CCM: Nafasi ya Makamu Mwenyekiti yageuka gumzo
ZIKIWA zimebakia wiki mbili kufikia uchaguzi Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya taifa joto limeanza kupanda kwa baadhi ya makada wanaotajwa kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti Taifa.
Kwa mujibu wa taratibu na kanuni za CCM nafasi hiyo haigombewi bali jina la atakayependekezwa na Kamati Kuu kushika wadhifa huo, litajadiliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na baadaye kupelekwa katika Mkutano Mkuu ili lipigiwe kura.
Nafasi ya Makamu Mwenyekiti kwa sasa inashikiliwa na John Malecela ambaye kwa mujibu wa Mwenyekiti wa CCM Jakaya Kikwete, ana nafasi sawa na makada wengine katika kutetea kiti hicho kufuatia muda wake kumalizika.
Malecela amekalia kiti hicho tangu awamu ya pili iliyokuwa chini ya Ali Hassan Mwinyi, kisha awamu ya tatu chini ya Benjamin Mkapa na sasa awamu ya nne iliyoanza chini ya Kikwete.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanaeleza kuwepo ugumu wa Malecela kubakiza kiti hicho kufuatia wimbi linalohitaji wazee kupumzika, ili kupisha damu changa.
Lakini hali ikiwa hivyo kwa Malecela, mkongwe mwingine kutoka awamu ya kwanza hadi sasa Kingunge Ngombale-Mwiru, naye anatajwa na baadhi ya wanachama wa CCM kuwa anaweza kuteuliwa kushika nafasi hiyo.
Wanaomtaja Kingunge wanaeleza kuwa kiongozi huyo amekuwa karibu na Mwenyekiti wa CCM kwa kipindi kirefu na ndiye pekee anayeweza kuzima harakati za makundi yanayoongozwa na wana CCM wakongwe ili kufanya uongozi wa Kikwete kufanikiwa bila mawimbi.
Jina lingine linalozungumzwa ni la Katibu wa sasa wa CCM, Yusuf Makamba. Makamba anatajwa kuwepo kwenye orodha ya kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti, ikiwa ni mpango wa Mwenyekiti Kikwete kumuengua kiustaarabu kutoka katika nafasi ya utendaji ambayo anaonekana kupwaya.
Katika siku za hivi karibuni Makamba amehusishwa na migogoro mingi katika sehemu mbalimbali anazotembelea, hasa kufuatia tabia yake ya kuwafokea viongozi wa chama hadharani na kuwapigia debe baadhi ya makada anaowataka kushinda nafasi za uongozi.
Katika orodha hiyo, pia limo jina la Spika Mstaafu wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdulrahman Kinana. Kinana anaelezwa kuwa karibu na Kikwete kuanzia wakati wa harakati zake za kuwania urais.
Baadhi ya makada wa CCM wanasema Kinana ni mmoja wa vigogo walio karibu na rais ambaye hajapewa nafasi ya juu ya uongozi katika serikali na chama, huku pia akionekana kutumika katika matukio ya kusuluhisha migogoro kadhaa ndani ya CCM hasa mkoani Mbeya.
Kazi hizo za usuluhishi zinaelezwa kupewa kwake moja kwa moja na Kikwete kama harakati za kumuandaa kwa wadhifa wa Makamu Mwenyekiti.
Kinana pia anaonekana kukubalika na kundi la vijana, ambalo linamtazama kama kiongozi anayeweza kukubaliana na mabadiliko yatakayowawezesha baadhi ya wakongwe kukaa kando na kubakia na kazi ya ushauri.
Pia kunatajwa jina la Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa sasa, huyu baadhi ya watu wamekuwa wakimtaja kuwa ana harakati za kuwania urais siku zijazo.
Watu walio karibu na Lowassa ambao walipata fursa ya kuzungumza na gazeti hili, walieleza kusikitishwa kwao kuhusu fikra hizo huku wakifafanua kuwa, Lowassa hana nia ya kusaka nafasi hiyo.
"Kazi aliyonayo katika serikali ni kubwa na inayomtaka kuwajibika kila siku. Hawezi kuwa na nia tena ya kutaka nafasi ya Makamu Mwenyekiti.
"Tena wanaozungumzia suala la yeye kutamani urais wanapoteza muda kwa kuwa muda wa Kikwete utakapomalizika atakuwa na umri zaidi ya miaka 60.
"Yeye alikuwepo katika kundi linalopinga wakongwe kung'ang'ania madaraka sasa iweje kesho ajitokeze kupingana na falsafa yake? Ni wazi wanaozungumza hivi wanakosea," mmoja wa watu wa karibu na Lowassa aliliambia gazeti hili hivi karibuni.
Uchaguzi Mkuu wa CCM unatarajiwa kufanyika wiki ya kwanza ya Mwezi Novemba.
Source: Mwananchi