Ungeweka hapo chini kuwa ni copy & paste. Huko ulipolitoa, copy hii post ukapste huko.
Sawa Mkuu ,Bandiko ni hili
WANAGOMBANA WANASIASA, WANAKUFA RAIA, WANARIDHIANA WANASIASA
WANANCHI ni mtaji wa wanasiasa. Yupo mtu atahoji, je, wanasiasa siyo wananchi? Zaidi ya karne moja iliyopita, mwanasosholojia na mbobezi wa sayansi ya jamii wa Ujerumani, Max Weber, alipata kusema kuwa mwanasiasa siyo mwananchi wa kawaida.
Weber alisema: “A politician lives for politics, or lives off politics. A normal citizen lives for his family. That is the difference” – “Mwanasiasa anaishi kwa ajili ya siasa, au ananufaika kupitia siasa. Mwananchi wa kawaida anaishi kwa ajili ya familia yake. Hiyo ndiyo tofauti.” (Max Weber, kitabu cha Politics as a Vocation - ‘Siasa kama Wito’ - cha mwaka 1919).
Dunia ni ileile. Machafuko Kenya baada ya Uchaguzi Mkuu 2007, watu wanaokadiriwa kufikia 1,133, walipoteza maisha, wananchi zaidi ya 350,000 waligeuka kuwa wakimbizi wa ndani. Hii ni kwa mujibu wa Ripoti ya Tume ya Jaji Philip Waki (CIPEV Report, 2008, Waki Commission).
Baada ya madhara makubwa kwenye nchi, vifo 1,133, wanasiasa, Mwai Kibaki na Raila Odinga, wakiwa na timu zao, walisuluhishwa na wanasiasa kutoka nje ya Kenya, maridhiano yalifanyika, wakagawana vyeo, Kibaki aliendelea kuwa Rais, Raila Waziri Mkuu. Maisha ya kugawana mkate.
Yule babu wa Naivasha aliyepoteza wajukuu zake, mama wa Kibera aliyegeuka mjane baada ya mume wake kuuawa, mwanafunzi wa Kakamega aliyebaki yatima, hawakuwepo Harambee House, Februari 28, 2008, wakati Kibaki na Raila walipotiliana saini kugawana mkate wa nchi.
Dunia ni hiyohiyo; Zimbabwe, baada ya Uchaguzi Mkuu 2008. Watu zaidi ya 200 waliuawa. Mgogoro wa matokeo ya uchaguzi baina ya aliyekuwa Rais, Robert Mugabe, na mpinzani wake, Morgan Tsvangirai. Mwisho, Mugabe aliendelea kuwa Rais, Tsvangirai, akawa Waziri Mkuu. Yalifanyika maridhiano ya kugawana keki kwenye dimbwi la damu za Wazimbabwe.
Ndicho kinaendelea Sudani Kusini. Nchi mpya kabisa duniani. Mwaka 2011 ilipata uhuru wa damu, baada ya kufanikiwa kujitenga kutoka nchi ya Sudan. Mwaka 2013 (miaka miwili baada ya uhuru), Rais wa Sudani Kusini, Salva Kiir na Makamu wake, Riek Machar, waliingia kwenye migogoro iliyozua mapigano ya kikabila. Jamii za Dinka na Nuer zinauana hadi leo.
Ukitafutwa mwafaka, Kiir na Machar wanapeana mikono na kuendelea kutafuna utajiri wa mafuta ya Sudani Kusini. Wakigombana, wanauawa raia. Watu zaidi ya 400,000 wameshapoteza maisha Sudani Kusini. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2021 ya Baraza la Uhusiano wa Kigeni la Marekani (Council on Foreign Relations, 2021).
Itafute dunia ya machafuko popote ilipo, utawaona wanasiasa katikati ya migogoro, kisha utawashuhudia wakipeana mikono kwa tabasamu, bashasha na vicheko, kama mashujaa wa maridhiano. Huchanua kama mashujaa wakati ndani ya familia zao hakuna damu iliyomwagika.
Januari 5, 2011, watu watatu waliuawa Arusha. Walikuwa vijana, wananchi wa kawaida. Sababu ilikuwa mvutano baina ya viongozi wa Chadema na polisi. Vijana walipokea wito kutoka kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, kuhakikisha Freeman Mbowe (Mwenyekiti Chadema wakati huo) na Godbless Lema (alikuwa mbunge Arusha Mjini), wanafuatwa Kituo Kikuu cha Polisi Arusha, walipokuwa wameshikiliwa mahabusu.
“Nawaagiza vijana, kabla sijaondoka hapa muwe mmewaleta hapa Mwenyekiti na Mbunge,” Dk Slaa, Viwanja wa NMC, Unga Limited, Arusha, Januari 5, 2011. Vijana waliitikia wito, walianza msafara kwenda Kituo Kukuu cha Polisi (Central) Arusha. Polisi walitumia risasi za moto, watu watatu walipoteza maisha.
Baada ya hapo ilifuata tamthiliya ya wanasiasa kuonesha kuguswa na vifo hivyo. Kila upande ukijisogeza kwa familia za marehemu. Mwisho, viongozi wa Chadema na CCM, walionekana Ikulu, kikaoni na Rais aliyekuwa madarakani, Jakaya Kikwete. Walikunywa chai, kahawa, tangawizi, wakatafuna korosho, karanga, almond, visheti. Walipata mlo wa pamoja na kusonga mbele.
Wazazi wa vijana waliopoteza maisha Arusha hawakuwa sehemu ya mazungumzo Ikulu. Taifa halikumbuki kilichojiri Arusha Januari 5, 2011. Hakuna chama cha siasa kimetunza kumbukumbu ya vifo vya watu hao. Hata mahali walipouawa, hamna alama yoyote kukumbuka kilichojiri na kutoa funzo la wanasiasa na matumizi ya watu kama mtaji wao.
Januari 12, 2011, Chadema walifanya tukio kubwa la ibada ya kuwaaga marehemu. Mbowe na Lema walikuwa mstari wa mbele kubeba majeneza ya marehemu. Baada ya hapo ikawa kimya. Waliouawa ni Denis Shirima, Omary Ismail, na raia wa Kenya, Paul Njuguna. Nani kati yao anakumbukwa kwa jinsi damu yake ilivyomwagika katika mapambano ya demokrasia?
Hisia hizohizo zielekee kwenye matukio ya Oktoba 29, 2025. Ripoti ya Tume ya Jaji Othman Chande imeeleza vifo ni zaidi ya 500. Hao ni wananchi wa kawaida, hasa vijana, wake kwa waume. Hakuna nyumba ya mwanasiasa anayefahamika kitaifa, kulitokea msiba. Maana yake, wanasiasa walilinda familia zao. Wananchi wa kawaida, damu za familia zao zikawa sadaka.
Walioanzisha vuguvugu la “No Reforms, No Election” – “Bila Mabadiliko ya Katiba, Hakuna Uchaguzi”, na waliosimama kidete kujibu “Oktoba Tunatiki”, walikuwa wanasiasa. Machafuko yalipotokea, wao walibaki salama na familia zao. Wananchi wa kawaida wakapoteza maisha. Familia zao zikaingia msibani.
Kama yalivyotokea mataifa mengine, ndivyo na Tanzania. Wito wa Maridhiano. Njia ileile, kuridhiana wanasiasa kwa wanasiasa. Waliosema No Reforms, No Election, wafanye mapatano na walionena, Oktoba Tunatiki.
“We cannot solve our problems with the same thinking we used when we created them." - “Hatuwezi kutatua matatizo yetu kwa kufikiri kwa namna ile ile tuliyotumia kuyaleta." – Mwanazuoni Albert Einstein, katika barua yake kwa aliyekuwa Rais wa Marekani, Harry Truman, kuhusu Elimu ya Atomic, mwaka 1946.
Wanasiasa walisababisha mkwamo wa kisiasa, kisha machafuko ya Oktoba 29, 2025. Hivyo, wanasiasa hawapaswi kutumika kama nyenzo kuu ya kuiponya nchi. Hata Januari 26 na 27, 2001, Zanzibar, wanasiasa walizua chokochoko, vifo vikatokea, baadaye yalifanyika maridhiano ya kisiasa, je, suluhu ya kudumu Zanzibar imewahi kupatikana?
Maridhiano ya ghasia za Oktoba 29, 2025, hayapaswi kuwatazama wanasiasa kama nyenzo kuu. Makundi ya ya umma (Minipublics), yatumike kuponya taifa. Bodaboda, madereva kwa makondakta wa daladala, mama kwa baba lishe, wamachinga, walimu, madaktari, wauguzi, wasusi kwa vinyozi saluni, na kadhalika, watumike kuijadili na kuirudisha nchi pamoja.
Makundi ya kijamii ni muhimu, maana wao siyo walioanzisha tatizo ila ndiyo walioathirika. Wanasiasa wanapoingia kwenye mazungumzo huzingatia masilahi, kwa hiyo hupima kwanza na kutoa masharti. Wananchi wa kawaida hawatangulizi masharti kwenye ustawi taifa lao. Mjadala wa uponyaji uwe mpana. Elimu itolewe. Maridhiano yafanyike, kisha ujenzi wa taifa bora uendelee.
Ndimi Luqman MALOTO