[h=1]Wasaliti CCM Kuwajibishwa[/h]Kutoka Uhuru
KATIBU wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, amesema Chama kitawawajibisha waliohusika na uchakachuaji kura ya maoni katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana. Amesema hatua itachukuliwa kwa kuwa uchakachuaji huo uliigharimu CCM kwa kupata matokeo mabaya katika baadhi ya kata na majimbo. Hata hivyo, amesema Chama katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 31, mwaka jana, kilipata kura nyingi za urais na viti vingi vya ubunge na udiwani. Nape alisema hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Fisi, Manispaa ya Lindi. Kwa mujibu wa Nape, wasaliti wa Chama wakati wa uchaguzi pia hawatasalimika, kwani hatua zitachukuliwa dhidi yao. "Tunatambua tunao viongozi na wanachama wengi waadilifu na wasiothubutu kukisaliti Chama, hawa tutawaenzi, lakini wenye tabia za usaliti na wachakachuaji wa kura ya maoni kwa faida ya matumbo yao hawa lazima tutashughulika nao katika uchaguzi mkuu ujao wa Chama," alisema.
Nape alisema hatua za kuwashughulikia ni miongoni mwa maazimio yaliyopitishwa na kikao cha NEC, kilichofanyika mjini Dodoma, Aprili, mwaka huu. Katika kikao hicho pia yalifanyika mabadiliko makubwa ya uongozi wa ngazi ya juu ya CCM kwa lengo la kukirejesha Chama katika kutekeleza matakwa ya kuasisiwa kwake.
Alisema Chama kinachukua hatua hizo, kwa sababu kinatambua kuwa bila usaliti wa viongozi wachache kisingeweza kupoteza baadhi ya majimbo na kata, katika uchaguzi mkuu uliopita.
Nape alitoa mfano wa jimbo la Lindi Mjini, ambalo lilikwenda mikononi mwa wapinzani, licha ya kuwepo wanachama wengi wa CCM ikilinganishwa na vyama vingine vya siasa.
"Baada ya matokeo kutangazwa, wakati huo nikiwa mkuu wa wilaya nilipita hapa Lindi mjini nikaona watoto wakishangilia kushindwa kwa CCM.
"Nikauliza mbona wanaoshangilia ni watoto, wakubwa waliopiga kura wako wapi? nikajibiwa na wenyeji waliopiga kura za kuiwezesha CUF kushinda ni wanachama wa CCM, hivyo hawawezi kutoka barabarani kushangilia kushindwa Chama chao," alisema.