Big Brother Africa: What a waste!

Huku tunaponda wakati watu huko utamu umekolea.

Utamu wa Big Brother waanza kukolea
Mwandishi Wetu
HabariLeo; Saturday,October 06, 2007 @00:04

Washiriki wa Shindano la Big Brother wakiwa katika picha zinazoonyesha matukio tofauti ndani ya jumba hilo.

JUMATANO wiki hii Richard, mshiriki wa shindano la Big Brother Africa kutoka Tanzania na ambaye anadai kwamba amechoka na anataka kujitoa kwa hiyari, alisababisha mtafaruku ndani ya jumba wanaloishi na wenzake nchini Afrika Kusini wakiwania donge nono la dola za Marekani 100,000 (sawa na Sh milioni 130) kwa mtu atakayekuwa wa mwisho kutolewa.

Chanzo cha mtafaruku huo ni kitendo cha Richard cha kumwita mshiriki Maureen kutoka Uganda kama Shorty. Neno hilo laweza kumaanisha fupi kwa Kiingereza cha mtaani, lakini kwa Richard na wenzake, neno hilo limekuwa likitumika kumaanisha kipenzi.

Kwa hiyo Richard alipomwita Maureen Shorty, lilikuwa jambo la kushtusha kidogo, hasa kwa Code kutoka Malawi, ambaye katika siku za karibuni yeye na Maureen wamekuwa wakionyesha mvuto wa kimahaba baina yao.

Kwa lugha nyingine, ilikuwa kama vile Richard alikuwa akimaanisha kwamba Maureen ni kidawa wake, jambo ambalo pengine haliwezekani kwa kuwa, ingawa ndiye mshiriki pekee mwenye mke miongoni mwa washiriki waliobaki, lakini naye pia ana mwandani wake ndani ya jumba la Big Brother, ambaye ni Tatiana kutoka Angola.
Alipoulizwa baadaye siku hiyo na mwongozaji wa Big Brother sababu za ‘uchokozi' wake huo kwa kumwita Maureen Shorty, Richard alisema alifanya vile kwa makusudi kwa sababu alitaka kuona ni kwa namna gani Code na Tatiana wangeumia kwa wivu.

Wivu? Naam. Hii ni kwa sababu kutoka katika lile kundi la watu 12 walioingia katika jumba lile mwanzoni mwa Agosti, kwa sasa kila mshiriki ni kama vile ana barafu wake wa moyo. Richard yuko na Tatiana kiasi kwamba mashabiki wanawaita Richiana, Code amekwisha kwa Maureen wakati Kwaku wa Ghana na Bertha wa Zimbabwe wanazidi kuiva chungu kimoja. Mshiriki anayeonekana kubaki ‘kivyake, kwa sasa ni Ofuneka wa Nigeria.

Na hapo ndipo wachunguzi wa mambo wanaposema kwamba utamu wa Big Brother ndiyo unaanza kukolea. Kwa nini?

Wakati utakapokuwa unasoma makala haya, itakuwa imebaki siku moja kabla hatujafahamu matokeo ya kura za watazamaji za nani atoke kwenye Big House kesho Jumapili usiku. Wanaopigiwa kura ni Kwaku na Bertha na inabidi kuamini ujumbe wa sms unaotumwa kutoka sehemu mbalimbali za Afrika na kuonyeshwa kwenye runinga ya DStv inayorusha matangazo hayo na katika tovuti yake, yaelekea upepo unamwendea vibaya Kwaku.

Kwa nini iwe Kwaku? Ujumbe kadhaa uliokwishatumwa hadi sasa dhidi yake umekuwa ukionyesha kwamba watazamaji wengi hawafurahishi na namna Mghana huyo anavyoendesha maisha yake katika jumba la Big House. Wanamwona kama ni mwenye majigambo na anayejiona bora kuliko wengine. Jingine linalowakera kuhusu Kwaku ni namna anavyoitumia lugha ya Kiingereza, lugha rasmi na pekee ndani ya Big House. Kwa watazamaji walio wengi Kwaku anajikwaza mno kwa kutumia lafudhi ya Kimarekani. Kwa kuwa anaonekana kama azungumzavyo lafudhi hiyo si kwa asili yake na anaiigiza, Kwaku anaonekana hana uasilia, msanii ambaye badala ya kuburudisha amekuwa kero kwa washiriki wenzake na watazamaji pia.

Ionekanavyo njia pekee ya kumfanya asiendelee kuwakera watazamaji ni kwa kumpigia kura za kumtoa ili awaache washiriki wenye kuburudisha na kuleta uhai ndani ya Big House waendelee kukonga nyoyo za watazamaji. Wanataka ‘wapendanao' ndio wabaki ndani ya jumba hadi hatma yao itakapofahamika Novemba 4, ya nani mshindi wa Sh milioni 130.

Mazingira haya yanaonyesha kwamba akina Richiana, na hasa mmoja kati yao, wana nafasi kubwa ya kunyakua zawadi hiyo nono. Kwa kutambua hilo inaanza kudhihirika kwamba baada ya Bertha au Kwaku kutolewa kesho, zitapigwa hesabu za haraka miongoni mwa watakaobaki kuhusu nani apendekezwe nao kupigiwa kura za kumtoa, si kwa sababu ni dhaifu zaidi, bali kwa sababu ndiye tishio zaidi na mwenye uwezekano mkubwa wa kutwaa zawadi.

ASEMAVYO RICHARD NA WENZAKE Dalili za nani wanaanza kuwekwa kwenye mtego zilijidhihirisha Jumatano wakati Big Brother alipokuwa amewaita washiriki, mmoja baada ya mwingine kwenye chumba cha mazungumzo ya faragha kinachofahamika kama Diary Room au Chumba cha Shajara.

Alipoitwa Ofunneka alidokeza kwamba ni dhahiri Bertha na Kwaku sasa wamekuwa chanda na pete. Akaongeza kwamba ingewezekana penzi lao hilo lingechipuka mapema bali lilikwazwa na ‘ubishoo' wa wote wawili. Akamwambia Big Brother kwamba Richard na Tatiana wako katika mazingira ya ‘pata potea' huku akilaani kitendo cha Richard kumwita Maureen Shorty kwa vile kimemuudhi Code.

Akafuata Maureen ambaye alisema katika siku za karibuni hayuko karibu sana na Tatiana kama ilivyokwa wakati walipoingia katika jumba hilo. Kwa nini? "Ni kwa sababu ya Richard," akasema. "Inabidi ampe (Tatiana) uhuru fulani. Naye pia anasema Code hajafurahi jinsi Richard alivyomwita Maureen Shorty.

Akafuata Richard na jitihada zake za kuhalalisha sababu za kumwita Maureen Shorty halafu ikawa zamu ya Tatiana aliyemweleza Big Brother kwamba Richard amemfahamisha kwamba alifurahia muda wa faragha aliotumia na Richard huko Penthouse ambako washiriki wawili tu hubaki, mbali na wenzao. Akasema alivyoambiwa na Richard kwamba ataomba kwa Big Brother ajitoe mwenyewe kwa ridhaa yake kutoka kwenye jumba hilo. Hata hivyo Tatiana alisema anafahamu Richard hana ubavu wa kufanya hivyo ingawa alipoulizwa itakuwaje pindi Richard akifanya kweli, ilibidi ajibu; "itauma sana."

Ilipowadia zamu ya Bertha alibainisha kwamba hana imani na Code. Akasema kwa jinsi ambavyo hivi sasa ni kama vile hakuna chumba cha wanaume wala cha wanawake ni rahisi kufahamu nini kinachoendelea ndani ya jumba hilo. Ndiyo maana na yeye analala kwenye chumba cha wanaume. Bertha alikuja na matamshi ya kushangaza kidogo kuhusu Maureen, akasema kwamba anashindwa kumwelewa binti huyo wa Kiganda ingawa anahisi ana ajenda ya siri. "Ndiye mtu wa hatari zaidi ndani ya Big Brother. Anasema hivyo kwa sababu Maureen anawasiliana vizuri na washiriki wengine wote na amenusurika mara mbili kutolewa ndani ya jumba hilo.

Kwaku alipoingia katika chumba cha Shajara alikuwa na mengi ya kusema, ikiwamo mashambulizi dhidi ya Richard huku akieleza kushangazwa na hatua ya Mtanzania huyo ya kuondoa godoro moja kutoka kwenye chumba cha wanaume ambalo analitumia kwenye chumba cha wasichana. Ingawa alisema hajali hata kama atatolewa kesho, anamhurumia Ofuneka kwa kumlinganisha na kishada ambacho hakina mwenyewe kwa vile hana uhusiano wa kimapenzi na yeyote ndani ya Big House.

Licha ya kutofurahishwa kwake na alichokifanya Richard, Code alikiri kwamba kama ni mbio, basi akina Richiana walizianza mapema na wako mbele. Akamweleza Big Brother kwamba anafahamu kuna nyufa katika uhusiano wa baadhi ya washiriki na anavyopanga kuwa na mkakati wa pamoja na Kwaku.

Mkakati wa pamoja? Itabidi watazamaji wasubiri kufahamu ni mkakati gani huo. Vyo vyote iwavyo, kama Kwaku hataenguliwa kesho, basi lengo la Code ni kukusanya nguvu zake na washiriki wengine watakaobaki – iwe yeye na Maureen; yeye Maureen na Ofuneka au yeye Maureen, Ofuneka na Bertha kukabiliana na Richiana.

WASEMAVYO WATAZAMAJI Watazamaji wanayaona yote hayo na ujumbe wao kwenye runinga na kwenye tovuti unabeba maana nyingi. Mifano ipo kama inavyotolewa hapa kwa tafsiri isiyo rasmi kutoka katika lugha ya Kiingereza.

Swali kwa Kwaku na Bertha. Kwaku, utakubali Bertha ashinde au Bertha utakubali Kwaku ashinde? Nadhani jibu ni hapana, aliandika mtazamaji anayefuatilia kutoka Uingereza.

Mwingine aliyejitaja kama MaMox kutoka Botswana alikuwa na haya ya kusema; Richard alikuwa anafanya mzaha, hafiki po pote. Nadhani ameanza kuhisi kwamba watazamaji wamechoka na masuala ya u-Richiana. Sasa anamjaribu Maureen ili awaudhi Code na Tatiana. Anajua anakichokifanya…endelea na mchezo wako bwana.

Mtazamaji mwingine alikuwa kama anajihoji mwenyewe aliposema ifuatavyo; Kwa hiyo Richard alimwambia BB (Big Brother) kwamba anataka kujitoa kutoka kwenye jumba hilo? Huyu Richard lazima amewahi kuwa na uhusiano na akina Tatiana wengi tu kabla hajaingia humo. Nionavyo mimi wanachezeana na kutaniana tu humo na hasa kwa ajili ya watazamaji.

Ujumbe wa Ronnie Blanks aliyejitambulisha anatoka Uganda ulikuwa na utabiri mwingi. Huyu Richard ameanza kunoa ubongo wake. Wote walioingia katika jumba hilo wamefuata fedha na si uhusiano wa kimapenzi. Kwa hiyo anachojaribu kufanya Richard ni kumuudhi Code ili Code apendekeze kwamba atolewe na ukweli ni kwamba Code ameudhika na atakuwa na kila sababu ya kupendekeza Richard atolewe. Hebu tuharakishe kumtimua Bertha ili tuanze kufaidi uhondo wa Big Brother. Watazamaji tutarajie moto (miongoni mwa washiriki) wiki ijayo…

Ukweli ulivyo ni kwamba wafuatiliaji wengi wamekuwa wakimlenga Richard na Tatiana wake akiwamo Yakikay kutoka Malawi aliyeandika;

Richard!! Richard!!!! Masikini Richard! Jamani tumtoe Richard baada ya Bertha . Richard amekumbuka mno kwao na hawezi kufanya lo lote bila Tatiana kuwa karibu naye. Tuokoe ndoa yake na akili yake kwa kumpigia kura za kumtoa.


Mwingine aliyejitambulisha kama Lydia Gauteng ameandika kutoka Marekani;
Hawa akina Richiana ni kero kwa kila mtu. Namlaani baba yake Richard kwa kumruhusu mwanawe afanye uchafu huu, kaka yake pia, nawalaani kwa kumuunga mkono Richard. Ingekuwa mimi nisingeruhusu mwanangu amdhalilishe binti wa mzazi mwenzangu kiasi kile. Na mnadai kwamba hiyo ni burudani?

Richard haheshimu wanawake. Jamaa ana tabia fulani ya kutojiamini. Mwanaume gani aliyeoa anaweza kumvunjia heshima mkewe kwenye kipindi cha televisheni namna ile. Hebu angalieni alivyomdhalilisha Tatiana.

Huyu Tatiana ni mwanamke mwenye hadhi yake kwenye nchi anayotoka. Huyu ni muigizaji na mwanamitindo lakini Richard amemfanya kama vile ni gunia la takataka. … sidhani hata kama bwana yake atamsamehe.

Richard ni kama mhuni tu. Anawazuga mashabiki wake kwa kusema kwamba anataka kutoka mwenyewe kwa hiyari kwenye Big House. Kwa bahati mbaya hawezi kutuzuga watu ambao tumekuwa tunafuatilia onyesho hilo tangu siku ya kwanza. Anafahamu kuwa mambo yataanza kupamba moto wiki ijayo na ili kujiepusha na shari na aibu ya kupigiwa kura ya kutolewa na kurudi kwa mkewe bila senti anataka kujiengua kwa ridhaa yake. Aibu iliyoje?

Mtazamaji kutoka Tanzania aliyejitambulisha kama Malmorr aliweka ujumbe ufuatao Jumatano wiki hii;

Mashabiki wa Richiana inabidi mfikiri kwa makini. Ingawa sikuwa nikimpenda Bertha na ninatamani nimtoe kutoka katika jumba hata sasa, inabidi nianze mikakati ya kumtoa Kwaku ili kuwalinda akina Richiana. Kwa hali ilivyo atakayefuata kupendekezwa na wenzake kutoka kwenye jumba wiki ijayo ni Bertha.

Lakini ikitokea kwamba Bertha atapigiwa kura ya kuondolewa wiki hii, basi atakayefuata kupendekezwa kutoka atakuwa Richard na Kwaku. (Natabiri) Maureen atapiga kura za kuwatoa Richard na Kwaku, Code atafanya vivyo hivyo, huku Kwaku akiwafanyia hivyo Richard na Tatiana au Maureen na Code…

Naam, moto unaanza kuwaka kwenye Big Brother na Richard … Tusubiri hatma yake Jumatatu.

Makala haya yameandikwa kwa kutumia vyanzo mbalimbali, ikiwamo kufuatilia onyesho la Big Brother katika runinga na tovuti yake.
 
Akirudi jamaa atakuwa kwenye Bongo celebrety http://bongocelebrity.com/ kama nyota wa kitanzania aliyepeperusha bendera ya taifa kwa mashindano ya nyuchi!

Kwa kweli umenichekesha sana mtoto wa Mkulima, eti mashindano, ya nini??&$#***%^& For sure huu ni udhalilishaji. Hata kama kuna shida ya ajira nchini, sio sababu ya watu kujidhalilisha kiasi hiki. Na hapa suala sio kuacha kuangalia, bali kuyapiga marufuku kwa hapa kwetu, kwasababu usipoangalia wewe wengine wataangalia so udhalilishaji utakuwa palepale.
 
Ndugu zangu wote milio changia.... Tanzani tumeshaharibika kwa kutaka kuiga uzungu.... rais wetu hawezi kukemea hili shindano wala serikari haiwezi kulikemea kwa sababu tu ni la kizungu.... Rais wetu mwenyewe ananyenyekea wazungu kama ndio waliompigia kura....... kila siku anatafuta misaada mara marekani, mara uk yaani kila nchi anaenda kuombaomba utafikiri watanzania tumekuwa matonya.PILI ajira ni kimeo tanzania ndio maana watoto wetu wanaamua kujitosa wadhalilike ili wapate pesa.... Tanzania yetu ukiamua KUJIAJIRI utavunjiwa kibanda chako eti wanasafisha jiji.... ukiuza mama ntilie mgambo watakula chakula chako na kukutilia mchanga.... je pesa ambazo ndio kila kitu kwa maisha ya sasa zitapatikana kwa njia ip??????????

DK,Nadhani kama nakuelewa
 
Kwa kweli umenichekesha sana mtoto wa Mkulima, eti mashindano, ya nini??&$#***%^& For sure huu ni udhalilishaji. Hata kama kuna shida ya ajira nchini, sio sababu ya watu kujidhalilisha kiasi hiki. Na hapa suala sio kuacha kuangalia, bali kuyapiga marufuku kwa hapa kwetu, kwasababu usipoangalia wewe wengine wataangalia so udhalilishaji utakuwa palepale.

Tafadhali,
Naomba nikuulize hivi tukupe kazi ya wale Madada poa au hata wafagizi mabarabarani,wewe utaifanya?
Kwa kuangalia jinsi unavyo jichukulia yaani heshima yako sidhani kama utafanya kwani itakua kama kuji dhalilisha.
Sasa kama hivyo ndivyo,wakina dada poa na wafagizi daily wako kwani huko ndiko wanako pata mshiko wa kula na kuendesha maisha haya mabovu ya kitanzania.Sasa wewe sema tu wanajizalilisha.Bwana mdogo akija na mshiko wake akawekeza kwenye magazeti sidhani kama hauta endea omba kazi ya uandishi wa habari eti kwa sababu amepata hela kwa kukaa uchii kwenye BBA.
Bongo akiri kumkichwa,watu wanaangalia BBA kwa sababu wanataka kumwona dogo anaendeshaje maisha yake na yule dada wa sijui.. Kiangola...!
BBA ni kama tamthiliya ya kweli yaani non-fiction watu wamewekeza ili vitu kama hivyo vionekane,wewe umevua nguo mala ngapi na unajua wangapi wanakuona kwa muda huo?
Hata kama utamwona dogo mle ndani ile ndude... yake ngoja atue pale DIA alafu tuone umwambie nimekuona ile nanilii.... yako .

kuna ule msemo wazamani'..tafuta kama mtumwa ili uje ishi kama mfalme...'
 
Huu ni ubidhaishaji 'commodification' wa mwili. Hapa mwili unatumika kama bidhaa ya kujipatia pesa.. Huu ni ubepari mkongwe...
 
Mkuu watu hao akili yao iko kwenye kupata ushindi na umaarufu. Hayo mambo ya utamaduni wao hawajali hilo. Na wala hawakulazimishwa hayo ndiyo masharti ya BB na wameridhika nayo.
 
Huu uzi wa miaka 10 iliyopita yanayojiri muda huu huku mitaani ni zaidi ya big brother maadili yamezidi kuteketea umagharibi umejijumlisha na umashariki kifupi dunia imevaa bikini
 
Back
Top Bottom