CCM yataka kila wilaya kuwa Jimbo
Martha Mtangoo, Dodoma
Daily News; Monday,November 10, 2008 @21:15
Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imeunda kamati teule ya kupitia mapendekezo kuhusu namna ya kuwapata wabunge na wawakilishi wanawake ambapo imependekeza kila wilaya kuwa jimbo litakaloongozwa na mwanamke na kufikia asilimia 50.
Ili kufikia asilimia 50, NEC hiyo ya CCM imetoa pendekezo la kuzifanya wilaya zote nchini kuwa majimbo ya uchaguzi kwa ajili ya wagombea wanawake. Aidha, NEC imeomba serikali kuharakisha kutunga sheria ya uchaguzi itakayomtaka kila mgombea kueleza fedha anazotumia katika kampeni amezipata wapi na zimetumikaje, sheria ambayo sasa haipo.
Katibu wa NEC wa Itikadi na Uenezi, John Chiligati aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa jana kuwa kwa utaratibu huo wa uwakilishi, utawezesha kupatikana kwa wabunge wanawake 137 kutoka wilaya 137 za Tanzania Bara sawa na asilimia 38 katika Bunge la Muungano.
Alisema kwa upande wa Baraza la Wawakilishi, wawakilishi wanawake 20 kutoka wilaya 10 za Zanzibar ambapo kila wilaya za Unguja na Pemba, watatoka wanawake wawili. Alisema pia wanawake wataendelea kugombea katika majimbo 232 yaliyopo hivi sasa katika Bunge la Muungano ambako asilimia 12 iliyobaki inaweza kupatikana ili kufikia asilimia 50.
Alisema Kamati hiyo teule chini ya aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Dk. Mohamed Gharib Bilal, imepewa jukumu la kuchambua kwa makini namna ya pendekezo hilo linavyoweza kutekelezwa. Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Makamu Mwenyekiti Anne Makinda; Dk. Maua Abeid Daftari, William Lukuvi, Jenista Mhagama, Machano Othman Said, Andrew Chenge, Mtumwa Kassim Idd na Dk. Milton Mahanga.
Chiligati alisema pia kamati hiyo itaangalia uwezekano wa kuundwa upya majimbo ya sasa kwa lengo la kuyapunguza ili kila jimbo liwe na wabunge na wawakilishi wawili, mmoja akiwa ni mwanamke na wa pili akiwa ni mwanamume ili idadi ya wabunge isizidi 360.
Alisema NEC imeipa kamati hiyo jukumu la kuona uwezekano wa Tanzania kutumia mfumo wa uwakilishi wa uwiano ambao vyama huandaa orodha ya wagombea wa ubunge na kuikabidhi kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ambapo baada ya uchaguzi, kila chama hupata idadi ya wabunge kulingana na wingi wa kura alizopata.
Aliitaja kazi nyingine ya kamati hiyo ni kuchambua utekelezaji wa pendekezo la namna ya kuwashirikisha wanaCCM matawini katika kupiga kura za maoni za kuwapata wagombea wa ubunge na uwakilishi. Alisema chini ya utaratibu huo, kura za maoni zitapigwa na wajumbe wa mkutano wa Jimbo tofauti na ilivyo sasa.
Alisema kamati hiyo imepewa muda wa mwezi mmoja kukamilisha kazi hiyo, na mapendekezo hayo yatajadiliwa na kupitishwa katika kikao kijacho cha NEC na baadaye kufikishwa kwa wananchi kwa kujadiliwa na kupata mwafaka iwapo serikali pia itaridhia mapendekezo hayo.
Kuhusu uharakishaji wa kutunga sheria ya fedha za kampeni, Chiligati alisema ombi hilo limetolewa kutokana na baadhi ya wagombea katika uchaguzi mbalimbali na hasa uchaguzi mkuu kutumia fedha nyingi, jambo ambalo limedaiwa kuwa limekuwa linaigawa CCM.
Chiligati alisema NEC imejadili na kuomba sheria hiyo itungwe haraka ili ianze kutumika katika Uchaguzi Mkuu ujao ili kuziba mianya ya rushwa na hasa katika kipindi cha uchaguzi. Alisema sheria hiyo itakapotungwa na kuanza kutumika, itadhibiti vitendo vya rushwa ambapo kila mgombea atatakiwa kuelezea ni namna gani ametumia fedha katika uchaguzi na fedha hizo amezitoa wapi na pia sheria hii itaweka kiwango cha juu cha fedha ambazo zitatakiwa kutumika katika uchaguzi.
Katika sheria hii, itamtaka kila mgombea kuelezea pesa anazofanyia kampeni amezitoa wapi na kwa akina nani na hao watu wataulizwa iwapo ni kweli na pia mgombea atatakiwa kuelezea pesa hizo amezitumiaje katika uchaguzi. Mgombea ndani ya chama kuwa na mapesa mengi anakigawa chama, alisema Chiligati.
Kuhusu rufaa ya Nape Nnauye, Chiligati alisema NEC haikuijadili kutokana na rufaa hiyo kwenda moja kwa moja kwa Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete. Aidha, Chiligati alisema NEC haikuwa na ajenda ya kumjadili Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba na kuongeza kuwa ajenda hiyo haikuwapo na haitakuwapo.
Alisema NEC ilipitisha majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali wa Jumuiya; na kwa nafasi Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Taifa ni Suleiman Muhsun Haji, Hamad Masauni Yussuf na Adilla Hilai Vuai; wakati kwa Makamu Mwenyekiti ni Beno Malisa, Zainabu Rashid Kawawa na Hussein Bashe.
Kwa upande wa Umoja wa Wanawake (UWT), waliopitishwa ni Janet Kahama, Joyce Masunga, Sophia Simba kwa Uenyekiti na Makamu Mwenyekiti ni Asha Bakari Makame. Kwa Uenyekiti wa Wazazi ni Alhaji Abdallah Bulembo, Athumani Mhina na Esther Nyawazwa huku nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni Khamis Suleiman Dadi, Haidar Haji Abdallah na Dogo Iddi Mabrouk.