema inataka mchakato wa Katiba mpya?
Je kuna ubaya gani mkirekebisha mfumo uliopo sasa hivi wa mikoa na kuondoa mamlaka ya kuteua watendaji na wakuu wa mikoa na wilaya kuota kwa Raisi na kuyafanya yawe mikononi mwa wananchi kwa kupigiwa kura?
Je mkishaunda hayo majimbo, yatakuwa na sheria zao binafsi na kuwa na mabunge yao ya kimajimbo ziada ya Bunge la serikali ya shirikisho?
Pemba wanadai uhuru wao wawe na serikali yao ndani ya Muungano tofauti na Zanzibar, je itakapofikia Kagera wakasema hawataki kuwa jimbo moja na Shinyanga mtawapa ruhusa?
Je hii ndiyo njia pekee ambayo Chadema inafikiri itakuwa suluhisho la
matatizo ya Tanzania?
Moelex kaongea vizuri sana kuhusu CCM kwenda uchagani na kusema Chadema wanataka kuzuia mapato ya madini yasitumike nchi nzima, yatumike Usukumani pekee, je mlipokuwa mnaandika hii sera mlilifikiria hili? maana katika sera hamna mahali mnapoonyesha ni jinsi gani serikali kuu ya shirikisho itapata mapato yake na ni jinsi gani Serikali kuu itajiendesha na kusimamia maendeleo ya Taifa.
La mwisho ni la sheria, ikiwa kila jimbo litakuwa na sheria zake, hivyo mnatutamkia wazi kuwa kunaweza kuwa na mgongano wa kisheria kati ya majimbo na hata serikali kuu, je ni sheria gani zitakuwa na nguvu bila wananchi kuona wanaonewa?
Rev,
Maswali yako mengi na magumu sana. Kiukweli tumetafakari sana juu ya mfumo huu wa majimbo na tukaona kuwa itasaidia sana nchi kuendelea kwa haraka kwa kutumia rasilimali zilizopo maeneo ya majimbo. Mlicholetewa hapa ni rasimu sifuri ili kupata michango na baadae kupata rasimu ya kwanza na kisha kuipitisha katika vikao na kuwa sera rasmi.
Madai ya Katiba Mpya ndio ajenda ya kwanza ya chama chetu na ushirikiano wa vyama vya upinzani. Sera ya majimbo tukitaka ipite ni lazima iingie katika mfumo mzima wa katiba na hivyo katiba mpya ni suala la lazima.
Sasa kuna mawazo kadhaa kuhusiana na katiba mpya. Kuna wanaosema ni vema katiba mpya iwe ni ajenda yetu ya uchaguzi na kuahidi wananchi katiba mpya mara tukishinda. Kuna watu wanasema inabidi kuidai sasa na kuingia katika uchaguzi na katiba mpya. Tukipigania sasa maana itakuwa ni katiba iliyoletwa na CCM kwa matakwa yao ya kukaa madarakani zaidi. Tukisubiri ni nini maana yake kama tusiposhinda kufuatia wananchi kutoona umuhimu wa katiba mpya.
Njia ya kati hapo ni kuwa na minimum demands ili uchaguzi uwe huru, kubadili mfumo wa uchaguzi na kuweka uwanja wa kisiasa sawa. Tukifanikiwa hili ndio tuanze kazi ya katiba mpya.
Kiukweli tunataka mfumo wetu uwe ni wa Kitanzania zaidi. Uzingatie umoja wa Taifa letu, Muungano wetu na juhudi za kuondoa ukabila zilizofanikiwa sana. Mifano ya Kanada tumetoa tu. Mfano wa Afrika Kusini ni mzuri kwetu kwani wao licha ya kuwa sio Shirikisho lakini wana majimbo yaliyo na uhuru
Kwamba mapato yoote yatabaki majimboni sio kweli. DRC wamegawana Taifa 60% na Majimbo 40. Kuna kodi zitakusanywa na majimbo na nyingine zitakusanywa naTaifa na pia hata serikali za mitaa zitakuwa na ushuru zinaokusanya.
Kwa vyovyote vile majimbo yatakuwa na mabaraza yake ya wawakilishi na watakuwa na uwezo wa kutunga sheria zinazohusu Jimbo husika. Watakuwa na Mkuu wao wa Mkoa (Premier) atakaetokana na chama chenye wabunge wengi ndani ya Baraza la Wawakilishi la Mkoa.
Zanzibar itakuwa na Serikali yake kama sasa bila ya kuwa na Rais maana Rais atakuwa ni wa Muungano tu. Lakini Pemba itakuwa na Premier wake na Unguja Premier wake na mabaraza yao ya kutunga sheria. Mji Mkongwe utakuwa ni city-state kama itakavyokuwa Dar es Salaam.
Kishoka, we mean it. Help us