CHADEMA washitukiwa wakitaka kuvuruga mkutano
Habari Zinazoshabihiana
Mwanry akamia kumfuatilia Mbowe 10.01.2007 [Soma]
Polisi yachunguza kauli za Mbowe, Kabwe 07.09.2007 [Soma]
mabadiliko ya jina la Wizara yaibua mjadala mkubwa 24.03.2006 [Soma]
*Wadaiwa kupanga kikundi cha kuzomea wana CCM
Na Francis Godwin, Iringa
MKUTANO wa viongozi wa CCM waliokuwa katika ziara ya kuelezea utekelezaji wa Ilani ya chama hicho mkoani wa hapa umeingia dosari baada ya kikundi cha wapinzani wakiongozwa na Katibu wa CHADEMA wa Mkoa, Bw. Paschal Bella, kuanzisha vurugu dakika za mwisho kwa lengo la kuvuruga mkutano huo.
Mbali ya tukio hilo, pia aliyekuwa kamishina wa NCCR -Mageuzi wa Mkoa wa Iringa, Bw. Hussein Mwaikambo, alirudisha kadi ya chama hicho kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Bw. Aggrey Mwanri na kujiunga CCM, kwa madai kuwa Upinzani hauna sera na ubinafsi umetawala katika vyama hivyo.
Bw. Bella na wenzake, walifikia hatua hiyo baada ya kada wa CCM, Bw. Shaibu Akwilombe, ambaye awali alikuwa kiongozi wa juu wa CHADEMA, kusimama katika jukwaa hilo na kuelezea upungufu ndani ya chama hicho.
Kutokana na hali hiyo, kikundi hicho kikiongozwa na kiongozi huyo kilipinga kwa sauti kubwa tuhuma za Bw. Akwilombe dhidi ya CHADEMA kuwa hazina ukweli wowote.
"Si kweli, mwongo huyo CHADEMA haiko hivyo... tunataka mjibu hoja za wapinzani dhidi ya mkataba wa mgodi wa Buzwagi, si kuishambulia CHADEMA," walisema wanakikundi hao.
Hata hivyo, kabla hawajaendelea makamanda wa CCM na baadhi ya wananchi waliwafuata na kuwaondoa kwa nguvu katika mkutano huo, huku baadhi yao wakitaka wawape kipigo kwanza ili liwe fundisho.
Kiongozi huyo wa CHADEMA na wenzake, waliokolewa na baadhi ya wasamaria wema kwa kuondolewa katika eneo la viwanja vya Mwembetogwa, ambako mkutano huo uliokuwa.
Ilidaiwa kuwa lengo la kikundi hicho kufika katika mkutano huo, lilikuwa ni kuwazomea viongozi hao, lakini kutokana na kuonywa na Katibu wa CCM wa Mkoa, Bw. Kilumbe Ng'enda kuwa atakayejaribu kufanya fujo katika mkutano huo atakiona cha moto, azma hiyo ilishindikana.
Baadhi ya wana CCM walililalamikia Jeshi la Polisi kwa kushindwa kuweka ulinzi wa kutosha katika mkutano mkubwa kama huo, tofauti na ilivyokuwa kwa wapinzani ambapo ulinzi ulikuwapo wa kutosha.
Wakati huo huo, uongozi wa CCM Taifa umesema jitihada za Rais Jakaya Kikwete katika kuliongoza Taifa zinaonekana kwa kila Mtanzania na wasio Watanzania katika kuiwezesha nchi kung'ara vyema ulimwenguni na kuwaonya wapinzani kuacha kuchafua jina lake.
Ulisema Rais hawezi kukurupuka kuwachukulia hatua wabadhirifu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) bila kuwa na uhakika wala uchunguzi wa kutosha kufanyika, kwani anaongoza nchi kwa kuzingatia misingi ya demokrasia tofauti na wapinzani wanavyotarajia.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Bw. Aggrey Mwanri, alitoa onyo hilo wakati akizungumza na wakazi na wana CCM wa manispaa ya Iringa katika uwanja wa Mwembetogwa.
Kidogo kidogo ukweli utadhihiri.....