Fundi Mchundo
Platinum Member
- Nov 9, 2007
- 8,409
- 6,060
Ingawa wazungu waliendeleza biashara hizo. Mfano mzuri ni Waafrica kuchukuliwa kwa nguvu kupelekwa America kuteswa na kuuzwa. Pia walituletea hata Africa. Kwa waliopata kutembelea Makanisa ya Mkunazini wataona athari zake hizo. Watumwa wakichukuliwa Bara na kuwekwa makanisani na kuuzwa. Hivyo ni kwa ufupi tuu. Ukitaka mengine Inshallah utapata majibu safi kabisa
Katika nchi nyingi za ulaya kukana kuwa palikuwa na Holocaust ni kosa la jinai. Wamefanya hivi kutokana kuwa na hofu ya kwamba kwa kukana ukweli huu kutaruhusu kupenyezwa tena imani na vitendo vya kibaguzi dhidi ya wayahudi. Hii ikiruhusiwa itapelekea kurudia hali iliyotawala katika miaka ya 30 ambapo jumuia ya kijerumani iliona ni haki kumdhalilisha, kumgandamiza na hatimaye kumuua myahudi. Hii hali wasingetaka irudiwe ndiyo maana wanakuwa wakali kuhusu mtu yeyote anayejaribu kuandika upya historia kufuta vitendo vya kikatili vilivyofanywa dhidi ya wayahudi na wale wengine waliioonekana hawana nafasi katika jamii ya kijerumani.
Watu weusi tulikuwa na holocaust yetu. Kwa miaka mingi, mataifa ya wale ambao rangi zao zilikuwa nyeupe kulingana na sisi walikuja Afrika kutuvuna na kutupeleka kutumikishwa katika mashamba yao huko marekani ya kaskazini na kusini, carribean na kwa hapa nyumbani huko Pemba na Unguja. Wengine wetu walichukuliwa kwenda kuhudumia majumbani mwa wale waliojiona bora kuliko sisi huko ulaya, uarabuni n.k. Huko uarabuni wengi walihasiwa. Msingi wa hii biashara nzima ulikuwa ni kuwa mtu mweusi hastahili kuhesabiwa kama binadamu wengine. Yeye alikaribiana na wanyama hivyo ilikuwa halali kumuuza na kumliki kama ambavyo unaweza kummiliki ng'ombe au punda wako. Mama zetu walikuwa watu wa kuzalishwa wasio na haki yeyote juu ya miili yao. Yote haya yalikubalika katika jamii za wazungu na waarabu.
Afrika ya magharibi biashara ilimilikiwa na mataifa ya Ulaya na yale ya kaskazini mwa Afrika. Wazungu waliwasafirisha watu weusi kupitia bahari ya Atlantiki na wale wa Afrika ya Kaskazini kuvuka jangwa la sahara. Hapa kwetu biashara ilimilikiwa na waarabu kutoka Oman ambao baada ya muda walifungua soko kubwa la watumwa unguja ambapo watu weusi waliosafirishwa kupitia bandari za Bagamoyo, Mikindani, Kilwa n.k. walipigwa mnada.
Moja ya vitu walivyovifanya waingereza walipoingia Zanziba ni kumlazimisha Sultan kusimamisha hiyo haramu. Pale palipokuwa na soko la watumwa pakajengwa kanisa na pale palipokuwa na mlingoti wa kuwauzia hao watumwa pakawa ndiyo altare ya kanisa.
Inakuwaje leo hii, mtanzania (Befair) anaweza kuamka na kudai kuwa biashara ya utumwa unguja iliendeshwa ndani ya makanisa kama alivyoandika mwandishi hapo juu kwenye sehemu ya Dini/Imani? Inakuwaje, mtanzania mwingine (Zomba) anakuja anatetea uwongo huo?
Sasa kwa nini nimeileta hapa? Hapa kinachonitatiza si suala la dini, ni hilo la historia yangu. historia ya wale walionitangulia, waliokamatwa, kubebeshwa mizigo na hatimaye kuuzwa kama punda na hao waliojiona kuwa ni waungwana. Uandikishaji upya wa historia ndiyo mwanzo wa kuweka mizizi ya chuki katika sehemu moja ya jamii yetu. Kama hao, ambao ni wachache, ndio waliosababisha babu zetu kuuzwa kwa nini tusibebe mawe na kuwavurumusha? Kwa nini tusibomoe hilo kanisa lao na kuweka kitu kingine mbadala?
Mawazo kama haya ya kichonganishi ndiyo yaliyowafikisha wenzetu huko Ireland, Rwanda, Yugoslavia ya zamani na sasa huko Kenya hapo walipo hivi sasa. Maneno ya kichochezi kama haya yanatakiwa kukemewa na wale wote wenye nia njema na taifa letu. Mimi sijui historia inafundishwa vipi huko Zanzibar. Lakini kama huu ni mfano wa matokeo ya mafunzo hayo, tuna matatizo makubwa mbele yetu. Ni imani yangu kwa dhati kuwa kuna vitu ambavyo inatubidi kama waafrika kusimama pamoja bila kujali itikadi au dini zetu. Hili ni mojawapo. Mungu atunusuru wote.