Alama za kutambua aina za maudhui ya filamu na umri sahihi wa mtazamaji

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
617
1,800
1644311584410.png

Kuna namna nyingi sana mtoto wako anaweza kufikia maudhui tofauti kwa kupitia vipindi vya televisheni na filamu kwa urahisi.

Watoto wa kizazi hiki wamekuwa na fursa nyingi zaidi za kutazama maudhui yasiyofaa. Uelewa wa mzazi kuhusu aina za filamu na vipindi vya TV au video za mtandaoni ni muhimu sana kwani mifumo ya ukadiriaji inaweza kutatanisha kutokana na mabadiliko au huenda ni kutokujua kabisa.

Ukadiriaji wa filamu (film rating) huwapa wazazi taarifa ya mapema kuhusu maudhui ya filamu ili kuwasaidia kubainisha ni filamu zipi zinafaa kwa watoto wao katika umri wowote. Ukadiriaji huwekwa kwa kuzingatia mambo kama vile vurugu, ngono, lugha na matumizi ya dawa za kulevya.

Hapa chini ni baadhi ya vipengele vinavyoainisha filamu kulingana na maudhui yake kwa mujibu wa Motion Picture Association of America (MPAA)


G General Audiences (Watazamaji Wote/wa Jumla)

Watu wa umri wowote wanakubaliwa kuangalia filamu hizi. Filamu ya G haina maudhui ya lugha chafu/mbaya, uchi, ngono, vurugu au masuala mengine ambayo yanaweza kuwaudhi wazazi ambao watoto wao wadogo hutazama.

Filamu zenye G haimaanishi kuwa ni za "watoto". Baadhi ya vijisehemu vya lugha vinaweza kwenda zaidi ya mazungumzo ya heshima lakini ni maneno ya kawaida ya kila siku. Uoneshaji wa vurugu ni kidogo. Hakuna uchi, matukio ya ngono au matumizi ya dawa za kulevya kwenye filamu hizi.

G.PNG

PG Parental Guidance Suggested (Mwongozo/Usimamizi wa Wazazi Unapendekezwa)

Baadhi ya maudhui huenda yasifae watoto. Filamu zenye PG zinapaswa kuchunguzwa na wazazi kabla ya kuwaruhusu watoto wao wadogo kutazama. Huenda kukawa na lugha chafu na vipande vifupi vya vurugu ndogo au uchi kwa kiasi kidogo lakini si ngono. Hakuna maudhui ya matumizi ya dawa za kulevya katika filamu hizi.

PG.PNG

PG-13 Parents Strongly Cautioned (Wazazi Wanatahadharishwa Sana)

Baadhi ya maudhui huenda hayafai kwa walio chini ya miaka 13. PG-13 ni tahadhari kali kwa wazazi ili kubaini kama watoto wao walio chini ya umri wa miaka 13 wanapaswa kutazama filamu hiyo, kwa sababu baadhi ya maudhui hayafai.

PG-13 inaweza kuwa na maudhui mazito zaidi ya kategoria ya PG katika masuala ya vurugu, uchi, uasherati, lugha, ‘shughuli za watu wazima’ au vipengele vingine. Maudhui ya dawa za kulevya yanaweza kuoneshwa hapa.

PG-13.PNG

R — Restricted (Imezuiwa)
Watoto walio chini ya miaka 17 wanahitaji kuandamana na mzazi au mlezi. Filamu yenye R ina maudhui ya watu wazima. Inaweza kujumuisha shughuli za watu wazima, lugha ya matusi, vurugu kali, utupu/ ngono na matumizi ya dawa za kulevya. Hivyo, wazazi wanashauriwa kuzingatia na kuchukua tahadhari sana. Watoto walio chini ya umri wa miaka 17 hawaruhusiwi kuangalia picha za filamu zilizokadiriwa R bila kusindikizwa na mzazi au mlezi mtu mzima. Pamoja na hayo yote, kwa ujumla, haifai kwa wazazi kuruhusu watoto wao wadogo kutazama filamu za maudhui haya.

R.PNG

NC-17 — No One 17 and Under Admitted (Hairuhusiwi kwa Walio Chini ya Miaka 17)
Kipengele hiki ni mrithi wa kipengele kichokuwa kikijulikana kama “X”. Nadhani hata hapa kwetu tulizoea kuita filamu zenye maudhui mazito ya ngono kama “Filamu za X” Filamu zinazopokea uainishaji wa NC-17 zinachukuliwa kuwa na maudhui yanayofaa watu wazima tu na si ya kuonekana kwa watoto. Hakuna aliye na umri wa chini ya miaka 17 anayeruhusiwa kutazama filamu hizi. Sifa za filamu ya NC-17 ni kwamba inapita filamu iliyokadiriwa R katika uoneshaji wake wa maudhui husika.

NC-17.PNG

Watoto huathiriwa kwa urahisi sana na ulimwengu unaowazunguka. Televisheni hutoa masaa ya burudani, lakini pia inatoa idadi kubwa ya maudhui hasi kwa watazamaji wadogo. Ni muhimu kuzingatia kile watoto wako wanatazama. Kama mzazi ni muhimu kudhibiti kile watoto wako wanapaswa kuona au kutoona katika filamu.

Tazama ufunguzi wa filamu ili kuona alama husika (zinazoonekana hapo chini) ambazo zinaeleza ni maaudhui gani yanapatikana katika filamu hiyo. Na siku hizi, ni muhimu pia kuwa mwangalifu na ukadiriaji hata wa PG.

Capture 1 PG.PNG

Capture 2 PG.PNG
 
Back
Top Bottom