Ukiritimba uliokithiri
Ufisadi wa mabilioni
Ubovu mitaala ya elimu
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema dawa pekee ya kumaliza tatizo la umaskini uliokithiri miongoni mwa Watanzania wengi nchini ni kuondoa ukiritimba na ufisadi.
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama hicho Taifa, Wilfred Lwakatare, alisema hayo alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Mgazini, Kata ya Kilagano, Wilaya Songea Vijijini, mkoani Ruvuma jana. Mkutano huo ni wa kwanza kati ya mikutano mitatu ya hadhara iliyofanywa na Lwakatare, uliofuatiwa na ule alioufanya katika kituo cha mabasi cha mjini Peramiho na katika Uwanja wa Shule ya Msingi ya Lilambo, Songea mjini.
Lwakatare ni miongoni mwa viongozi waandamizi wa Chadema walioko katika timu sita zinazoendesha operesheni maalum ya chama hicho nchini inayohusisha maandamano na mikutano ya hadhara, kwa lengo la kuishinikiza serikali kusikiliza kilio cha wananchi, ukiwamo umaskini na hali ngumu ya maisha. Operesheni hiyo, ambayo ni muendelezo wa ile iliyofanyika katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, inayohusisha mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Kagera na Mara mwezi uliopita, ilianza Mei 6, mwaka huu, katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, mkoani Mbeya.
"Dawa ya umaskini ni ndogo. Ni kuondoa ukiritimba na ufisadi," alisema Lwakatare, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kagera.
Alisema ukiritimba unaonekana katika serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ni pamoja na kushindwa kutengeneza barabara nyingi vijijini na hivyo kuwafanya wananchi kupata tabu ya kusafirisha mazao wanayoyalima kuyapeleka kwenye masoko. Pia alisema Sh. bilioni 133 zilizokuwa kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kama zisingeibwa na wajanja wachache, zingeweza kutumika kujenga vyumba 19,000 vya madarasa na kusaidia watoto wa maskini kupata elimu bila tabu.
Alibainisha kuwa, chini ya CCM kamwe umaskini hauwezi kuondoka nchini kwani badala ya kushughulikia tatizo hilo, imekuwa ikiendekeza propaganda kupitia nyimbo za kikundi chake cha burudani cha Tanzania One Theatre (TOT) kuwahadaa Watanzania kwamba, 'wanapendeza', huku wengi wao wakiishia kuusikia mlo wa asubuhi (chai) redioni. Lwakatare alisema chama hicho kimekuwa kikiulea umaskini na imekuwa ikiutumia kama ndoano ya kuvuna kura za wananchi nyakati za uchaguzi.
Alizifananisha shule za sekondari za kata sawa na vituo vya kukulia watoto kutokana na kukosa nyenzo za kufundishia, kama vile maabara. Lwakatare alisema Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama, ni miongoni mwa wabunge wa CCM, ambao wamekuwa wakipitisha bajeti za mabilioni ya shilingi bungeni kwa ajili ya kujenga shule za kata lakini zikishajengwa wabunge hao awawapeleki watoto wao kwenda kusoma kwenye shule hizo. "Wanajua shule hizi hazitatoa madaktari na wataalamu wengine. Badala yake wanawapeleka watoto wao kwenda kupata elimu nzuri Ulaya. Matokeo yake imekuwa akiondoka Kawawa anakuja Kawawa, akiondoka Mwinyi anakuja Mwinyi," alisema Lwakatare.
Alisema CCM imekuwa na tabia ya kuwahitaji wananchi wakati wa uchaguzi tu, mithili ya kuku wa kienyeji, ambaye mmiliki wake akihitaji kitoweo, humdanganya kwa mahindi ili amkamate na kumchinja. "Kama Tanzania bila ukimwi inawezekana, basi Tanzania bila CCM pia inawezekana," alisema Lwakatare. Aidha, alisema vijiji vinavyoongozwa na CCM, havina maendeleo, na kuwataja wananchi kujiunga na Chadema kwa sababu inauwezo wa kuleta mabadiliko nchini.
Lwakatare alisema ndani ya CCM kuna makundi matatu; kuna 'CCM tafuta kivuli', 'CCM maslahi' na 'CCM kiherehere'. Alisema miongoni mwa wanaoteseka nchini, ni askari polisi, ambao wengi wao wamekuwa wakiishi katika nyumba za mateso. "Kule kwetu Kagera askari wamejengewa nyumba, juu bati, pembeni bati. Likija jua mnaokwa kama mikate, ikija baridi utadhani mochwari gani sijui.
Sasa haya ni maisha gani?" alihoji Lwakatare.
Kabla ya kuhutubia mkutano huo, Lwakatare akiongozana na viongozi wa Chadema Mkoa wa Ruvuma, alifungua matawi matatu ya chama likiwamo tawi la Mapambano Kata ya Majengo, Londoni na Kichangani, yaliyoko mjini Songea na Songea Vijijini.
IPPMedia